Kutoka ippmedia.com
Kwa tafsiri yangu nyepesi nyepesi, ufisadi ni wizi, udanganyifu, ulaghai, ubadhirifu, umaaluni, ufedhuli, ubaradhuli na mengineyo yanayofanana na hayo. Vitendo vyote hivyo siyo tu vinafanywa na baadhi ya watu dhidi ya serikali na taasisi za umma, bali pia dhidi ya mke au mume wa mwenzako. Unabisha? Subiri nikutoholee.
Naam, mpenzi msomaji, nimeanza kuchombeza hivyo ujiandae kwa vionjo vinavyodhihirisha kirusi cha ufisadi kinavyozitafuna pia familia zetu. Kirusi hiki, ama kinabomoa nyumba zetu au kuzitia nyufa, na zaidi kinazisambaratisha kwa baba na mama, kila mmoja kufikia hatua ya kutafuta sehemu ya kujishikiza nje ya ndoa.
Kwanini hali hii inatokea? Je, ni umasikini ndani ya familia? Au ni utajiri umewakolea kiasi cha kupagawa na hivyo kutafuta maisha mbadala pembezoni? Au ni kitu gani hasa! Majibu yote haya msomaji wangu utayapata ndani ya mtiririko wa makala hii.
Hivi majuzi yupo fundi ujenzi wangu alinisimulia kisa kimoja ambacho kilinivuta kimawazo nikaona nikimwage hapa, ili pengine kirekebishe wenye mwelekeo huo. Hakifurahishi, lakini kina mafundisho muhimu ya kimaisha.
Katika simulizi yake, fundi huyu anasema kwamba yupo baba mmoja wa makamo mwenye mke na watoto wake wanne, wawili ni wasichana. Wawili wako sekondari, wengine vyuo.
Familia hii ina mji kule Mbagala wenye nyumba ya kisasa yenye eneo lenye nafasi.
Jirani na nyumba yao wakaamua kuanzisha baa na duka. Hapo huja wateja kununua na kuondoka na wengine huketi na kupata vinywaji, nyama choma.
Wazee hawa(baba na mama) wa mji huu, nao mara kwa mara huwa sehemu ya wanywaji. Pale hupata fursa ya kukutana na wezee wenzao kubadilishana mawazo. Ni wakamata maji wazuri na yakiwakolea hawasiti kuzua mitafaruku.
Unajua tena, wagidaji pombe ikiwakolea adabu na heshima huchepuka, hivyo kutoa fursa kwa ibilisi kulaghai. Simile hutoweka kwa wengine na kuanza kuongea ovyo.
Unaweza kudhani wanapofanya hivyo wanatania kumbe ni kweli toka kwenye nafsi zao zilizolegezwa na kilevi. Mfano mtu anamwambia mke wa rafiki yake eti ‘nakutamani sana’, na maneno haya anayasema mbele ya mumewe.
Je, mume mtu ataelewa kuwa ni utani? Ipo mitafaruku iliyoibuka kutokana na utani wa aina hii. Na pengine aliyetamka maneno hayo hakuwa anatania bali alimaanisha hivyo kupitia ibilisi wake wa pombe.
Kwa maelezo ya fundi huyu, wazee wa familia ninayozungumzia mara nyingi wamekuwa wakizozana wakiwa wanakunywa kwenye baa yao hiyo na zaidi ni wivu. Hofu yao ni kwamba huenda kila mmoja anao wateja anaowahusudu wanapokuja kunywa mahali hapo.
Baba anamshuku mume kuwa anao kinamama anaoonekana kutaniana nao au kuongea nao sana na huenda mmojawao ni mpenziwe wa pembeni. Na baba vivyo hivyo huhisi kuwa mama ana wazee anaochekacheka nao sana au vijana na huenda wapo anaowahusudu. Ili mradi kila mmoja anamtilia shaka mwenzake.
Chanzo cha mzozo wote huu ni uwepo wa baa hiyo karibu na nyumbani. Pengine isingekuwepo na kila mmoja angevinjari kivyake na migongano ya aina hiyo isingeonekana.
Kwa mtizamo, mama ndiye anayeonekana chakaramu zaidi na mshekumsheku anapoona wanaume, tofauti na mumewe ambaye ni mpole, mkimya ila mpepesaji mzuri wa macho anapoona kinamama au wasichana wanapitapita mbele yake wakija kupata huduma kwenye baa hiyo.
Upole na ukimya wa baba huyo, ulimzidishia mkewe jeuri kwamba hawezi kufurukuta. Hata ndugu za mume hufikiria mara mbili mbili kwenda kumtembelea ndugu yao(mume) kutokana na ukali wa mke.
Ilitokea mama huyu akamgundua mumewe akimkazia macho mwanamama mmoja. Hali hiyo ambayo ilikuwa ikijirudia mara kadhaa, ilimfanya mke ampige marufuku mwanamke yule kutokanyaga kwenye baa yao.
Hisia kuhusu mahusiana ya baba huyo na mwanamke huyo zilipelekea mkewe kumbonda mara nyingi kila wanapokolewa pombe na kutafutiana vijisababu vya kukosana. Na kila zikizuka vurumai, baba huchukua kibegi chake na kutokomea. Inaelezwa kuwa huenda kulala gesti.
Lakini kumbe halali gesti huenda kujichimbia nyumbani kwa mwanamke yule yule anayesababisha mipasuko ndani ya nyumba yao. Na mwanamke huyo baada ya kufukuzwa kwenye baa ile akaapa kutomwacha mzee huyo hadi kieleweke.
Misukosuko ambayo mume huyo alikuwa akipata kwa mkewe ilikuwa kama kichocheo cha kuzidi kumpenda mwandani huyo wa pembezoni.
Fumba na kufumbua mwandani huyo akapata mimba na kukaa sawa mtoto akazaliwa. Mtoto dume.
Taarifa zilipomfikia mama mwenye nyumba inaelezwa hadi sasa ameshikwa na bumbuwazi, na mume naye ndiyo amekuwa mbogo haoni wala hasikii.
Tena humpasulia wazi kwamba nakwenda au nimetoka kwa mke mwenzio. Naye mwandani huyo kila anakopita anatangaza ushindi kwa kumuopoa mume wa mwanamke mwenzake. Ufisadi mkubwa huu. Inauma lakini maji yakimwagika si hayazoleki?
Mpenzi msomaji, huo ndio ufisadi niliogusia tafsiri zake nyepesi nyepesi mwanzoni mwa makala haya. Ukali wakati mwingine huleta kilio. Kumbe pengine hekima ingetumika hata mpasuko uliojitokeza ndani ya familia hii usingekuweko. Hii ni kutokana na ukweli kwamba hekima ni bora kuliko kutumia nguvu. Na kwamba afadhali kusikiliza maneno matulivu ya mwenye hekima kuliko kusikiliza kelele za mfalme katika kikao cha wapumbavu.
Ufisadi mwingine unaozibomoa nyumba zetu ni huu unaofanyika kupitia simu za kiganjani. Mtu anamdoea mke au mume wa mwenzake na kisha anatumia ujumbe wa simu kumchanganya.
Wenye mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa zao wameshaonja joto la kasheshe zinazotokana na ufisadi huu. Na wenye kiherehere zaidi ni wale washikaji wa nje ya ndoa. Hao huwa wakali kuliko wenye nyumba zao. Kisa wanawaonea wivu na wanaponogewa hudiriki kubomoa nyumba zilizojengwa kwa gharama kubwa.
Anachofanya yule dowezi ni kutafuta simu ya mke wa mshikaji wake na kumtumia maneno ya kashfa kumdhihirishia kuwa mumewe anamdhibiti. Tabia hii wanayo sana wanawake.
Mwingine hupagawa na kuamua ku-forward ujumbe aliotumiwa na mume wa mwanamke mwenzake ili kumringishia kuwa hayuko peke yake na kwamba mumewe anaye kila anapomhitaji. Huu ni ufedhuli, ubedui, umaaluni, ufirauni wa hali ya juu.
Nyumba nyingi zimejikuta katika mpasuko mkubwa kutokana na mahusiano nje ya ndoa. Nyumba inachipuka ndani ya nyumba(nyumba ndogo hizi). Hata mtu akiona mwenzake akapatwa na balaa fulani, badala ya kujifunza na kuepuka, naye hujitosa kama vile shamba la majaribio. Matokeo yake naye anatumbukia.
Kwa ujumla mipasuko ndani ya familia zetu tunaisababisha sisi wenyewe. Kama baba na mama wako imara, hawatamani vya nje, hata Mungu hubariki nyumba hiyo na kuwa imara. Zipo nyumba chache za aina hii. Nyingi ni zile zinazoiga eti kama yule kafanya vile kwanini na mimi nisifanye hivyo. Kumbuka kuiga tembo ku… utapasuka msamba. Au siyo? Maisha Ndivyo yalivyo.
Niishie hapa msomaji wangu niruhusu nawe uchangie maoni, au nipe kisa ukijuacho tukijadili kwa pamoja.
Niandikie:
flora.wingia@guardian.co.tz
Wasalaam.

ndomana mkaambiwa oa hata wanne rukhsaaa!
ReplyDeletemh! lakini mkate wa wizi mtamu sana bwana...!!!
ReplyDelete