Wednesday, September 10, 2008

Ajali ya Gari Dar - Wapambe wa wanaarusi wafariki!

Jamani mmetoka kusherekea arusi halaffu kitu kama hii kinatokea. Mungu awape nguvu hao wanaarusi maana lazima marehemu ni ndugu au marafiki wa karibu. Nawapa pole maana ni njia mbaya sana ya kuanza maisha ya ndoa. Leo mnasherekea arusi kesho kilio. Jamani!

*******************************************************
Kutoka IPPMEDIA.com
Ajali mbaya Dar!

2008-09-10

Na Moshi Lusonzo, Jijini

Watu wawili wanaotajwa kuwa ni wapambe wa maharusi wamefariki dunia huku wengine kadhaa wakiwemo bwana na bibi harusi kuumia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuvaana na lori la mizigo.

Tukio hilo la kusikitisha, limetokea hivi karibuni, katika eneo la Ubungo ambapo gari lililobeba maharusi na wapambe wao lilipoteza muelekeo na kulivaa lori la mizigo kwa mbele kabla ya kupinduka.

Wakizungumza na Alasiri, baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo akiwemo dereva wa lori la mizigo lililogongwa kwa mbele, Bw. Juma Gwao, 38, wamesema tukio hilo lilijiri mishale ya saa 7:00 usiku.

Wameeleza mashuhuda hao kuwa mara tu baada ya ajali hiyo, bwana na bibi harusi walijeruhiwa na kukimbiziwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, huku wapambe wawili kati ya wale walioambatana nao wakifariki dunia papo hapo.

Akisimulia zaidi ajali hiyo, dereva Gwao ambaye bado amelazwa wodi 17 ya Jengo la Sewahaji pale katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI, amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari lililobeba maharusi na wapambe wao kushindwa kuumiliki vyema usukani wa gari na kusababisha aajali ya kugongana uso kwa uso.

Akiasema Gwao kuwa wakati ajali hiyo ikitokea, yeye alikuwa akiendesha gari lake lenye namba T 908 aina ya Fuso, akitokea Ubungo kwenda mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuchukua shehena za mizigo.

Akasema wakati akiwa ndio kwanza anaianza safari hiyo eneo la Ubungo, ghafla likatokea gari aina ya Canter ambayo ilibeba maharusi pamoja na wapambe wao kibao.

Akasimulia dereva Gwao kuwa pamoja na kujitahidi kukwepa, bado gari hilo lilimfuata aliko na kuigonga gari yake kwa mbele na kisha kupinduka.

``Nadhani dereva mwenzangu alishindwa kuhimili usukani... kwani licha ya kujitahidi kumkwepa, bado alinifuata niliko na kuigonga gari yangu kwa mbele,`` akasema Gwao.

Shuhuda mwingine akasema mara tu baada ya ajali hiyo, wapambe wawili waliokuwa wakiwasindikiza maharusi hao wakapoteza maisha huku wengine kadhaa wakijeruhiwa na kukimbiziwa Muhimbili.

Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Almas Jumaa, amesema ukiacha dereva Gwao, majeruhi wengine wote wa ajali hiyo walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi makwao.

Akaeleza vilevile kuwa hadi sasa, majeruhi Gwao ambaye ni pekee aliyelazwa hadi sasa, angali akiendelea vyema na matibabu na tayari ameanza kupata nafuu kubwa, ukilinganisha na hali aliyokuwa nayo wakati akifikishwa hospitalini hapo.

SOURCE: Alasiri

No comments:

Post a Comment