Thursday, November 01, 2007

Wimbi la Ajali za barabarani Tanzania!


Nimetumiwa haya maoni na msomaji Born Again Pagan:

*******************************************************************************
Born Again Pagan said...
Chemi, naomba uruhusu haya yangu kuhusu Ajali Barabarani Nchini:


Hivi karibuni, katika mojawapo ya blogu nyingi mashuhuri za wa-Tanzania, niliahidi kwa kuwaomba wanakijiji kujipa muda wa tutafakuri na kuchangia suala la ajali barabarani na jinsi ambavyo tunaweza kupunguza “balaa” hili ambalo linaendelea kutusibu siku hadi siku, mchana na usiku.

Ingawa ni wanakijiji kama wawili hivi walichangia, sikukata tamaa. Nazidi kuwaombeni tujaze blogu hizi kwa maoni yetu kuhusu maafa ya ajali barabarani. Blogu hizi zinasomwa na wengi, wakiwemo viongozi wa serikali, wabunge wetu, viongozi wa dini na mashirika yasiyo ya serikali.

Napenda kurudia mchango wangu wa awali kuhusu ajali nchini mwetu, ikiwa ni sehemu ya maombolezo ya kutokwa na Naibu Waziri Salome Mbatia. Mhariri wa gazeti maarufu nchini la kila siku aliandika, “…taifa limeghubikwa na majonzi makubwa kufuatia kifo (cha Naibu Waziri Salome Mbatia) kilichotokana na ajali ya gari eneo la Kibena, Njombe mkoani Iringa Alhamisi.”

Lakini yatubidi kuzingatia kwamba si Salome Mbatia peke yake aliyekufa katika ajali hiyo. Dereva wake na utingo wa lori nao walikufa. Na sio ajali hiyo tu iliyotokea siku hiyo na kusababisha mauaji! Karibu watu kama kumi hivi walikufa kwa ajali barabarani siku hiyo! Lakini kifo cha Naibu Waziri Salome Mbatia kimepewa kipaumbele zaidi ya vifo vya wengine. Sababu zinaeleweka; sina haja ya kuzirudia.

Mhariri huyo alitoa tahadhari kali kuitaka “Serikali na vyombo husika na sekta ya usafirishaji” kudhibiti ajali: “[Y]afaa tatizo hili la ajali za barabarani zinazotokana na uzebe na mwendo wa kasi litizamwe tena kwa makini. Bado linapoteza maisha ya watu wengi wasio na hatia wakati zinaweza kuepukwa.

Madereva wengi bado wamekuwa ni vichwa maji katika uendeshaji wao barabarani.”Kauli kama hiyo ya mhariri, sambamba na kauli nyingi za umma zisizotangazwa, inaitaka serikali yetu kamwe isingoje “kifo cha mzaliwa wa kwanza”, kama mtawala Firauni wa Misri, ndipo iamke na kufanya lolote dhidi ya “janga” hili ambalo hudonoa maisha ya wa-Tanzania wetu!

Tumezoea kusema, “Ajali haina kinga!” Lakini ukweli ni kwamba ajali inaweza ikakingika! Wengine husema, “Ngoja ajali ziwamalize kwa kumwonea Kabwe Zubeir Zitto!”

Hili nitalizungumzia kwa kifupi:Katika magazeti na blogu nyingi kumeibuka tabaka la washirikina au niwaite “wanajimu wabaya, watabiri mabaya, wenye ndoto mbaya, wenye maono” wenye kungojea “kiyama” kiikumbe serikali na CCM yake.

Wenzetu wanamwomba m-Bunge wetu “kijana” Zitto Zubeir Kabwe aombe miungu ya huko kwao Kigoma kuweka breki ili isiwamalize wote wale waliomnyoshea kidole - mizimu ya Kigoma inalipa kisasi!

Wanaoanisha msululu wa ajali ambazo zimetokea kwa baadhi ya viongozi wa CCM kufuatia mzozo wa m-Bunge wetu “kijana” Zitto Zubeir Kabwe eti zinatokana na “kumwonea Zitto”!

Natarajia kuchangia hili la mzozo wa Zitto, kulingana na maoni ya wasomi wetu wawili: Prof. Gidion Shoo (Zitto Hakuwatendea Mema Wananchi,” kwa mujibu wa “Kanuni za Bunge”.

Msomi mwingine ni Prof. Shivji (Zitto Kabwe’s Suspension an Episode or an Epitah?) Kero ya Zitto yaonyesha jinsi ambavyo nchi yetu imejigawa. Kuna ukweli kwamba wote hatuimbi, “Tanzania, Tanzania,
nakupenda kwa moyo wote;
nilalapo nakuota,
jina lako ni tamu sana”!

Ni lazima kuna sababu zake, mbali ya vitendo vya rushwa na ufisadi!Kuna baadhi yetu ambao wamegeuka washirikina na kuonyesha hali ya chini kabisa. Hawa wanaomba mabaya zaidi yawapate wana-CCM, kwa jumla, na hasa wale viongozi waliojeruhiwa katika ajali mbali mbali!Sioni kama hili ni ombi la kiungwana!

Ni matakwa ya wendawazimu kwani endapo CCM inafanya mabaya, kuitakia mabaya nako ni vibaya! Makosa mawili hayajengi au hayazai haki!Kumtakia mwenzako kifo ni sawa na kumwua tu. Leo tunatakiana vifo; kesho tutauana kimacho macho!

Kuna wengine wenye kuamini kuwa ajali “Ni mipango ya Mungu - Mungu kapenda; siku yako ya kufa ikifika, imefika!” Hili pia yanataka ufafanuzi: Je, maisha yetu yamewekewa“blinkers” za “determinism”? Je, hakuna lolote tunaloweza kufanya kuepusha hiyo “determinism”? Mbona tunataka kuingilia kati nguvu za asili (nature) kwa kualika nchini “wachawi wa mvua” kutoka Thailand?

Maisha yanajengeka kutokana na kuoana kwa akili zetu na maingilio ya mazingira tuliyomo. Tunaweza kuyabadili kwa kupata elimu tosheleza na hekima ya kuweza kutafukari na kutafuta njia za kusuluhisha au kutanzua tatizo la ajali barabarani. Wengine, hasa wadini walokoke huamini kuwa Mungu huadhibu kwa sababu ya dhambi. Hii sio kwa wa-Tanzania tu bali pia wahubiri wengi walokoke duniani, hususani, Marekani.

Mhubiri mmoja mlokoke wa Amerika aliwahi kutamka kuwa Jimbo la Florida lilipatwa na madhara ya kuwaka moto kutokana na dhambi za kisenge na kishoga. Mlokoke huyo huyo alimshutumu Waziri Mkuu wa Israel kwa kupatwa na mshituko uliomlemaza kuwa ni kwa sababu kagawa nchi ya Palestine - nchi ya Mungu - kwa Wapalestina!

Kisa kingine cha hivi karibuni: Jaji wa “federal” hapa Amerika ameamuru kanisa moja la Ki-Baptist la Westboro - kanisa lenye kuhubiri na kueneza chuki - kulipa faini ya dola millioni 10.9 kwa kushangilia kifo na kukielezea kifo hicho cha askari Lance Cpl Matthew Snyder vitani Iraq Machi 2006 kuwa ni adhabu kutoka kwa Mungu.

Washirika walokoke wengi wa hapa Amerika wanahubiri ‘injili ya chuki” dhidi ya ushoga na kubagua mazishi ya watu waliokufa kwa ukimwi. Walokole wengine wanaamini kuwa Amerika inapata majanga, kama hilo la 911, kwa sababu wameacha kumcha Mungu! Je, Mungu anatuadhibu na hizo ajali zitokeazo barabarani?Pengine hilo la ajali na kudra za Mwenyenzi Mungu nalo linahitaji muda wake maalum wa kutafukari kwa undani, hasa kwa wale wenye kutaka kujua kutoka kwa wanaolielewa vizuri.

Kuna baadhi yetu wenye kuziona na kuzitafukari ajali barabarani na kwinginepo, kama matukio ya kawaida tu. Tusitekwe nyara na fikra za kufungwa macho yetu na akili zetu kuamini kwamba ajali haina kinga; ajali ni adhabu ya Mungu, au ni matakwa mengine ya ushirikina.

Ajali husababishwa na/au mchanganyiko wa haya matatu:dereva, gari na barabara. Kuna Ripoti ya Mwaka 1994 inayoelezea rasmi na kwa undani kuhusu usafiri nchini. Sijui ni wangapi kati ya matrafiki husika, wamiliki wa magari, maderera na abiria wa kawaida wameipitia ripoti hii?

Kuna vitu vitatu muhimu katika njia za usafiri wa nchi kavu kwa kutumia magari barabarani: dereva, gari na barabara. Kila kimoja kina masharti yake sawa na “social environment”: mshiriki (actor/participant), kusudi (purpose), sheria (rules and regulations), mipaka (boundaries), maadili (morality), siasa (what is to be done), na lugha (technical language).

Dereva: Kulingana na Ripoti hiyo, sababu kubwa ya ajali nchini mwetu hutokana na madreva wenyewe. Ajali za namna hii ni kiasi cha asilimia 76. Napenda kuongezea kuwa u-mahiri na u-makini wa kuendesha unatokana na mafunzo tosheleza na utahini usiopendelea; dereva kujiandaa vya kutosha kabla ya safari; asiendeshe huku amelewa au amechoka; afuate sheria za barabarani; na uwezo wa dereva kubaini endapo gari lake lina udhaifu au kasoro.

Ajali nyingi za mabasi, malori yetu na magari madogo yetu kugongana vichwa kwa vichwa, kama ajali hiyo iliyotokea na na kuchukua maisha ya wakina Waziri Mbatia, dereva na utingo wa lori. Hii ina maana kuwa sababu kubwa ni pale dereva wa gari linalofuata kutaka ku-“overtake” lililotangulia karibu na mwisho wa kilima au kwenye kona kali bila kujua kuwa kuna gari lingine linakuja mbele.

Wakati mwingine gari hupata kasoro na dereva kushindwa kuliongoza. Sababu nyingine ni kwa dereva kuchoka na kusinzia sinzia na mwisho kupoteza saiti yake. Madereva wengine huendesha kulingana na wimbo wa mapenzi wa Daudi Kabaka (Kenya), ambapo abiria anamsihi dereva wa basi aongeze spidi ili abiria afike au awahi “date” yake:

Dereva,Choma gari moto;
Nifike upesiNikaone mtoto.
Mtoto ananingojaStendi ya basi;
Fanya haraka!

Kuna pia baadhi ya abiria wenye kutaka kufika mapema kungali na jua kule waendapo. Abiria kama hao huimiza dereva aendeshe kwa kasi. mMadereva wengine nao wanapenda sana kuendesha kwa kasi ili wapate muda wa kupumzika, na kupata angalau “moja baridi” au kuwaona wapenzi wao huko waendapo au mwisho wa safari.

Madereva wengine ni walevi; hupenda kunywa vileo kabla ya safari na wakati mwingine kupumzika safarini kwenye visima vya ulevi. Ukiwa Dar es Salaam, mabasi ya kwenda katika mikoa mingine yanaitwa “mabasi ya kwenda mikoani”, kana kwamba Dar es Salaam si mkoa.

Kuna mabasi mengine, kwa mfano, huondoka Dar kwenda Mwanza kupitia Nairobi (Kenya) huwa yana madereva wawili tu. Kuna pia mabasi yanayoondoka Dar es Salaam kwenda Lubumbashi huko Kongo (Kinshasa) kupitia Kitwe (Zambia). Habari za kuaminika zinaeleza kuwa wakati mwingi madereva huchoka kuendesha na kuanza kusinzia sinzia na huku wakiendesha.

Kuna madereva wengine wenye ka-tabia ka kuendesha magari kana kwamba wana-“enjoy the cruising moment.”Madereva wengine vichwamaji huwazuia wenzao wasipite; ni kama umewatukana. Hivyo huendesha kwa ujeuri kana kwamba kuna ugomvi au vita.

Madereva wengine, hasa kwenye barabara zetu zisizo na lami, wanapenda sana kutangulia kuepuka au kuogopa mavumbi yanayoachwa na gari liliotangulia. Huwa ni mashindano. Kuna wengine, hasa wamiliki, hupenda sana kushindana kuwa wa kwanza kuchukua abiria au shehena kabla ya wenzao. Tabia hii ni ya kawaida kwenye barabara zetu nyingi.

Dereva wa basi ataliendesha basi lake kwa “ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya” ili awahi kuchuma. Na mara nyingine basi linaweza kupata ajali.Barabara nyingi hazina maafisa wa trafiki. Na kama wapo wengi wanahongwa; na wananyamaza, kana kwamba mambo yote ni sawia. Lakini ukificha maradhi, kifo kitakuumbua.

Wamiliki wa magari na madereva wamewaweka wakuu wa trafiki wa wilaya na mikoa mikononi. Hata kama afisa wa trafiki mdogo akimkamata mhalifu, kesi yake itafutwa na “wakubwa”.Barabara: Ripoti hiyo hiyo inaelezea kuwa ajali asili mia 7 husababishwa na matatizo ya barabara. Napenda kuongezea kuwa barabara zetu ndo hivyo tena; zilitengenezwa wakati magari yalikuwa ni ya serikali au machache kwa ajili ya abiria. Ieleweke wazi kuwa hakuna uwiano wa moja kwa moja kati ya barabara nzuri na kupungua kwa ajali.

Huko Ulaya kufika mwaka 1648, barabara zake nyingi zilizokitengenezwa tangu enzi za Warumi zilikarabatiwa kukabili mapinduzi ya viwandani yaliyoleta magari ya kukokotwa na farasi hadi mwingilio wa magari ya sasa.

Huko Ulaya, Ujerumani wakati wa Hitler ikawa ya kwanza kuwa na “autobahns” “highways”) kukidhi mahitaji wa maendeleo ya uchumi wa nchi hiyo na endapo kutatokea vita. Nchi nyingi za Ulaya/Amerika na zingine zilizoendelea zina barabara nzuri na pana.

Nitatoa mfano mdogo wa hapa Amerika:New Jersey Turnpike (Highway) ipitayo karibu na Newark Liberty International Airport ina barabara zenye safu (lanes) sita za kwenda upande mmoja. Kwa hiyo barabara kuu hiyo ni kama ina barabara 12. “Highways” nyingi zina safu 3. Kwa kuwa Amerika inaendeshea mkono wa kushoto, safu ya upande wa kushoto ni kwa wale wenye kutaka kwenda kasi bila ku- “exit”.

Safu ya katikati ni kwa wale wenye kuendesha mwendo wa kawaida. Na safu ya upande wa kulia ni kwa wale wenye kutaka ku-“exit”.Pamoja na “administration and management” ya uedeshaji wa namna hiyo, kuna matrafiki wakali wa mikoa (State Troopers) wanaolinda sheria za barabarani.

Wengine hufanya kazi zao wazi wazi.Endapo msafara wa magari unakwenda kwa kasi, gari la trafiki hao litatangulia mbele na kwenda spidi inayotakiwa. Hakuna dereva atakayethubutu kuli-“overtake”! Kuna wakati madereva iliwabidi kuwasiliana kwa njia ya "Citizen Band - CB" ili kujiepusha na "State Troopers".

Wakati mwingine matrafiki hao hujificha vichakani kando ya marabara na kuwalopoa (kwa njia ya rada) wale wenye ku-“overspeed”, na wakati mwingine kufanya ukaguzi wa ghafula wa gari .Magari ya kubeba shehena (“rigs” au “long distance trucking or haulage”) haya yana sheria zake kali. Kila dereva ni lazima abebe utambulisho wa kile alichobeba, kinatoka na kwenda wapi, ameanza kuendesha saa ngapi, na amepumzika kwa kiasi gani. Gari lake pia ni lazima lionyeshe ukaguzi uliofanyika.

Na katika mabarabara ya mikoa mingi kuna “weighing stations” za kupima magari hayo yamebeba shehena ya uzito gani, pamoja na kuchunguza mambo mengine muhimu ya ki-trafiki. Dereva mwenye hatia, hutozwa faini pamoja na kupoteza pointi fulani kutoka kwa leseni yake, hadi kiasi cha kutoruhusiwa kuendesha Gari. Ripoti hiyo niliyotaja hapo juu inaeleza kwa ajali asili mia 1 husababishwa na gari lenyewe.

Napenda kuongezea kuwa baadhi yetu wanaweza kusema gari haliui; anayeua ni dereva, sawa na kusema kuwa bunduki haiui; anayeua ni mwanadamu. Gari halina budi kuwa katika hali nzuri ya kuendeshwa. Matairi yawe katika hali nzuri na kiasi cha upepo uliojazwa, na viungo vingine muhimu vya gari vichunguzwe mara kwa mara kuona na kuhakikisha kuwa havina kasoro. Gari ni lazima lifanyiwe “servicing”.Kuna ka-tabia ka kupenda kutunza pesa kwa madai kwamba gari bado linakwenda. Wamiliki hawapendelei kukarabati magari yao.Ajali nyingi zinazotokea huwa ni za mabasi mapya. Hii haina maana kuwa basi jipya halipati ajali.

Mengine huanguka kwa sababu ya spidi (ku-“overtake”) na kujaza abiria na shehena (overload). Mara nyingi mabasi ya namna hiyo hushindwa ku-“balance” kutokana na mshituko wa kona au kwa ghafla kujaribu kukwepa wakati wa ku-“overtake”.

Nchini Amerika ni Jimbo la Connecticut peke yake lenye 55 m.k.s. (majimbo mengi yanaendesha 60, 65, 70 na 75 m.k.s.). Lakini takwimu za spidi na ajali hazikubaliani. Hakuna uwiano kati ya spidi kali na kutokea kwa ajali! Pengine hii ni kwa sababu ya huduma za haraka za ambulance na hospitali katika kunusuru waliojeruhiwa. Kukosekana kwa huduma za namna hiyo nchini Tanzania kunawafanya waliojeruhiwa kutokwa damu sana.

Lakini hapa Amerika endapo itatokea ajali, basi magari huwa yanavaana nyuma kwa nyuma. Kumekuwepo na ajali nyingi za mashangigi nchini mwetu. Lakini hatuna utafiti yakini wa kuonyesha au kuelezea ni mashangigi ya aina gani au modeli gani, ua magurudumu ya aina gain hupasuka pasuka na kusababaisha ajali.

Wakati mwingine, gari au matairi yake huwa vina hitilafu ambazo madereva wengi hawazifahamu! Ajali nyingine hapa Amerika zimesababishwa na hililafu, kama nilivyoelezea hapo juu. Ikibainika kuwa aina au modeli fulani ya magari au matairi ndio yenye makosa, basi aina au modeli au matairi hayo yatarejeshwa viwandani.

Je, Tanzania itahakikishaje kuwa hitilafu kama hizo, na makosa mengineyo yanadhibitiwa? Yasemekana Tanzania yetu ni maskini haiwezi kutengeneza barabara kama za Ulaya/Amerika au kuwa na teknolojia ya kisasa ya kudhibiti nidhamu ya uendeshaji na upakizi. Nakubalina na hilo hapo juu.

Lakini kuna mengi ya kufanya kudhibiti ajali barabarani. Mabasi kutoka na kurudi Mwanza/Dar yanayopitia nchi ya jirani ingefaa yawe na madereva wanne. Mmoja kati ya Dar na Arusha (apumzikie Arusha); Arusha na Nairobi (apumzikie Nbi); Nairobi na Tarime (apumzikie Tarime); na Tarime na Mwanza (apumzikie Mwanza). Kila dereva aweze kuendesha kwa muda wa kati ya masaa manane na masaa kumi hivi. Mabasi yanayokwenda Lubumbashi (Kongo-Kinshasa) nayo yadhibitiwe kikamilifu: Dar hadi Iringa; Iringa hadi Tunduma; Tunduma hadi Kitwe. Kitwe hadi Lubumbashi.

Kuhusu madereva, sioni sababu kwa nini kusiwe na matrafiki wa tarafa au wilaya. Hawa matrafiki wetu waheshimike na wapokezane zamu toka tarafa hadi tarafa au toka wilaya hadi wilaya.Na kama madereva watathubutu kuwahonga, watahonga mpaka lini? CID, TAKUKURU. na Usalama wa Taifa viwashughulikie!

Yafaa sana mabasi yawekewe ratiba na yazifuate ili kuzuia hiyo “marathon” ya uchu wa kuchuma pesa. Tuwape madereva mafunzo bora ya usanii elekevu wao kupitia semina, majopo au mikutano sawa na “refresher courses” za kuzidi kunoa umahiri wa kuendesha. Pengine haitawezekana kuwakutanisha maderera wetu huko Ngurdoto Hotel au Bagamoyo!Lakini tunaweza kupitia kwenye restauranti za “Mama Ntilie” ili nao wapate mtaji wa kuendeleza ulishaji mijini kwa walalahoi.

Kwa wale madereva wanaoendesha wakubwa, mara nyingi kumekuwepo na malalmiko ya hao madereva kutopata muda wa kupumzika wawapo safarini. Badala ya kumwambia dereva aende akapumzike na aje amchukue wakati fulani, dereva huyo analazimika kungojea kwenye gari bosi wake amalize shughuli rasmi au za ubinafsi hadi zaidi ya usiku wa manane! Dereva anaambiwa kuanza safari ndefu asubuhi na mapema, tuseme kurudi Dar es Salaam.

Na wakati mwingine madereva hao hata posho hawapati vizuri! Tatizo la kupakia abiria na shehena nyinginezo zaidi ya kilichoruhusiwa, limesababaisha ajali kwa vyombo vetu vya usafiri si barabarani tu bali pia relini, angani na majini.

Gari la moshi lilishindwa kupanda miinuko na ghafla ku-“reverse” na kurudililipotoka. Ndege zetu nyingine zimeshindwa kuruka shauri ya uzito wa shehena (magunia ya vyakula na matunda). Meli, boti, mashua na mitumbwi yetu imezama shauri ya uchu wa pesa kutokana kujaza sana abiria na shehena. Umuhimu wa “servicing” uzingatiwe na kuelezeka kwa msemo wa mambo ya uganga, “Wakia moja ya kinga ni bora kuliko tani ya tiba.”

Tanzania si masikini; ni tajiri. Tunafuja mapesa yetu bure. Fikiria, hao mawaziri karibu sitini ya 60 ni wa nini, kama sio kuzidi kutonesha kidonda cha umasikini wetu? Hawa “mawaziri” na “wizara” zao wanamaliza mapesa kwa mishahara ya wafanyakazi, kuwapamba kwa magari ya fahari na majumba, marupurupu, ubadhirifu, ufisadi, na kurudufisha huduma.

Tulishindana na Benki Kuu ya Dunia, washauri wetu wa uchumi, kututaka tupunguze sekta ya umma (serikali) ambayo ilikuwa imetuna, mithili ya mwenye kitambi. Tukashauriwa kuipeleka “gym” ikafanye mazoezi ya kukonda; ikakonda! Lakini sasa tumerudia yale yale ya kuota kitambi, tena kikubwa zaidi! Ikiwa kitambi kwa binadamu leo hii ni “skandali”, basi hata kitambi cha serikali nacho ni “skandali”!

Najua nchi kongwe (kama Uingereza, Ujerumani, Ufaransa) zilikuwa tayari na dola (the State) kabla vyama vya siasa kuanzishwa. Nchi changa (kama Tanzania) zilikuwa ni lazima ziunde vyama vya siasa ili zijenge (the State) na State ijenga nchi. Kwa kifupi, chama tawala cha siasa ndicho kiliunda State ijenga nchi.

Matokeo ya kuota kitambi kitambi hicho yalikuwa ni mafanikio ya kujenga nchi. Leo hii eti tunaambiwa mambo yamebadilika. Kuna kuoana baina ya sekta ya ummana ya binafsi. Ndoa hiyo ndio kitovu cha maendeleo ya kujenga nchi….bado tunajenga nchi mpaka leo!

Ubinafsi tuliouona kwa darubini ya ujamaa kuwa kama dhambi, leo hii ni nyenzo muhimu ya kuleta eti maendeleo! Tunalipendelea sana Jiji la Dar es Salaam. Wengine kati yetu wanalifananisha na New York au Shanghai kwa madhari yake.

Tuliache Jiji hili lilivyo bila ya kulinyonga.Lakini Jiji la Dar limeshindwa kudhibiti wingi wa magari kwenye barabara zilizotengenezwa wakati wa Gavana akiwa ndiye mwenye gari, na wakati wa kutaka kutoka na gari hilo, barabara zilifungwa.

Mpaka sasa, serikali imekataa kuhamia Dodoma; inazidi kujenga nyumba za mawaziri mjini hapo Dar! Nchi imetumia mapesa mengi kwa ajili ya hayo “makao Makuu ya Dodoma” toka enzi za “Sir” George Clement Kahama! Na “over cost” yake inazidi kila mwaka,licha ya kutojua ni mapesa mangapi Mamlaka ya Mji wa Dodoma ilitumia kuwakopesha wafanyakazi wake kujijengea nyumba zao binafsi! Tuache kuhamia Dodoma! TAKUKURU mnayajua hayo!

Itatubidi tuunde utaratibu wetu wenyewe wa madaraka mikoani ili kuendeleza baadhi ya miji yetu mingine na kupunguza msongamano wa magari jijini Dar,ikiwa ni pamoja na watu kusafiri kwendaDar es Salaam kwa ajili ya kununua vitu na huduma. Niruhusu nifupishe orodha ya wizara zetu ziwe wizara 15 tu.

Orodha iwe fupi kama mini-sketi lakini ndefu kiasi cha kusetri huduma za lazima, kama ifuatavyo:Dar es Salaam: Fedha na Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Mipango (Mipango, Uchumi, Uwezeshaji na Kazi); Habari, Utamaduni na Michezo; Nje (Mambo ya Nje, Mashirika ya Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Mashariki); na Ulinzi na JKT.Dodoma: Uhusiano wa Ndani (Muungano, Siasa na Uhusiano wa Bunge); Elimu (Elimu, Ufundi, Sayansi na Teknolojia; Sheria (Katiba na Utawala Bora); pamoja na kuwa Makao Makuu ya Vyama vya Siasa.Arusha: Maendeleo (Makazi, Jamii, Jinsia na Watoto); Mambo ya Ndani na Usalama wa Raia; ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa Nairobi na Kenya Kusini.Mwanza: Afya na Ustawi wa Jamii, na Mazingira Nishati, Madini na Miundombinu, ikiwa ni pamoja na kuwa jiji la kuhudumia biashara ya Ziwa Victoria, Uganda, na sehemu za Kenya Magharibi.Kigoma: Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Maendeleo ya Vijana, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa biashara ya Ziwa Tanganyika, na DCR Mashariki.Mtwara: Uzalishaji (Viwanda, Biashara na Masoko).

Mtwara hauna budi kupewa hadhi mpya kama mji wa huduma za mpango wa “Mtwara Corridor” (Tanzania, Malawi na Zambia na sehemu za Msumbiji Kasikazini). “Daraja la Umoja” kwenye Mto Ruvuma ili kuunganisha Tanzania na Msumbiji sasa linajengwa baada ya kulisubiri kwa miaka mingi tangu Awamu ya Kwanza – wakati Msumbiji inapata uhuru wake!

Mbeya: Ardhi, Maji, Mifugo, Kilimo, Chakula na Ushirika; ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa nchi za Malawi na Zambia. Ni kitu cha kutia shime kuona kuwa uwamja wa ndege wa kimataifa unaendelea kujengwa mjini Mbeya.

Uwanja huu utasaidia pia kuinua maendeleo kwa mikoa ya kusini. Tuwe na Mawaziri Wadogo 15 tu wakisaidiwa na nyongeza ya Makatibu Wakuu, endapo italazimika. Wizara hizi zitagawanya katika mafungu matano.Kila fungu litasimamiwa na afisa mwenye sifa za nidhamu na uchapaji kazi ili kuweza kufuatililia maazimio na miradi mbali mbali ya serikali kulingana na”manifesto” ya “chama tawala” (na kudhibitiwa na “chama tawala kivuli” kikisaidiana na vyama vingine vya siasa. Afisa huyo asaidiane na tawala za mikoa.

Wakuu wa mikoa na maafisa wao wasaidizi (hadi wilayani) wafanye kazi karibu zaidi ili kufanikisha wajibu wao kwa wananchi. Naona kumekuwepo na kuteuliwa kwa maafisa wapya wa kumsaidia Waziri Mkuu katika kusimamia mipango ya sera za serikali.Hii itasaidia sana kuangalia ni vipi tunavyotekelza yale ya Hotuba Rais aliyotoa alipokifungua Bunge la Awamu ya Nne. Na itawasaidia sana Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kuweza kufuatilia, kukagua na kudhibiti miradi na maazimio yaliyowekwa.Sambamba na kupunguza wingi wa wizara, juhudi ifanywe pia kupunguza idadi ya wa-Bunge wetu!

Wa-Bunge wengine “hulala sana”! Sioni sababu kwa nini kila wilaya isiwe na na m-Bunge mmoja tu wa kuiwakilisha katika Bunge la Taifa, Dodoma! Shughuli za “wa-Bunge” wa Seriali za Mitaa wapewe hadhi na majukumu makubwa ya kusimamia maendeleo katika sehemu zao za majimbo ya uchaguzi, kulingana ana usemi wa serikali za mitaa wa nchi moja iliyoendelea: “Using local people, with local knowledge to serve the local area”.

Huku tukitilia mkazo wa sera ya “madaraka mikoani” (kama kweli bado inatekelezwa), mikoa yetu haina budi kushiriki zaidi katika kupanga na kutekeleza hayo ya “maisha bora kwa kila m-Tanzania”, ikiwa ni pamoja na kudhibiti athari za ajali barabarani. Naamini Tanzania si masikini; ni tajiri! Fikiria leo hii tunajivuna kuwa tu nchi ya tatu katika Bara la Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu!Michanga ya dhahabu inachimbwa na kusafirishwa nchi za nje.

Makapuni ya kigeni kwa muda wa miaka mitatu ya kuvuna dhahabu yetu bila kulipa kodi. Yanaweza kuichimba usiku na mchana kabla ya miaka hiyo mitatu kuisha. Miaka mitatu iishapo, ili yaanze kulipa kodi, aidha yanaweza kulalamika kuwa yatafunga migodi kutokana na uhaba au ugumu wa kuchimba dhahabu yenyewe.Au wakati mwingine makampuni hao yanatishiwa na wakubwa wenye kutaka kuila Tanzania kwa kuyalazimisha kuwahonga ili waidhinishe mikataba hiyo na kuanza kulipa kodi. Hii inayafanya makampuni hayo kuuza “business” kwa wamiliki wengine wa kigeni au kuunda kampuni mpya yenye jina tofauti!Tatizo hili lipo pia katika mikataba ya gesi yetu.

Utajiri wa madini na gesi yetu umeingiliwa na unyarubanja unaotekelezwa na wawekezaji wa kigeni Makampuni hayo yamepewa dhahabu ya bure. Mikataba tunatiliana na hao wawekezaji wageni ikiwa na kipengere cha “production sharing agreement”, psa (kugawana uzalishaji).

Lakini inaonekana kuwa wanaonufaika na kipengere hiki ni wawekezaji, ambao kila mra huongeza vikampuni vingine vya kigeni vidogo vidogo na kunufaika. Je, huo si “unyarubanja”? Hakuna hata kikampuni cha wazawa kinachonufaika na kipengere hicho, kama ilivyo katika mikataba ya madini na gesi yetu.

Labda, Tanzania iko pembeni mwa kipengere hicho! Tangu mkataba wa kwanza kusainiwa (na pengine mpaka sasa hivi) kuna kutafuta “production sharing agreement”, psa (kugawana uzalishaji). Si ajabu mzozo wa Buzwangi umetokana na “production sharing agreement”, kama ilivyo mikataba mingi ya madini na gesi yetu!

Ukifungua http://www.globeinvestor.com/servlet/story/RTGAM.20071030.wbarrick1030/GIStory/ utapata ripoti ya mgomo unaoendelea huko kwenye Mgodi wa Barrick. Mwisho wa stori hii kuna para moja juu ya vile walivyovuna mwaka uliopita: “The mine, which Barrick acquired in 1999, produced 330,000 ounces of gold last year at a total cash cost of $339 (U.S.) an ounce. It had proven and probable reserves of 11.2 million ounces as of the end of last year.” Sijui kama wameanza kulipa kodi au kutupatia 3% (royalities) zetu? Hata kama wakitupa kiasi hicho, Tanzania itapata dola ngapi? Fanya hesabu! Mwisho, naipongeza serikali kwa juhudi zake za kuwapa msasa kidogo madereva. Lakini hii haitoshi kabisa. Naomba juhudi hii isiwe ndani ya majengo tu bali huko nje barabarani ambako ajali hutokea.

Matrafiki wafanye hiyo kwa maadili ya hali ya juu (mithili ya madaktari na wahubiri dini) ili kuokoa maisha na mali ya wa-Tanzania.Hivi karibuni tulizawadishwa na serikali ya Amerika (kupitia mfuko wa Rais wa Millennium Challenge Corporation - MCC) ya zawadi (“grant”) ya dola 698 milioni kuboresha mabarabara nishati na maji nchini kwa kipindi cha miaka mitano.

Pili, kulikuwa na habari kutoka Makao Makuu ya African Development Bank mjini Tunis kuwa Benki hiyo imetoa kiasi cha dola za ki-Marekani million 92 (72%) (serikali ya Tanzania itagharimia 28%) kwa ajili ya kutengeneza mabarabara ya mikoa ya Dodoma na Singida ili kuuunganisha mikoa na mikoa ya kasikazini hadi Kenya.

Je, ki-mapatano, mapesa hayo yatatumikaje katika kudhibiti baadhi ya mienendo mibaya yetu inayosababisha ajali barabarani?

8 comments:

  1. Born Again, Nashukuru kwa maelezo mazuri na ya kujenga taifa letu. Kuna mambo nimejifunza kutokana na maelezo yako. Ningeshauri ungetoa kwa awamu mawazo yako. Mawazo ni mazuri lakini ni marefu sana.

    Kungekuwa na awamu tatu na ukaipa kila awamu siku tatu baada ya nyingine ili wanakijiji waweze kutoa maoni yao. Nionavyo mimi, napenda kuwakilisha

    Kishimba255

    ReplyDelete
  2. Asante Born Again Pagan. Umetuelimisha. Next time jaribu kupunguza maana article ni ndefu mno. Na kwa nini usianzishe blogu yako mwenyewe?

    ReplyDelete
  3. Born again, huwa una point nzuri, ila wengi wetu hatuna muda wa kusoma article ndefu namna hiyo-wakati mwingine fupisha bwana.

    hilo swala la ajali mie nimeshatoa mawazo yangu huko nyuma-narudia tena. inabidi tuangalie pande zote iwezekanavyo:
    -madereva
    -barabara
    -sheria
    -elimu ya usalama mashuleni; n.k.

    hili swala la kulaumu madereva tu halitoshi!!

    na pia Viongozi wa siasa inabidi waache kutoa kauli za kuwa "ajali ni mpango a mungu"-
    hapo ndio tunaweza kusonga mbele na kutatua hili tatizo.

    ReplyDelete
  4. Asante kwa mawaidha yenu. Nitayazingatia moyoni!

    ReplyDelete
  5. BAP

    kaka maelezo mazuri, ila si unajua kuwa wabongo hawana hoby ya kusoma sasa hapo watasona nusu, nusu wanaacha, huku wakisema aaaaaaaaaagh makala ndefu.

    ReplyDelete
  6. Dada Chemi aliandika jina la dereva wa Mama Mbatia. Ni Anaclet Mongella. Majina ya dereva wa lori na utingo wake ndo hatukuzisikia kabisa.

    ReplyDelete
  7. ukiona ndefu acha kusoma. sidhani kama kuna mtu analazimishwa kusoma. na ukiona inakuhusu au unajifundisha kitu fulani basi utafuatilia tu. wala isiwe tabu.

    kuendesha gari ni jukumu. lakini wengi wanafanya holela holela.

    ReplyDelete
  8. Greetings! Very usseful adice in this particular article!
    It is the little changes which will make the largest changes.
    Thanks for sharing!

    Also visit my blog ... Regal trial kit

    ReplyDelete