Wednesday, May 07, 2008

Tanzania Breweries yapongezwa - Tuzo za Vinara

PRESS RELEASE kutoka ONE GAME:

TBL yapongezwa kudhamini tuzo za Vinara!

Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya bia Tanzania (TBL) hivi karibuni ilimwagiwa sifa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kutokana na kutoa kipaumbele katika kusaidia sekta ya sanaa nchini ikiwa ni pamoja na kudhamini tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania (Vinara Film Award).

Pongezi hizo kwa kampuni hiyo zilitolewa na mmoja wa maofisa wa Baraza hilo Omari Mayanga katika hoteli ya Regency jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa semina ya siku moja ya majaji wa tuzo hizo iliyofanyika hotelini hapo Jumamosi iliyopita.

Ofisa huyo alisema kuwa, kwa kipindi kirefu kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kufadhili na kudhamini shughuli za sanaa nchini jambo alilosema kuwa limekuwa likichangia sana kujinua sekta ya sanaa nchini ambayo kwa sasa imekuwa ni sehemu ya ajira kwa sehemu kubwa ya vijana.

"Kwa niaba ya Basata, nawapongeza sana hawa TBL kwa kuwa siku zote wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika shughuli za sanaa... Kama hivyo wamedhamini tuzo za muziki na sasa wamedhamini tena tuzo za filamu, siyo kung'ang'ania mpira tu kama makampuni mengine," akasema.

Aidha, ofisa huyo alizitaka kampuni nyingine kuiga mfano wa TBL kujitokeza katika kufadhili au kudhamini shughuli za sanaa nchini hasa kutokana na kuwa sehemu ya ajira kwa kundi kubwa la vijana kwa sasa.

Kampuni hiyo ya bia imejitokeza kudhamini tuzo hizo kupitia bia yake ya Ndovu Special Malt ikishirikiana na kampuni za Global Publishers na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Kwa mujibu wa mratibu wa tuzo hizo zinazotolewa na One Game Promotions, Khadija Khalili, baada ya semina hiyo majaji hao walianza kazi ya kuzipitia filamu zilizoingizwa kuwania tuzo hizo, kazi watakayoifanya kwa kipindi cha wiki mbili kabla ya kuibuka na majina ya waliofanikiwa kuingia katika hatua ya mwisho.

"Kazi imeanza kwa kasi na kwa uhakika, muda si mrefu nimetoka kuongea na mwenyekiti wa jopo la majaji ameniambia kuwa kazi inaendelea vizuri, hivyo wana imani kubwa ya kuimaliza kazi hiyo kwa wakati muafaka," akasema.

Siku chache zilizopita, Khalili alisema kuwa, zaidi ya filamu sabini zimeingizwa na watengenezaji wa filamu nchini kuwania tuzo hizo.

No comments:

Post a Comment