Jamani, mbona kuna vituko huko Dar. Unapanda daladala mzima, unashushwa maiti! Mola ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amin.
*************************************************************
Hatari! Abiria Dar kauawa ndani ya daladala
Kutoka ippmedia.com
2008-08-25
Na Moshi Lusonzo, Pilosi Kati
Ukusimulia tukio hilo, utadhani ni zile hadithi za kubuni za elfu lela ulela siku alfu na moja. Lakini amini usiamini, limetokea Jijini Dar es Salaam.
Mtu katoka nyumbani kwake salama, akavuka barabara salama, akapanda basi salama, halafu akauawa akiwa ndani ya daladala!
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Kandihabi amesema tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana mishale ya saa 3: 45 usiku katika barabara ya Kilwa eneo la Madafu Jijini.
Amemtaja aliyeuawa kuwa ni Suleiman Namumila, mkazi wa Mbagala Kwa Mangaya aliyekuwa kwenye daladala yenye nambari za usajili T989 ARL aina ya Toyota DCM inayofanya safari zake kati ya Mwenge na Mbagala.
Akisimulia mkasa huo kwa undani, Kamanda Kandihabi amesema kwenye daladala hiyo alipanda abiria mmoja mwenye asili ya Kiarabu, ambaye alianza kuzozana na konda akidai amepilizwa kituo.
Kwa mujibu wa Kamanda Kandihabi, mzozo huo ulianza mara baada ya daladala hiyo kuondoka kituo cha Kwa Aziz Ally ambapo abiria huyo alidai kuwa alipaswa kushushwa.
Akasema gari hiyo ilipofika kwenye kituo cha Kwa Madafu, ikasimama ili abiria huyo ashuke.
Hata hivyo akasema wakati abiria huyo akishuka, alimkaba na kumkunja shati konda wa daladala aitwaye Yusuph Hassan, 27, akidai kuwa ndiye aliyesababisha yeye apitilize kituo chake cha kushukia.
Kamanda Kandihabi akasema baada ya abiria wengine kuona hivyo, wakaingilia kati kumtetea konda wao, kwa madai kuwa abiria huyo amepitiliza kituo chake kutokana na uzembe, kwa kuwa gari lilisimama pale kwa Aziz Ally.
Akasema Mwarabu huyo alipoona abiria wote wanamjia juu, akachomoa kisu kutoka mfukoni na kumchoma kifuani Suleiman ambaye alionekana kuwa alikuwa akimsaidia konda.
Akasema baada ya tukio hilo, Suleiman alikimbizwa katika hospitali ya Temeke kwa matibabu, lakini alifariki wakiwa njiani.
Kamanda Kandihabi amesema Mwarabu huyo baada ya kumchoma kisu Suleiman alikimbia na jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.
Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Temeke.
No comments:
Post a Comment