Thursday, March 12, 2009

Aliyempiga Mwinyi Afungua Mdomo

Wadau, navyoona wasingempa nafasi huyo kijana aongee. Watatokea wengine wenye agenda zao na kufanya fujo. Mshenzi huyo anastahili kipigo cha nguvu! Nchi yetu Tanzania, ni nchi ya amani. Pia tunajivunia kuwa waKristo na waIslamu wanapatana na hakuna bugudha, Wenzetu barani Afrika wanatuonea wivu! Nina hisi huyo kijana katumwa na watu fulani!

****************************************************
Kutoka ippmedia.com

Aliyempiga Mwinyi afungua domo

2009-03-12
Na Waandishi Wetu

Wakati taasisi mbalimbali za kidini, wananchi wa kawaida na Kamati ya Bunge zikilaani kitendo cha Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, kupigwa kofi shavuni, muumini aliyefanya kitendo hicho, Ibrahim Said, ameeleza kuwa alifanya hivyo kupinga matumizi ya kondomu kwa waumini wa dini ya Kiislamu kwa madai kwamba, yanachochea vitendo vya zinaa.

Pia alisema alifanya kitendo hicho kupinga kuwapo kwa umoja kati ya Waislamu na Wakristo wakati wa kusherehekea sikukuu zao (Maulid, Idd, Krismas na Pasaka), uliozungumzwa na Mwinyi katika hotuba zake alizozitoa wakati wa mkesha Jumatatu usiku na kwenye Baraza la Maulid, jijini Dar es Salaam juzi.

Alisema hakuwa na nia ya kumdhuru Mwinyi na wala hamchukii, bali alikuwa na lengo la kufanya kituko chochote ili ujumbe wake uwafikie watu wengi.

Alitoa maelezo hayo alipohojiwa na polisi saa chache baada ya kufanya kitendo hicho wakati Mwinyi alipokuwa akihutubia Baraza la Maulid, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam juzi jioni.

Kutokana na kitendo hicho, Jeshi la Polisi, jana lilimpeleka kijana huyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa akili na damu ili kubaini kama ana matatizo ya akili au la, kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kijana huyo, ambaye anajulikana pia kwa jina la `Sultani`, alifanya tukio hilo juzi wakati Mwinyi akihutubia Baraza la Maulid katika ukumbi huo na alikuwa amekaa mstari wa tatu kutoka mbele.

Hata hivyo, alisema licha ya kumpeleka Muhimbili, wanatarajia kumfikisha mahakamani leo baada ya jalada la kesi yake kukamilika.

Alisema baada ya kufanya tukio hilo, kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi cha Salander Bridge na baadaye alihamishiwa kituo cha Polisi Kati kwa mahojiano.

``Nilimhoji kijana huyu ambapo katika maelezo yake alisema kuwa, yeye hakuwa na nia ya kumdhuru Mwinyi na hamchukii bali alikuwa na lengo la kufanya kituko chochote kile ili ujumbe wake uwafikie watu wengi. Alidai hakubaliani na hotuba za viongozi wa Kiislamu zinazosisitiza Waislamu na Wakristo kushirikiana kama vile kusherehekea kwa pamoja sikukuu za Maulid, Idd, Pasaka na Krismas,`` Kova alisema akimkariri kijana huyo.

Kova alisema kijana huyo aliendelea kumweleza kuwa, kwa maoni yake sikukuu za Kiislamu wanasherehekea wenyewe na Wakristo hivyo hivyo na sio kwa pamoja.

Kuhusu kondomu, Kova alimkariri kijana huyo akieleza kwamba, anapinga matumizi ya mpira huo kwa madai kwamba kuhimiza matumizi yake ni kuhalalisha uzinifu kwa Waislamu.

Hata hivyo, Kamanda Kova alisema katika mahojiano naye alimuuliza kwa nini aliamua kutumia njia hiyo kufikisha ujumbe wake, na yeye alieleza kuwa ujumbe wake usingefika kwa sababu ni mtu mdogo mwenye hadhi ya chini hivyo ungechelewa.

Akisimulia zaidi tukio hilo, Kamanda Kova alisema siku ya tukio kijana huyo alinyanyuka kwenye eneo alilokuwa amekaa muda mfupi baada ya waandishi wawili wa televisheni kurekebisha vipaza sauti vyao mbele ya Mwinyi, naye akijifanya anafanya hivyo (kurekebsiha kipaza sauti), lakini akaishia kumpiga kofi kiongozi huyo mstaafu.

``Mtu huyu baada ya kufika pale mbele alijifanya anarekebisha vipaza sauti kama walivyofanya waandishi, na alisogea karibu zaidi na Sheikh Mkuu na kujifanya anaongea naye ndipo aliponyanyua mkono wake wa kulia na kupiga kipaza sauti alichokuwa akikitumia Mwinyi na kiganja cha mkono sehemu ya nyuma ulimpata kwenye shavu la kulia,`` alisema.

Alisema kufuatia tukio hilo, uchunguzi unaendelea kufanyika ili kujua kama alitumwa na mtu au kikundi fulani au ni mwanaharakati.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Kova alisema wataangalia uwezekano wa waandishi wa habari pindi wanapohudhuria kazi za viongozi kuwa na kadi maalum za kuwatambulisha ili mtu yeyote asije akaonekana kama mwandishi.

Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Bakwata walaani
Wakati kijana huyo akijieleza, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Jumuiya inayoratibu safari za Hijja na Umra ya Taibah pamoja na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), zimelaani vikali kitendo cha Mwinyi kushambuliwa na kijana huyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Wilson Masilingi alisema analaani vikali kitendo hicho kwa vile kimelitia taifa aibu.

``Nalaani vikali, kwani ni aibu. Ninawaomba wananchi watoe ushirikiano ili kitendo kama hicho kisijirudie katika siku za usoni,`` alisema Masilingi, ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kusini (CCM).

Hata hivyo, alisema hajui mazingira ya tukio hilo na kwamba, waliokuwapo katika eneo la tukio wana nafasi nzuri ya kueleza kama kuna uzembe wowote uliofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama, na kutoa mwanya kwa mtuhumiwa kumshambuliwa Mwinyi.

Kutokana na hali hiyo, alishauri marais wote wastaafu waongezewe ulinzi kwa kuwa jambo hilo ni haki yao na ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kuwasibu baadaye kutokana na kufanyiwa vitendo vya kihuni kama hicho.

``Marais wastaafu wanastahili kuongezewa ulinzi. Ni haki yao. Kwani anaweza kutokea mwendawazimu katika dunia ya sasa, akaleta fedheha,`` alisema Masilingi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taibah, Sheikh Ali Mubarak, alisema kitendo cha kushambuliwa kwa Mwinyi ni cha kulaaniwa na Watanzania wote wanaopenda amani na kuvumiliana katika masuala ya kila aina kwa vile kitendo hicho ni cha kinyama.

Sheikh Mubarak alisema mbali ya kuwa ni cha kinyama, kitendo hicho ni kinyume cha utamaduni wa Watanzania, hivyo kinapaswa kulaaniwa na kudhibitiwa ili kisitokee tena.

``Uongozi wote wa Taibah umepokea kwa masikitiko makubwa tukio la kushambuliwa kwa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi wakati akihutubia maelfu ya waumini wa Kiislamu jana (juzi) ukumbi wa Diamond Jubilee. Kitendo hicho kwa vyovyote vile ni cha kulaaniwa na jumla ya Watanzania wanaopenda amani na kuvumiliana katika masuala ya kila aina,`` alisema Sheikh Mubarak.

Kutokana na hali hiyo, aliishauri serikali kuchukua hatua dhidi ya kitendo hicho ili kupata undani wa tukio lenyewe.

Alisema Taibah inampa pole Mwinyi, serikali na uongozi wake kwa vile inaamini kuwa kiongozi huyo ni mzee mwenye busara na anayetegemewa.

Naye Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Suleiman Gorogosi, alisema jana kuwa Bakwata inalaani vikali kitendo cha kushambuliwa Mwinyi kwa vile kitendo hicho ni cha kihuni na ni kinyume cha mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Hata hivyo, Gorogosi ambaye pia ni Sheikh wa Bakwata Mkoa wa Lindi, alisema bado wana wasiwasi huenda mtuhumiwa aliyefanya kitendo hicho, ana matatizo ya akili, ingawa alisema kuwa uongozi wa Bakwata haumjui.

Kanisa lapigwa na butwaa
Nao viongozi wa dini nchini, wamesema kitendo cha Rais Mstaafu Mwinyi kupigwa kibao jukwaani, kimeidhalilisha Tanzania na kuwafedhehesha wananchi wote.

Aidha, wamesema kutokana na kitendo hicho hivi sasa ipo haja kupima na kutathimini kiwango cha amani na utulivu nchini.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Mhashamu Methodius Kilaini, alisema kitendo hicho hakikumvunjia heshima na kumdhalilisha Mwinyi pekee bali Watanzania wote.

Alisema kwa kifupi Kanisa nchini limepigwa na butwaa na kubaki na mshangao.

``Lakini pamoja na hayo yote tunampa pole nyingi Mzee Mwinyi. Tunamtaka asifadhaishwe na kitendo hicho,`` alisema.

Kilaini alisema jambo hilo linashangaza zaidi na kulifanya Kanisa liwe kama limemwagiwa maji, hasa ikizingatiwa kuwa kitendo hicho kimefanyika katika shughuli za kidini.

Hata hivyo, alisema pamoja na dosari hiyo, bado anaamini kwamba Watanzania hawajawa na tabia ya hujuma na kujitoa mhanga kama hiyo.

``Naomba suala hili lichukuliwe kama ajali tu, kwa vile siamini kwamba hali ya amani katika nchi yetu imefikia hapo,`` alisema.

Askofu huyo alisema hakuna jambo lolote baya ambalo alizungumza Rais Mwinyi ambalo lilifanya iwe sahihi apigwe.

``Lakini jambo hili sasa lisipotazamwa kwa makini, mambo ya dini yatakuwa sio ya kuaminika tena kama ilivyozoeleka,`` alisema.

Alisema kitendo hicho kinaweza kuwaweka viongozi mbali na wananchi kwa kuhofia usalama wao.

Askofu Kilaini aliwataka Watanzania hasa watu wa dini, kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kuvumiliana hata kama mtu anazungumza au anatoa msimamo ambao hukubaliani nao.

Naye Askofu Dk. Stephen Munga wa KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki, alisema wakati Kanisa limebaki mdomo wazi, kuna haja ya vyombo vya dola kuchunguza kwa kina jambo hilo na kulikomesha.

Alisema haelewi hasa lengo la muumini huyo lilikuwa nini, lakini akasisitiza kwamba huenda kuna kikundi au watu wapo nyuma ya `mbabe` huyo.

``Kama yale mambo ya kujitoa mhanga yameshaanza kuota hapa petu, basi ni ishara kwamba Watanzania tunaelekea gizani, jambo hili haliashirii mema katika nchi yetu,`` alisema.

Askofu Munga alisema Kanisa limepigwa na butwaa na kujiuliza kuwa mtu huyo aliyefanya kitendo hicho, amezaliwa katika nchi gani?

``Jambo hili lina maswali mengi kuliko majibu, kweli kijana wa Kitanzania aliyezaliwa hapa, hajui wala hajaona ustaarabu wetu wa kuwaheshimu viongozi kama ni Mtanzania, basi anao uovu mkali kichwani pake, ambao amepandikizwa na kikundi fulani. Haya kama kweli ni punguani kama wengine wanavyosema, huo upunguani umeanza lini, tunaambiwa amekuwa akihudhuria ibada zote za Maulidi, kwanini upunguani wake ukamsubiri hadi Mwinyi aongee? Kwa nini huo upunguani haujaonekana kwingineko? Ndio maana tunasema jambo hili lina maswali mengi kuliko majibu,`` alisema.

Hata hivyo, Dk. Munga alionya kwamba suala hilo ni kubwa hivyo lisitolewe majibu rahisi kwamba mhusika ni punguani.

Alimtaka Mzee Mwinyi kutofadhaika na kukata tamaa kwa vile bado Watanzania wengi wanamheshimu, kutokana na mchango wake mkubwa wa kisiasa, kujamii, kiuchumi na kiutamaduni alioutoa wakati wa uongozi wake.

UVCCM walaani
Baraza Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), limetoa tamko la kulaani kitendo cha kupigwa kwa Rais Mstaafu Mwinyi, kilichotokea juzi wakati wa sherehe za Baraza la Maulidi.

Akitoa tamko hilo jana kwa waandishi wa habari kwa niaba ya Baraza hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya UVCCM, Masauni Yusuf Masauni, alikiita kitendo hicho kuwa ni cha kihuni, udhalilishaji, fedheha na utovu wa nidhamu.

Alisema kwa kauli moja Baraza hilo limesikitishwa na kitendo hicho, hasa ukizingatia kuwa kimefanywa na kijana wa Kitanzania ambaye amewaaibisha vijana wote wa Tanzania, kwa kuonyesha kuwa hawana nidhamu.

``Kwa ujumla Baraza limepokea kwa masikitiko makubwa kitendo hicho cha kihuni, udhalilishaji na cha fedheha alichofanyiwa kiongozi wetu mpendwa Mzee wetu Alhaji Ali Hassan Mwinyi,`` alisema Masauni.

Aliongeza kuwa kitendo hicho kilichofanywa na kijana huyo ni kinyume cha maadili ya dini zote na utamaduni wa Kitanzania kwa wazee wetu, viongozi na jamii kwa ujumla.

Kutokana na kitendo hicho, Baraza hilo limeitaka serikali ufanyike uchunguzi wa kina na wa haraka ili kubaini nia ya kitendo hicho cha kihuni na hatua kali za kisheria dhidi ya mhusika, zichukuliwe mara moja.

Pia alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama viimarishe ulinzi kwa viongozi wastaafu na waliopo madarakani, ili kusiwe na matukio ya namna hiyo tena.

Baraza Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Vijana lilikutana mjini Dodoma kwa muda wa siku sita kujadili mambo mbali mbali yanayohusu mustakabali wa CCM.

Mbeya nao waja juu
Wananchi wakiwemo viongozi wa dini mkoa wa Mbeya wameelezea kusikishwa na tukio la kupigwa kibao Rais Mstaafu Mwinyi ambapo wamewatupia lawama walinzi wake kwamba walikuwa wazembe kwa kushindwa kumlinda kwa umakini kiongozi huyo.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti walisema tukio la kupigwa Rais Mwinyi limeiweka nchi katika kashifa mbaya mbele ya uso wa dunia na Tanzania kuonekana ni nchi isiyokuwa makini katika kuwalinda viongozi wake.

Mmoja wa wananchi hao, Abdallah Bugano, akizungumza na Nipashe alisema mazingira ya jinsi tukio lilivyotokea yanaonyesha kuwa walinzi wa Rais Mwinyi hawakuwa makini na ndiyo maana mtu aliyefanya kituko hicho aliweza kujipenyeza hatimaye kumnasa kibao kiongozi huyo.

``Tukio hili walinzi wa Rais Mwinyi ni wazembe sana, kwanini yule kijana alikwenda pale kama vile anataka kurekebisha vipaza sauti, ina maana hakukuwa na watu maalum wanaojulikana waliowekwa kuifanya kazi ya mitambo, huu ni uzembe,`` alisema Bugano.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste mkoa wa Mbeya, Askofu Amos Igundu, alisema Wakristo wamelipokea tukio hilo kwa maskikitiko makubwa na kwamba kuna haja kwa vyombo vya usalama kujipanga upya kwa namna ya kuimarisha ulinzi kwa viongozi wakuu, hususani kwenye mikutano ama sherehe zinazojumuisha watu wengi.

Askofu Igundu alisema tukio hilo limeitia doa nchi na hivyo ni jukumu la vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina sababu za kijana huyo kuamua kuchukua hatua ya kumpiga kibao Rais Mstaafu Mwinyi.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Albert Mgumba akizungumza na Nipashe kwa simu akiwa wilayani Kyela, alisema kitendo kilichofanywa na kijana aliyempiga kibao Rais mstaafu Mwinyi ni utovu wa nidhamu na kwamba inabidi achukuliwe hatu kali.

Imeandaliwa na Muhibu Said, Romana Malya, Simon Mhina, Mary Edward na Thobias Mwanakatwe.

SOURCE: Nipashe

4 comments:

  1. Hatukubali! Huyo kijana achukuliwe hatua kali. Afungwe hata maisha! Nchi yeti ni ya Amani na ibaki hivyo! Kama anadhani shujaa ajue tunamwona mjinga!

    ReplyDelete
  2. Namvizia huyo jamaa nimlambe kibao hapo kisutu! hawezi kumpiga Mzee wetu na sisi tukamwachia! Dini inaheshimu sana watu wakubwa waliokuzidi umri...huwezi kumpiga mzee wako kofi tena mbele ya hadhara eti kwa kisingizio cha dini!!Mbona sijaona mtu anapigwa vibao au hata kutukanwa anapozungumzia kondom barabarani??/ kwa nini iwe mzee Mwinyi?? alaaniwe huyo kijana hata kama anatetea Dini!! Namlaani huyo kijana na hata asipofungwa hilo kosa alilofanya litamfata kila atakapokuwa na hatafanikiwa maisha yake yote!! Kitendo cha kumpiga kosa Mzee wetu mpendwa kimeniuma sana na sina raha toka siku ile...Namwomba mzee wangu Mwinyi atulie na mimi nitamlipizia kisasi!!Wadau tushirikiane kumlaani huyu kijana

    ReplyDelete
  3. Da Chemi nimependa namna ulivyoonesha hisia katika tukio hilo. Ni kweli binadam hatupo wakamilifu, mara nyingi nafuatilia kwa umakini unapotoa hoja na ninajiridhisha sana kwamba wewe ni mtu mwenye kupenda utawala wa sheria. Rejea picha ya Rais Museveni!
    Upande wa pili nimeshangazwa na kauli yako kwamba asingeruhusiwa hata kusema. Ni namna gani sheria itachukua mkondo kama mtu hata ruhusiwa kusema. Pls umepotoka! Kipimo kizuri cha utekelezaji wa haki ni pale unapokuwa umeghadhabishwa.
    Tamati!!!

    ReplyDelete
  4. hata usikubali na hata akinyongwa unadhani ujinga wake utafuta upumbavu wako.na nani amekwambia nchi yako ina amani na ni amani gani unayoiongelea bwege weye.maalbino wanauwawa,watu wasio na hatia wanauliwa,watu wanadhulumiwa haki zao na viongozi mafisadi wanaendelea kutuzamisha baharini,unatakiwa ujue hatuna amani ya ndani ya nchi bali ya nje ya nchi.Ibrahim ameonyesha mfano wa kuigwa tanzania na bado wengine.

    ReplyDelete