Thursday, September 11, 2008

September 11, 2001 - Marudio


Nikikumbuka siku ya Septemba 11, mwaka 2001, naweza kusema ni siku nchi ya Marekani ilibadilika. Maana waMarekani hawakutegemea kuwa kitendo cha kigaidi hivyo kingeweza kutokea hapa japo mwaka 1995, mzungu Timothy McVey alilipua jengo la serikali huko Oklahoma.

Siku enyewe kwangu ilikuwa hivi. Nilienda kazini kama kawaida. Ajabu hali ya hewa ilikuwa ni nzuri sana, jua na si joto sana. Wazungu wanasema ilikuwa ni "perfect day". Nilivyofika kazini mume wangu alinipigia simu na kuniambia anaangalia TV na wanaripoti kuwa ndege imegonga World Trade Center. Wala sikutilia manani sana, nilidhani labda ndege ndogo.

Haijapita muda, mume wangu kanipigia simu tena. Alisema kuwa akiwa anangalia taarifa ya ile ndege ya kwanza, aliona ndege nyingine ikigonga jengo la pili huko World Trade Center na sasa wana hofia kuwa ni terrorism!

Sasa mimi niliingia kwenye internet, lakini ilikuwa haifanyi kazi vizuri. Pages hazifunguki. Hatukuwa na TV ofisini. Dada moja ofisini alifungua redio. Mume wangu alinipigia simu nyingine na kusema kuwa ndege imeanguka Pennsyvania na nyingine imeangusha Sears Tower Chicago. (Kweli ilitokea uzushi kuwa Sears Towers imeanguka). Kukaa kidogo kanipigia simu na kusema kuwa ndege imeguka huko Washington D. C. na Pentagon inaugua moto. DUH! nilivyowaambia watu hivyo kuna mzungu moja alisema," Ah, huwezi kuamini kila kitu unachosikia, hata siku moja Pentagon haivamiwi!" Yule dada aliyekuwa anasikiliza aliwaambia watu kuwa nilichosema ni kweli naye alisikia kwenye redio.

Basi wazungu ofisini walianza kuingiwa na kiwewe na kuanza kulia. Wengine walisali, maana ofisi yetu nayo ni ghorofani na tulikuwa financial district kama World Trade Center. Wengine walisem ni mwisho wa dunia! Watu walisema huenda wakavamia Boston. Nilienda dirishani na kutazama nje. DOH! Sijawahi kuona! Wazungu walikuwa wanatembea haraka haraka, wengine walikuwa wanakimbia na suti zao na ma briefcase kuelekea South Station kupanda matreni!

Na mimi nilirudi kwenye deski yangu na kuanza kumpigia simu mdogo wangu ambaye alikuwa anafanya kazi karibu na World Trade Center. Simu zilikuwa haziendi! Wakati huu walianza kutangaza kuwa Tower imeanguka na watu 20,000 wamekufa!

Huko nami nasali namtafuta mdogo wangu. Wake wa watu waliosafiri kutoka ofisini nao walianza kupiga simu kujua hali za waume zao maana walitangaza kuwa ndege ziliondoka Boston, Logan Airport na wengine walikuwa wanasafiri siku hiyo. Bahati hakuna aliyekuwa kwenye ndege iliyoangushwa. Ila huyo shujaa Amy Sweeney, aliyekuwa Flight Attendant na ndiye alitoa habari za nani kateka ndege alikuwa ni jirani wa bosi wangu. Kukaa kidogo walitangaza kuwa jengo letu linafungwa na kila mtu aondoke kwenda makwao.

Basi tuliondoka. Njiani kwenda subway ungeona macho ya watu walivyokuwa wanazubaa na kushangaa. Ajabu watu wasiofahamiana walikuwa wanaongea habari hizo mitaani. Na kama unajua maisha Marekani hiyo siyo kawaida. Nikiwa kwenye treni ndo nilisikia kuwa Tower ya pili imeanguka!

Nilianza kumtafuta mdogo wangu wa New York. Ubaya simu landline na cell phones zilikuwa hazifanyi kazi kwa long distance ilikuwa ukipata ni bahati. Wanasema simu zilikuwa overloaded siku hiyo ndo maana hazikufanya kazi. Ajabu nilishindwa kupiga simu New York, na sehemu zingine Marekani, lakini niliweza kupata simu ya Tanzania mara moja. Nilipiga simu nyumbani kwa wazazi wangu na kuongea na baba. Alikuwa na wasiwasi kweli na alisema mama analia hajiwezi na hawezi kuongea, maana aliambiwa kuwa watu laki mbili wamekufa na alijua mdogo wangu anafanya kazi karibu na pale.

Doh, ilikuwa kwenye saa kumi na moja jioni tukapigiwa simu na mdogo wangu mwingine. Alisema kuwa aliongea na rafiki wa mdogo wangu wa New York na yuko salama. Mbona tulipumua. Nilipiga simu Tanzania kutoa taarifa. Mbona ilikuwa shangwe kule nyumbani.

Jioni ile niliongea na mdogo wangu, aliniambia kuwa alienda kazini kama kawaida. Alivyotoka kwenye subway aliona makaratasi mengi hewani naoshi, na alishangaa imetokea nini. Aliendelea mpaka ofisini kwake. Kufika huko ofisini, waliwaambia watu waondoke ana walikuwa wanatoa chupa za maji ya kunywa na matunda mlangoni. Anasema watu walikuwa na wasiwasi kweli, huko mbele kuna nini.

Alisema kuwa kulikuwa hakuna usafiri wa treni, basi wala teksi, hivyo ilibidi atembee mpaka Brooklyn alipokuwa anakaa. Na alisema hata hivyo hayuko kwake bali kwa rafiki yake anakaa karibu zaidi na New York City. Pia alisema watu madukani walipandisha bei ya vinywaji na chakula.

Kuna rafiki yangu mwingine wa New York, aliniambia kuwa alikuwa karibu na World Trade Center alijaa mavumbui, hakujua nini inatendeka, lakini alijikuta yuko kwenye ferry kwenda New Jersey. Anasema hajui hata alifikaje kwenye hiyo ferry, lakini alishukuru Mungu kuwa alikuwa hai.

Sasa nikirudi hapa Boston, macho yetu kwenye TV. Walikuwa wanaomba wenye utaalamu wa medical waende New York kusaidia. Misafara ya magari ilienda New York na watu wa kusaidia jitihada za kuokoa watu huko New York.

Kesho yake, Septemba 12, kwenda ofisini ilikuwa kama vile unaenda kumtembelea mtu gerezani! Kuna geti na lazima uonyeshe kitambulisho, wakati jana yake unaingia tu hadi kwenye floor yako, ndo unaingiza kadi kwenye security scanner.

Asante bin Laden, mtu aliyefanana na mwarabu alipata shida kweli. Kusimamishwa na polisi mara kwa mara. Kupanda kwenye ndege ndo ilikuwa usiombe, hiyo security na warabu na wahindi walivyokuwa wananyanyaswa na kupekuliwa. Kuna jirani yangu MPalestina, alikamatwa na uhamiaji siku hiyo ya 9/11 na hatujamwona hadi leo. Watu walijitolea kwa wingi kujinga na majeshi ya Marekani.

Jambo cha kusikitisha, watu walikuwa wanavaa hijab, au nguo za kiislamu na hata wahindi singasinga walikuwa wanapigwa ovyo na wengine walipoteza maisha. Nakumbumuka msingasinga jirani yangu alivua kilemba chake na kuvaa baseball cap kwa muda.

Pia ilikuwa kila sehemu kuna bendera za Marekani, watu wakionyesha uzalendo wao. Na biashara za waarabu na wahindi walijaza hizo bendera na hata kuweka bendera kwenya ma Pizza box.

Cha kusikitisha zaidi ni kuwa kabla ya 9/11 ilikuwa rahisi kuja Marekani na kupata Visa. Sasa hivi ulie tu, ni kama bahati nasibu. Watu wanachunguzwa na inabidi watoe na fingerprints ndo wapte hiyo visa!

Na waarabu waliokuwa wanapendwa kwa pesa zao za mafuta sasa ni maadui! Na nukuu usemi wa kizungu, "HOW THINGS CHANGE!"

Ubaya huyo Rais Bush alienda kuvamia Iraq na vita iko mpaka leo, lakini hiyo ni hadithi nyingine. Juzi kuna Mbunge wa Marekani alisema kuwa, "Bush kuvamia Iraq ni sawa na Marekani kuvamia Mexico baada ya Pearl Harbor kuvamiwa na Wajapani"

2 comments:

  1. Ni kumbukumbu ya kusikitisha.
    Ila najiuliza kwa nini Bush alivamia Iraq badala ya saudi Arabia hasa ukizingatia wengi wa wateka nyara wa hizo ndege walitoka huko (Saudi Arabia)? Au kwa kuwa Saudi Arabia ni mshirika wa Marekani? Isijekuwa waliona wakivamia Saudi Arabia basi watakosa 'wese'!

    ReplyDelete
  2. Pole sana Dada Chemi. Ni kweli huyo Bush alikosea alitakiwa avamie Saudi Arabia na si Iraq. Iraq alikuwa analipiza kisasi kwa vile baba yake alishindwa na Saddam.

    ReplyDelete