Wednesday, April 04, 2012

Waliopata 'Kikombe cha Babu' Wafariki Dunia - Habari Leo

Mgonjwa wa  UKIMWI
Waliopata ‘Kikombe cha Babu’ Wafariki Dunia
Imeandikwa na Waandishi Wetu; Tarehe: 4th April 2012
 
Idada kubwa ya wagonjwa waliokwenda kutafuta tiba kwa Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile, Loliondo wamepoteza maisha.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo sasa itatangaza matokeo ya utafiti wa tiba hiyo ya ‘Kikombe cha Babu’ imesema wengi ni wale wenye Ukimwi walioacha matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARVs).

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Regina Kikuli, aliiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) jana Dar es Salaam, kwamba hadi sasa Serikali inafanyia utafiti watu 206 ambao walipata kikombe hicho.

Utafiti unaofanywa na Wizara hiyo inataka kubaini kama kweli dawa hiyo ina uwezo wa kuponya Ukimwi, kisukari, saratani na magonjwa mengine sugu. Wanaofanyiwa utafiti huo walipata ‘kikombe’ hicho baada ya kuugua kisukari na Ukimwi.

“Kwa sasa ni vigumu kusema dawa hiyo inaponya au haiponyi, tusubiri utafiti wa kitaalamu. “Baada ya miezi miwili tutatangaza matokeo kwa umma,” alisema Kikuli na kuongeza kuwa utafiti huo unafanywa katika hospitali mbalimbali nchini chini ya usimamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Utafiti huo unafanywa katika hospitali za Bugando, Mwanza; Mbeya; Mount Meru, Arusha; Hydom, Manyara na KCMC, Kilimanjaro. Hospitali hizo ziko maeneo ambayo wananchi wengi walijitokeza kupata ‘kikombe’ Loliondo. Kikuli pia alisema kwa sasa idadi ya Watanzania wanaokwenda Loliondo kupata tiba hiyo imepungua; lakini bado wananchi wa kutoka Kenya na nchi zingine wanaendelea kwenda kupata ‘kikombe’ hicho.

Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Donan Mmbando, alikiri kuwa wagonjwa wengi wa Ukimwi waliokwenda kupata tiba hiyo na kuachana na ARVs wamepoteza maisha. Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy Mohamed (CCM), aliishauri Wizara hiyo kuacha siasa badala yake iwaambie wananchi kwamba dawa ya Babu wa Loliondo haina madhara kwa binadamu, lakini pia haina uwezo wa kuponya magonjwa.

“Msiogope kusema kama wanasiasa, ninyi ni wataalamu, ni kweli kuwa ile dawa haina madhara kama yalivyo maji, lakini tusidanganyane, haitibu, kwa nini mnaendelea kudanganya wananchi?” Alihoji Mbunge huyo. Makamu Mwenyekiti wa PAC, Zainab Vullu, ndiye aliyetaka Wizara itoe taarifa ya utafiti wa tiba ya ‘kikombe cha Babu’.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, alitaka kujua kama bado kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaokwenda kupata tiba hiyo Loliondo. Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola, alitaka kujua kama Wizara hiyo imewasiliana na nchi zingine za Ulaya ambazo raia wake walikwenda kupata tiba ya ‘kikombe’ kama walipona magonjwa waliyokuwanayo.

“Wenzetu wale Wazungu ni wepesi katika masuala haya ya utafiti, nataka kujua kama mmefanya juhudi za kuwasiliana nao?” Alihoji mbunge huyo na kujibiwa na Kaimu Mganga Mkuu kuwa kila nchi ina utaratibu wake wa utafiti.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA!

***********************************************

Hii imetoka kwenye gazeti la Habari Leo.   Mwaka jana saa hizi kila mtu alitaka kwenda kwa Babu. Inasikitikisha kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wamekufa.  Babu yuko wapi leo hii, je, watu bado wanajazana kule Loliondo kutafuta 'Dawa ya Babu'?

6 comments:

  1. Tusisahau kuwa magonjwa yote yana tiba, isipokuwa `kifo' na uzee!

    ReplyDelete
  2. Kibinaadamu inaeleweka mtu unapoumwa unakuwa desperate kutafuta tiba hali hii pamoja na familia ya mgonjwa.Kuna biaadamu wengine ambao hawana uwezo katika utoaji wa tiba lakini hujifanya wanajua na hata kama wanaweza utafiti wa Dawa yenyewe hauridhishi.Serikali kabla ya kukimblia kusema dawa haina madhara kwa binaadamu ingefanya uchunguzi wa kujua kama inatibu.Kwa suala hili kwa mara nyigine tena Serikali pia imepotosha Umma kwani tumeona viongozi wengi wakinywa hicho kikombe.Tuwe wangalifu na SANGOMA wetu kamba nyigi[uongo].

    ReplyDelete
  3. It's obvious that, "kibombe cha Babu" doesn't cure anything. It's amazing that people "get taken in" by such ridiculous claims of "miracles"!

    ReplyDelete
  4. Mbona watu wanakufa kila siku duniani kote.

    Kwani na dawa za huko kote duniani haziponyi?

    ReplyDelete
  5. WATU WALITAJIRIKIA LOLIONDO! ASANTE BABU!

    ReplyDelete
  6. Hii ni kati ya habari zilizoandika vibaya zaidi katika mtandao wa Habari Leo

    ReplyDelete