Saturday, June 30, 2007

Dada Ummie Alley Hamid Amsuta Eric Shigongo (Amina Chifupa)

BURIANI MWANANGU AMINA CHIFUPA: PRINCESS WA TANZANIA

Na Ummie-Mahfoudha Alley Hamid

Kifo hakina wakati, huruma wala subira, huja kwa saa na muda uliopangwa na mwenyewe Subhana wa Taala Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwanaadamu hawezi kukipangua. Ya laiti ingelikuwa uwezekano huo upo, basi tungalipangua vifo vya wengi ambao ni vipenzi vyetu kikiwemo hichi cha juzi cha mbunge wa Viti Maalum CCM anaewawakilisha vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Amina Chifupa Mpakanjia.

Wa kale walisema chema hakidumu. Nimeuthibitisha ukweli wa usemi huu kwa kifo cha binti huyu. Marehemu Amina alikuwa na sifa zote za kupendeza. Alikuwa kijana, mrembo, mtanashati, mcheshi, msomi kwa kiasi chake na zaidi ya yote alikuwa mtu wa watu.

Si muda mrefu tangu nimjuwe Marehemu. Nilimsikia sauti yake wakati akiwa mtangazaji wa redio, na nikamjuwa kupitia magazeti na runinga. Nikaja kumjuwa baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa vijana kupitia chama tawala cha CCM. Kabla ya kumjuwa fika, nilikuwa najisemea ki moyo moyo, “Hmmmm, binti kama huyu mwenye sifa zote hizi, kweli atakuwa na uwezo wa kuongea na watu wa hali ya chini anaowawakilisha? Hivi huyu si anaringa na kujiona kuwa hakuna wa kumgusa?” Hakika dhana ni dhambi na kweli nilipata dhambi kwani nilivyomdhania ikawa ni tofauti na nilivyomjua. Ukweli nilijikumbuka mimi enzi zangu nilipokuwa natikisa na namna watu walivyokuwa wanaona najivuna

Nilimwmjuwa Amina kwa muda wa miaka chini ya miwili ya ubunge wake. Aliniita “mama” nikamwitika “mwanangu”. Alikuwa ni mtu “Simpol” kwa lugha ya mjini. Alikuwa mchangamfu na pia alikuwa ni mtu mwenye sikio la kusikiliza watu na shida zao ingawa shida nyengine zilikuwa si rahisi kwake kuzitatua.

Umaarufu, ujana, urembo, wema wake ulimfanya alengwe shabaha na kila chombo cha habari, iwe kwa wema au utelezi alioufanya. Ujana wake ulimfanya awe au afanye mambo mengi ambayo yanafanywa na yalifanywa na wengi ambao walio na umri wake. Binaadamu tunasahau kuwa “ujana ni moshi” na mwishowe hupita tu. Tunasahau kuwa tumepitia hatua zote hizo na zaidi ya hizo katika ujana wetu.

Alifanya mambo ya kawaida ya ujana na urembo, alikuwa mlevi? Sikumfahamu hivyo, mvuta sigara au bangi? Sikumjuwa hivyo, mtumiaji wa madawa ya kulevya? Sikumuona na sidhani kama alikuwa hivyo. Lipi geni alilokuwa nalo Marehemu Amina hata kusakamwa na kudhalillishwa hadi kufikia kupoteza roho yake changa?

Tujiambie na tujiulize, hivi sisi tukiwa kama waandishi wa habari, ni lazima tuwe na habari mbaya (negative) ndio tuandike au ndio ziuzike? Hatuwezi kuwa na upande mzuri (positive) side of issues? Kwa nini muandishi wa habari mwenzetu anaeanza maisha na malengo yake awe ndio chanzo chetu cha habari mbovu zilizopo na zisizokuwepo? Vijarida vya udaku haviuziki bila ya kuwepo uwongo usokifuniko?

Nasema hivi kwa sababu nimesikitishwa na muandishi Eric Shigongo wa gazeti la IJUMAA ambalo slogan yake ni “We belong to God” yaani wao ni waja wa Mungu, na namna alivyomsakama mwana wa watu na kusahau hiyo slogan yake ya kuwa yeye ni mja wa Mungu na Marehemu Amina pia ni mja wa Mungu. Amemuekea makala spesheli ya kumdoboa na kumnazi’i kadmnas bila kimeme. Anamkashifu na kuashiria kuwa Marehemu amefika kumfata kwake na kujitakisha!

Shigongo amemkejeli Marehemu eti asijifananishe na Mhe. Migiro na Mhe. Meghji. Kwa nini iwe vibaya kuwa na malengo? Hata Waheshimiwa hao walimhusudu Margaret Thatcher, Golda Meyer, Bandaranaike, Madeline Albright, Indira Ghandi na Bi Titi hawa wakiwa wachache tu kati ya wengi. Hakuna aliezaliwa na ujuzi usio weza kufikiwa na wengine. Hakuna kati yetu aliejuwa tu bila kuiga au kuweka malengo. Amemkejeli kwa bezo eti hata nae awe katika NEC na awe Mwenyekiti UVCCM. Mbona huyu Mwenyekiti wa sasa nae ni mjumbe wa NEC? Kwa nini kilicho “Good for the goose” kisiwe “Good for the gander?” Au hii ni kwa sababu ya jinsia yake? Kwa Marehemu alijiwekea malengo kuwa “Even the Sky was not the limit” because there is Outer Space after the sky, and may be that is where she wanted to set the limit.

Nathubutu kusema kuwa nilivyomjuwa Marehemu kwa muda mfupi na tukawa karibu sana kiasi cha kuwa wiki haipiti bila kujuliana hali siamini kama alikwenda kwa Shigongo na kukaa kwa saa sita kupindukia usiku wa manane kwa lengo la kutumia ujanajike wake. Maalesh, na iwe kweli kenda kwa lengo hilo, kwani Marehemu Amina atakuwa wa kwanza kujitakisha? Eric Shigongo hajapata kutaka au kutakwa na mwanamke? Anasema alimshikisha Marehemu kitabu kitakatifu ili aape kama aliwahi kutakiwa na Shigongo, na Marehemu akakataa kukishika; jee Shigongo anajuwa sharia za Kiislamu na sababu zinazomfanya mwanamke wa Kiislamu kukataa kushika Mas-hafu kwa sababu na nyakati fulani fulani?

Shigongo ameendelea na makala zake za kashfa juu ya uhusiano wa Marehemu na Mheshimiwa mmoja bungeni, jee tumuite yey ni mtafiti wa habari za ndani za wabunge wote walio bungeni? Ni kweli anajuwa mahusiano binafsi ya baina wabunge wote au alimkandia Marehemu tu? Kama anazijuwa habari zote mbona asiziandike kwa mapana na marefu na akakazania za Marehemu tu? Mbona asitoe habari za kina za huyo mbunge wa kiume na kumuandama Marehemu peke yake? Wangereza wanasema “It takes two to tango and it takes two to quarrel”. Au hii ni ile dhana ya mfumo dume uliotutawala kuwa mwanamke ndie anaefaa kuitwa M……a (siwezi kuliandika hili neno) na mwanamme anafaa uitwa “KIJOGOO”. Kama kazi hii ni ya wawili, vipi iwe sifa kwa mmoja na kashfa kwa mwengine? Shigongo anaogopa mwanmme mwenziwe na akamuonea Marehemu. Au ana ajenda ya siri?

Nimemjuwa Marehemu Amina kwa muda mfupi, na nikajuwa ni mtu mkweli, muaminifu, mwenye ithibati, asiekwenda kinyume na kauli yake. Nasema hivi kwa uthibitisho kamili nilionao binafsi. Miezi michache nyuma alitowa kauli yake kwa mtu mmoja kwamba angempa msaada fulani. Baadhi ya watu hawakupenda Marehemu afanye vile na akawekwa kiti moto na majopo si mawili si matatu, ya watu wazito sana ili aende kinyume na kauli yake ile. Marehemu Amina aliwasikiliza, na baadae akawajibu kuwa hangeweza kwenda kinyume na kauli yake na kwamba kama alivyoahidi, atampa mtu yule msaada wake.

Hapa niliweza kuona tafauti baina ya Marehemu Amina na wanawake na wanaume wengine wengi, wakiwemo vijana kama yeye waliotokea huko Umoja wa vijana CCM, na wanawake na wanaume wakongwe waliokomaa waliotokea katika vilele vikubwa vya Chama. Tafauti ilikuwa wengi wao walitia ulimi puani na kwenda kinyume na walivyotamka, wengine wakawa washiriki wa kumuweka Marehemu kiti moto na kumtishia kuwa wangemfanyia hivi au vile.

Marehemu Alikuwa hamtishi mtu wala hatishiki au kutikisika. Alikuwa ni mtu ambae akishatoa kauli yake, basi hata ashuke malaika gani haibadili abadan. Aliweka msimamo wa kupiga vita madawa ya kulevya kwa nguvu zake zote, jambo ambalo lingemtetemesha mtu mkubwa na mwenye nguvu. Niliwahi kuongea nae na kumwambia “Mwanangu pole pole, wasije wakakudhuru!”. Kauli aliyonijibu ni kuwa amejitolea nafsi yake katika ukweli na haki na chochote kitachomfika ni maktub na hakifutiki. Kweli kilichoandikwa hakifutiki.

Nikiacha hili nitakwenda kwenye utanashati wake ambao ulifika kumponza bungeni kwa kuambiwa na Mheshimiwa Spika atoke nje ya kikao aende akabadili kivazi kwani hakistahili bungeni. Bila kinyongo Marehemu alitoka na tabasamu na akaenda akafanya kama alivyoamriwa. Binafsi wakati huo mimi nilikuwa katika maeneo ya Bunge Dodoma. Kivazi kilichomponza hakikuwa cha uchi au kuvunja heshima, kilikuwa na kidokezo cha kofia ambapo kwa sharia za bungeni tulizorithi kwa wakoloni, kilipaswa kiendane na uvaaji wa gloves na ndipo kiwe kimetimia. Marehemu Amina alitoka nje na akavua kofia ile na kurudi bungeni. Alifika hata kufanyiwa usaili na stesheni moja ya runinga na ilipoletwamada hiyo Marehemu alicheka na kusema kuwa hiyo ilikuwa ni changa-moto ya ukomavu wake na zaidi ya yote ilikuwa ni funzo la kupitia kanuni kabla kutenda jambo.

Wacha niwambie unafiki wa sisi watu. Kwenye runinga nimeona watu wanalia karibu ya kugaragara na kutiririkwa na machozi wakimsifia Marehemu. Jamani wengine katika hao ni wale ambao walichekelea Marehemu alipoamriwa kutoka nje kwa ajili ya kivazi chake, wengi ya hao walidiriki kumbeza na kusema kuwa pale ni pahala pa kazi na si pahala pa fashen na ubishoo. Wengi wetu ambao wakati umeshatupita kushoto na jua limekuchwa tulijisahau kuwa nasi kwa wakati wetu tulipiga vimini na kutesa mjini. Wengi ya wale ambao bado ni vijana walijawa na wivu wa kutomiliki vivazi vya “designer goods” vya Marehemu Amina, au ki maumbile kutopendeza kama yeye. Wivu na choyo vilitutawala na tukasahau kuwa “kila ndege anaruka na ubawa wake na nyota ya mwenzio usiisafiire”.

Kila mtu ana mapungufu yake. Kwa sasa, ilivyo khulka ya binaadamu, utasikia sifa tu atakazo mwagiwa Marehemmu Amina. Kashfa zitatulia kwa wengi wetu kwa ile dhana ya “Never speak evil of the dead”. Bwana Shigongo alisema katika makala yake ya Ijumaa iliopita kuwa anasitisha kuandika mengine kemkem ya Marehemu Amina na kashfa zake kwa vile ni mgonjwa kitandani. Aliahidi kuwa atatuletea uhondo huo baada ya kupona Marehemu Amina. Naomba nimnukuu marehemu bibi yangu ambae alikuwa ndio mentor (muongozi au dira) wangu. Alipokuwa katika “sakarati-l-mauti” nilikuwa namsomea na kumuombea dua huku nikilia na kumwambia “Bibi utapona”. Alinitupia macho akanijibu “Nikipona nimepona, nikifa nimepona”. Nami namuomba bwana Shigongo aliemsakama Marehemu hata wakati alipokuwa mgonjwa mahtuti kitandani, asitunyime conclusion ya uhondo wa hadithi yake tamu maana sasa Mhe. Amina AMEPONA na ni rukhsa kwake kutumalizia makala yake na asituache na shauku na duku duku la kutaka kujuwa kulikoni.

Kwa makala hii namuombea marehemu Amina malazi pema peponi, Mungu amsamehe madhambi yake, ampe kauli thabit, ampe kitaabu chake kwa mkono wa kulia, malaika wema wawe marafiki na wapokezi wake kaburini, apate nuru katika kaburi lake, liwe linatoa harufu ya rehani nasumini na mawaridi, awe mkono wa kulia wa Bwana Mtume siku ya Kiama pamoja na Ma-abrar wema, awape subira wazee wake, mwanawe, marafiki zake na kila aliempenda na aliependwa na Marehemu.

Marehemu Amina namfananisha na Princess Diana wa Uingereza alivyoandamwa na mapaparazi wa ulaya hadi akato(ka)lewa roho yake. Wema, Utanashati,ukarimu, ukweli, huruma, usaidizi na mengi mazuri ya Princess Diana yanafanana na yale ya Mrehemu wetu. Vifo vyao vinatafautiana mazingira lakini vinafanana sababu nazo ni kuandamwa kwa hili na lile. Tarehe pia zinapishana kidogo kama mwezi tu kufikisha miaka kumi kamili.

Diana alikuwa ni Princess wa Uingereza ambae ana andamwa hadi leo miaka 10 baada ya kifo chake. Marehemu Amina ni Princess wetu Tanzania. Natumai Paparazzi wenzangu tutakuwa na hishma za Ki Afrika na utu wa Ki Tanzania na tutamwacha marehemu apumzike kwa amani baada ya kumpa Bwana Shigongo nafasi ya mwisho ya kutueleza yaliyobaki juu ya Marehemu Amina. Baada ya hapo tutamwachia Mungu atamhukumu kwa amali zake nzuri, na zikiwa mbaya atamsamehe.

Naomba kumaliza kwa kunukuu maneno ya Jesus Christ alipowambia Mayahudi walipokuwa wanataka kumpiga mawe Mary Magdalene kwa sabau eti alikuwa mzinzi. Jesus aliwaambi hivi: “Let that among you with no sin cast the first stone”. Yaani naanze kati yenu yule asie na dhambi kutupa jiwe la kwanza. Jee tupo kati yetu tulio malaika bila dhambi? Tukumbuke kuwa mtu akimyooshea mwenziwe kidole kimoja, basi vidole vine vinamgeukia yeye na kumsuta. Upo Bwana Shigongo?

Briani mwanangu Princess Amina. Mungu akulaze pema peponi Amin.

Wakatabahu

Mahfoudha Alley Hamid

E mail: umimah@zanlink.com

21 comments:

  1. kwa kweli dada nimependa sana jinsi ulivyomudu kutumia hiyo kalamu na karatasi i mean kebord yako vyema kufikisha ujumbe huu mzito ni jambo ambalo waandishi wengi tu wa tanzania wanapaswa kuwa wawazi na kuandika positive things pia,hasa hasa haya magazeti yake huyu bwana shigongo huwa hayana kitu encouragement,they always talk vitu ambavyo vinajenga picha mbaya, alafu u can't imagine watu wengi wanaosoma hayo magazeti sijui niseme ni wavivu wa kuchanganua na kufikiria mambo huwa wanaibeba hiyo habari hivyo hivyo na inastik vichwani utadhani ni jambo la maana, kitu kinaweza kikaandikwa front page ukienda kwenye habari yenyewe ni tofauti na alichomaanisha katika front page, hii ni kuonyesha kwamba hawajiamini na kazi wanayoifanya,wangekuwa wanandika heading katika front page inayoendana na habari iliyopo ndani am telling u nobody will buy those things, kwani ni nini walichoandika wale watu wa sanifu ikawafanya wafungiwe,na nini wanandika hawa watu wa shigongo kinachowafanya wasifungiwe. ni haaaaaayo tu.

    ReplyDelete
  2. dada umeandika vizuri sana kuhusu uandishi wa kibababishaji wa tanzania japokuwa uandishi wa udaku (ki-tabloid) siku zote na sehemu nyingi duniani uko biased kweli kweli
    kitu kimoja tu,naomba nisikubaliani na wewe unaposema kifo kinapangwa na mungu .kama ni kweli basi huyo mungu ni ni wa namna ya pekee kwa sababu nafahamu kwamba maisha ya mwandamu yanaletwa na mungu hata kuumbwa tunaumbwa na yeye,kheri,faraja na yoote mazuri tunapata kwa mungu sijawahi kusikia ati mungu anawaua watu mungu gani hyo mwenye kuua watu? anapata faida gani au inamfurahisha nini huyo mungu mu-uaji anyeua hata watotot wachanga ? ili waende huko kwake peponi (kama ni kweli watu wanaenda huko kama si vumbini tulipotoka)
    na labda nikuulize tu swali mtoto mdogo wa anyekufa baada ya kuzaliwa say siku moja au wengine wanakuwa hai kwa masaa kadhaa au wengine hufia tumbaoni je hii ina maanisha mungu alipanga kuwaua kwa staili hiyo ? au labda niulize hivi au mtu anakufa kwa gonjwa la ukimwi na hasa baada ya kuambukizwa na mume wa mtu kisha akafa baada ya kuugua muda mrefu je hapa dada yangu ndio kusema mungu alimpangia huyo kufa namna hiyo ?
    ninavyofahamu mimi japo kidogo tu ni kwamba mungu anatoa maisha kwa mwandamu na shetani ndiye alituleta kifo tunakufa kwa sababu ya shetani mungu ni mzuri sana anatulinda ,anatufariji anatuwezesha katika kila jambo lilojema lakini shetani ndiye mwaribifu wa maisha yetu dada kama nimekosea nirekebishe na unaonekana ni mtu mwenye hekma basi nitashukuru unifahamishe juu ya huyu mungu anyeua watu
    may almight God give us all strength to endure the pains cause by the loss of our sister amina , amin

    ReplyDelete
  3. Kwa muda mrefu sana nimekuwa nikifuatilia maoni mbalimbali yanayotolewa na wachangiaji katika blogu hizi za ndugu zetu. Kila mara nimekwa nikiona watu wanasifiwa, wengine wanakashifiwa na kubezwa kabisa. La Amina lilitawala vyombo mbalimbali vya habari wakati wa uhai wake. Kashfa nyingi na nzito za ajabu zilitawala mtoto wa watu akaandamwa hadi akawa haonekani machoni pa watu kwa kuhofia kila apitapo macho yote yapo kwake, na kwa kuzingatia nafasi aliyokuwa nayo kijamii, vyote hivi vilimchanganya. Wachangiaji mliandika mengi sana kuhusu yaliyomsibu, mkaongezea chumvi na sukari. Sasa hivi naona watu wale wale mnajaribu kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa, kwa kuporomosha sifa kem kem ambazo hapo awali hakuna hata moja iliyotanda. Sasa sijui wasomaji wawachukulieje.

    Kwa upeo wangu mdogo nilionao ni dhahiri kwamba tusikubali ama tukubali ukweli ni kwamba, watoa maoni wote katika blog zetu hizi mmechangia kwa asilimia 99 kumuua dada yetu Amina.

    Hivyo nawapeni changamoto kila mmoja wenu akae chini na atafakari kwa kina ni jinsi gani amechangia kifo cha Amina, jaribu kufanya ile wenzetu wanaita "examination of conscience".

    Na kama mambo yataendelea kama hivi yalivyo, msishangae ndani ya siku hizi chache mkampoteza mtu mwingine. Maana yanayoandikwa na shutuma zinazotolewa ni dhahiri kuna baadhi ya watu kwa namna moja ama nyingine wana "feel guilty".

    Mpakanjia naamini kama ni mtu kama mtu "so to say", atakuwa ni wa kwanza kujutia uamuzi alioutoa na kuufanya.

    Mpakanjia ni mtu ambaye nimemfahamu kwa sura kwa kipindi kirefu lakini sikutarajia mtu kama huyu kukosa busara namna hii. Maana naona kila anapokuwa katika maongezi yake, pumba ndo zinatawala, sasa sijui huyu ni mtu wa namna gani.

    Nimeshangaa sana mtu kama mpakanjia kutangaza upotevu wa simu yake kwenye shughuli nzito kama ile ya kumzika mkewe. Sasa sijui watanzania watamuelewa vipi.

    Hili nawaachia nyĆ­e wanajamii sitaongeza zaidi.

    Nasi ni vyema tukajifunza kutokana na haya yanayotokea kwenye jamii zetu.

    ReplyDelete
  4. Mpakanjia anweza kupata simu nyingine tenz ya bei mbaya zaidi. Ila amina hatarudi.

    ReplyDelete
  5. Tatizo wasomaji wamagazeti ya shigongo niwale ambao upeo wao ni mdogo wakuchanganua mambo,mtu mwenye upeo wake hawezi kupoteza muda kusoma mambo ya kipumbavu yanayoandikwa nashigongo.na katika jamii ya kitanznia majority ni watu wenye upeo mdogo wanaopenda kushabikia mambo ya kipumbavu.ndo maana huyu bwwana shigongo anapata support kubwa yakuandika, anajua atauza angekuwa hana mnunuzi wa upumbavu wake asingeandika na kuandika mambo ya maana.ukichunguza zaidi hao wateja washigongo hawaingii katika blog au midahalo yoyote kuona watu wanavyoendesha debate na kuzichanganua katika mitazamo mbalimbli ya kujenga, kwa hiyo siku zote watendelea kuwa mental signant.

    ReplyDelete
  6. jamani mimi simlaumu saaana shingongo bali sisis wenyewe wasomajai yeye ni mwana udaku waaandishi wa ki-tabloid wapo kila kona ya dunia hii na staili zao za uandishi au habari wanazoziandika always ni za kidizaini fulani yaani zina utata mwingi inapokuja kwenye authenticity japokuwa mafano hapa marekani wanaandika habari na picha sometimes ni kweli japao njia wanzotumia kupata habari hizo si za KIUNGWANA na zingine ni HATARI na sometimes WANALIPA PESA nyingi kwa sources hasa authentic and first hand sources

    nataka kusema hivi ,sisi wenyewe tulaumiwe sio waandishi kwa sababu wanaandika habari za udaku kwa ajili yetu nasi tunazipenda ,zinatufariji .tunaona raha kweli kujua yanayomsibu mtu mashuhuri na ndoa yake yoote hii ni kwa sababu kwa kawaida watu (hasa watu masikini wasio na tumaini lolote ktk maisha hapa Tanzania ) wanakuwa na curiosity kujua kumbe agh! hata marehemu kumbe alikuwa hivi na vile na hivi !
    msishangae hivi sasa hat hao mnaowaona intellects kwa taarifa yako wansoma udaku huko maofisini tena wanpoteza muda kujadili
    lakini yyote tutasema ila lazima sisi wasomaji tubadilike kama mnataka hali halisi ibadilike alimradi kwamba sisi wanunuzi tupo na tunataka habari za ki-tabloid basi shigongoz watatendelea kwa sana na watafanikiwa sana na sito shangaa kama mimi na wewe tutaendelea kufarijika ,kuwa na shauku ya udakuz basi siku moja wadakuz kama hasa shigongo jamii yetu kinyume na wengi wanvyofikiri atakuwa ni institution ktk media ya bongo

    jamani hivi hamfahamu kuwa sasa hivi ni suala la supply and demand kwenye media pia ? hivi sasa hata nchi zilizoendelea wanstruggle ktk kuingiza fedha na suala la ratings linakuwa muhimu kuliko hata maadili ya kiundishi.
    mungu wape faraja ya kweli familia ya marehemu Amina there is no loss like the loss of your loved ones

    ReplyDelete
  7. salam dada ummy.
    nimefarijika sana kwa kusoma hiyo post yako. nimefarijika kwa sababu nilikuwa nikidhani labda mimi ndo nna mapungufu kwa moyo wangu kumshutumu sana shigongo.
    nimekuwa nikimsoma tangu dada Amina alipojaribu kugombea ubunge. shigongo katika magazeti yake alikuwa akimchafua sana kana kwamba yeye shigongo ni mtakatifu mno.
    akimpaka matope sana hata akijaribu kujumlisha mapungufu ya hayati Amina wakati wa uanafunzi wake.mimi siku zote najiuliza, ni nani anayeweza kudiriki kuapa kwamba ana rekodi safi toka utotoni hata sasa utu uzima?
    pengine amekuwa akitumiwa na wabaya wa Amina kisiasa.maana yeye ni mwenyekiti wa kampeni ya ukimwi wa UVCCM.nadiriki kuamini kuwa shigongo na marafiki zake ambao ni top leaders wa uvccm wamekuwa wakiiogopa sana kasi ya Amina.
    badala ya wao kuongeza kasi katika kuwatumikia wananchi ambao ndiyo tumewachagua, wakatumia kalamu zao kumchafua na kumchafua dada wa watu.
    mimi nasema kitu kimoja.
    maandishi ya shigongo yamedhihirisha upungufu mkubwa sana katika uwezo wake wa kufikiria.kama ambavyo amekuwa akitafsiri na kuandika stori ndeeeffu ambazo ukizisoma kwa makini unagundua kuwa hazina logic, basi si ajabu kwake kuitumia kalamu yake kuuandika ujinga kama ule.
    mi nadhani, kwa kuwa ni kweli Amina kama binadamu yeyote awaye yule, anao mapungufu yake, angekuwa na busara sana kumsaidia kuyaondoka.
    pengine sasa tumwite mtakatifu Shigongo wa kwanza. kwa maana anapenda sana kuwanyooshea vidole watu wengine.
    shigongo ni mfano mkubwa wa uandishi mbaya sana katika jamii yenye upendo ya Kitanzania. ni mfano mbaya kwani watu hawana la maana la kujifunza zaidi ya kujua Amina kafanya hivi, Nora kafanya vile, Ray hivi.
    amemtumia sana Amina kuuza magazeti yake.mi namshauri kitu, aendelee kuandika bila kuchoka juu ya Amina, nitapenda pia kuona akiandika hata maisha ya Amina huko aliko maana bwana mkubwa anafahamu sana mambo ya wengine.
    aandike sana kwa sababu wakati wenzake tukijaribu kwa kila hali kujifunza kujenga japo kidogo yeye anatumia pesa yake kuwabomoa watu.
    labda katika kumaliza nimwulize swali.
    bwana mkubwa, baada ya kumsimanga sana Amina na kuchangia kuathirika kwake kisaikolojia na kuchangia kifo chake, nasema hivyo, umepata faida gani?
    kama kuna faida umeipata, hongera sana kwa hilo.
    kazi njema.

    ReplyDelete
  8. Shigongo hana utakatifu wowote,unafiki tu umemtawala.ANAMFUATA FUATA MKE WA MTU AMBAYE ANAFANYA SHIRIKA MOJA LA UMMA AMBALO LINAMILIKI BENKI PIA,ANATAKA WATU NA YEYE WAMUANDIKE ANAYOYAFANYA AU KWA SABABU HATUMILIKI MAGAZETI YA UDAKU?Kama alivyosema mchangiajia mmoja hapo juu aendelee kumuandika Amina hata huko aliko kwa sababu anajua sana mambo yaliyojificha.AMINA ameenda umeepoteza chanzo kizuri kweli cha kuuza magazeti.Ni kitu gani alichokukosea kwa miaka kumi wewe unamuandika yeye tu.Mimi nadhani ni ukosefu wa ubunifu wa kupata habari zengine,kama ndiyo hivyo basi umepoteza chanzo kizuri cha habari nakupa pole sana itabidi ujipange upya kutafuta chanzo kingine cha habari
    Unajua mchawi siyo lazima atumie tunguli ili ajulikane mchawi hata maneno tu ni uchawi KWA BWANA SHIGONGO NI MCHAWI WA AMINA.

    ReplyDelete
  9. Ummie... I salute you!!! You said it all na nikiongeza nitaharibu point zako zenye hisia ya ajabu. I only want to ask Shigongo one question... How do you feel? Shigongo, how do you feel? Sad? Sorry? Pity? Guilty? Just tell us how you feel!!!!

    ReplyDelete
  10. Ummie... I salute you!!! You said it all na nikiongeza nitaharibu point zako zenye hisia ya ajabu. I only want to ask Shigongo one question... How do you feel? Shigongo, how do you feel right now? Sad? Sorry? Pity? Guilty? Just tell us how you feel!!!!

    ReplyDelete
  11. Dada ummie nakubaliana na wewe kwa 100% na wachangiaji wengine walio changia hapa. Kweli pamoja na kwamba uandishi upo kwa ajili ya kuandika mema na mabaya ya watu maarufu na waliobeba dhamana ya wananchi lakini Shigongo umezidi kusakama watoto wa watu ambao wanakimbiza ndoto zao na pale wanapotaka kufanikiwa wewe unawavuta warudi walipotoka, zaidi ya yote umetaka kusababisha kifo cha sinta japo labda ulikua na sababu za msingi lakini ulimwandama mno hata mzazi wake sidhani kama alikua akifurahia, akataka kunywa sumu afe ukaona pia ni kichekesho ukamwandika kwa kebehi hatimaye mtoto wa watu kahama nchi. Ukamgeukia amina bila huruma ambae kwa wakati huo aliwekwa kiporo ukamwandika kila baya ulilofikiria kwamba watu watamwona hafai kuanzia Shule,ndoa yake kuilinganisha na ya Monalisa kinyang'anyiro cha ubunge wakati huo shigongo akimpigia debe vick kamata walietoka mkoa mmoja mpaka lakini lakini Marehemu akafanikiwa na pia baada ya ubunge akaendelea kumwandama kila kukicha thanks God marehemu alikua na mzazi ambae alimpigania na kumpa support ambayo ilimfanya akaweza kumudu kila kitu na kufikia alipofikia manake kwa upande wangu ilifika mahali hata kusoma tu vichwa vya habari vya hayo magazeti vilinichefua manake ni amina amina mpaka basi na hakuna kizuri kuhusu amina. Ni binadamu gani asiye na jema na bado wananchi walimpenda wadogo kwa wakubwa.

    Shigondo anajifanya anakipaji cha uandishi ila ukweli ni kwamba anabahatisha na pia anapenda sifa sana na ni mzinzi kupindukia ila kwa sababu ni yeye tu mwenye ubongo wa samaki wa kupenda kuandika mambo ya wenzie hakuna mwenye muda wa kuyaweka hadharani ya kwake kwani hakuna binadamu aliyemsafi......

    Mbona hajaandika skendo lake na miss mmoja ambae nae alivuma sana ila yeye alikua akiandikwa mema yake tu kisa alimkubali shigongo na watu hawajui upande wa pili wa huyu binti kwa kua alikua mpenzi wake. Wale wote waliomkataa amewaandika vibaya. Mbona skendo lake na mfanyakazi wake anti liz kwenye sherehe ya ofisi yake hajaaandika... Haya ni machache tu akitaka wanablog wote tuandike madhambi yake tutajaza ukurasa mzima.

    Sina nia mbaya na yeye lakini ni kumfahamisha tu kwamba tunajua madhambi yake mengi ila hatukutaka kuongea kwani hata sisi tunayakwetu. Ila hunasababu ya kuvaa kivuli cha ulokole ilhali wewe ni mbwa mwitu ndani ya vazi la kondoo. Ole wao walio wanafiki ufalme wa mbinguni watausoma kwenye vitabu vitakatifu tuuu! Na usihukumu usije ukahukumiwa. Amina ameondoka ukiwa mchangiaji mkubwa wa kifo chake na Mungu atamrehemu popote alipo alale kwa amani. tunakuonya atakuja shujaa mwingine (japo sio kama Amina) ukimfuata fuata kama ulivyofanya kwa Marehemu tutaanzisha chombo cha habari cha kuandika ya kwako tuuu kama utaweza kuhimili, na si unajua MTENDA AKITENDEWA SIKU ZOTE KAONEWA. Shigongo toa boriti kwenye jicho lako uone kibanzi kwenye jicho la wenzako.

    ReplyDelete
  12. AMINA alikua shujaa na nilimpenda huyu binti toka akiwa kwenye kipindi cha lunch time nimekua nikisikiliza vipindi vyake vyote hadi alichohojiwa na jahazi wiki moja kabla ya talaka. Alikua ni binti aliyekua anajua anachokifanya alijitolea kwa nchi yake alikua shujaa aliyeshinda wivu, asiye na maringo zaidi ya yote angekuwa mwanamke ambae Tanzania ingejivunia siku moja, kwani alikua na ndoto kubwa sana na alimaanisha kuzifikia pasipo kipingamizi lakini kama binadamu kuna mambo yalimshinda kuvumilia kimoja wapo ni kuvunjika kwa ndoa yake ambayo aliipigania kufa na kupona sasa baada ya mambo yake kuwekwa hadharani na magazeti ya udaku nadhani hilo lilimshinda.

    Mbona sikuona front page ya magazeti ya udaku kuandika amina alivyojitolea kusomesha watoto yatima kwenye front page, alivyosaidia wazee kigamboni na watoto walio katika mazingira magumu misaada iliyo na idadi aliyokua akiitoa. Zaidi tulisoma kwenye magazeti yenye akili na kwenye luninga tuu! na kama udaku waliandika kwani huwa siyasomi kwa ndani itakua wamesema kwamba anataka umaarufu (sifa) ila ni waheshimiwa wangapi kuacha mengi ambao wanapesa na wanapenda umaarufu ila moyo wa kutoa hawakujaliwa? Matajiri wangapi ambao kama wangejitolea kwa kuwa wanapenda umaaru wakasomesha watoto 20 kama Marehemu tungekuwa tena na shida ya kuwaombea yatima nguo na pesa kutoka kwa wafadhili. Au tuseme pesa yake haikuwa na kazi? Jamani shigongo ni mwandishi ila si ni binadamu wa kawaida kwa nini usijiweke kwenye nafasi ya muhusika ukiwa unahariri ile habari? Kwa ulaya ni sawa watu kuandikwa mnavyoandika lakini sisi ni waafrika tuna asili na utamaduni tofauti tumeumbwa na haya pamoja na huruma bila kusahau upendo wa ajabu. Unawezaje kuandika eti mtu kakutwa uchi (norah) ilhali unaona kabisa picha zimechukuliwa bila ridhaa yake? Umemuuliza umekanusha unaziwekaje gazetini. Jamani tuwe waangalifu mambo mengine hayafumiliki hasa Ulivyokua ukimwandika amina ilhali yupo kitandani ukijua fika ni mgonjwa nilibahatika kusoma kipande cha barua uliyomwandikia marehemu kweli inasikitisha sana ulimchambua ndani na nje bila huruma. Ila ulichokitaka umekipata na malipo ni hapa hapa duniani Mungu halali usingizi.

    NAWASHAURI WANASHINGONGOZ KAMA MLIVYOWAITA ANDIKENI NA MEMA YA WATU MNAOTAKA KUWAANDIKA ILI MSIONEKANE MNAANDIKA MABAYA

    ReplyDelete
  13. nimesoma maoni ya hawa wenzangu ,kwa kweli mnanaisikitisha sina maana kwamaba nawaunga mkono maandishi wa udakuz! NO! ispokuwa maoni yenu yananionyesha kwamba wengi wenu pia niwasomaji wa wa udakuz ni dhahiri kabisa tena udakuz huo wa shigongo.mngekuwa si wasomaji wa hayo madakuz basi nsingejua kama anamwandika marehemu
    narudia tena kumbukeni jamani kwanza
    shigongo anapata nguvu na kichwa kuandika udakuz sababau ninyi wenyewe mnautaka na mpo tayari kununua

    udakuz haujali kama wanaadika jema au baya la mtu na si kama wadakuz hawajui mema ya mtu lah hasha wanafahamu fika.

    asilimia kubwa ya wanunuzi wa udakuz au uchochez kama wengine wanvyoita ni watu wa daraja la chini la maisha na kidogo daraja la kati na wachache ni daraja la kwanza
    walalahoi(daraja la chini)kwa kawaida HAWANA MUDA WA KUCHAMBUA KUTATHMINI NK kiasli wanasikia raha sana kusikia na kusoma juu ya mapungufu ya watu mashuhuri tena hufurahia sana kwao ni raha kujua kwamba hawa mashuhuri wana shida kama wao tuu .

    pia siku hizi trends na tamaduni za kimaadili zinabadilika watu wametoke tu kupenda kujua mapungufu au mabaya ya wengine hasa yale yanayoanikwa hadharani yaani hamana wanchofaidika lakini basi tuu kujua hayao na kuendelea kufuatilia kama vile soap opera ya tv kwao ni raha

    kwa kifupi ni kwamba kwa maoni yangu wengi wenu mliochangia hapao inidhihirishia kwamba ninyi pia mnasoma udakuz wa shigongo
    manjuaje habari za uchochoz zilizomo ndani yake kama hamvutiwi nzao au hata vichwa vya habari?

    jamani acheni kusupport udakuz ,mauzo yakianza kuporomoka basi down the drain udakuz has gotta go!

    ReplyDelete
  14. KUNA NJIA NYINGI ZA KUTAFUTA PESA ILA YA KWAKO(SHIGONGO) SI NZURI.HUO WAKALA ULIOMWANDIKIA AMINA KAMA UNAMJALI SANA UNGEMWAMBIA YEYE PEKE YAKE SIO KWENYE GAZETI .HOW DO U FEEL NOW UNAMUANDANA MTU HADI KAFA!!SASAHIVI UNAWASINGIZIA WA MADAWA YA KULEVYA.NYIE MAGAZETI YENU HAYO YA UMBEYA/UDAKU HAYAANDIKI MEMA HATA SIKU MOJA WHY? ARE U A GOOD BELIAVER? AU UNATUABISHA WAKRISTU WENZIO???????????
    DONT JUDGE OTHER PEOPLE BRO!!!!!!

    ReplyDelete
  15. Ummie, kila nikisoma makala yako nashikwa na hasira sana. Kwa nini Shigongo yuko hivyo??????????? I hate him.... I hate him with all my heart.... How can he be so insensitive? Amina yuko kitandani hoi yeye anaandika makala ya kumsakama???

    ReplyDelete
  16. jamani,
    shigongo shigongo.naomba nimwite mtakatifu shigongo. narudia kumwita hivyo kwa sababu ni bingwa wa kuwanyooshea vidole wenzake.
    mmoja hapo juu amemshauri kuendelea kumwandika Amina juu ya maisha yake huko aliko. nilidhani ni utani vile, la hasha.
    kumbe shigongo anamtumia Amina kuuza magazeti yake.
    ona hadi leo bado Amina anapamba kurasa zake za mbele.
    mara Amina kufufuliwa, soma Risasi ya jumatano wiki hii. kweli huna jipya Shigongo. huna sera. hutufai kanisani wala msikitini. ni mtu wa biasness sana. wasanii walipogoma kushiriki mfalme wa rhymes 2005 walikuwa sawa.kwa sababu ulishaonesha kumpendelea fid q kwa kuwa unatoka naye mwanza. nasema tena, Shigongo huna la kutusaidia watanzania zaidi ya kutuongezea machungu kwa tabia yako.
    Mwenyekiti wa MCT kipindi kile Bw Jenerali Ulimwengu alipoyaandama magazeti ya udaku ulilalamika sana hata ukajitoa kwenye baraza hilo.kumbe uliona kanuni za baraza hazikutendei haki kwani hazina urafiki na upuuzi wa magazeti kama yako.
    sasa nimekufahamu wewe ni mtu wa namna gani.
    labda nami nikuulize swali, umepata faida gani uliposababisha kifo cha Amina?
    asibishe mtu hapa!
    umechangia sana kumewathiri kisaikolojia baada ya kuchangia kuvurugika kwa ndoa yake.
    haya kaka mshindi wewe, umetushinda wa-tz milioni nyingi tulikuwa tunapendezewa na kazi za Amina.
    lakini Tanzania haipo hivyo na hatupendi iwe hivyo asilani.
    labda unaweza uklajirekebisha japo kidogo ijapokuwa kiburi cha pesa ulizozichuma kupitia mambo hayo hayo hakitakupa nafasi wewe kukubali makosa.
    kila la kheri.

    ReplyDelete
  17. dada ummy thanks kwa kupost comments zako huyu shigongo ni shetwani! amekuwa akivunja ndoa za watu kutwa kucha na kusambaratisha familia za watu ni nani zaidi ya agent wa shetani anayeweza kulifanya hilo. yeye shigongo ni mfiraji namba moja tena nina uhakika marehemu amina angemtaka lazima angamkubali kwani kwa uchafu wake hamna anayeweza kumkataa. pia nadhani ni wazi kuwa shigongo na makala yake anayoandikia ni wazi kuwa anafanya kazi za mashetani jamani tuwe very careful na huyu mtu kwani kazi yake ni mopja tu kusambaratisha familia za watu. kunyanyasa wanawake now u have t6o stop it shigongo unachekesha.

    ReplyDelete
  18. Amina its Known....hacheni kusingizia watu watu bure!Kinga za Amina zilikuwa na utata sana(Cd4 bellow 250-WHO stage III) sasa mnataka kujifanya hamjui na kusingizia watu......damn mbona hmtaki kukubali...mnaongeza unyanyapaaji jamani!Accept the scenario watanzania...apo ndo tutatokomeza pandemics!

    ReplyDelete
  19. Sidhani kama wewe ni genuine "Doctor'. Hii revelation ambayo sio ethical practice inajionyesha. Hata hivyo wewe ndio mnyanyapaa wa nguvu. Kwani Mtu kuwa na CD4 <250 ndio anakuwa justified kuandamwa ?.

    ReplyDelete
  20. Wewe comment yako inaonyesha wewe sio Daktari kwa kureveal such a comment which is un-ethical. Hata hivyo kwani mtu akiwa na CD 4 < 250 ndio anapoteza haki zake za msingi za privacy...? Acha unyanyapaa...! Usimtetee Shigongo. Ethics zake za uandishi zinasemaje..?

    ReplyDelete
  21. Nimerudi kuisoma hii tena. Ni miaka 10 na ushei tangu Amina aende. Nasikia sasa kuna mtu analia machozi na chama chake. Basi sawa.

    ReplyDelete