Asante Kaka Johnson kwa kuandika habari hizi. Nimesoma na roho imeniuma kweli. Yaani ni yale mambo aliyokuwa anasema Mwalimu Nyerere. Tunanyonywa na makupe. Unaedelea! Lini tutakata mirija yao na rasilimali zetu zifaidi wananchi wa Tanzania.
************************************************************
Bilionea wa Barrick anapoitumia Tanzania kujitakasa...!
Na Johnson Mbwambo
Toleo la 238
9 May 2012
WIKI iliyopita Rais Jakaya Kikwete alilifanyia mabadiliko kidogo baraza lake la mawaziri. Wasomaji wangu wengi walinitumia ujumbe wa e-mailna sms wakinishauri, safari hii, niandike kuhusu mabadiliko hayo ya Kikwete, na kueleza iwapo yataleta unafuu wowote kwa Watanzania.
Jibu langu kwao ni kwamba hakuna kipya cha kuandika ambacho hakijaandikwa, hakuna kipya cha kumshauri Rais Kikwete ambacho hajashauriwa na wabunge, wasomi, wachumi na wachambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii wa hapa nchini.
Binafsi, niandike kumwambia nini kipya Rais Kikwete? Kwamba baraza lake ni kubwa mno sawa na timu tano za soka, na kwamba linateketeza bure tu fedha za walipakodi?
Niandike kumwambia kwamba hapakuwa na haja yoyote kuwa na manaibu mawaziri katika baadhi ya wizara kama vile Wizara Habari, Vijana na Michezo?
Niandike kumwambia kuwa naibu waziri katika wizara kama hiyo hana kazi nyingi za kila siku, na kwamba muda mwingi ataishia kusoma tu magazeti ofisini na kusubiri mialiko ya kuzindua albamu za bongo fleva au kuhudhuria mashindano ya walibwende?
Niandike nini kipya kuhusu mabadiliko hayo madogo ya baraza la mawaziri la Rais Kikwete? Kwamba hawa wapya aliowateua ndo watamaliza ufisadi uliokithiri katika serikali yake? Kwamba impunityimefikia mwisho kwa sababu ya hawa mawaziri wapya aliowateua?
Hapana ndugu zangu. Sina jipya la kumwambia Rais Kikwete. Nilishasema katika safu hii, toleo Na. 237, kwamba “ya Kikwete tumeshayaona, tusibiri ya rais ajaye”.
Niliandika hivyo nikimaanisha kwamba katika miaka mitatu na ushee aliyobakisha Ikulu, hakuna jipya kubwa la kimaendeleo tunaloweza kutarajia kutoka katika serikali yake. Na bado naendelea kuamini hivyo.
Kwa hiyo, ndugu zangu, sitaandika kuhusu mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri; bali ninaandika kuhusu tukio jingine linalotuhusu la wiki iliyopita lililotokea huko Toronto, Canada.
Nazungumzia tukio la mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa wa kampuni inayoongoza duniani kwa uchimbaji dhahabu – Barrick. Kampuni hii ndio ambayo pia imetwaa karibu migodi yetu yote mikubwa ya dhahabu nchini.
Mkutano huo uliofanyika Jumatano ya wiki iliyopita ulikuwa wa aina yake kwa sababu, nje ya ukumbi wa mkutano, kulikuwa na mamia ya wanaharakati kutoka sehemu mbalimbali duniani wanaopinga uwekezaji wa kinyonyaji na usio wa kibinadamu wa Barrick.
Mkusanyiko huo mkubwa ulioratibiwa na Occupy Toronto Movement, nje ya ukumbi wa mkutano, ulikuwa na wanaharakati wenye hasira juu ya uwekezaji huo wa kinyonyaji na usio wa kibinadamu wa Barrick sehemu mbalimbali duniani.
Ni kutokana na hali hiyo ilikuwa ni vigumu wanahisa ndani ya mkutano huo kutolijadili suala la kuendelea kuchukiwa kwa Barrick sehemu nyingi duniani inakomiliki migodi ya dhahabu. Baadhi ya wanahisa (akiwemo wa Chile) walichachamaa kweli kweli mkutanoni na kuitaka Barrick ijirekebishe.
Lakini kulikuwa na mtu mmoja ambaye hakuamiani kirahisi kile kilichokuwa kikitokea nje ya ukumbi huo wa mkutano, na huyo si mwingine bali ni mmiliki na mwanzilishi wa kampuni hilo kubwa la dhahabu duniani, Peter Munk (84).
Peter Munk alikuwa akitetemeka kwa hasira, dhahiri akishindwa kuamini kuwa kampuni yake ilikuwa inachukiwa kiasi hicho; licha ya misaada mingi ya ‘huruma’ ambayo imetoa katika nchi ilikowekeza.
Kwa mujibu wa gazeti la Toronto Metro la Canada, Munk alilazimika kutoka na gari lake kupitia mlango wa nyuma ili kuwakwepa wanaharakati hao, lakini alipoona wingi wao kwa mbali, alimlazimisha dereva wake aendeshe hadi kwa wanaharakati hao ili “awapashe” kuhusu ‘huruma’ ya Barrick kwenye nchi zao.
Kwa sababu ya kuhofia usalama wake, dereva alimkatalia na kumpeleka moja kwa moja nyumbani kwake. Hata hivyo, alipofika nyumbani kitu cha kwanza alichokifanya bilionea huyo ni kupiga simu ofisi kwake na kuelekeza atayarishiwe haraka orodha ya misaada ya kijamii ambayo Barrick imetoa katika nchi ambako ina migodi.
Kesho yake mkutanoni, Bilionea Munk aliisoma orodha hiyo kujaribu kuwashawishi wanahisa waamini kuwa Barrick ni kampuni yenye ‘huruma’ kweli kweli.
Miongoni mwa nchi masikini duniani ambazo bilionea Munk alizitaja kuwa Barrick inatoa ‘misaada ya hiari ya huruma’ ni Tanzania, Papua New Guinea, Peru na Chile.
“Ningependa nitoke nje nipambane na waandamanaji hawa na kuwaambia ukweli,” alifoka Munk mkutanoni na kuongeza:“Sizungumzii tu kodi tunazolipa katika nchi hizo, sizungumzii tu ajira tulizotengeneza; bali nazungumzia ukweli kuwa kama si sisi, basi, ajira na fursa kwenye maeneo hayo zingekuwa ziro”.
Sidiriki, kwenye safu hii, kuzizungumzia Chile, Papua New Guinea au Peru, lakini kwa hapa kwetu Tanzania, nina hakika kilichosemwa na Munk si ukweli wote kuhusu uwekezaji wa Barrick.
Hiyo inayoitwa na Bilionea Munk kuwa ni ‘misaada ya hiari’ inayothibitisha ‘huruma’ ya Barrick, si chochote wala lolote ikilinganishwa na mapesa wanayoyapata kutoka katika mauzo ya dhahabu za migodi yetu.
‘Misaada ya hisani’ anayoizungumzia Bilionea Munk, ni kama ule wa dola 350,000 zilizotolewa na Kampuni ya Dhahabu ya Barrick Tanzania kwa ajili ya ukarabati wa Sungusungu Hospital kule North Mara. Hapa tunazungumzia ukarabati tu, na si ujenzi wa hospitali.
Hivi kweli ukarabati wa hospitali na zahanati na ujenzi wa madarasa na uchimbaji visima hapa na pale, ndio stahili yetu kwa mamilioni ya dola ambayo Barrick hujipatia kila mwaka kutoka katika dhahabu ya nchi masikini kama yetu?
Katika mkutano huo mkuu wa Barrick huko Toronto, Canada, Bilionea Munk alitamba kuwa mapato ya Barrick kote dunia yaliongezeka kwa asilimia 18 hadi kufikia dola bilioni 3.6.
Lakini hapo hapo ripoti ya African Barrick Gold (ABG) inaonyesha kuwa bajeti iliyopangwa kwa Tanzania kwa ajili ya hiyo inayoitwa ‘misaada ya huruma ya hiari’, ni dola milioni 10 tu! Hivi dola bilioni 3.63 na ‘msaada wa hiari’ wa dola milioni 10 ni wapi kwa wapi?
Hata kama katika nchi zote 10 ambako Barrick ina migodi mikubwa ingetenga dola milioni 50 tu, bado kisingekuwa kiwango cha kuridhisha kiasi cha Munk kukitumia kutamba mkutanoni.
Vyovyote vile; ukweli unabakia uleule, nao ni kwamba Barrick itaendelea kuchukiwa katika nchi masikini kama Tanzania kwa sababu uwekezaji wake umeendelea kuwa wa kinyonyaji na usio na ubinadamu.
Na ninapozungumzia uwekezaji usio wa kibinadamu, nawakumbuka Mama Otaigo wa kijiji cha Weigita na kijana Paul wa kijiji cha Nkerege (nikitaja wachache) kule North Mara ambao miili yao imeharibika vibaya kwa sababu ya kutumia maji ya Mto Tigithe yaliyokuwa na sumu inayotoka kwenye mgodi wa Barrick. Mpaka leo waathirika hao wa unyama huo wa mwaka 2009 hawajalipwa fidia na kampuni hiyo tunayoambiwa na mwasisi wake kuwa ni yenye ‘huruma’ nyingi.
Lakini pia ninapozungumzia uwekezaji huo wa Barrick usio wa kibinadamu, nawakumbuka wale wakazi wa Geita ambao sasa wanaishi kwenye mahema katika kambi iliyopachikwa jina la Dafurbaada ya kuwa wametimuliwa kwenye makazi yao ya asili kumpisha mwekezaji mwenye “huruma” ya kupindukia – Barrick. Katika hili rejea makala ya Raia Mwema ya toleo Na.237 yenye kichwa cha habari: Utajiri wa dhahabu wageuka laana Geita.
Ndugu zangu, Bilionea Munk anaweza kuwa amefanikiwa kuwaghilibu wanahisa wenzake kwenye mkutano huo wa Toronto, Canada, kwamba eti Barrick ni kampuni yenye “huuma” , na kwamba imetoa misaada mingi ya kijamii katika nchi ambako ina migodi; lakini ukweli unabakia pale pale, nao ni kwamba Barrick ni kampuni ya kishetani.
Na nijuavyo, kama CCM hakitaondolewa madarakani kwenye uchaguzi wa 2015, Tanzania tutaendelea kunyonywa na Barrick hadi dhahabu katika migodi hiyo zitakapoisha kabisa na wao kuondoka na kutuachia mashimo matupu! Si inasemwa wajinga ndio waliwao?
Tafakari.
Chanzo: Gazeti la RaiaMwema
Ni lini sisi waafrika tutaacha kulia kama watoto wadogo? Sisi wenyewe tumeiweka ccm madrakani. Kwani hatukuyajua hayo? Hao wazungu utamaduni wao unahalalisha hayo wanayofanya maana kwao the winner takes all. Nyerere tulimuona mjinga. Hatuna sababu yoyote ya kulalamika sasa. Tunavuna tulichopanda.
ReplyDelete