Wednesday, October 26, 2011

Gaddafi Aliwatendea WaTanzania Mabaya - Vita Vya Kagera


Inaelekea waTanzania wengi wamesahau historia kati ya Libya na Tanzania. Marehemu Gaddafi alikuwa rafiki yake mpenzi nduli mshenzi Dikteta Idi Amin Dada wa Uganda!  Gaddafi alitaka Amin amwoe binti yake! Gaddafi alituma wanajeshi kutoka Libya kuwasaidia Uganda katika vita vya Kagera mwaka 1978-79.  Sisi wazee tunaukumbuka huo vita na miezi kumi na nane (miaka 18) ya shida iliyofuata!  Maoni chini yameandikwa na mwanachama la kundi - Wanabidii
Gaddafi alipotembela Uganda mwaka 1973
 ...Wanabidii!


Binafsi nachukia sana kuandika bila ya ushahidi! Na zaidi sipendi kuandika "propaganda" na taarifa za uzushi; isipokuwa napenda kuandika taarifa zilizotafitiwa kwa kuandikwa na mtafiti mwenyewe (na au mwandishi aliyeandika matokeo ya utafiti au kufanya upembuzi wa utafiti husika). Takriban wiki moja sasa (tangu Alkhamis ya tarehe 20 Oktoba, 2011) uwanja wa "Wanabidii" na majukwaa mengine ya kijamii yamekuwa yakijadili "Kuuawa kwa Kanali Muammar Gaddafi" kulikofanywa na wale wanaoitwa waasi (wa NTC) wakisaidiwa na NATO wakiongozwa na Uingereza, Marekani, Ufaranza na washirika pamoja na Waarabu (Saudia na Qatar). Gaddafi ameuawa; kwa jinsi gani, kila mmoja amesoma, ameona (kwenye picha za mnato) na au kwenye picha za video!

Ninachotaka kuandika na pengine kuanzisha "mjadala" wa kiakili ni juu ya "GADDAFI KUMSAIDIA IDI AMIN DADA KWENYE VITA VYA KAGERA [UGANDA DHIDI YA TANZANIA MWAKA 1978 HADI 1979]". Napenda niweke wazi kwamba, "historia haisomwi ili kufufa 'chuki' bali husomwa kujua yaliyopita, kuyasanifu yaliyopo na kupanga mipango kwa yajayo!". Hivi ndivyo tunavyosoma historia iwe yenye kuhuzunisha au kufurahisha! Tanzania ilipigana vita na Uganda, vita iliyoitwa VITA YA KAGERA (japokuwa ilipiganwa hata ndani ya Uganda na Idi Amini Dada kufurushwa na kuikimbia Ugnda!).

Kwa ujumla, tangu pale kifo cha Muammar Gaddafi kilipotangazwa kwa mara ya kwanza na kituo cha runinga cha Al-Jazeera na kukaririwa na vituo vingine na mashirika ya habari ya kimataifa kama BBC, CNN, Reuters, Xinhua, AFP, AP na IRNA (Press Tv) kumekuwa na mchanganyiko wa "mawazo" kwa wananchi wa Tanzania juu ya "hali" ya Gaddafi kisiasa katika mtazamo wa kifalsafa...hususan wengi wa wachangiaji kwenye mijadala hiyo wanamuona Muammar Gaddafi kama "shujaa" na "mwanamapinduzi" na "kiongozi mtukuka" na "aliyejitolea kuunganisha Afrika" na hata wengine kufikia kiasi cha kuonyesha kwamba hajawahi kutokea kama Muammar Gaddafi na hata kumpa "daraja" ya kuwa "Baba wa Afrika" na mshumaa uliyozimika! Hata hivyo wengi wamesahau kamba ni Muammar Gaddafi ndiye aliyemsaidia Idi Amin Dada kwenye Vita vya Kagera! Naomba sasa tuangalie nini alifanya Gaddafi wakati wa vita vile.

Vita vinahitaji rasilimali watu (askari na wataalamu wa kijeshi), fedha za kuendeshea vita na zana (za kivita na za mawasiliano ya kivita). Kwa mujibu wa taarifa rasmi na zinazothibitishwa na taarifa rasmi za kihistoria Muammar Gadafi alimpa Idi Amin Dada usaidizi ufuatao:

1. WANAJESHI (WAPIGANAJI) 3,000 (Elfu tatu kutoka Libya na nchi zilizokuwa na mahusiano na Libya ambazo Gaddafi likuwa anazisaida na zenye uzowefu wa mazingira ya vita [military knowhow and skills on interlocustrine terrain]);

2. ZANA KAMA VIFARU AINA YA T-54, T-55, BTR, APCs, BM-21, Katyusha MRLs;

3. MIZINGA; na

4. NDEGE ZA KIJESHI AINA YA MiG-21s na Tu-22 Bomber.

Wanajeshi wa Libya waliyotumwa Uganda walikuwa katika makundi yafuatayo: ASKARI WA KAWAIDA; WANAMGAMBO; NA ASKARI WA VITA VYA MSITUNI (WENYE UZOWEFU WA VITA VYA KIENYEKI KUTOKA JANGWA LA SAHARA [MAARUFU KAMA WATUAREG KUTOKA TCHAD, NIGER, ALJERIA NA DARFUR]). Hata hivyo, shukrani za pekee kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) waliyefanyakazi ya ziada ya kujitoa mhanga kupigana "kiume" na hatimaye kuyashinda majeshi ya Idi Amin Dada akisaidiwa na Muammar Gaddafi. Hata ilipofika mwezi wa Aprili, 1979 na Idi Amin Dada alipopoteza udhibiti wa nchi ya Uganda aliamua "kuikimbia" Uganda na kituo chake cha kwanza kilikuwa Libya (kwa Muamar Gaddafi) na alipewa "hifadhi" ya muda na baadaye kwenda "uhamishoni" nchini Saudi Arabia (alikoishi hadi kufa kwake akiwa Jeddah).

Kwa wasomaji na "wanabidii" na wengine wanaomtazama Muammar Gaddafi kwa kusahau "aliyoyafanya" dhidi ya kumsaidia Idi Amin Dada kuendesha vita na Tanzania nadhani wana wajibu wa kujiuliza masuala haya (hii ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inawajibu wa kusema ukweli):

1. Wamesahau "hadithi" hii ya Vita vya Kagera? Au, vita hivi vilikuwa "propaganda" ya kisiasa?

2. Gaddafi alidhamiria nini kumsaidia Idi Amin Dada aliyeapa kuisambaratisha nchi (Tanzania) na kwa kuanzia aliteka Kagera na kuifanya sehemu ya Uganda?

3. Kama Idi Amin Dada wa Uganda alitangazwa "dikteta", "bundi", "joka", "fisi mla watu", na masimulizi mengine ya kutisha (hata ya kula nyama za watu); mtu aliyekuwa akimsaidia mtu wa aina hiyo (kama Gaddafi) anaitwaje?

4. Je, historia ya Vita vya Kagera iliandikwa kwa wino "gani" hadi leo imesahaulika?

5. Au, wote wanaodhani kwamba Muammar Gaddafi ni "shujaa" wa Afrika wamezaliwa miaka ya 1980? Na kwa jinsi hiyo hawajui kilichotokea kati ya miaka ya 1978 na 1979?

Mwisho, siandiki haya katika kuwakumbusha "majonzi" wananchi wa Kagera waliyeuawa kikatili na Idi Amin Dada; siwakumbushi machungu ya kutiwa vilema vya maisha; siwakumbushi madhila ya "kubakwa" wanawake kulikofanywa na askari wa Idi Amin Dada; na wala siwakumbushi jinsi mali zao (mashamba na nyumba) zilizvyoharibiwa na "ushenzi" wa Idi Amin Dada! Nataka niwakumbushe kwamba, "hatuwezi kurudisha nyuma historia; lakini ni wajibu kuisoma ili vizazi vijavyo vipate kumbukizi yenye kujenga mujtamaa wao." Gaddafi alikuwa "rafiki" na wakati huohuo alikuwa "adui" kwa vile alikuwa na "sura mbili ndani ya moja".

Na kwa serikali (iliyoonekana kumuunga mkono); hii ni dhana (binafsi) inawezekana Muammar Gaddafi alilipa sehemu ya "maumivu" ya vita alivyomsaidia rafiki yake mpenzi Idi Amin Dada...kama ndivyo, basi ni vema watuambie! Hatuwezi kusomeshwa historia ya "uongo" juu ya Muammar Gaddafi kumbe "mtu" huyu (yaani Gaddafi) alikuwa "mtu mwema" na kiongozi "mzuri" kuliko hata Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere...naomba tuwe "wakweli" na kwa kusisitiza: UKWELI UTATUWEKA HURU; KAMA GADDAFI ALIKUWA RAFIKI WA AFRIKA KWA NINI ALIMSAIDIA IDI AMIN DADA KUTUPIGA? TAFAKARI SEMA UKWELI JAPOKUWA UKWELI WENYEWE NI DHIDI YA NAFSI YAKO!

Bakari M Mohamed, BBA[PLM], CPSP[T], MSc (PSCM)

12 comments:

  1. Ni kweli lakini pia ni lazima ujiulize pia ni kwa nini Nyerere aliunga mkono nia ya kujitenga ya Biafra mwaka 1967? Na kuvunja uhusiano na nchi ya Naijeria?

    Ukiweza kujibu maswali hayo. Na hili litajibiwa. Ukweli ni kwamba baadaye Ghaddafi alikuja kukiri na kuomba radhi na hata hotuba za baadaye za Mwalimu zinaeleza wazi kwamba Gaddafi hakujua kilichokuwa kikiendelea Afrika Mashariki wakati ule na alipotoshwa na Idd Amin. Suala la kusema kwamba Gaddafi alimsaidia Amin katika vita ni propaganda tu. Kwa taarifa yako Iddi Amin alikuwa ana support pia ya Uingereza.

    Na Tanzania tulikuwa tunasaidiwa na Marafiki zetu wa Jamhuri ya Watu wa Uchina. Kama historia ingekuwa inatufundisha kujenga uadui, basi tungekuwa maadui dhidi ya Waarabu waliotufanya Watumwa, Maadui dhidi ya Wazungu waliotunyonya na wanaozidi kutunyonya kila kukicha Ama nchi ya Angola iwe na uadui na nchi za Marekani na mataifa mengine mfano Zaire na Afrika Kusini jinsi zilivyoshiriki kumsaidia Savimbi na UNITA kuendeleza mauaji yake. Ama hayo huyajui?. Tuache Propaganda tuangalie ukweli uko wapi. Katika hili bara la Afrika hakutatokea kiongozi kama GHADDAFFI. Hawa waliobakia wote ni vibaraka ukimwacha Mugabe ambaye anapata misukosuko.

    Ni kweli Gaddafi alimsaidia Idd Amin. Lakini ni kweli pia Gaddafi amefanya mambo mengi katika kuisaidia Tanzania na Afrika kwa ujumla. Wengi wanadhania alijenga msikiti wa Dodoma pekee. Kawaulizeni viongozi wenu wa serikali wawaambieni. Njaa zetu za kufuata propaganda za Kimagharibi zitatuua.

    ReplyDelete
  2. at least there are some tanzanian folks who cannot be blindly dragged on a false bandwagon of praising a lunatic who manipulated his way into a long-serving leader of such otherwise blessed country, libya. may be it's because most of us were either innocent infants or not yet born to see the atrocities and aftermath of the kagera war (1978-79). we see gaddafi of today in his diabolic regalia handing out bribes to other african despots in the name of aids. we really have been foolishly blindfolded by the aids and the so-called devedlopment projects that came our way as a price of the innocent blood of our fathers and mothers who fought galantly against the invasion of the in-law of gaddafi, another lunatic called idd amin.

    it's better to die standing than to live begging from gaddafi. his money is bloody money no matter what!

    poor beggars we are!!

    ReplyDelete
  3. Tanzania tumepumbazwa. Mtu au nchi ikitoa msaada tunamwona Mungu! Bora turejee siasa za Mwalimu za KUJITEGEMEA! Tumekuwa wajinga, kila kitu mpaka mfadhili. DISGUSTING!

    ReplyDelete
  4. Na wewe mwaipopo ukitaka kumjua lunatic, lunatic hawezi kuwasilisha hoja kwa lugha yake mwenyewe.

    Kuhusu kujitegemea, hivi enzi ya mwalimu kumbe tulikuwa tunajitegemea? Mahindi ya njano yalikuwa yanatoka wapi? katerero? au mwakareli? vikombe vya udongo vilikuwa siyo "maden china"?

    ReplyDelete
  5. Kwa hivyo kama katutendea mabaya tufanye nini??? Usishadidie vitu ambavyo havina manufaa kwetu!!

    ReplyDelete
  6. Nyerere alianzisha Vita vya kagera hadi Uganda ili kumrudisha rafiki yake Obote madarakani kwa damu za wabongo ambao hata familia zao hazkulipwa fidia,na hatima Obote akarudi na kuchinja Waganda kushinda hata Amin,hadi Museveni alipo mtimua.Kwahiyo Gaddafi alikuwa na haki ya kumsaidia rafiki yake Amin.

    ReplyDelete
  7. Chemi.....waswahili hawakukosea.....ukipenda chongo utaita Kengeza!.......! Kwa hiyo kama Amini alikuwa na support ya Waingereza....kuna ubaya gani Gaddafi akamsaidia Amini kuwaua Watanzania.......? Nadhani utasikia mengi hapa.....hata Amini hakuwahi kuwa Dikteta.....ni propaganda za Magharibi.......inawazekana kabisa....hata akina Mobutu.....Bokassa.......!Chemi umeishaambiwa Gaddafi kafanyia mengi Afrika......kwani huoni msikiti pale Dodoma? Huoni Msikiti Kampala......!Chemi huyu alikuwa Mwanapinduzi.....!!Hivyo usijaribu kuufuta ukweli huu na hizo "data" za zako za Kiihistoria.....kwanza hatuna hakika kama hata vita vya Kagera vilikuwepo.....inawezekana kabisa ni Propaganda za Nyerere kumpaka matope mwanamapinduzi huyu shujaa wa Afrika.....!

    ReplyDelete
  8. Duh! huyu mgalatia wa October 29, 2011 7:39 PM na chuki yake dhidi ya uislamu mpaka inachekesha.
    Na waziri mkuu wa uingereza, David Cameron keshasema kwamba anataka muwe wasenge. Na mtakuwa tuu, kwa sababu wazungu wakisema jambo nyinyi lazima mtafuata tuu.
    Nenda kaangalie tena sinema ya "rise and fall" ya Idi Amin. Inapatikana kwenye youtube pia. Kisha utajua kwamba propaganda ipo kweli na inafanya kazi. Au kama wewe "umesoma sana" basi amini kwamba Amini ndivyo alivyokuwa vile.

    ReplyDelete
  9. Nimekuwekea kipande kidogo tuu hapa cha "rise and fall"

    http://www.youtube.com/watch?v=qCGwqR3SU1o

    Kama una akili utaona kwamba propaganda na islamophobia vipo kweli na havikuanza leo.

    ReplyDelete
  10. "Nyerere alianzisha Vita vya kagera hadi Uganda ili kumrudisha rafiki yake Obote madarakani kwa damu za wabongo ambao hata familia zao hazkulipwa fidia,na hatima Obote akarudi na kuchinja Waganda kushinda hata Amin,hadi Museveni alipo mtimua.Kwahiyo Gaddafi alikuwa na haki ya kumsaidia rafiki yake Amin."...UKWELI NDIYO HUO WENGI TULIPUMBAZWA BILA KUJUA NINI HASA KIINI CHA VITA VYA KAGERA,JIULIZE JUMUIA YA KIMATAIFA KWA NINI ILISHINDWA KUMKEMEA AMIN ALIPOIVAMIA TANZANIA?LAKINI KWA KUSAIDIWA NA MTANDAO HEBU GOOGLE MOJA YA DOCUMENTARY MPYA ZA NDULI AMIN UONE JINSI JESHI LA UGANDA LILIVYOKUWA LIKIKAMATA SILAHA KUTOKA KWA ASKARI WAASI KUTOKEA PANDE ZA TZ!ULIKUWA NI MPANGO WA KUMRUDISHA OBOTE MADARAKANI ULIOPELEKEA AMIN KUTUSUMBUA NA KUUA NDUGU ZETU KAGERA NA MWANZA!NDIPO TUKATANGAZA VITA,HISTORIA INAANZIA AMIN KUTUVAMIA KITU AMBACHO SI KWELI,NI SAWA NA HISTORIA YA AFRIKA KUANDIKWA NA MZUNGU LAZIMA AJISIFU KUWA YEYE NDIYO KAVUMBUA KILA KITU AFRIKA WAKATI WENYEJI HAWATAJWI!

    ReplyDelete
  11. KAMA TULIWASAIDIA WAGANDA KUMNG'OA AMIN, KWANINI WAGANDA WANACHUKIA LUGHA YA KISWAHILI?

    ReplyDelete
  12. Idd Amin tunawaachia waisilamu Kwa waislamu Idd Amin alikuwa mtu mzuri tu. Mwalimu Nyerere ndio amekuwa mbaya wao.

    Kweli watu wasiosoma hawana uwezo wa kufikiri kabisa.

    ReplyDelete