Monday, November 13, 2006
Massachusetts yapata Gavana mweusi! (Ni wa pili katika Historia ya Marekani)
Wiki iliyopita siku ya tarehe saba Novemba, 2006, ilitokea jambo la kihistoria hapa Massachusetts, Marekani. Ni Gavana mweusi wa pili tu katika historia ya Marekani. (Wa kwanza alikuwa Douglas Wilder wa Virginia mwaka 1990). Wingi wa wapiga kura walimchagua mtu mweusi kuwa Gavana! Na walimpigia kura kwa wingi mpaka mpinzani wake ilibidi akubali kuwa kashindwa vibaya mno!
Aliyechaguliwa kuwa Gavana mpya wa Massachusetts ni, Deval Patrick ambaye yuko kwenye chama cha Democrats. Bwana Patrick alizaliwa na kukulia ghetto ya Chicago. Bahati nzuri alikuwa na kipaji kimasomo na alifanikiwa kusoma Milton Academy kwa scholarship na Harvard University. Kwa habari zake zaidi unaweza kusoma hapa.
Mpinzani wake alikuwa bibi mmoja wa kizungu, Kerry Healey. Huyo mama ni tajiri na alikuwa Naibu Gavana wa Bwana Mitt Romney ambaye ni Gavana wa sasa na hashindi hapa Massachusetts. Si uwongo kuwa mwaka 2002, Romney alidanganya watu wa Massachusetts na kusema kuwa hawanii uraisi, kumbe kama Republicans wenzake ni mwongo mkubwa. Anagombea urais mwaka 2008! Na alimchagua Healey asiyekuwa na sifa za siasa zaidi ya kuwa tajiri kuwa Lieutenant wake.
Wakati wa kampeni ya Healey hivi majuzi, Romney alimtupa pia na wala hakumsaidia. Lakini niachane na mambo ya Romney maana nitasema mengi juu yake akigombea uraisi. Na si mazuri.
Healey aliishia kuchukiwa vibaya na watu. Hata Republicans wenzake walimgeuka na kumtupa. Huyo mama alikuwa na kampeni chafu na ya kibaguzi. Tangazo lake la mwisho kwenye TV ilikuwa na mzungu dume aki-jog kwenye eneo la wazungu huko tukimsikia mawazo yake. Yaani alisema mabaya mpaka tulisema alichoacha kusema ni kuwa hataki kuongozwa na Gavana mweusi.
Na pia alikuwa na tangazo la mbakaji mweusi ambaye Deval alimsaidia akiwa akifanya kazi ya mwendesha mashitaka. Heh! Jamaa si alikuwa anafanya yake. Na Healey alidiriki kutuma watu nyumbani kwa Patrick na Naibu wake Tim Murray kufanya maandamano wakiwa wamevaa nguo za wafungwa. Bahati yake mbaya mtoto wa Tim Murray mwenye miaka 12 alikuwa nyumbani peke yake akijiandaa kwenda shule. Waliishia kumtisha mtoto! Watu walimgeuka, na wakasema huyo mama hafai kabisa. Kaishia kuonekana kama mtu mwenye roho mbaya ajabu. Pia sikumwona akifanya kampeni kwenye maeneo ya weusi au waspanish. Walimwonyesha kwenye TV akiwa kwenye barbecue eti kwenye nyumba za wananchi wa kawaida. Doh, mbona nyumba zenyewe zilikuwa za wazungu tena nyumba za fahari.
Patrick wakati huo alikataa kabisa kufanya kampeni chafu dhidi ya mwenzake na alishinda. Tena kwa kura nyingi mpaka Democrats nchi nzima wanamtazama kwa mshangao na wanataka kujifunza kutoka kwake.
Januari, ndo Gavana Patrick ataanza kazi yake rasmi na naamini kuwa atakuwa Gavana mzuri maana ukiwa mweusi ni lazima ufanye kazi mara nne ya mzungu kusudi uonekane kama unafanya kazi.
Mengine, Democrats watawala sasa, walifanikiwa kunyakua Congress na Senate! Raisi Bush alie tu! Udikteta wake umekwisha! Watu wameamka sasa. Na wanasema kuwa Bush alikuwa Mnyonge kweli kweli siku ya uchaguzi baada ya kuona Republicans wanaangushwa vibaya! Watu wanasema Republicans waliangushwa katika ‘Tsunami’ ya kura! Na kweli ilikuwa tsunami na watu walimpiga kura kwa wingi mpaka sehemu nyingi walishiwa kura.
Ama kweli Demokrasia inafanya kazi Marekani.
No comments:
Post a Comment