Sunday, April 29, 2012

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU SHUTUMA DHIDI YA WAZIRI WA FEDHA YA KUHUSIKA NA UUZAJI WA KIWANJA CHA NHC NA. 10 BILA KUZINGATIA TARATIBU

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU SHUTUMA DHIDI YA
WAZIRI WA FEDHA YA KUHUSIKA NA UUZAJI WA KIWANJA CHA
NHC NA. 10 BILA KUZINGATIA TARATIBU

UTANGULIZI

1.0            Wakati PSRC ilipokuwa chini ya Wizara ya Mipango na
Ubinafsishaji, mwaka 2002 iliuza kiwanja Na. 192 kwa Mohamed
Enterprise (T) Limited (METL) na mwaka 2003 ikauza kiwanja Na. 191 kwa
Dar es Salaam RTC. Viwanja hivyo viliuzwa kabla ya PSRC kuvunjwa
tarehe 31 Desemba, 2007 na shughuli zake kukabidhiwa CHC tarehe 1
Januari, 2008, ambapo ndiyo shughuli za CHC zilihamishiwa Wizara ya
Fedha.

Kiwanja Na. 192 (au Na. 11 kwa sasa), cha GAPEX (iliyovunjwa na baadhi
ya mali zake kukabidhiwa PSRC) na kiwanja Na. 191 cha Dar es Salaam
RTC, vilikuwa katika eneo moja vikitumia barabara moja kuingia kwa
kupitia ndani ya kiwanja Na. 191 kutokea barabara ya Nyerere (Pugu
Road).  Hata hivyo, PSRC waliuza viwanja hivyo bila kwanza kutoa njia
(access road) kuingia kiwanja Na. 192.

2.0            Dar es salaam RTC walianza kupatiwa hati ya kiwanja
Na. 191, hivyo kukawa na mgogoro wa muda mrefu kwa sababu METL
hakuweza kupatiwa hati na Manispaa ya Temeke bila ya kuwa na njia.
Vile vile Dar es Salaam RTC kutokana na kero ya magari makubwa ya
METL, walikataa yasiendelee kupita katika kiwanja chao bila malipo.
Malipo ya madai ya Sh. 2.34bn ya barabara yanayodaiwa na Dar es Salaam
RTC hayakuwahi kulipwa na Serikali hadi sasa.

3.0            Kwa misingi hiyo PSRC ilitakiwa kutoa access road kwa
METL. Kamati ya Serikali chini ya CHC ilitafakari suala hilo nakuona
kwamba, kiwanja Na. 10 ambacho kiliwekwa chini ya PSRC kupitia mali za
TANGOLD iliyokuwa kampuni tanzu ya NMC, kingeweza kutumiwa kutatua
tatizo hilo. Kiwanja Na. 10 kilikuwa kimepangishwa kwa M/s Noble
Azania Investment Ltd (NAIL) na aliweka pingamizi asinyang’anywe na
PSRC.  METL alikubali kwamba endapo atapewa kiwanja hicho ili apate
barabara atachukua na kesi na madai ya NAIL.

4.0            Katika Mkutano wake wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, masuala kadhaa yalijitokeza na kujadiliwa.
Aidha, katika majadiliano hayo baadhi ya waheshimiwa wabunge
walichangia hoja za POAC na PAC kwa kumshutumu Mhe Waziri wa Fedha.
Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakichangia hoja walisema kuwa, baadhi
ya Mawaziri ni wezi na kuwa wanatafuna fedha za Watanzania bila ya
woga, na kuwa Mhe. Waziri wa Fedha ameuza viwanja vya CHC. Aidha,
walidai kuwa, alihusika katika uuzaji wa mali ya Serikali katika
kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere na kwamba ameingilia utendaji wa
Mashirika ya Serikali ikiwamo CHC.

5.0            Tungependa kutoa ufafanuzi kuhusu hoja hizo kama
ifuatavyo:- Kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere hakikuuzwa na Wizara ya
Fedha, wala na Waziri wa Fedha. Kiwanja hicho kiliuzwa na aliyekuwa
Mwenyekiti na Kaimu Mkurugenzi wa CHC kinyume na maelekezo ya Wizara
ya Fedha na Kamati ya Wataalam (DTT), kwamba kiwanja hicho kiuzwe kwa
bei ya soko kwa kuzingatia Sheria na Taratibu.

6.0            Ukweli upo kwamba, baada ya maelekezo ya Wizara ya
Fedha kwamba bei ya soko na taratibu na sheria zitumike, Kamati ya
Wataalamu wa Serikali, ilikaa na kushauri kwamba taratibu na sheria ni
kutangaza ili kupata bei ya soko.

7.0            Bodi ya CHC ilikaa na kujadili maelekezo ya Wizara ya
Fedha na ushauri wa Kamati ya Wataalam. Baadhi ya Wajumbe wa Bodi
walishindwa kuelewa maana ya taratibu na sheria na bei ya soko, hivyo
Bodi iliagiza Waziri wa Fedha aombwe ufafanuzi. Mwenyekiti na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa CHC walitumwa na Bodi wamwone Waziri wa Fedha ili
warudishe majibu kwenye Bodi. Waziri wa Fedha alitoa maelezo kwao
kwamba, tayari alishatoa maelekezo kwa maandishi hivyo waendelee kwa
kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.

8.0            Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa CHC hawakurudi kwenye Bodi baada ya kupata ufafanuzi kutoka kwa
Waziri wa Fedha, bali waliamua kuuza kiwanja hicho kwa bei ya
Mtathmini, badala ya kutangaza na kupata bei ya soko kama
walivyoelekezwa na Wizara ya Fedha na Kamati ya Wataalam. Aidha,
hawakurudi kwa Wizara ya Fedha kutoa taarifa ya utekelezaji wa
maelekezo ya Wizara.

9.0            Aidha ni vyema ijulikane kwamba, ukaguzi maalumu
uliofanywa huko CHC na Mkaguzi wa Nje, wakati wote wa ukaguzi Wizara
ya Fedha haikuhusishwa kutoa ufafanuzi au taarifa yoyote.

10.0        Tuhuma kuhusu kwamba, Wizara ya Fedha ilihusika katika
uuzwaji wa kiwanja hicho kwa kutoa maagizo kwa uongozi wa Shirika
kuuza kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere bila kuishirikisha Bodi ya
Wakurugenzi, hazina ukweli.

11.0        Hakuna maagizo yoyote ya Wizara ya Fedha yanayosema kuwa,
kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere kiuzwe kwa kampuni ya METL kwa
kiasi cha shilingi bilioni 2.46 bila kuzingatia sheria ya Manunuzi ya
mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2006.

12.0        Kwa kuzingatia maelekezo ya Waziri wa Fedha ni dhahiri
kuwa, Mhe. Waziri wa Fedha, hakuhusika na uuzaji wa kiwanja Na. 10
barabara ya Nyerere na wala hakuingilia utendaji wa CHC. Maelekezo
aliyotoa yaliitaka CHC ifanye maamuzi kwa kufuata sheria, taratibu na
kanuni.

Badala yake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa CHC waliamua kuuza kiwanja hicho bila kuzingatia ushauri wa
Kamati ya Wataalam (DTT) na maelekezo ya Wizara ya Fedha.

13.0        Kwa misingi hiyo, tuhuma kwamba, Mhe. Waziri wa Fedha
alihusika na uuzaji wa kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere sio za
ukweli.


KATIBU MKUU
WIZARA YA FEDHA
APRILI, 2012

No comments:

Post a Comment