Saturday, September 30, 2006

TUUNGEJUA!!!!

Mwaka juzi mimi na rafiki yangu Alina tulikuwa tunaongea habari za kuweka pesa za kuishi na za kutosha tukiwa tumestaafu kazi. Miezi mitatu baada ya hayo maongezi Alina alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya mapafu. Siku hiyo tuyliyovyo kuwa tunaongea hakujua kuwa anaumwa. Kazini kwangu kuna mama fulani alienda lunch, hakurudi maana alipata massive heart attack na kufa barabarani kwenye sidewalk. Kijana mwingine aliaga kuwa tutaona wiki ijayo lakini alipata ajali ya gari na kufa kesho yake.

Mnafahamu wimbo wa maiti? “Nimekufa leo, kesho ni zamu yako!” Ukweli, watu wanakufa kila siku. Wengine wanakufa shauri ya uzee, wengine kwa ajali, wengine kwa kuuliwa na binadamu wenzao au wanyama wa porini, wengine kwa ugonjwa. Hakuna mtu anayajua atakufaje. Nadhani watu wangejua wangekaa kwa woga, wangeshinda wanalia na kutetemeka ovyo.

Nadhani ni vizuri kuwa sisi bindamu hatujui siku ambayo tumepangiwa kifo. Fikiria kama tungejua. Dunia ingekuaje?

Tuseme fulani anajua kuwa atakufa leo jioni saa mbili usiku. Basi ingekuwa hekaheka kuomba kupiga simu kwa watu na kuomba msamaha kwa watu aliyowakosea. Au angesema mi nakufa kleo ngoja nilipize kisasi kwa kumwua fulani na fulani. Mtu angeenda kuichoma moto nyumba ya mtu akijua kuwa hata akifungwa jela siku yake ya kufa ni karibu. Mtu asingehangaika na shule akisema haina faida maana atakufa siku fulani hivyo hiyo shule haitamsaidia na anapoteza muda. Asingeenda kazini, maana angesema nakufa siku fulani ngoja nifanye shughuli zangu binafsi.

Haya tuseme fulani anajua kuwa atakufa wiki ijayo Ijumaa saa tatu asubuhi. Basi anamaliza pesa kwenye credit card kwa kula laifu, na kuachia familia yake madeni tele. Huko anafanya ngono ovyo bila kujali magonjwa wala nini. Huenda angekunywa pombe kupita kiasi na kumaliza siku zake akiwa kwenye coma hospitalini! Wengine wangeenda kutapeli watu wakijua kuwa kifo kiko karibu hivyo hawana shida.

Wengine wangejua siku yao, basi ndo wangemaliza vitu walivyoanza halafu hawakumaliza kama vile kuandika vitabu, kushona gauni, wangemaliza kujenga nyumba zao, wangekazania kumpachika mtu mimba, wangeenda kwao kuona wazee na ndugu zao ambao hawajaona miaka mingi. Mtu angekaa na watoto wakae anawaambia kuwa anawapenda badala ya kushinda baa anakunywa pombe. Wangekuwa kanisani, miskitini, temple na sehemu zingine za dini wakitubu madhambi zao. Mtu kwenye foleni angeomba apishwe maana ni karibu saa yake ya kufa. Kwa kweli kama watu wangejua siku yao ya kufa ingekuwa pilika pilika.

Mungu aliumba kila kitu na sababu. Kwa kweli tunapita tu katika hii dunia. Mabibi na mababu zetu walitangulia na vizazi vijavyo vinafuata. Na ni maksudi alituumba kusudi tusijue siku ya kuondoka duniani. Hivyo kaeni mfikirie je, ningejua nitakufa lini ningefanya nini.

Friday, September 22, 2006

Tanzanian Model Tausi Likokola - International Star



Huenda mmesikia jina la Tausi Likokola. Tausi ni model wakiTanzania anayejulikana kimataifa. Amekuwa kwenye maonyesho ya Urembo ya Gucci, Christian Dior, Tommy Hilfinger, Issey Miyake, na Escada. Mambo yake si mchezo. Huenda amepishana na Naomi Campbell na Tyra Banks kwenye Catwalk (jukwaa inayotumika kwenye maonyesho ya urembo).

Zaidi ya kazi za urembo Tausi amekuwa akifanya kazi ya kusaidia wagonjwa wa UKIMWI kupitia NGO yake iitwayo Tausi AIDS FUND . Aliaanzisha baada ya ndugu na marafiki wengi kuaathirika na huo ugonjwa hatari.

Akina Dada watapenda site yake. Anatoa tips za urembo kama kutunza ngozi, nywele, vyakula bora na mengine. Pia ametunga vitabu na kuna muhtasari za vitabu vyake.

Website ya Dada Tausi Likokola:

http://www.tausidreams.com

Ama kweli WaTanzania tunaweza kujivunia kuwa nasi tuko kwenye jukwaa la fesheni ya kimataifa. Hongera Tausi, mfano wako ni wa kuigwa.

Saturday, September 09, 2006

Cynthia Masasi - The Original Tanzanian Pin-Up Girl

Nilipokuwa nasoma Tabora Girls niliwahi kumwambia clasasmate wangu kuwa naona kawa, "Popular " sana. Nilisema hivyo kwa vile niliona kila mtu anampenda kuanzia wasichana wa O level na walimu wavulana wa shule zingine. Basi kusema hivyo aliona kama nimemtukana. Kwa kweli nilisema hivyo kwa nia ya kumsifia na siyo nia ya kumkashifu. Na aliona mbaya mapaka tunamaliza Form 6.

Sasa nasema kuwa Cynthia Masasi amekuwa ‘pin-up’ kwa nia ya kumsifia na siyo kumkashifu. Na sijui kama nimekosea kusema kuwa dada Cynthia Masasi ni pin-up girl wa kwanza Mtanzania. (Site yake ni http://www.cynthiamasasi.com) Kwa sasa anaishi Atlanta, Georgia, USA.

Ngoja niwaeleze maana ya ‘pin-up’ girl. Ni mrembo anayekuwa kwenye poster au calendar na mara nyingi mrembo anakuwa kavaa nguo ya kuogelea, mara nyingi bikini. Picha inaitwa pin-up kwa vile unakuwa chomekwa ukutani. Akina Marilyn Monroe na, Jayne Kennedy (mweusi), walikuwa pin-up girls. Na enzi zao nadhani wanajeshi wengi, vijana wa shule waliweka picha zao ukutani na kwenye locker. Na kila wiki gazeti la ‘Jet’ inatoa pin-up girl wa wiki. Wanawake wengi hawakubali iwekwe kwenye sebule zao. Wanaume ndo watakuwa wanunuzi wakuu. Lakini ndo swimsuit kalenda zilivyo. Unazikuta mfano kwenye maklabu ya wanaume, barbershop, vyuoni kwenye bweni za wavulana.

Kama hamjasikia, Cynthia anatoa kalenda enye picha zake akiwa amevaa swimsuit. Kila mwezi na picha yake. Nimesikiliza interview Cynthia aliyofanya na Kaka Deus Gunza wa Pod Radio Butiama huko Columbus, Ohio.

Cynthia anasema alikuwa na copy 5,000 za kalenda yake na zimeisha. Imebidi agize zingine. Nasema ‘Hongera ‘kwa kupendwa hivyo! Kwanza hapa Marekani model wangapi watauza kalenda nyingi hivyo kama si Supermodel au wana-promote kitu kama pombe na sigara.
Modelling una sehemu nyingi mfano kuna runway model, catalog model, store model, kalenda model. Nampongeza Cynthia kwa kuingia katika fani ya modelling, tena ana model akiwa amevaa bikini. Umezua maneno kwa vile watu wanahushisha na umalaya. Kwa mila na desturi za kiTanzania naweza kusema kavunja miiko maana tumefundishwa kujifunika . Lakini nikiona bikini na picha za wanawake huko Swaziland, tena wanaacha matiti na matako nje, nasema bora ya hiyo bikini. Kwa Marekani si wengi wanaweza kuwa na mwili wa model. Na hao supermodel wanajishindisha njaa na kujikondesha mno.

Kwa wapenzi wa rap na MTV, Cynthia ametokea kwenye music video za Nelie, Bow Wow, na Ludacris akiwa kama mcheza densi. Anasema amekuwa kwenye video 15. Kwa mashindano yaliyoko kapiga hatua, maana kwenye audition wanatokea mamia ya wasichana. Kuchaguliwa wakati mwingine ni kama bahati nasibu. Huenda kuna siku tutamwona kwenye fashion show ya Boateng.

Kwa binti zetu wa kiTanzania nasema, fanyeni kama moyo wenu unavyowatuma. Na kama umebarikiwa na mwili wa kuwa model, na unapenda fania hiyo fuatilia. Si lazima uwe swimsuit model, tunaweza kukuona kwenye mafashion show. Nani atakuwa 'pin-up' girl ijayo?

Cynthia atakuwa na Calendar party Chicago, Illinois, September 30th. Atazindua Calendar yake ya 2007.

Monday, September 04, 2006

Crocodile Hunter Steve Irwin Kafa


Loh! Leo asubuhi nimeamka nakufungua TV na kuona habari kuwa Steve Irwin au kwa jina lingine Crocodile Hunter (mlinda mamba) kafa. Wanasema kauliwa na samaki aina ya Sting Ray. Hicho kichomi chake chenye sumu kilimchoma kwenye moyo.

Nilisikitika sana kuwa kafa lakini huko najiuliza je ansingekuwa anacheza na wanyama hatari si angekuwa bado yu hai? Siku zote nilisema ngoja tutasikia kuwa kaumwa na nyoka na kafa. Hata siku moja sikudhania kuwa hatima yake ingekuwa samaki Sting Ray.

Nilipokuwa nakaa Chuo Kikuu cha Dar es Salaaam, jirani yetu mzungu akawa anatulaumu kwa kuua majoka. Na kama kulikuwa na nyoka nyumbani kwake, analazimisha houseboy wake amkamate na kumpelea idara ya Zoology pale UDSM. Mzungu mwenyewe alikuwa mshenzi, anamfuata na gari yake kuhakikisha kuwa anampeleka kweli!

Ilikuwa sisi wengine tukiona nyoka, tunatafuta fimbo, mawe na kuua! Kwanza ukiumwa na huyo nyoka, kutakuwa na dawa kweli dispensary ya kukukutibu. Au unaweza kuchelewa kupata usafiri wa kwenda hospitalini na kufa. Na mara nyingi tulisikia mtu kafa kwa kuumwa na nyoka, hivyo kwa nini tusiwaue! Ua au uliwe!

Lakini wazungu sijui wakoje, wakiona mnyama hatari wanataka awe pet. Lakini mnyama pori ni mnyama pori tu! Mnakumbuka yule tiger alivyomtafuna Roy, huko Las Vegas kwenye Seigfried & Roy Show. Yule tiger alifugwa nao taokea azaliwe. Je, mnakumbuka yule kijana wa kizungu mwenye miaka 17 aliyekufa baada ya kuumwa na pet kifutu (viper) wake huko Kenya? Alikuwa anafuga majoka wa kila aina nyumbani kwake, macobra, chatu, nk. na alishumwa nao, lakini huyo kifutu ndo kamwuma na kumwua.

Haya nirudi kwa marehemu Steve Irwin. Ilikuwa wakati mwingine nikitazama show zake nasema anajiona mungu wa wanyama na hawatadhuru. Utamwona yuko Afrika anakamata black mamba na cobra mwenye hasira. Mara anacheza ma mamba mkubwa kweli kweli huko kashika mtoto wake, tena mdogo mwenye umri miezi michache tu. Tena anamtembeza mbele ya mamba kama kitoweo vile. Halafu alidiriki kusema, alijua kuwa mamba hawezi kumdhuru mwanae. Bora angesema ilikuwa bahati mamba hakumdhuru.

Na leo tunasikia alikuwa anaogelea na sting rays huko Australia kwa ajili ya show yake, ndo alikuwa anaogelea juu ya sting ray na stingray kanyanyua kichomi chake na kumchoma kifuani kwenye moyo! Naona huyo sting ray alikuwa si rafiki yake, au alichoka naye.

Mungu amlaze kaka Steve Irwin mahali pema mbinguni. Amen. Na kifo chake iwe fundisho kwa wengine, mnayama pori ni mnyama pori.