Monday, May 22, 2006

Barbaro Anusurika Kugeuzwa Gundi!





Nadhani kuna wengine hapa mnashangaa naandika kuhusu nini. Ngoja niwaeleze.

Barbaro ni farasi aliyeshinda mashindano ya Kentucky Derby hivi karibuni. Kentucky Derby ni mashindano inayofanyika kila mwaka kwa ajili ya mafarasi. Ni kama Olympiki ya farasi. Watazamaji wanavaa nguo kama vile wanakwenda kwenye arusi au kula chakula White House na MaRais. Hao farasi wana majina yao. Na wenye farasi wanatumia mapesa chungu nzima kumlea na kumfunza kukimbia kwenye mashindano. Ni sifa kubwa kuwa na farasi kwenye haya mashindano. Huwa nangojea kwa hamu Kentucky Derby kusudi nione jinsi hao mafarasi wanavyotembezwa kabla na baada ya shindano. Wanapendeza kweli hasa wakifanya miondoko (trots) yao.

Kama unajua mafarasi gani ni wazuri unaweza kutajirika maana wanawafanyia ‘betting’ (kama kamari, bahati nasibu). Ukicheza combo inayoshinda kwa dola 5 unaweza kutoka na dola zaidi ya 40,000. Halafu mashindano hayo yanakuwa sinema kabisa maana utaona watu wanvyofurahia wakishinda na wanavyolia wakishindwa. Mwaka juzi mzee wa kizungu aliyeonekana mahututi lakini alienda akiwa kwenye kiti cha wagonjwa (wheelchair) alivua Oxygen mask yake na kuanza kurukaruka farasi wake ‘Smarty Jones’ alivyoshinda. Mbona watazamaji walianza kuwa na wasiwasi kuwa atafia hapo kwenye track!

Sasa wiki mbili tu zilizopita Barbaro alishinda Kentucky Derby. Juzi maskini ya Mungu, kavunjika mguu wake vibaya akiwa kwenye mashindano ya Preakness. Loh! Watu walianguka kilio kama vile mtu kafa. Ni hivi, kwa kawaida farasi akivunjika mguu anauliwa mara moja kusudi asiteseke. Na walitakiwa wampeleke pembeni wampige risasi. Halafu nzoga ya farasi inatumika kutengeneza gundi, lakini bila shaka anagezikwa kwa heshima zote za farasi mshindi. Lakini hawakumwua. Badala yake ilitokea gari la wagonjwa (ambulance). Na walimpeleka kwenye hospitali ya wanyama wakubwa. Farasi kama umemona live ni mnyama mkubwa sana. Huko hospitalini walimpiga ma X-ray na kugundua kuwa mguu wake umevunjika vipande vipande. Basi walimfanyia upasuaji na kujaribu kutengeneza huo mguu. Upasuaji huo ulichukua muda wa masaa manane. Alivyotoka, Barbaro kaamka na kutafuta chakula na mabibi pamoja na kuwa na lizinga la POP mguuni. Cha kuchekesha watu walipeleka maua, kadi, mabango yakumtakia afya njema na apone. Huyo mtalaamu wa upasuaji wa wanyama lazima atatafutwa sana na kutengeneza kibunda kwa vile alimfanyia upasuaji mshindi wa Kentucky Derby.

Na nilisahau kuwaeleza, baada ya Barbaro kuumia, mshindi wa Preakness, Bernardini ,hakupata sifa kamili. Macho yote yakawa kwenye hali ya Barbaro. Sasa hali ya Barbaro ni habari kubwa kuliko ushindi wa Bernardini.

Haya sasa Barbaro akipona na akiweza kuishi, hatakuwa anakimbia tena. Kazi yake itakuwa ni kupanda mbegu tu! Watu watakuwa wanalipwa kusudi farasi zao majike yapate nafasi ya kupandwa mbegu na Barbaro aliyeshinda Kentucky Derby 2006!

Najua kuna wanaume lazima wanamwonea wivu! Wanafikiria kazi yake pekee ya kupanda mbegu! Haya tungojee kuona mwakani dunia ya mafarasi itakuwa na drama gani.

3 comments:

  1. Ahsante kwa habari hii,
    Kila mara nikiona habari kama hii huwa siishi kuchekecha bongo yangu nikifanya tafakuri ya jinsi gani sisi tutokeao afrika tunatofautiana na hawa wenzetu.Kwao haijalishi wasudani wangapi wanakufa kwa njaa inapokuja kuhusu wanyama wao hususani kama wale pets.Hao hupendwa kuliko wanadamu wengine.Ni watoto katika familia.Kwa kweli tupo tofauti jamani.

    ReplyDelete
  2. Naunga mkono kabisa hili swala Jeff. Hawa watu wanapenda ma pet wao hasa Mbwa na Paka.Farasi ni ghali zaidi katika nchi nilizo ishi hivyo nivigumu kustukia mapenzi yao kwao. Nilishawahi kukosana na jirani kwasababu nilitoa hoja kuwa ana mbwa wengi ndani ya nyumba, alafu walikuwa wananifurahia sana ,kutaka kuninusanusa basi akastukia kuwa siwafurahii.Hakunificha akasema Simon najua hupendi Mbwa wangu hivyo usitegemee kama nitakukaribisha kwangu tena.Na ukweli ikatoka hiyo.

    ReplyDelete
  3. Hii imenichekesha sana hadi natoa machozi. Imenifurahisha sana. Lakini pia imenikumbusha mbali sana. Kaka yangu mtoto wa baba mkubwa (45) ni mlemavu wa miguu tangu utotoni kwa sababu alikosa matibabu mazuri ya miguu baada ya kuvunjika. huyu ni mfano wa watazania wengi na waafrika kwa ujumla wanaopata ulemavu kwa kukosa msaada mzuri, hospitali nzuri na hasa uwezo wa kifedha wa kuwapatia matibabu. Ni hospitali chache hadi sasa, hapa Tanzania zenye uwezo wa kuwatibu wagonjwa wa mifupa ikaunga sawa sawa bila wasiwasi, achilia mbali kwamba wanaopona wanatumia miezi lukuki kitandani. Wengine wameshindwa kurejea hospitalini kuondoa vyuma walivyofungwa kushikishanisha mifupa. lakini huko ughaibuni wanapata fedha hata za kutibu wanyama na kuwaponyesha vizuri kwa lengo la burudani. Inatia moyo, inafurahisha na kuhuzunisha kwa upande mwingine. Asante sana Chemponga.

    ReplyDelete