Namwomba mungu hao waliofanya huo unyama wakamatwe!
Mungu alaze roho za marehemu mahala pema mbinguni. AMEN.
*****************************************************
Kutoka ippmedia.com
Mwinjilisti, mkewe wauawa kwa bomu
2008-11-21
Na Leonard Mubali, Ngara
Mwinjilisti wa Kanisa la Anglikana na mkewe, wakazi wa kijiji cha Mukubu, Tarafa ya Murusagamba, wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameuawa kwa bomu la kutupwa kwa mkono lililorushwa kwenye nyumba yao usiku wa manane wakiwa wamelala.
Bomu hilo lilimkata kichwa Mwinjilisti, Reverian Mlengera (52 ), na kusababisha kifo chake papo hapo.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi baada ya bomu hilo kurushwa katika nyumba ya Mwinjilisti huyo na kundi la watu wasiofahamika.
Ilielezwa kuwa, siku hiyo ya tukio, kundi hilo la watu, lilifika kijijini hapo na kuvunja dirisha la nyumba ya Mwinjilisti huyo na kurusha bomu la mkono kitandani alipokuwa amelala na mkewe ambalo lililipuka na kumkata kichwa huku likimkata mkono wa kulia mkewe, Leokadia Reverian (44).
Hata hivyo, mkewe huyo alipoteza maisha saa chache baadaye kutokana na kuvuja damu nyingi.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, waliiambia PST kuwa, baada ya kufanya unyama huo, watu hao waliingia ndani ya nyumba ya Mwinjilisti na kupora redio kaseti moja, kilo 20 za karanga na debe moja la maharage vyote vikiwa na thamani ya Sh. 60,000 na kisha kutokomea.
Mtendaji wa kijiji hicho cha Mkubu, Nicodem Daniel, aliiambia PST kuwa mauaji hayo ni ya kinyama na yamefanywa na watu wanaodhania kuwa wametoka nchi jirani ya Burundi wakishirikiana na baadhi ya wenyeji wasio waaminifu.
Alisema walimlenga marehemu kwa kuwa alikuwa kipingamizi kwa baadhi ya watu waliokuwa wakipita maeneo hayo wakiwa na silaha kuelekea nje ya vijiji hivyo kwani alikuwa mmstari wa mbele katika utoaji taarifa zinazohusu ulinzi na usalama.
Aidha, mtendaji huyo aliongeza kuwa marehemu alikuwa akiwazuia wahamiaji haramu kuingia na kulima katika kijiji hicho suala ambalo wanalihusisha kwa karibu na uvamizi huo uliosababisha kifo chake.
Nicodem alisema tukio hilo la aina yake ni la pili kutokea kijijini hapo ambapo miezi mitatu iliyopita mtu mmoja na mke wake waliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga katika kitongoji cha Nyakapandi kijijini Mkubu.
Jeshi la polisi wilayani Ngara wamefika eneo la tukio na kuthibitisha kuuawa kwa mwinjilisti huyo.
Mwinjilisti huyo ameacha watoto watatu, mvulana mmoja na wasichana wawili.
SOURCE: Nipashe
No comments:
Post a Comment