Friday, December 07, 2007

Vigogo wakatiwa maji

Kama umekaa Dar lazima umekumbwa na tatizo la kukosa maji. Unaweza kusikia eneo fulani umekosa maji kwa karibu wiki! Siku hizi biashara ya kuuza maji, na matenki ya maji umekuwa kubwa kweli kweli. Hiyo ni kwa vile maji ya bomba hayamiki usafi wake, na pia hakuna uhakika kuwa kutakuwa na maji kwenye mabomba.

Sijui wanaweza kufanya nini mjini Dar kupata suluhisho ya kudumu ya tatizo la maji. Ujenzi holela una maana mabomba ya maji yameunganishwa ovyo. Kama mtu una bahasha ya kutosha utapata maji. Wengine wanaofuata sheria za kupata huduma ya maji hawapatiwi. Na wengine hawapati bili kabisa wengine wanapata bili kubwa aajabu.

Jana, DAWASCO, ilikata huduma ya maji kwenye nyumba za baadhi ya mawaziri na manaibu wao kwa vile walikuwa na bili za muda mrefu ambazo hazijalipwa. Nawapongeza kwa hatua hiyo. Natumaini hizo bili zitalipwa sasa. Serikali watunge sheria kuwachukulia hatua kali watu wanaozuia wasoma mita kufanya kazi yao. Kama hutaki mtu asome mita basi usiwe na huduma ya maji!

Tatizo siyo hao vigogo tu, kuna tatizo kubwa zaidi. Maji mengi yanapotea kutoka 'source' (chanzo) mpaka yanafika kwa mteja. Watu wametoboa mabomba makusudi kuiba maji. Mabomba mengine yanavuja. Je, DAWASCO inajua kila sehemu mambomba yametobolewa?Hakuna usimamizi mzuri wa kukagua watu wanaojenga juu ya mabomba makubwa. Mtu anachimba choo na kinatoboa bomba la maji, hajali, uko uchafu unaingia kwenye 'maji safi'!

Lazima serikali iingilie swala ya maji. Swala huu inazidi kuwa sugu miaka inavyozidi kwenda.

Enzi za Ujamaa, Mwalimu aliahidi kila mTanzania atakuwa na maji safi karibu. Bado kabisa!

************************************************************************

Mawaziri wakatiwa maji
2007-12-07

Shirika la Maji safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASCO), jana lilifanya kweli kwa kuwakatia maji baadhi ya Mawaziri na Naibu wao kadhaa wanaoishi maeneo ya Masaki na Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam kutokana na malimbikizo makubwa ya bili zao. hatua hiyo ilikuja baada ya mwanzoni mwa wiki, DAWASCO kueleza bayana azma yake ya kuwakatia maji vigogo hao kwa maelezo kuwa madeni yao ni ya muda mrefu.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa, hadi kufikia jana, Mawaziri na Naibu wao kadhaa, tayari walikuwa wamekatiwa huduma hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea vituo mbalimbali vya DAWASCO jijini jana, Meneja Uhusiano wa mamlaka hiyo, Bi. Badra Masoud, alisema huduma ya maji ilikatwa eneo la Masaki asubuhi na zoezi la kukata maji eneo la Mbezi Beach, lilikuwa likielekea kukamilika.

Alisema zoezi hilo pia litaendelea katika maeneo ya Msasani, Mikocheni, Ada Estate, Mikocheni na Mwenge. Alisema baada ya ziara hiyo, amegundua kwamba wananchi wengi wamejitokeza kulipia ankara zao, ili kuepuka usumbufu na adha ya kukatiwa maji. Hata hivyo, Bi. Badra alisema bado kiwango cha ukusanyaji wa madeni hakiridhishi, hivyo hawatasitisha zoezi hilo. Alisema wamebaini kwamba watu ambao hawalipi bili ya maji wengi wao ni wale wenye uwezo na vipato vikubwa, na hatua yao ya kutolipa inatokana na kupuuza wajibu wao.
Bi.
Badra alisema visingizio vya kusema mimi sijapata ankara ya mwezi huu au ule, havitasikilizwa na wala havisaidii. Alisema imekuwa tabia ya wateja wakishakatiwa huduma hiyo, hutoa visingizio kama “Unajua mimi ni mtu wa kusafirisafiri sana au silipi kwa vile sijapatiwa ankra” Bi. Badra alisema suala la kusafiri na kukosa nafasi ya kulipa bili haliingii akilini kwa vile DAWASCO inaendelea kuwapatia huduma. Pia alisema si kweli kwamba kuna mteja ambaye hapelekewi ankara.

Katika kituo cha Kawe, ambacho kinawahudumia watu wa maeneo ya Mbezi, wafanyakazi walimlalamikia Bi. Badra kwamba wanapata adha kubwa, za kutukanwa, kukimbizwa na Mbwa na kutishiwa maisha, wanapokwenda kusoma mita.
Mmoja wa wafanyakazi hao, alimweleza Meneja huyo kwamba kuna siku aliwekwa `rumande` ndani ya chumba cha mkaa cha kigogo mmoja huko Mbezi beach, baada ya kuonekana akisoma mita ya maji.

Mfanyakazi mwingine alisema Sisi wafanyakazi wa Dawasco wanatuona nuksi kiasi cha kufukuzwa na walinzi tunapofika kusoma mita, yote hayo yanatokana na ukweli kwamba watu hawataki kulipa bili. Akihitimisha ziara hiyo katika Kituo cha kinondoni, Bi. Badra aliwataka wateja wa DAWASCO, waelewe kwamba mamlaka hiyo inatumia gharama kubwa kuwapatia huduma ya maji hivyo wajenge moyo wa kulipa, ili kurahizisha kazi ya kuwapatia watu wengi zaidi huduma hiyo muhimu.

No comments:

Post a Comment