Wednesday, January 03, 2007

Poleni Wafiwa


Kwanza naomba mnisamehe kwa kuongea kuhusu kifo. Najua si jambo la kufurahisha.

Leo nimekwenda kwenda 'Wake' (kilio) ya Mama Anastazia Rupia. Alifariki hapa Boston siku chache kabla ya Krismasi. Alikuwa amekuja kwenye mahafali ya mwanae, Septemba na kwa bahati mbaya alianza kuumwa muda mfupi baada ya hapo.

Kwa kweli waBongo walitokea wengi kuwafariji wenzao waliofiwa na mama yao. Mchungaji mzungu alisoma misa mzuri sana. Watu walikuwa na majonzi hasa mtoto wa marehemu John Rupia, alivyosimulia habari ya maisha ya mama yake na alivyougua. Alivyomaliza naye, John alianza kulia ndo hapo chumba chote tuliishia kulia.

Maiti anawasili Dar Jumamosi na ndege ya SwissAir, naomba muwepokea vyema huko. Poleni.

Lakini jamani ukweli uchungu wa kufiwa unaujua wewe uliyofiwa. Hata tukikupa pole ngapi, marehemu ni marehemu, hatarudi. Watu wataenda zao kwenye shughuli zao na wewe mfiwa utabakia na majonzi yako.

Watu wengi wanajua uchungu wa kufiwa na mtu wa karibu. Nilivyofiwa na mume wangu wa kwanza, mwaka 1995 hata sikumbuki nilifikaje Tanzania. Nilikuwa nasoma hapa Boston, nikapata taarifa, nikakatiwa tiketi na nikashutukiwa niko Dar uwanja wa ndege na wafanyakazi pale walinipa pole na kuniuliza kama nina mtu wa kunipokea. Ile safari yaani ilikuwa kama vile ndoto mbaya na niseme miezi kadhaa baada ya kufiwa si kuwa mzima maana nilijisikia kama sijui niko wapi. Wakati mwingine nilikuwa najiona kama niko kwenye wingu, mara naona mwili mzito kutembea shida. Mungu alinisaidia kipindi kile. Amini usiamini, miaka zaidi ya kumi imepita na bado nina omboleza ila siku hadi siku uchungu unapungua. Unapungua lakini haushi kabisa.

Lakini sisi tuliyobaki inabidi tuendelee kuishi na kujenga maisha yetu na kusimulia kwa wanaetu kuhusu ndugu zao waliowatangulia hapa dunia.

Kwa kila mtu aliyefiwa na ndugu au rafiki yake nasema, pole. Poleni wafiwa wote popote mlipo, na Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu. AMEN.

2 comments:

  1. Poleni wafiwa, pole da'Chemi, nilishawahi pia kusoma habari yako nadhani katika web yako ya Paka shume. Kusahau kitu cha ajabu sana.

    Mwaka mpya mwema.

    ReplyDelete
  2. Mimi naamini sana kuwa wapendwa wetu waliotuacha, wako nasi kila siku. Na tukiwaomba watusaidiae, wanaweza kutusaidia. Na kila tukitaja majina yao, wanaitikia.
    POLENI WOTE.

    ReplyDelete