Saturday, January 08, 2011

TAMKO LA CUF KUHUSU MAANDAMANO YA CHADEMA ARUSHA

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)

VYOMBO VYA DOLA VINAHATARISHA AMANI YA NCHI.

CUF - Chama Cha Wananchi kimeumizwa sana na kitendo cha kinyama kilichofanywa na jeshi la polisi na serikali ya chama cha mapinduzi kuwapiga na kuwaumiza viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) na wananchi mbalimbali wapenda demokrasia na haki ndani ya nchi yetu waliokuwa wakiandamana kwa amani jijini Arusha jana tarehe 05 Januari 2011. Tunalaani vikali kukamatwa na kwenda kuhojiwa kwa Wabunge wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa Taifa Mhe. Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai , Mhe. Godbless Lema Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Joseph Selasini Mbunge wa Rombo na Mhe. Philemon Ndesamburo, Mbunge wa Moshi Mjini.

CUF inaamini kuwa CHADEMA kama chama cha siasa kilichosajiliwa kihalali ndani ya nchi yetu kilikuwa na haki ya kikatiba na kisheria ya kufanya maandamano yao ya amani ambayo mwanzoni tayari jeshi la polisi jijini Arusha kupitia kwa kamanda wa polisi wa mkoa lilishaahidi kutoa ulinzi wa kuyaweka maandamano hayo salama.

Jeshi la Polisi na Serikali ndiyo wanaostahili kulaumiwa kwa uvunjifu wa amani uliotokea Arusha. Ushahidi wa kimazingira unaonyesha wazi kuwa amri ya kusitisha maandamano iliyotolewa na IGP saa chache kabla hayajafanyika ilitokana na shinikizo za kisiasa. Hoja iliyotolewa kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonyesha kutakuwa na uvunjifu wa amani na ndiyo maana maandamano yanazuiliwa ni usanii mtupu. Kama kweli polisi wana taarifa za kiintelijensia kuwa kuna watu watavunja amani basi wazitumie taarifa hizo kuwadhibiti watu hao na siyo kuyasitisha maandamano na kuwanyima wananchi uhuru wa kisheria wa kufanya maandamano.

Nchi hii inapaswa kuongozwa na katiba na sheria na Watanzania tusikubali Serikali iliyoko madarakani kutumia vyombo vya dola kuua uhuru na demokrasia ya nchi yetu.

Hivi sasa jeshi la polisi limekuwa mstari wa mbele kuzuia kila aina ya madai yanayotolewa na vyama ili mwisho wa siku jeshi lifanye kazi yake kuu ya kulinda CCM na utawala wao kijeuri na kisanii. Haiwezekani kila watu wakitaka kuandamana jeshi la polisi lianzishe hoja ati “kwa sababu za ki-intelijensia” maandamano hayo yanafutwa. Hizi taarifa za ki-intelijensia ni zipi?

CUF inaamini kuwa polisi na serikali ya CCM wanataka kutumia kitisho cha ugaidi kilichozikumba Kenya na Uganda kama sababu ya kupinga mikusanyiko mikubwa ya kisiasa kwa lengo la kuitetea Serikali. Lazima tujiulize,hivi magaidi wakitaka kulipua Tanzania mbona kuna sehemu nyingi sana ambazo wanaweza kufanya hivyo bila kusubiri maandamano ya CHADEMA au CUF au vyama vingine?

Hivi tujiulize kama kweli pana tishio la ugaidi iweje mechi za mpira ziendelee bila kuzuiwa na polisi? Mikusanyiko yote inafanyika isipokuwa maandamano ya vyama vya siasa tu? Hawa magaidi walio tishio kwa jeshi la polisi wanaotaka kulipua maandamano peke yake wametokea wapi? Kwa nini nchi hii iendeshwe kisanii na kiujanja ujanja namna hii? Kwa nini serikali inaogopa maandamano?

CUF inalaani ukatili waliofanyiwa wakazi wa Arusha katika maandamano ya CHADEMA na kuwa ukatili huo hauvumiliki na unahatarisha amani na utulivu wa kweli wa nchi yetu.

Ukatili huu hauna tofauti na ule tuliofanyiwa CUF – Chama cha Wananchi tarehe 28/12/2010 ambapo maandamano ya amani yaliyokuwa yaongozwe na Kaimu naibu katibu mkuu Julius Mtatiro yalipigwa marufuku ghafla na kisha mamia na mamia ya polisi wakisheheni silaha za kila aina wakaanza kuwapiga na kuwakamata wafuasi wa CUF na wananchi wengine walioshiriki katika maandamano yale. Kitendo kile ambacho polisi walikifanya kimetia doa kubwa sana jeshi la polisi linaloongozwa na kiongozi tunayemheshimu IGP Said Mwema.

Kitendo hiki cha pili kilichofanyika Arusha kinazidi kuharibu kabisa sifa na uaminifu ambao vyama vya siasa vilikuwa nao juu ya IGP Mwema. Ni muhimu sana kwa taifa letu kwa IGP Said Mwema kulinda heshima yake na asikubali kutumiwa kisiasa kukandamiza demokrasia ndani ya nchi.

Chama cha wananchi CUF kinaamini kuwa ustawi wa demokrasia, utawala bora, usawa, maendeleo ya nchi yetu na amani ya nchi havitaletwa kwa mtutu wa bunduki wala mabomu wala kila aina ya nguvu, hata kama CCM wataendelea na mbinu zao za kuwadhibiti wapinzani hatutokaa kimya na wala hatutoacha kutumia fursa za kikatiba kutoa maoni yetu kwa njia ya amani kama walivyofanya CHADEMA tarehe 05/01/2011 na CUF tarehe 28/12/2011.

Tunaamini walichokuwa wakipigania CHADEMA jijini Arusha ni kitu cha msingi sana,walikuwa wakipinga kitendo cha kukiuka demokrasia katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha. CHADEMA hawakuwa na budi kutumia njia za kidemokrasia kuonyesha kutokukubali na kutotambua utaratibu huo wa kinyemela ulioendeshwa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kwa manufaa ya CCM.

CUF inawapa pole wahanga wote waliopigwa na kuumizwa na mabomu, risasi, maji ya kuwasha n.k katika tukio hilo la kihistoria la kudai haki ya wanyonge jijini Arusha. CUF iko pamoja nao katika kuendelea kupigania haki. CUF inawapa pole viongozi wote wa CHADEMA waliokamatwa katika maandamano ya Arusha na tunawataka waendelee na juhudi za kupigania ukombozi kama inavyofanya CUF.

CUF inamtaka Rais Jakaya kikwete kutumia busara za hali ya juu sana katika kuendesha nchi katika kipindi hiki ambacho anamalizia miaka yake mitano ya mwisho. Rais Kikwete ana fursa ya kujenga misingi imara ya demokrasia ili akitoka madarakani akumbukwe kwa mambo ya heri na siyo kwa mambo ya shari.

Kukaa kimya kwa Rais wakati polisi wanatumia nguvu kubwa kuua demokrasia ndani ya nchi kunaashiria kuwa wanatimiza amri ya Rais.

Pamoja na mambo yote hayo CUF inawataka Watanzania kuendelea kutuunga mkono ili tuweze kuendeleza mapambano ya kudai demokrasia na maendeleo ya kweli ya nchi yetu kama chama mbadala kitakachomkomboa Mtanzania.

Mwisho tunawataka wakazi wote wa Arusha, Dar es salaam na mikoa mingine wazidi kuungana na CUF na wadau wengine wote muhimu katika madai mazito ya kudai katiba mpya.

CUF inaamini suluhisho la sehemu kubwa ya ukatili unaofanywa sasa ni kukosekana kwa katiba mpya itakayotoa mwongozo sahihi wa taifa letu. Tofauti na sasa ambapo jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola vinaweza kufanya lolote wanalotaka juu ya maisha ya watanzania huku katiba ikiwalinda au wanaivunja na hakuna mwenye mamlaka ya kuwauliza.

Tanzania inahitaji Katiba Mpya ya Wananchi wenyewe na Tume Huru ya Uchaguzi. Tamko la Rais la kuunda Tume Maalum ya Katiba na ishara nzuri ukilinganisha na matamko ya awali ya Waziri wa Sheria na Katiba. Hata hivyo ni muhimu Rais akawafafanulia Watanzania kuwa lengo la mchakato mzima ni kupata Katiba Mpya yenye misingi imara ya demokrasia itakayotokana na ushiriki wa wadau wote. CUF inawaomba na kuwasisitiza Watanzania watuunge mkono sana ili tuhakikishe kwa pamoja tunapata katiba itakayoandikwa upya na kubeba matumaini ya Watanzania na siyo kuwekwa viraka kwa katiba iliyopo.

Imetolewa na

Prof Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti - CUF.
06 Januari 2011.
Dar es salaam.

2 comments:

  1. Yule naibu Meya ndugu Kivuyo wa Jiji la Arusha kupitia TLP ambaye uchaguzi uliompatia cheo hicho na unaoelezwa ndo ulowasukuma CDM kuandamana amejiuzuru muda si mrefu kwa anachoelezea kuwa ni sababu ya mauaji ya polisi mjini arusha.

    ReplyDelete
  2. Mary chitanda aliyepiga kura isivyostahili na Meya aliyepatikana kwa uchakachuaji ndio watakaodaiwa damu za watu waliouwa kudai haki

    ReplyDelete