Wednesday, October 14, 2009

Tatizo la Umeme Tanzania

Jamani, mbona habari ya mgao wa umeme kuanza tena Tanzania inasikitisha sana. Lini tatizo litaisha? Kweli habari hizi zinavunja moyo. Badala ya kwenda mbele tunakwenda nyuma!

Someni maoni ya mhariri wa Nipashe.

********************************************************************
Tunahitaji umeme wa uhakika si malumbano

Na Mhariri

13th October 2009

Ukifuatilia kwa karibu yanayotokea katika sekta ya nishati ya umeme nchini, huwezi kuepuka kufikia hitimisho jepesi tu, kwamba hakuna anayejali kinachotokea.

Kama taifa tumekosa ujasiri si tu wa kutenda, bali hata wa kusema. Tumekosa hata soni ndani ya nafsi zetu, kiasi cha kubakia kupiga domo mwaka hadi mwaka.

Taifa kwa sasa lipo kwenye mgawo mkali wa umeme wa zaidi ya saa 14 kwa siku kokote ambako gridi ya taifa imepita. Ni kero, shida na kila aina ya kuvunjika moyo, kwamba mwaka baada ya mwaka tunabakia pale pale, watu tusioweza si tu kujifunza kwa makosa ya watu wengine, bali hata kwa yetu wenyewe.

Tangu mwaka 2006 serikali ilipoamua kuachana na mchakato wa kubinafsisha Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) tulitarajia kuona watu wakikimbizana usiku na mchana kuiondoa nchi katika adha hii ya umeme wa mgawo.

Tuliona juhudi za kutafutwa kwa umeme wa dharura wa megawati 100 wa kampuni hewa ya Richmond, ambayo ilipewa kandarasi ya kuzalisha nishati hiyo kwa kutumia gesi asilia.

Kwa bahati mbaya, umeme huo uliingia ruba, haukupatikana kwa wakati, kwa hakika ulipatikana wakati dharura ikiwa imekaribia kufikia ukingoni, lakini kwa kutambua ukiukaji wa taratibu za kumpata mkandarasi Richmond, mkataba wake ulivunjwa na hivyo, Richmond na mrithi wake, Dowans wakatakiwa wafungashe virago.

Tangu hatua hizi za kuvunja mkataba zichukuliwe, si tu kumekuwa na ngonjera za kutakiwa kwa mitambo ya Dowans, bali pia juhudi za lazima kabisa za kutaka Tanesco inunue mitambo hiyo, hoja inayojengwa ni moja, mitambo ni mizuri na kwamba mitambo si mkataba, kweli inawezekana kuna ukweli wa jambo hilo.

Lakini kwa bahati mbaya, nchi haiendeshwi tu kwa uhalali wa kisheria na ubora wa hiki au kile, bali pia na siha ya kisiasa ya wakati husika. Kwa maana hiyo kama siha ya kisiasa si mwafaka kwa wakati fulani si vema wala busara kung’ang’ana na jambo fulani.

Kwa hali hii haijalishi kwamba eti mitambo ya Dowans ni mizuri kiasi gani, kama siha ya kisiasa si mwafaka kwa mitambo hiyo kuchukuliwa, na kwa sababu wahusika serikalini na ndani ya Tanesco walikwisha kuonywa juu ya hali hiyo, tulidhani kwamba nguvu zao zingeelekezwa kwa mbadala wa Dowans.

Lakini inavyoelekea watu wamejaza vifua visasi na vinyongo vya kutaka kuonyeshana nani zaidi. Nguvu kubwa hazijaonekana zikielekezwa huko na huko kusaka mitambo mengine kama mbadala wa Dowans, hata kama ilijulikana wazi kwamba mkataba wa Richmond kuanzia mapema ulikuwa ni wa miaka miwili tu, sasa kufikiri kwamba bila wao (Dowans) adha ya umeme haiwezi kutatuliwa, tunashawishika kuuliza kuna nini Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini?

Kama taifa hatuwezi kukamatwa mateka wa Dowans na siasa zote zinazohusu Richmond na wote waliokuwa kondoo wa kafara kwa utendaji mbovu wa baadhi ya watendaji serikalini na au maamuzi dhaifu ya wanasiasa; tunataka umeme.

Tanesco ni lazima itambue kwamba inawajibika kutupa umeme, ni lazima iumize kichwa kutupa umeme, kutupa sababu za mgawo wa umeme na ratiba ya mgawo, si vitu vinavyosaidia taifa hili kusonga mbele.

Tunahisi kwamba kwa kitambo kirefu mno, Tanesco si tu wameachwa hadi kulewa vilivyo ukiritimba wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini, bali pia wamebobea mno katika uzembe na kutokujali kwa kiwango cha hali ya juu.

Uongozi wa Tanesco umeamua kubweteka, si leo wala jana, ila kwa miaka na miaka, wameruhusiwa kuishi kwa kuamini wananchi ndio wanaowahitaji na si vinginevyo, ndiyo maana Tanesco daima hawashituki wanaposikia mteja wao kapata hasara kwa sababu ya kuunguliwa na nyumba kutokana na huduma zao mbovu, wala hawasumbuki wanapokuwa na mlolongo wa maombi ya wananchi wanaohitaji huduma yao. Tanesco wakikosa kabisa mkakati wa kumaliza kero hizo.

Tanesco walitutisha kwamba kwa kuikataa Dowans tutajuta, na sasa wameanzisha mgawo, ndiyo kusema walikusudia kuliadhibu taifa, walipanga na sasa wametekeleza. Hii haikubaliki, kama wapo walioshindwa kazi Tanesco wanasubiri nini, hili ni shirika la umma si kampuni binafsi, ni vema na haki wakapisha wengine watakaothubutu kujaribu na hivyo kutatua kero ya umeme nchini.


CHANZO: NIPASHE

5 comments:

  1. Wakomeshe na mafisai wa TANESCO! TUMEWACHOKA!

    ReplyDelete
  2. Dada Chemi: Tatizo la Nchi yetu TZ ni kwamba Siasa ina-determine kila kitu; halafu watu wanaona tatizo lakini hawataki kufanya "obvious effective decision" just becuase it might have negative impact on them politically, nitatoa mifano mitatu:
    1. TANESCO: Ni wazi kwamba CEO na Board Chairman wamekuwa wakigombana kupitia vyombo vya habari now-and-then kila mmoja ana uhusiano mzuri na Rais politically or otherwise. Hakuna uamuzi ulifanywa juu ya hawa jamaa waweze kufanya kazi jointly kwa manufaa ya TANESCO na nchi... Hivi haikuwezekana kuwabadilisha... How did the government expect the CEO and Board Chairman both officially Presidential appointees will work for the better TANESCO if they do not talk to each other harmonously. On the other hand Wabunge na Serikali, hivi serikali inafanyaga analysis ya maamuzi inayofanya kuwaridhisha wabunge na watu wengine politically or not??? Kukubaliana na wabunge kuto kununua Dowans plants is OK given that you have clear Plan B in place, hakuna alternative plan but government complies with Wabunges. Hivi serikali kwanini haikukubali in public kwamba kwa wakati ule hakukuwa na effective alternative but go ahead with Dowans au wabunge wangekuja na plan B kama walikuwa wanaendelea kudai Dowans wawe thrown out. Hakuna BUSARA HAPA......

    2. ATCL: Hapa ndiyo kabisaa ni siasa juu ya siasa na upuuzi mwingi sana unafanyika.... The airline business is highly competitive now, nobody can deny this fact..... Lakini kumweka Mzee Nxxxxxxxx kuwa Board Chairman wa ATCL is purely political nothing nothing is business based decision here... Tuna tatizo la siasa kutawala kila mahali...Huyu jamaa amakuwa kwenye veyeo vya juu serikalini tangu mimi naanza kupata akili over 30 years ago na amekuwa ubalozi for over 15 years.. sasa amerudi home anapewa post ya Leadership and visionary for recovery of ATCL??????????? isnt it strange??? no, politics!! He could be smart in business as well apart from politics...Lakini hajali taabu za watanzania, Yaani kodi za wa-TZ serikali inazipeleka ATCL to keep it alive yeye na CEO wake wanazitumia kuleta Posh cars (Mashangingi)... sasa unafikiri hawa wako makini au wanajali fate ya wa-TZ wenzao?? Do they care about losing their jobs for such decisions, hapana kwasababu they got the jobs through politics or know who not competency... so, no need to care about that no-one of them will loose his job.
    3. TRL: The investment is done what you need is just to run efficiently.....nothing works well here too..
    4. TTCL: This was supposed to be the most profitable company in Tanzania, it is struggling....

    TANZANIA POLITICAL LEADERS MUST ACCEPT THE DYNAMICS OF BUSINESS HAVE CHANGED .... POLITICS SHOULD BE KEPT AWAY FROM BUSINESS.... ELSE DO NOT EXPECT MUCH IN BUSINESS... LONG LIVE AND GOD BLESS TANZANIA.

    ReplyDelete
  3. hatuna viongozi, tunawapa vichaka kuongoza nchi ndiyo matokeo yake. wao walidhani kuongoza ni kupeperusha bendera ya gari.

    ReplyDelete
  4. Kweli ni aibu! Siasa kabla ya manufaa ya nchi!

    ReplyDelete
  5. Tatizo ni kulundika madaraka makubwa mno kwa mtu mmoja aitwaye Rais. Karibia viongozi wote ni appointees wa Rais. Hii inasababisha kutokuwepo kwa uwajibikaji mtu aki-mess up kwani mwenye uwezo wa kum-fire huyo kiongozi ni Rais tu. Tatizo jingine ni kuwa uswahiba na urafiki unaplay part kubwa katika kupeana nyadhifa badala ya uwezo na ubunifu. Kwa mtindo huu tutaendelea kuchapa mguu wakati nchi zingine zinasonga mbele kwa kasi. Kuna haja ya kubadilisha mfumo tulio nao ili kuwe na vyombo vya kuweza kuwawajibisha viongozi wasio na tija badala ya kutegemea mtu mmoja tu!

    ReplyDelete