Saturday, November 26, 2005

Ugonjwa wa Mafua ya Ndege (Bird Flu) – Disease of the Day!

Ugonjwa wa Mafua ya Ndege (Bird Flu) – Disease of the Day!

Haya jamani, kuna huo ugonjwa unaitwa Bird Flu ambayo wanasema iko hatarini kuingia bara Marekani na kuangamiza maelfu ya watu. Kila ukifungua TV unasikia mtu au ndege kapatikana na ugonjwa huo hatari huko China au bara Asia eti kapata kwa kula kuku mwenye huo ugonjwa. Basi watangazaji wanaanza kujadili na kutabiri lini utaingia Marekani.

Lakini nataka kuzungumzia hasa jinsi watu Marekani walivyo waoga wa magonjwa yanayotoka barani Asia na Africa. Miaka ya nyuma kulikuwa na tishio la ugonjwa wa Ebola. Basi waafrika waliotoka barani Afrika walikuwa wanachunguzwa kwa makini. Yaani mtu atoke Africa hasa Congo, aende kwa daktari hapa USA, basi kisirisiri daktari anajaza ile fomu ya CDC (Center for Disease Control) halafu mtu anashutukia anatembelewa na mtu wao! Mtu atasumbuliwa na simu, visits, halafu medical record yake itachunguzwa we! Nia yao ni kuwa huo ugonjwa usisambzwe kwa watu wengine.

Halafu ulitokea ugonjwa wa West Nile Virus. Huo ugonjwa unasambazwa na mbu. Iliingia na iliua watu wachache. Yaani huo uoga wa mbu ilikuwa balaa. Mpaka walichora katuni ikionyesha ndege ya jeshi inatumwa kuua mbu moja! Caption ilisema (West Nile Mosquito sited!) Walikuwa wanapuliza miji mizima na mapori dawa ya kuua mbu kusudi waue mbu. Wanadai uliletwa nchini Marekani na ndege iliyotoka Africa. Eti mbu mwenye West Nile alidandia lifti kwenye baggage compartment ya ndege kutoka Africa na alishukia Logan International Airport! Basi hata ndege zilizotoka Afrika zilikuwa zinapulizwa dawa mara wakifungua mlango wa baggage compartment!

Kutokana na huo uwoga waBongo ma waafrika wengi wamegunda ni bora kusema unaumwa UKIMWI kulikoni usema unaumwa Malaria! Kuna MBongo alifukuzwa kazi baada ya kutoka likizo Tanzania. Alirudi na malaria, kachukua off (sick days) siku mbili. Aliporudi kazini, na bosi kamwuliza alikuwa anumwa nini. Jamaa bila kusita alijibu kuwa alikuwa na Malaria! Loh! Yule bosi aliogopa nakumfukuza kazi mara moja eti alihofu ataambukiza watu wafanyakazi ofisini huo ugonjwa. Na hata mwafrika akienda hospitalini USA analalamika anaumwa malaria utaona wafanyakazi, manesi na hata madaktari wanamkwepa na kumtenga na wagonjwa wengine. Sijui wanadhania malaria ni ugonjwa wa aina gani! Wnagejua hiyo malaria ndio common cold ya waafrika!

Na tusisahau tishio la SARS mwaka juzi! Mbona waChina wenye Restaurants hapa USA walilia shauri ya kukosa wateja! Watu kwenye TV na magazetiu walidai ukienda Chinatown au kula Chinese food unaweza kupata SARS! Jamani! Na kweli watu hawakwenda huko!

Haya nimegusia hayo mgonjwa mengine, lakini leo hii naona watu hapa USA wanahofia hiyo Bird Flu. Halafu wanadai kuna chanjo lakini ni watu wachache wanaoipata, ni wenye hela ya kulipia na watu wakubwa yaani wenye vyeo. Wanasomba hiyo chanjo ya Tamiflu na kampuni mwenye patent haitaki makampuni mengine yaitengeneze generic version, ambayo inaweza kuuzwa kwa bei rahisi. Huo ndio ubepari hasa… kujali pesa mbele ya maisha ya binadamu! Kwa sasa hapa Marekani mtu wa kawaida akina kamchape class, tulie tu. Lakini hata hivyo najiuliza kama kuna haja ya kupata hiyo chanjo kweli, na je, Bird Flu ikiingia USA itakuwa hatari kama wanavyotabiri?

WaMarekani wako macho sana. Nyama ya kuku na bata kutoka bara Asia imepigwa marufuku kuingia USA kwa sasa. Kuku, bata, bata mzinga (turkey) wanapimwa kabla ya kwenda kwenye bucha. Na siku akipatikana kuku, bata, au bata mzinga mwenye huo ugonjwa mtasikia, nyama ya kuku hakuna madukani! Maana serikali wata- recall yote na kuichoma moto! Au hata ile nyama iliyo salama, watu wataogopa kununua. Heri tuliyozoea kula maharagwe na mchicha!

Halafu watu wanaotoka barani Asia/ China kwa sasa wanapimwa Airport wakishuka kwenye Ndege. Kama wana dalili ya ugonjwa wanawekwa quarantine. Nasikia hata marubani na ma-air hostess wa Ndege wamembiwa wawe macho kwa watu wanaokohoa au wenye dalili za mafua kwenye ndege halafu wawa ripoti! Juzi juzi hapa USA kuna Mzee wa Kichina alifariki baada ya kurudi kutoka likizo huko China. Walizuia familia yake wasimzike mpaka maiti ilifanyiwa uchunguzi. Lakini kumbe hakufa kwa Bird Flu bail Natural causes, yaani ilikuwa wakati wake.

Halafu hapa USA watu wanapenda kulisha ndege chakula yaani Birdfeeding kama hobby. Wengine wameacha eti kwa vile wanaogopa hao ndege wataleta bird flu kwenye balcony na yard zao. Serikali wamekwisha tangaza kuwa kulisha ndege ni salama, hivyo hakuna haja ya kuacha! Ndege wenyewe hasa ni wa porini na hapa USA kuna akina blue jay, sparrows, robins, njiwa, lark woodpecker, na aina mbalimbali. Wakati wa winter wanapendeza kweli.

Pamoja na yote hayo nashukuru kuwa watu wako macho kwa magonjwa tishio. Na ni bora huko Afrika watu wawe makini pia maana ukiingia huko itakuwa balaa. Kwa kweli ukiingia barani Afrika maelfu ya watu watakufa. Hivi waliopewa jukumu la kufuatulia masuala ya Public Health Afrika wanafuatilia kweli? Au wana tumia muda mwingi kwenye miradi kusudi wapate pesa za kutosheleza mahitaji ya familia ya mwezi?

Pamoja na uwoga kuna mengi ya kujifunza kuhusu jinsi wanavyoshughulikia magonjwa yanayohatarisha usalama wa jamii! Mko macho Lakini?

Tuesday, October 18, 2005

Acheni Ushamba

Acheni Ushamba!

Jamani, jamani, jamani! Siku hizi nikiona vijana waBongo hapa mitaani Boston nakimbia! Hao vijana siyo wale wa miaka ya nyuma waliokuwa tayari kufanya kazi mbili/tatu ili waweze kuishi vizuri na kupeleka zawadi nyumbani. Hapana vijana wa siku hizi wanataka vya dezo! Wamekuja Marekani wakidhania maisha USA ni kama vile kwenye video za Rap. Hapana vijana, maisha siyo hivyo kabisa.

Hapa USA kama hukuja na hela zako basi uwe tayari kuchapa hizo kazi mbili/tatu, utafanikiwa!

Lakini kinacho niudhi hasa ni hao vijana wanaoenda madukani na kuiba, yaani shoplifting! Yaani mtu anaingia dukani anasomba vitu, tia ma-cap kichwani halafu wanatoka nje ya duka. Wanakamatwa halafu unaombwa uwawekee dhamana! Si waliiba wao wacha wakome huko jela! Tena jela za Boston ni nzuri kuliko kupelekwa Keko!
Nasema hao vijana ni washamba maana ukiwauliza kwa nini waliiba, watasema, “Oh, sikujua kama wananiona!” Hawakuoni???? Heh!

Mjue mkifika kwenye mall tena parking lot, mnaanza kuchgunguzwa na makamera yaliofichawa kila mahala isipokuwa chooni! Yale mapambo na magololi yanayoing’inia si urembo tu, bali ni masecurity camera. Hivyo huwezi kusema, “Oh sikuiba!” huko store detective anakutolea kanda ya video ambacho wewe ndo star! Wanaona kwa vile mlango huko wazi hakuna security, au watu wengi basi ni free for all.

Kitu kingine hao vijana,utasikia wanaongea, sijui vitu gani, wakidhania English! Wanajaribu kuiga ma-slang wanaosikia kwenye movies. Nyie! Watu hawaongei hivyo! Ukitaka kazi ya maana ujfinze kuongea English! Yaani inatisha maana huwezi hata kuelewa ansemaje na Slang zake zenye Bongo accent!

Na acheni kuvaa kama gangsta! Kwanza ukikosea rangi utapigwa risasi na ma-gang au utasumbuliwa na polisi wakidhania wewe ni gang banga! Ngojea niishie hapo… maana!

Sinema Mpya - TUSAMEHE

Watu wanangojea kwa hamu sinema mpya iitwayo, TUSAMEHE. Hiyo sinema ni kitoto cha Ndugu Josiah Kibira wa Minneapolis, Minnesota. Sinema hiyo una husu janga la ukimwi kwa sisi waTanzania na Afrika kwa ujumla. Hadithi yake ni hivi, Ndugu Bilantanya kasoma USA na kafanikiwa kupata kazi nzuri, anaoa Mtanzania mwenzake. Lakini anatembea nje ya ndoa na kupata ugonjwa wa ukimwi na kumwambukiza mke wake. Lakini cha kusikitisha mke wake anapata mimba huko Bilantanya anazidi kuumwa. Anaomba aweze kuishi mpaka mtoto atakpozaliwa. Je, atafanikiwa! Kwa habari zaidi nenda kwenye site ya Kibira Films, http://www.kibrafilms.com/tusamehe.

Walioigiza hiyo sinema ni waTanzania waishio USA, na mimi nimo kama Mama Kurusumu. Nilifurahi sana kupewa nafasi ya kushiriki katika hiyo sinema, kwanza sinema kuhusu sisi waafrika hapa USA ni chache. Pia, mimi ni sawa na waTanzania wengine, nina Ndugu, marafiki, majirani na wafanyakazi wenzangu waliokufa shauri ya ukimwi. Kama huo ugonjwa utasaidia kupunguza kasi ya ukimwi au kusaidaia dawa zipelekwe Afrika kusaidia waathirika tutatkuwa tumefanya la maana.

Thursday, September 29, 2005

Barack Obama

Hii ni jambo la kujivinia sisi wana Afrika Mashariki kuwa huenda rais wa kwanza wa Marekani Mweusi huenda akawa Barack Obama ambaye ni Senator huko Illinois. Senator Obama ni hafukasti, mama yake ni Mzungu na baba yake ni Mkenya. Ajabu zaidi ni kuwa mama yake ni mtukuu wa Jefferson Davis ambaye alikuwa Kiongozi wa Confederates. Yaani enzi za utumwa Marekani, Davis alikuwa ni rais wa maConfederates waliochukia weusi na kutaka wabakie katika utumwa na kusababisha Civil War, vita vya wenyewe kwa wenyewe (1860’s). Watu wa Kaskazini hawakutaka utumwa na watu wa Kusini walitaka utumwa udumu. Huyo Jefferson Davis bila shaka anajigueza huko kaburini kwake.

Mwaka jana, Obama alipewa nafasi kuwa keynote speaker katika Democratic National Convention, wana Demokrat walivyomchagua bwana John Kerry kuwa mgombea wa rais katika uchaguzi uliyopita. Na nilishangaa jinsi alivyoweza kuongea na watu kumsikiliza kwa makini kama vile wanamsikiliza Martin Luther King au Mahatma Gandhi. Kila mtu alimpenda na wazungu ndo kabisa sikusikia neno baya juu yake isipokuwa kutoka kwa mpumbavu Alan Keyes (MRepublican) aliyekubaliwa kuwa toi.

Na hivi karibuni alitoa shutuma kali dhidi ya serikali ya Marekani kuhusu Jinsi walivyowasaidia walioathirika na Hurricane Katrina. Bila haya, alisema kuwa serikali ilikuwa legelege na response yao kwa vile walioathirika wengi walikuwa ni weusi na maskini. Katika siku zijazo tufuatilie kawa makini matendo na maneno ya Senator Barack Obama.

Wednesday, September 28, 2005

Any time is Swahili Time

Baada ya kuongo waBongo wenzangu wakiblogu wa Kiswahili na mimi nimeamua nianzishe blogu ya kutoa maoni kwa Kiswahili. Hii ni posti ya kwanza.