Wednesday, July 30, 2008

Spika wa Bunge amlilia Wangwe!

Kutoka ippmedia.com

Spika amlilia Wangwe

2008-07-30

Na Waandishi Wetu Dar es Salaam , Dodoma

Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, jana aliangua kilio kwa sauti ya juu wakati akitangaza kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime kupitia CHADEMA, Bw. Chacha Wangwe.

Kilio cha Spika, kilisababisha baadhi ya Mawaziri na Wabunge kuangua vilio huku nyuso za wengine zikiwa zimejaa huzuni. Spika Sitta alilia baada ya kumalizia kutoa matangazo kuhusu kifo hicho. Alisema ajali iliyomuua Mbunge huyo ilitokea juzi saa 2:55 usiku wakati akiendesha gari lake aina ya Toyota Corolla akitokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam.

Alisema Bw. Wangwe, alikuwa ameongozana na rafiki yake, Bw. Deus Mallya, ambaye alinusurika na sasa amelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu. Kwa mujibu wa Spika, ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Pandambili, kilomita 100 kutoka mjini Dodoma.

Alisema gari hilo liliacha njia na kugonga miti kadhaa iliyopo pembeni mwa barabara kabla halijabingirika na kuanguka. Kufuatia kifo hicho, Spika Sitta aliahirisha Bunge jana saa 3:10 asubuhi hadi saa 6:00 mchana ili Kamati ya Uongozi wa Bunge na Tume ya Maadili iweze kuwasiliana na familia na kuweka mipango ya mazishi. Saa 6:00 mchana, Spika alitoa matangazo ya ratiba ya kuaga mwili wa marehemu na mazishi yatakayofanyika kesho huko Tarime mkoani Mara.

Spika aliahirisha Bunge kwa siku nzima ya jana kwa kutumia kanuni ya 149 inayosema kama Mbunge akifariki, Bunge linatakiwa kuahirishwa kwa siku nzima. Rais Jakaya Kikwete alifika mjini Dodoma jana na kuongoza Mawaziri na Wabunge kuaga mwili wa marehemu Wangwe Bungeni kuanzia saa 10:15 jana jioni. Leo asubuhi mwili wa marehemu utasafirishwa kwa ndege maalum kuelekea Tarime ukiwa na familia yake na Wabunge wawili.

Spika Sitta alisema kesho asubuhi (Alhamisi) Wabunge 20 wanaowakilisha Bunge kwenye mazishi hayo wataondoka Dodoma asubuhi kuelekea Tarime kwa ndege maalum ili kuhudhuria mazishi na watarejea Dodoma jioni. Kabla ya kifo hicho, Bw. Wangwe alikuwa awasilishe Bungeni hoja binafsi kuhusu mapigano ya kikabila na wizi wa mifugo lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana ratiba kutoruhusu kufanya hivyo.

Nipashe ilipotembelea nyumbani kwa marehemu eneo la Kisasa nje kidogo ya mji wa Dodoma saa 4:00 asubuhi ilikuta Mawaziri, Wabunge na majirani wakiwa wanaomboleza.

Mmoja wa watoto wa marehemu, Zakayo Chacha (18), alisema tangu juzi baba yake alikuwa akisumbuliwa na malaria. Alisema baba yake alilazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam ili kuhudhuria mazishi ya mwanasiasa wa zamani, marehemu Bhoke Mnanka aliyefariki dunia mwishoni wa wiki iliyopita.

``Ingawa alisafiri, lakini alikwenda hospitali kupima na kukutwa na malaria, siku moja kabla ya safari hiyo, alimeza dawa mseto za malaria hali iliyosababisha aamke kwa taabu na uchovu kabla ya safari hiyo,`` alisema.

Alisema awali walipoanza safari, gari hilo liliharibika nje kidogo ya mji wa Dodoma na kulazimika kurudi mjini kwa matengenezo. Alisema hali hiyo ilisababisha wachelewe kuanza safari na ilipofika saa 3:00 juzi usiku, ndipo wakapokea taarifa za kifo hicho.

Kwa mujibu wa Bw. Zakayo, marehemu ameacha wake wawili na watoto 10. Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete, jana aliwaoongoza Mawaziri, Wabunge na viongozi mbalimbali wa serikali kuuaga mwili wa marehemu Chacha Wangwe.

Mwili huo uliwasili katika eneo la Bunge saa 11.00 jioni na kupokewa na Wabunge huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Bw. Zitto Kabwe akiwa amebeba msalaba. Akitoa salamu za marehemu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Bw. Hamad Rashid Mohamed alisema tukio hilo ni pigo kubwa mno.

Alisema kambi ya upinzani ina wabunge 45 ambapo wawili kati yao, wamewatoka akiwemo aliyetolewa na Mahakama na mwingine ni marehemu Wangwe. Aliongeza kuwa, enzi za uhai wake wakati akianza Bungeni, Wangwe alikuwa Waziri Kivuli wa Maji na kwamba hadi mwisho wa uhai wake, alikuwa Waziri Kivuli wa Mazingira.

Bw. Hamad alimsifia marehemu kuwa mtetezi mkubwa wa masuala ya wananchi na wapiga kura wake wa Tarime. Hata hivyo, alisema hoja ya Wangwe itashughulikiwa na kambi ya upinzani. Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda , akiwasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali alisema hadi sasa Bunge limepoteza wabunge watano tangu kuanza kwa awamu ya nne na kwamba ni dhahiri si jambo ambalo wanalichukulia kwa wepesi.

Alitoa pole kwa ndugu zake akiwemo kaka yake Profesa Samwel Wangwe, familia, Spika na Kamati ya Uongozi ya Bunge . Spika wa Bunge Bw. Samuel Sitta, akiwasilisha salamu za Bunge alimsifu marehemu Wangwe kuwa alikuwa jasiri, aliyetetea hoja zake kwa nguvu kwa kila alichokiamini bila kujali.

Alisema alijiamini na alikuwa hodari wa kusema kwa ujasiri mkubwa kila alichokiamini bila kujali kuwa lile analosema lingeweza kumfanya atofautiane na wenzake. Alisema Bunge limepoteza mtu ambaye anahitajika sana bungeni, jimboni na serikalini na taifa zima.

Kaka yake marehemu, Profesa Samuel Wangwe alitoa salamu za shukurani kwa niaba ya familia na kulishukuru Bunge kwa kugharamia msiba wa ndugu yao. Naye Bw. Deus Malya, ambaye alinusurika, alisema kabla ya ajali hiyo, Wangwe ambaye alikuwa akiendesha gari hilo, alimtaka ahame kiti cha mbele na kukaa cha nyuma.

Akizungumza na PST katika wodi ya wagonjwa daraja la kwanza alikolazwa, Bw. Malya, alisema Wangwe alimwambia asikae kiti cha mbele kwa vile sio salama kwake na kumtaka akae kiti cha nyuma.

Alisema baada ya kuambiwa hivyo, alihamia kiti cha nyuma na baada ya kama kilomita 20, ndipo ajali hiyo ilipotokea na Wangwe kupoteza maisha. Akisimulia mwanzo wa safari hiyo, Bw. Malya, alisema saa 2:00 asubuhi, alimsindikiza Wangwe bungeni lakini alimweleza kwamba, alikuwa akijisikia kuumwa.

Alisema, hata hivyo hakufahamu kama alikunywa dawa yoyote, isipokuwa ilipofika mchana, alirudi naye nyumbani na kupata chakula cha mchana, kisha akapumzika kidogo. Bw. Malya, alisema ilipofika saa 9:00 alasiri, walianza safari ya kuelekea Dar es Salaam, lakini walipofika kama kilomita 20 hivi nati za tairi la kushoto upande wa dereva, zililegea na wakaamua kusimama na kuzikaza.

Alisema baada ya kurudi gereji, walitengeneza gari na ilipofika saa 12:30 jioni, Wangwe alipitia nyumbani kuchukua `chaji` ya simu. Akizungumzia jinsi ajali hiyo ilivyotokea, Bw. Malya alisema, alisikia kishindo kikubwa na baadaye kutimka vumbi nyingi iliyomfanya ashindwe kuona mbele.


Alisema kilichofuatia ni gari hilo kuserereka umbali wa kama mita 50 kutoka barabarani na kisha kubiringika mara kadhaa. ``Baada ya hapo, sikuweza kutambua chochote na niliposhituka nikamkuta Wangwe akiwa amelala pembeni yangu huku kiti chake alichokuwa amekalia kikiwa kimenibana,`` alisema. Bw. Malya, ambaye ameteguka mguu wa kushoto na kuumia kidogo katika paji la uso karibu na jicho la kulia, alisema kila kitu walichokuwa nacho katika gari, yakiwemo mabegi ya nguo, Laptop na vitu vingine, viliibiwa.


Bw. Malya, alisema alifahamiana na marehemu tangu mwaka 2003 walipokutana jijini Dar es Salaam ambapo kuanzia hapo walianza kushirikiana katika mambo mbalimbali. Alisema kwa jinsi gari lilivyopondeka hasa sehemu za mbele alikokuwa amekaa, kama asingehama, bila shaka asingeweza kupona katika ajali hiyo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Godfrey Mtei, alisema hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri na baada ya siku mbili ataruhusiwa. Baadhi ya wabunge ambao walizungumza na marehemu Wangwe juzi kabla ya kufikwa na umauti, walisema alionekana mnyonge wakati wote.

Mbunge wa Muhambwe (CCM), Bw. Felix Kijiko, alisema alimkuta Wangwe katika mgahawa wa Bunge akiwa hana furaha kama siku zote. ``Nilimuuliza mheshimiwa mbona sijakuona siku kadhaa bungeni, akanieleza kuwa, alikuwa na mambo kadhaa yaliyokuwa yakimtatiza, lakini wakati huo, hakuwa anakula chochote,`` alisema.

Alisema baada ya hapo, alimweleza kuwa atamwambia kinachomsumbua muda si mrefu. Kwa upande wake, Mbunge wa Mchinga (CCM) Bw. Mudhihir Mudhihir ambaye alizungumza naye kwa mara ya mwisho kabla ya kuanza safari katika viwanja vya Bunge, alisema alipokutana na Chacha hakuwa na hali ya kawaida ya uchangamfu aliyoizoea siku zote na alipojaribu kumdadisi zaidi, hakuweza kubainisha ni kwa nini yuko katika hali hiyo.


Kwa upande wake mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), Bw. John Cheyo, alisema kambi ya upinzani imempoteza mtu muhimu mno na pengo lake kamwe halitazibika. ``Alikuwa ni mtu mpambanaji, hakuogopa kitu kusema kweli, aliwatetea wananchi wake bila woga...kwa kweli kifo chache sio pigo kwa kambi ya upinzani pekee, bali ni pigo kubwa kwa wananchi wa Tarime,`` alisema.

Mbunge wa Same Mashariki (CCM), alisema Wangwe alikuwa mpiganaji mkubwa wa haki za wananchi wake, pia alikuwa anashirikiana na kila Mbunge bila kujali itikadi za chama.

Naye Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, ambaye alionekana wazi kujawa na simanzi, hakuweza kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa wamemzonga wakitaka kusikia neno kutoka kwake, alizungumza neno moja tu kuwa, ``Chacha alikuwa rafiki yangu.`` Na katika hatua nyingine Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge, kufuatia kifo cha Mbunge wa Tarime (CHADEMA), Bw. Chacha Wangwe, aliyefariki juzi kwa ajali ya gari.

Katika salamu hizo, Rais Kikwete, alisema amepokea habari hizo kwa masikitiko na majonzi makubwa. Aidha, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo Bw. Wangwe. Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam, na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Bw. Francis Kiwanga, ilisema inatambua mchango mkubwa uliotolewa na marehemu Wangwe katika kuimarisha demokrasia nchini.

Alisema marehemu Wangwe alikuwa mpigania haki sio tu za wananchi wa jimbo lake bali hata kwa Taifa lote. Alisema marehemu Wangwe alikuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi bungeni na kuchangia hoja nzito akishirikiana na wabunge wengine na kukifanya chombo hicho cha wananchi kuwa mhimili imara.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba, amesema chama kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwasisi wa TANU na CCM, Bw. Bhoke Munanka. Taarifa ya Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, ilisema marehemu Munanka aliyefariki Julai 25 aliwahi kuwa mweka hazina wa TANU pamoja na kushika nyadhifa mbalimbali kama uwaziri katika serikali ya awamu ya kwanza chini ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

SOURCE: Nipashe

No comments:

Post a Comment