Monday, June 16, 2008

WaBunge Waogopa Kukalia Viti Vyao! Vina uchawi!


Ilibidi nicheke baada ya kusoma hii habari hasa nikifikiria wabunge kwenye ukumbi wa bunge wakichunguza viti vyao. Hivi kweli unaweza kufuta uchawi/juju hivi hivi?

*******************************************************************

Ndumba Bungeni: Wabunge wahofia viti vyao
2008-06-16
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Ikiwa leo ni siku ya kwanza kwa wabunge kuingia tena ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya kuwapo kwa uvumi wa kunyunyizwa vitu vinavyodhaniwa kuwa ni vya kichawi kwenye viti vyao, baadhi ya wabunge wameonekana leo asubuhi wakiwa bado wanahofia siti zao na hivyo kulazimika kuangalia na wengine kuvipangusa na leso zaidi ya mara moja kabla ya kuketi.
Tukio hilo la wabunge kudaiwa kuwekewa vitu vya kichawi kwenye siti zao, limedaiwa kutokea katikati ya wiki iliyopita na kuzua hofu kubwa, hivyo kuilazimu ofisi ya Bunge, kupitia kwa Kaimu Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilillah kutoa taarifa kuwa ukumbi uko shwari na hakuna tishio lolote la usalama kwa waheshimiwa wabunge.
Hata hivyo, licha ya kuhakikishiwa kuwa hakuna hofu yoyote bungeni humo, bado baadhi ya wabunge walionekana wakiwa na hofu na kuchunguza sana viti vyao kabla ya kukaa.
Hata hivyo, hofu ya wabunge hao waliokuwa bado wamejawa na hisia kuwa pengine wamefanyiwa kitu mbaya kwa kuwekewa vitu vya kudhuru, iliondolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Samwel Sitta, ambaye alitoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na sakata lenyewe kabla ya kuwataka wasiwe na hofu na badala yake waendelee na majukumu yao bungeni humo kama kawaida kwani ukumbi ni salama.
Akizungumza wakati wa kikao cha asubuhi ya leo, Spika Sitta amesema vyombo vya usalama, ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa, vimefanya uchunguzi ukumbini humo na kumhakikishia kuwa hauna hatari yoyote.
Akizungumzia sakata lenyewe, Spika Sitta akasema lilianza kwa kuonekana watu wawili wakitangatanga bungeni humo siku ya Jumanne iliyopita, mishale ya saa 2:00 usiku. Akasema taarifa za kuwapo kwa tukio hilo, alizipata siku ya Alhamisi baada ya kuambiwa na Katibu wa Bunge kuwa kamera za usalama ndani ya ukumbi wa Bunge, zimenasa watu wawili wakitangatanga Bungeni.
Akasema picha hizo zikamuonyesha mtu mmoja kati yao akiwa na vitu mkononi ambavyo alikuwa akivinyunyiza sehemu mbalimbali.
Spika Sitta akasema siku hiyo baada ya kupewa taarifa wakati kikao cha Bunge kikiendelea, akatumiwa kimemo na Mbunge Victor Mwambalaswa, akimjulisha kuwa Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe alikuwa ameugua ghafla ndani ya ukumbi huo.
Akasema alipohusianisha matukio hayo, alihisi huwenda vitu vilivyoonekaka vikirushwa na mtu aliyenaswa na kamera za usalama ilikuwa ni sumu ya kisasa. Akasema hapo ndipo akachukua hatua ya kulikabidhi suala hilo kwa Polisi na Usalama wa Taifa ili kulifanyia uchunguzi wa kina.
Akasema Jumamosi ya juzi, Polisi na maofisa wa Usalama wa Taifa walimpatia ripoti ya uchunguzi, wakimhakikishia kuwa ukumbi huo ni salama. Akasema hata hivyo, suala la kuwabaini watu walionaswa na kamera wakitangatanga ndani ya ukumbi wa bunge, bado linaendelea kuchunguzwa na kuwa litachukua muda mrefu kidogo.
Akasema kuwa suala hilo linahitaji muda kwa vile uchunguzi wake unahitaji kurejea kwenye matukio ya nyuma kwa zaidi ya saa 72 ili kujua kilichotokea siku hiyo. Baada ya ufafanuzi huo, Bunge liliendelea na kikao chake kama kawaida, ambapo mjadala kuhusu bajeti ulianza na hadi tukienda mitamboni, wabunge 56 walishajiorodhesha kwa ajili ya kuchangia mjadala huo.

3 comments:

  1. Mganga Simbanyoka kawatengenezea dawa kali kusudi wasahau mambo ya ufisadi.

    ReplyDelete
  2. pumbafu sana hao. Hii ndo nchi yenye sheria ya ajabu ya kukataza watu kuvaa kandambili (ingawa wazungu wanaruhusiwa),
    Na eti ili ugombee "ulahisi" basi lazima uwe na angalau digrii moja. Wabunge wanaogopa visivyoonekana.

    ReplyDelete
  3. kama unamwamini Mungu wala uchawi haukupati maana nguvu za Mungu si mchezo.
    Ms Bennett

    ReplyDelete