Saturday, January 10, 2009

Msiba Daily News - Cassian Malima

Kutoka Lukwangule Blog:


ALIYEKUWA Mhariri wa 'HabariLeo', Cassian Kigeso Malima (44),pichani, amefariki dunia.
Taarifa iliyotolewa jana na Mhariri Mtendaji wa TSN Media Group, Issac Mruma, ilisema Malima alifariki dunia jana jioni katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa tangu Jumamosi iliyopita.
Ilisema Malima ambaye hivi karibuni alipandishwa cheo kuwa Mhariri Msaidizi wa Magazeti ya Mwisho wa Wiki ya Kampuni ya TSN Media Group, alijiunga na kampuni hiyo Oktoba 10, 2004 akiwa Mwandishi Mkuu Daraja la Pili.


Baadaye alipanda cheo na kuwa Mhariri wa Habari wa Daily News na kuwa mmoja wa waanzilishi wa 'HabariLeo' baada ya kuteuliwa Agosti mosi 2006 kuongoza timu iliyoanzisha gazeti hili la Kiswahili linalomilikiwa na Serikali.


“Alitegemewa sana katika utendaji kazi, lakini pia alikuwa mcheshi na rafiki wa kila mtu … aliheshimu kila mtu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mruma katika taarifa yake alisema kampuni imepoteza si tu mfanyakazi, bali rafiki aliyekuwa tayari kubeba jukumu lolote alilopewa na alikuwa mtiifu kupindukia.

Mkewe Malima, Hellen Maro, ambaye walizaa binti, Elizabeth, alifariki dunia Mei 19, 2006.
Malima alizaliwa Mwanza Julai 14, 1965, alipata elimu yake ya msingi katika shule mbalimbali nchini, kati ya mwaka 1972 na 1979; elimu ya sekondari katika Sekondari ya Mwanza kati ya 1980 na 1983.
Alipata elimu ya sekondari ya juu katika Shule ya Sekondari ya Lake Mwanza kati ya 1984 na 1986 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Rostav State cha Urusi kati ya mwaka 1988 na 1994 na kuhitimu Shahada ya Uzamili katika Uandishi wa Habari.
Katika uhai wake, Malima alifanya kazi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA) kati ya 1987 na 1988; Mwandishi wa Habari Uhuru/Mzalendo tangu Mei 1988 hadi 1996 alipokuwa Mhariri.

Machi 1998 hadi Septemba 1999 alikuwa Mhariri wa Habari wa Gazeti la Mtanzania na kuwa Mhariri wa Mtanzania na Mtanzania Jumapili kati ya Septemba 1999 hadi Julai 2003 na kisha Mhariri wa Habari wa The African tangu Julai 2003 hadi Oktoba 2004 alipojiunga na TSN.
Aliwahi pia kuwa kiongozi katika vyama mbalimbali kitaaluma ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Bunge Tanzania, mbali na kuhudhuria semina, makongamano, warsha na kampeni mbalimbali nje na ndani ya nchi. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Mruma alisema mipango ya mazishi inafanywa na taarifa kamili itatolewa baadaye.

No comments:

Post a Comment