Makombora
Thursday, 17 February 2011
Na Waandishi Wetu (Gazeti la Mwananchi)
JIJI la Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo limetaharuki kufuatia milipiko mikubwa ya mabomu iliyotokea ghala la kutunzia silaha la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Gongolamboto, huku kukiwa na taarifa za watu kufa na zaidi ya 100 kujeruhiwa. Timu ya waandishi wa Mwananchi waliotembelea eneo la tukio usiku wa jana, walishuhudua nyumba kadhaa zikiteketea kwa moto baada ya kuangukiwa na mabomu.
Kadhalika waandishi hao wa Mwananchi walishuhudia nyumba moja ambayo ukuta wake ulibomoka baada ya kuangukiwa na bomu na ukuta huo kuangukia kundi la zaidi ya watu 12, watu watano wanadaiwa kufa.
Mmoja wa walionusurika kwenye tukio la kuangukiwa na ukuta, Juma Nganyanga, alisema kuna uwezekano ya maiti wengine kuwa chini ya ukuta huo.
Nganyanga alisema aliona kundi la watu wakiwa wamekimbilia kupumzika kwenye baraza la nyumba hiyo baada ya kukimbia nyumba zao, wakati wakiwa katika maombi ya kuomba Mungu awaepueshe na janga hilo, ghafla aliona vumbi likitimka kwenye nyumba hiyo.
Mwenye nyumba hiyo, Farida Magwa, ambaye alikuwa akibubujikwa na machozi alisema akiwa barabarani na familia yake, aliambiwa kuwa nyumba yake imepigwa bomu na kuna watu wameuawa.
Magwa alisema baadaye waliweza kutoa maiti za watu watano, wakiwamo watoto wawili, lakini kuna uwezekano wa wengine bado wapo wamefunikwa na kifusi cha ukuta huo.
Katika tukio jingine, Mwananchi ilishuhudia maiti ya mwanamke ikiwa kwenye nyumba ambayo imeteketea baada ya kupigwa na bomu eneo la Mzambarauni na maiti nyingine ikipandishwa kwenye gari eneo la gereza la Ukonga.
Pia, Mwananchi lilishuhudia jengo la hosteli ya Kanisa Katoliki Ukonga likiwa linateketea kwa moto baada ya kuangukiwa na bomu, huku wakazi wa hosteli hiyo wakiwa wamekimbia.
Moto huo ambao ulikuwa ukiendelea kuwaka hapakuwapo na jitihada zozote za kuweza kuuzima, kwani watu wote walikuwa wamekimbia.
Mlinzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Tanzania (KKKT) lililopo jirani na hosteli hiyo, alisema alishuhudia mabomu mawili yakitua eneo hilo, moja likitua kwenye nyumba ya hosteli hiyo na lingine pembeni karibu na gereza la Ukonga.
Milipuko hiyo ilianza majira ya saa 2.00 usiku na kuendelea mfululizo hadi saa 6.00 usiku, huku watu wakitaharuki na baadhi ya wanandungu na familia kupotezana.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadiq, alithibitisha kutokea kwa kifo cha mtu huyo ambaye hata hivyo jina lake lilikuwa halijafahamika.
Katika Hospitali ya Amana, Ofisa Mwandamizi wa Wagonjwa wa Nje, Mussa Wambura, alisema watu wawili walifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo na kwamba, hadi saa 7:00 usiku walikuwa wamepokea majeruhi 88, wengine hali zao zikiwa mbaya.
Waandishi wa Mwananchi walishuhudia magodoro yakiwa yametandikwa nje ambako wagonjwa walikuwa wamelazwa na wahudumu wa afya kutoka hospitali za TMJ na Hindu Mandal walipelekwa Amana kuongeza nguvu.
Pia, Sadiq alithibitisha kujeruhiwa kwa watu 43 na kwamba, serikali ya mkoa ilikuwa imetenga hospitali mbili za Ilala (Amana) na Temeke kwa ajili ya kupokea majeruhi na kuwatibu.
Awali, taarifa za zisizo rasmi zilizolifikia Mwananchi zilidai kuwa, mabomu yaliyolipuka ni ya masafa marefu.
Taarifa hizo zilithibitshwa na Sadiq ambaye aliwanukuu JWTZ wakisema, mabomu yaliyolipuka yanaweza kwenda umbali wa kilomita 11 kutoka eneo la tukio, Gongolamboto.
Alisema kwa mujibu wa taarifa hizo, wananchi walipaswa kuondoka eneo hilo na kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kwamba, wangekuwa salama baada ya kufika eneo la Tazara wakati kwa wale walioelekea Kisarawe alipaswa kwenda hadi eneo la Pugu Kajiungeni.
Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, alinukuliwa akiwataka wakazi wa Gongolamboto na maeneo ya jirani kuhama makazi yao kutokana na milipuko hiyo.
Kadhalika Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alinukuliwa akiwataka wakazi wa maeneo hayo kuondoka kuepusha athari zinazotokana na milipuko hiyo.
Wananchi wakimbia makazi
Habari zaidi zilisema mamia ya wananchi waliyakimbia makazi yao, wengi wakielekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lakini baadaye matangazo yaliyotolewa na vyombo vya usalama yaliwataka kwenda Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kupata hifadhi ya muda.
Kwa mujibu wa mashuhuda, watu walikuwa wakikimbia ovyo huku wakipanda magari yaliyokuwa yakielekea katikati ya jiji, kusalimisha maisha yao.
Baadhi ya wananchi waliolazimika kuyakimbia makazi yao, walikuwa wakipiga simu chumba cha habari wakilalamikia kupotezana na ndugu zao.
Mamia ya watu kutoka Gongolamboto, Karakata, Tabata, Segerea, Ukonga, Kitunda, Banana na maeneo mengine jirani, walionekana wakipanda daladala, wengine wakining'inia nyuma ya magari hayo yaliyokuwa yakielekea katikati ya jiji, huku mamia kwa mamia ya watu walikuwa wakitembea kwa miguu kuokoa maisha yao.
Kadhalika pikipiki, bajaj na magari ya kama pick-up pia yalitumika kuwahamisha watu kutoka eneo la tukio kwenda kutafuta sehemu ya hifadhi ya muda.
Uwanja wa ndege wafungwa
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, ulifungwa kwa muda na ndege zote hazikuruhusiwi kuruka wala kutua hadi hapo itakapoarifiwa baadaye.
Waandishi wa Mwananchi walishuhudia abiria wengi wa kigeni wakiwa kwenye uwanja wa huo wakisubiri kujua hatma ya safari zao, baada ya ndege walizokuwa wakizisubiri kuamriwa kutua viwanja vya Kia na Zanzibar hadi hapo watakapopewa maelekezo mengine.
Barabara ya Pugu katika njiapanda inayoingia kambi ya jeshi, ilifungwa na magari yote yaliyokuwa yakielekea katikati ya jiji na yale yaliyokuwa yakielekea Kisarawe yalizuiwa.
Mkazi mmoja wa Kigamboni aliyepiga simu ofisi za gazeti hili jana usiku wakati milipuko ya mabomu hayo ikiendelea, alisema wakazi wengi wa Kigamboni walikuwa nje ya nyumba zao, huku wakishuhudia makombora yaliruka juu kuelekea baharini hali ambayo iliwafanya wakazi hao kukumbwa na wasiwasi mkubwa.
"Hivi ninapokupigia wewe, makombora yanapita juu na kila mtu na familia yake wako nje kwa hofu...unasikia muungurumo huu kombora jingine linapita hapa juu kuelekea baharini," alisikika mwananchi huyo.
Kauli ya Dk Mwinyi
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi, alisema milipuko hiyo ilitokea ghala namba tano na kwamba, kilichokuwa kikifanyika ni kuzuia usienee sehemu nyingine.
Dk Mwinyi alisema kambi ya Gongo la Mboto wanaishi wanajeshi na familia zao, lakini maghala ya mabomu yako mbali na kuongeza kuwa, kutokana na milipuko hiyo kuwa mikubwa hawezi kuzungumzia athari.
“Ile ni kambi ya jeshi, watu wanakaa mbali na maghala lakini kwa sababu tukio lenyewe ni kubwa sasa hivi hatuwezi kusema lolote,” alisema Dk Mwinyi.
Wakati mabomu hayo yakiendelea kulipuka mwananchi mmoja alipiga simu chumba cha habari cha Mwannchi, akisema Waziri Mwinyi yalipolipuka mabomu ya Mbagala, aliahidi kujiuzulu iwapo ingebainika kulifanyika uzembe.
Hata hivyo, Dk Mwinyi alipoulizwa usiku wa kuamkia leo kuhusu utekelezaji wa ahadi yake hiyo na majibu ya tume zinazoundwa, alisema kilichokuwa kinafanyika usiku ni kuokoa maisha ya watu, masuala mengine yatazungumzwa baadaye.
“Sasa hivi kuna jambo linaathiri watu, kwanza tuwaokoe halafu haya mengine tutazungumza,” alisema Dk Mwinyi.
Milipuko ya kwanza ilitokea barabarani mwaka 1972 wakati mabomu hayo yalipokuwa yanahamishwa kutoka Kambi ya Kunduchi kwenda Gongolamboto.
Kwenye kambi hiyo ni mara ya pili kutokea kwa milipuko ya mabomu, milipuko ya kwanza ilitokea mwaka 2008 na kusababisha maafa kwa wananchi wanaozunguka kambi hiyo, wanajeshi na familia zao.
Kila mwaka wataalam wa mabomu jeshini ambao hujulikana kama Ammo tech, wanaofanya kazi chini ya Chief Logistic and Equipment (CLE) hukagua mabomu ambayo muda wake umemalizika ili yaweze kupelekwa Kimbiji kuteketezwa.
Mbagala
Hali ilikuwa tete maeneo ya Mbagala na kusababisha watu wakiwa na watoto kukimbia ovyo, huku wengine wakijikusanya pembeni mwa barabara.
Wakazi wa Mbagala ambao walikumbwa na milipuko kama hiyo Aprili 2009, walionekana kuchukua tahadhari mapema baada kuanza kusikia milipuko kwa kuondoka ndani ya nyumba zao.
Mwananchi ilishuhudia wananchi hao wakiwa wamekusanyika pembeni mwa barabara ya Mbagala Rangi tatu-Mbande, hasa eneo la Muhimbili wanakopelekwa wagonjwa wa akili baada ya kupata nafuu, ambako kuna nafasi kubwa.
Maeneo ya Chamazi, Mbande, Charambe na Mbagala Rangi tatu, nyumba zilikuwa zikitikisika kutokana na milipuko hiyo, huku angani kukiwa kumetanda miale ya moto.
Mwandishi wa gazeti hili, Midraji Ibrahim, alisema kwenye nyumba yake iliyopo Chamazi, mikanda ya dari (ceiling board) ilidondoka kutokana na kishindo cha milipuko ya mabomu hayo.
Mlipuko wa 2008
Mwaka 2008 kulitokea mlipuko ghala la silaha kwenye kambi hiyo ya jeshi la Gongo la Mboto katika tukio ambalo vyombo vya usalama vilidai kuwa ulitokana na silaha hizo kupata joto kali.
Imeandaliwa na Julius Magodi, Neville Meena, Midraji Ibrahim na Andrew Msechu (Mwananchi)
Nafikiri huu ndio wakati mwinyi kujiuzulu. Wakati wa mbagala
ReplyDeletealipotakiwa kujiuzulu aliruka na kusema kikubwa ni kuhakikisha hali
hiyo hairudi tena sasa imerudi akae pembeni. Jeshi la kutisha watu wa
upinzani huku likishindwa kudhibiti siraha zake halifai. Kama livyo la
polisi hili nalo linastahili kufumuliwa na kusukwa upya. Shimbo na
mwamunyange nao waachie ngazi
Rafiki yangu anayeishi maeneo ya Kipunguni jirani na Gongo la Mboto. Juzi alipata Mgeni wa dharura anayeitwa Kombora. Rafiki yangu huyo ana Nyumba mbili, Moja ya dhamani na moja
ReplyDeletempya ambayo haijahamiwa. Nyumba zote ziko kwenye kiwanja kimoja, Na zimekaribiana.
Bomu lilingia moja ya chumba hicho kwa kutoboa Nyumba na kuingia ndani.
Bomu hilo halikuleta madhara ya kujeruhi kwakuwa tayari watu wote walisha kimbia na kuondoka kwenye eneo hilo.
Leo asubuhi nilikutana na Rafiki yangu huyo akimtafuta Mtoto wake wa Mwisho aliyepotea siku ya Mlipuko wa Mabomu. Bado Bomu hali jaondolewa pamaja na kuripoti kwenye vyombo vya Usalama.
Rafiki yangu huyo anaitwa SHEHE MNYANI Simu no 0754942993 Hata hivyo amepewa maelekezo kuwa wasiwashe moto jirani na kwenye Bomu hilo.
Jamani maafa mengine hayo, Likilipuka itakuwaje? Ni wazi kuwa Rafiki yangu atakufa na familia yake na Nyumba zote mbili kuteketea. Hivi hawa wanajeshi wanasubiri nini hawaendi kulichukua.
Rafiki yangu bado na mahitaji.
Ndugu yangu Joyce Che-Mponda wa Gongo la Mboto alipotelewa na mtoto wake mdogo katika mkasa huo. Nimepata taarifa kuwa mtoto amepatikana sasa. Nitawapa details mara nikimpata kwenye simu.
ReplyDelete