Tuesday, July 29, 2008

Tanzia - Chacha Wangwe (Mbunge Chadema)


Mbunge wa Tarime kupitia chama cha CHADEMA Mh. Chacha Wangwe(Pichani) amefariki dunia usiku huu kwa ajali ya gari ilitotokea sehemu ya Kongwa Mkoani Dodoma. Alikuwa analekea Dar es Salaam kwenye msiba wa Mzee Bhoke Munanka.

Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahala Pema Mbinguni. Amen.
***********************************************************
Kutoka Habari Leo (Daily News)

Wasifu wa Wangwe

MAREHEMU Chacha Zakayo Wangwe alizaliwa Julai 15,1956. Nyumbani kwao ni Kijiji cha Kyamakorere,umbali wa kilomita 20 kutoka Tarime Mjini.

Alipata elimu ya msingi katika shule za Rosana na Magoto kati ya mwaka 1962 na 1968 kabla ya kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Nyaroha.Baadaye alihamia Dar es Salaam na kujiunga na Sekondari ya Kinondoni Muslim ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1974. Alisoma kidato cha tano na sita katika Sekondari ya Mkwawa kati ya 1975 na 1976.

Alijiunga na masomo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978, lakini hakumaliza. Aliwahi kufanya kazi na Benki ya NBC,Shirika la Kujitolea la Ujerumani,Kampuni ya Lacop na Mgodi wa Dhahabu wa Afrika Mashariki.

Kisiasa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ukiwamo uenyekiti wa tawi la vijana wa Tanu katika sekondari ya Mkwawa,Mwenyekiti wa Wilaya wa Chadema,Tarime,kati ya 1994 na 1998 kabla ya kujiunga na NCCR-Mageuzi ambako alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa kati ya 1998 hadi 2000,lakini akarejea tena Chadema mwaka 2002 na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara wa chama hicho.

****************************************************************************

SALAMU ZA RAMBIRAMBI kutoka kwa Rais Kikwete


Mheshimiwa Spika,Nimepokea taarifa ya kifo cha Mbunge wa Tarime, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) Mheshimiwa Chacha Zakayo Wangwe kwa masikitiko makubwa.

Kupitia kwako, napenda unifikishie rambirambi zangu za dhati kwa wabunge wa Bunge lako Tukufu kwa kumpoteza mbunge mwenzao katika kipindi hiki ambacho wako katika kutekeleza majukumu yao waliyotumwa na Watanzania, ya uwakilishi.

Kwa masikitiko makubwa napenda kutoa salamu zangu za pole kwa wana familia, ndugu, wananchi wa Jimbo la Tarime, wanachama wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) na Watanzania wote.

Kifo huleta masikitiko na majonzi mengi katika familia na jamii, naungana nanyi ndugu zanguni katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo, Mwenyezi Mungu awape imani na subira katika kipindi hiki kigumu na huku tukimuombea ndugu yetu, Chacha Wangwe mapumziko mema peponi. Amina.

1 comment:

  1. Kafa kwa ajali ya gari! Hebu tupeni details nyie waandishi wa habari. Huyo ali vocal sana!

    ReplyDelete