Mafuta kuwa suala la Muungano tulikoseaby zittokabwe |
- Kila upande wa Muungano uchimbe Mafuta na Gesi Asili yake na Mapato yawe ya Serikali ya upande husika.
- Shughuli za Utafutaji kwenye vitalu vyenye mgogoro ziendelee mara moja
- Zanzibar ianzishe Shirika lake la Mafuta (PetroZan)
- Katiba mpya itofautishe utafutaji (upstream) na Biashara (uchimbaji, midstream na downstream)
Moja
ya suala linalosubiriwa kwa hamu kubwa katika mjadala na hatimaye
uandishi wa Katiba mpya ni suala la Mafuta na Gesi Asilia kuwa jambo la
Muungano au liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano. Suala hili
limezusha mjadala mkubwa sana mara kwa mara nchini Tanzania kiasi cha
lenyewe kuwa ni hoja ya wale wasiotaka tuwe na Dola ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Wakati
Muungano unaanzishwa mwaka 1964 Mafuta na Gesi hayakuwa masuala ya
Muungano. Nimeangalia katika Hati ya Muungano ambayo ilikuwa ni sehemu
ya Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1965, suala hili
halikuwamo katika orodha ya mambo Kumi na Moja ya Muungano. Nyaraka nilizoziona
zinaonyesha kwamba suala la Mafuta na Gesi Asilia liliongezwa katika
orodha ya Mambo ya Muungano mwaka 1968. Kuna watu wanahoji kihalali
kabisa kwamba nyongeza ya jambo hili ilifanywa bila kufuata taratibu na
hivyo kufanywa kinyemela na kuna wengine wanasema jambo hili lilifuata
taratibu zote za kisheria ikiwemo kupigiwa kura na Bunge la Muungano na
kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge kutoka pande zote za
Muungano.
Katika
moja ya vikao vya Bunge katika Bunge la Tisa, aliyekuwa Naibu wa Waziri
wa Nishati na Madini Ndugu Adam Malima alileta kumbukumbu za mjadala
Bungeni (Hansard) za mjadala wa suala la Mafuta na Gesi ili kuthibitisha
kwamba jambo hili halikuuingizwa kwenye Katiba kinyemela.
Wakati
umefika kwa Watafiti wa Masuala ya Muungano wakapekua nyaraka hizi na
kutwambia ukweli ulio ukweli mtupu wa namna suala la Mafuta na Gesi
lilivyoingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano. Hata hivyo, jambo
hili sasa ni jambo la Muungano kwa mujibu wa Katiba na ni dhahiri kuwa
WaTanzania wa Zanzibar hawafurahiswhi nalo na hivyo kuazimia kupitia
Azimio la Baraza la Wawakilishi kwamba jambo hili liondolewe kwenye
orodha ya masuala ya Muungano. Kwa vyovote vile Katiba mpya ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inapaswa kutoa uamuzi wa mwisho utakaomaliza
mjadala huu.
Jambo
la kusikitisha ni kwamba licha ya Bunge la Muungano kuamua kuongeza
suala la Mafuta na Gesi asilia katika masuala ya Muungano, mwaka mmoja
baada ya uamuzi huo likaundwa Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania
(TPDC) kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano (establishment order).
Shirika hili halikuanzishwa kwa Sheria ya Bunge au kwa Sheria ya
Makampuni kama yalivyo Mashirika mengi ya Umma hapa nchini bali kwa amri
ya Rais ya mwaka 1960. Katika amri hii ya Rais, Shirika la TPDC
halikupewa ‘mandate’ ya kimuungano. Shirika hili mipaka yake ilianishwa
kuwa ni Tanzania bara peke yake. Hivyo suala la Muungano likawekewa Shirika la Tanganyika kulisimamia!
Kama
ilikuwa ni bahati mbaya au makusudi au kupitiwa kwa viongozi wetu wa
wakati huo ni vigumu kujua lakini huu ni mkanganyiko mkubwa ambao
ulipaswa kurekebishwa mapema sana.
Shirika
la TPDC limekuwa likifanya kazi ya kusimamia Sekta ya Mafuta na Gesi
ikiwemo kutoa vibali vya kutafuta mafuta, kuingia mikataba na Makampuni
ya kimataifa na kuisimamia mikataba hiyo. Miongoni mwa mikataba hiyo ni
kwenye maeneo ambayo kama isingekuwa Muungano yangekuwa ni Maeneo ya
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Mbaya zaidi Mikataba yote ya utafutaji na
uchimbaji Mafuta inafanywa inaingiwa na Waziri wa Nishati na Madini
Wizara ambayo sio ya Muungano. Hakuna hata eneo moja ambalo taratibu
zimewekwa kwamba pale ambapo eneo hilo ni eneo lilikuwa chini ya himaya
ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar basi mikataba isainiwe na Mawaziri wawili
wa sekta hiyo kutoka kila upande wa Muungano.
Ni
dhahiri kwamba kama ni kusahau hapa kulikuwa na kusahau kukubwa ambako
hakustahmiliki kwa mtu yeyote mwenye upeo achilia mbali mwananchi wa
kawaida wa Zanzibar ambaye anaona anaonewa na kugandamizwa na Bara.
Mnamo
miaka ya mwanzo ya 2000, Shirika la TPDC liliingia mikataba ya Vitalu
kadhaa vya Mafuta miongoni vya vitalu hivyo ni vitalu nambari 9, 10, 11
na 12 mashariki ya visiwa vya Pemba na Unguja. Vile vile Shirika na
Wizara ya Nishati waliingia mkataba mwingine katika Kitalu kilichopo
kati ya Pemba na Tanga (mahala ambapo kumekuwa na dalili za wazi za
kuwapo Mafuta kutokana na kuonekana kwa ‘Oil sips’ mara kwa mara.
Vitalu
9, 10, 11 na 12 vilipewa kampuni ya Shell ya Uholanzi na kitalu cha
kati ya Tanga na Pemba walipewa Kampuni ya Antrim ya Canada ambayo
baadaye waliuza sehemu ya Kampuni yao kwa Kampuni ya RAK Gas kutoka Ras
Al Khaimah huko United Aarab Emirates. Kwa kuwa Vitalu hivi vipo katika
eneo la iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kabla ya Muungano,
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikataa shughuli zozote kufanyika mpaka
suala la Mafuta na Gesi kuondolewa katika orodha ya Mambo ya Muungano
lipatiwe ufumbuzi.
Uamuzi
huu wa Serikali ya Zanzibar ni uamuzi ambao ungechukuliwa na Serikali
yeyote ile yenye mapenzi ya dhati na watu wake. Uamuzi huu ulileta
mjadala mpana sana katika masuala ya Muungano na ambao hawana taarifa
waliubeza sana. Hata hivyo suala hili likafanywa ajenda katika vikao vya
masuala ya Muungano vinavyoitwa Vikao vya Kero za Muungano. Miaka kumi
suala hili linajadiliwa na Maamuzi hayafanyiki! Hivi sasa kila suala lenye kuangukia kwenye Katiba husukumwa huko na hivyo kutoa ahueni kwa wanaogopa kufanya maamuzi.
Katika
medani za uchumi kila suala lina muda wake. Masuala ya utafutaji wa
Mafuta ni masuala yanayoongozwa na msimu na kuendelea kuchelewa kufanya
maamuzi juu ya suala hili kunalitia hasara Taifa, Hasara ya Mabilioni ya
Fedha na hasara kubwa zaidi ya kufahamu utajiri uliojificha chini ya
Maji ya Bahari inayozunguka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivi
sasa Pwani ya Afrika Mashariki inarindima (trending) katika utafutaji
wa Mafuta na Gesi asilia. Huko Msumbiji Makampuni mbalimbali yamegundua
Gesi asilia nyingi inayofikia zaidi ya futi za ujazo trillion 107
(107TCF) kwa makadirio ya chini. Hapa Tanzania utajiri wa Gesi asilia
uliogunduliwa hadi hivi sasa na kutangazwa umefikia futi za ujazo
trillion 20 (20TCF) ambazo ni sawa na utajiri wa thamani ya dola za
kimarekani trillion 6. Makadirio yanakisiwa kuwa Tanzania kuna futi za
ujazo trillioni 85 (85TCF) za Gesi Asilia katika eneo la Kusini kuanzia
vitalu namba 1 mpaka namba 5 ikiwemo vitalu vya nchi kavu na vile vya
Songosongo.
Iwapo
kasi ya utafutaji mafuta itaendelea kama sasa katika kipindi cha miaka 2
ijayo Tanzania itaweza kuwa kati ya nchi mbili za Afrika zenye Utajiri
mwingi zaidi wa Gesi Asilia. Hivi sasa Nigeria ndio inaongoza kwa kuwa
na futi za ujazo trillion 189 (189TCF) ikifuatiwa na Algeria na Angola
ambazo zote zina utajiri wa juu kidogo ya 100TCF kwa Algeria na chini ya
100TCF kwa Angola. Msumbiji sasa imeifikia Algeria na kushika nafasi ya
pili.
Katika masuala ya Mafuta na Gesi hatua ya kwanza ni kujua kama utajiri huu ambayo kitaalamu inaitwa gas exploration.
Shughuli za utafutaji zinapandisha sana thamani ya nchi na eneo la
nchi. Kwa mfano hivi sasa kitendo cha Kampuni ya Uingereza ya BG/Ophir
na ile ya Norway ya StatOil kupata mafanikio makubwa katika utafutaji wa
Gesi asilia kumeongeza thamani ya Pwani ya kusini ya Tanzania katika
medani za utafutaji (Exploration Activities).
Hata
hivyo kama ilivyogusiwa hapo juu, shughuli za Utafutaji ni shughuli za
msimu. Pia huchukua muda mrefu wa kati ya miaka 5 mpaka 10 kati ya
kutafuta, kupata na kuanza kuchimba. Hivi sasa ni muda wa pwani ya
Afrika Mashariki. Ni lazima kuhakikisha kwamba vitalu vyote
vilivyogawiwa hivi sasa vinafanyiwa kazi. Hata hivyo vitalu vingine
vyovyote visigawiwe kwanza mpaka hapo matunda ya vitalu vya sasa
yaonekane. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imependekeza kusimamisha
kugawa vitalu vipya. Matokeo ya utafutaji katika vitalu vya sasa yakiwa
mazuri kama ilivyo sasa, thamani ya vitalu vipya itapanda sana na nchi
itakuwa na nguvu ya majadiliano (strong negotiation position) dhidi ya
makampuni makubwa ya mafuta.
Tufanyaje
kuhusu vitalu vilivyogawiwa katika eneo ambalo lina mgogoro kuhusu
suala la Muungano? Sio kazi rahisi lakini imefikia wakati tuamue. Kwa
kadri nionavyo, Itabidi kuwe na maamuzi ya mpito (interim decisions) na
maamuzi ya muda mrefu.
Kwanza,
ni lazima kukiri tulipokosea. Hata kama ilikuwa ni sahihi kiutaratibu
kuweka suala la mafuta na Gesi katika orodha ya mambo ya Muungano,
haikuwa halali Shirika la TPDC lenye mipaka ndani ya Tanzania bara
kuingilia ugawaji wa vitalu na kuingia mikataba katika maeneo ambayo ni
ya Muungano. Ni Taasisi ya Muungano tu ndio inaweza kushughulikia suala
la Muungano na sio vinginevyo.
Ilikuwa
ni dharau kubwa sana kwa Waziri wa Nishati ambayo sio Wizara ya
Muungano kuingia Mikataba katika eneo la Zanzibar (ambapo kikatiba
tumelifanya eneo la Muungano) bila kushauriana na kukubaliana na Waziri
wa Nishati wa Zanzibar. Kukiri kosa sio unyonge, ni uungwana. Hata
tukifanya vikao milioni moja chini ya Makamu wa Rais, bila kukiri kosa
hili tatizo hili na mengine ya aina hii hayataisha.
Pili,
ni vema kukubali kwamba shughuli za utafutaji katika vitalu vyenye
mgogoro ziendelee kwenye hatua ya utafutaji tu. Kama mafuta au Gesi
ikipatikana, uchimbaji usianze mpaka uamuzi wa mwisho kuhusu suala hili
uwe umepatikana. Pia ninapendekeza ufumbuzi wa mwisho hapa chini.
Kuchelewesha utafutaji ni hasara kwa pande zote za Muungano kutokana na
taarifa za kijiolojia zitakazopatikana na hivyo kupandisha thamani ya
nchi hizi mbili kijiolojia.
Hata
hivyo, utafutaji huu katika eneo lenye mgogoro kati ya pande mbili za
Muungano ufanyike baada ya mkataba wa PSA kufanyiwa marekebisho makubwa.
Marekebisho hayo ni pamoja na Mkataba kusema wazi kwamba shughuli za
uchimbaji zitafanyika iwapo tu makubaliano ya kugawana mapato ya Mafuta
na Gesi kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar yamefikiwa.
Pia Mkataba uzingatie maendeleo ya sasa ya kusini mwa Tanzania na hivyo
mkataba uboreshwe kwa faida ya nchi ikiwemo kutolewa kwa ‘signature
bonus’. Hii ni Fedha inayotolewa na Kampuni za utafutaji Mafuta kwa
Serikali kabla ya utafutaji kuanza. Kiwango hutokana na majadiliano na
kukubaliana. Nchi zenye jiolojia iliyopevuka hutumia njia hii kuongeza
mapato ya Serikali.
Mkataba
pia useme kinaga ubaga kwamba utasainiwa na Mawaziri wa pande mbili za
Muungano na kwamba Kampuni inayofanya utafiti itatoa taarifa zake za
Utafiti sawia kwa Mawaziri wote kwa mujibu wa vipengele vya mkataba.
Kwa
upande wa maamuzi ya muda mrefu, ushauri wangu ni kwamba; kwa maana ya
kuandikwa kwenye Katiba mpya ni kwamba Suala la Mafuta na Gesi Asilia
liendelee kuwa suala la Muungano kwenye eneo la usimamizi wa Tasnia na
leseni za utafutaji (Upstream Regulatory mechanism). Hili ni eneo
linalohitaji usimamizi wa dhati kabisa na kwa pamoja pande mbili za
Muungano zinaweza kufanya vizuri zaidi.
Eneo
la Uchimbaji na hasa kugawana mapato ya mafuta na Gesi (Profit Oil)
lisimamiwe na kila upande wa Muungano kivyake. Biashara ya Mafuta isiwe
jambo la Muungano na hivyo kila Upande wa Muungano uwe na Shirika lake
la Mafuta na Gesi ambalo litashiriki kama mbia wa Mashirika ya Kimataifa
katika uchimbaji, usafirishaji na uuzaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
Mapato yanayotokana na Mafuta (Profit Oil) na kodi nyingine zote
isipokuwa mrahaba (royalty) yawe ni masuala yanayoshughulikiwa na
Serikali ya kila upande wa Muungano kwa mujibu wa Sheria ambayo Serikali
hizo zimejiwekea.
Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ilipendekeza Bungeni kwamba
kuwepo na Mamlaka ya Mafuta na Gesi Asilia Tanzania (Tanzania Petroleum
Authority) ambayo itakuwa ni msimamizi (upstream regulator) kama suala
la Muungano. Mrahaba wa Mafuta na Gesi ambao sasa ni asilimia 12 ya
Mapato ya Mafuta itakusanywa na Msimamizi huyu na ndio mapato pekee
katika tasnia ya Mafuta na Gesi yanapaswa kuwa mapato ya Serikali ya
Muungano.
Kamati
pia ilipendekeza kuanzishwa kwa Shirika la Mafuta na Gesi (Petroleum
Tanzania - PetroTan) ambalo litakuwa mbia kwenye Makampuni ya utafutaji
na uchimbaji wa Mafuta na Gesi kwenye Vitalu vya Tanzania bara. Mapato
yote ya vitalu vya Tanzania bara na kodi zote isipokuwa Mrahaba
zitakwenda kwa Mamlaka za bara tutakazo kuwa tumeamua baada ya Katiba
mpya kuanza kazi. Hivi sasa TPDC inafanya kazi hii mpaka Zanzibar jambo
ambalo hata kwa akili ya kawaida halipaswi kukubalika.
Aidha,
napendekeza kwamba Zanzibar ianzishe Shirika lake la Mafuta sasa. Jambo
hili halina haja ya kusubiri vikao vya kero za Muungano kwani ni
dhahiri TPDC haina mamlaka,ushawishi na uthubutu kusema uhalali wa
kusimamia vitalu vya Mafuta vilivyopo Zanzibar.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ipeleke muswada katika Baraza la Wawakilishi
kuanzisha Shirika la Mafuta na Gesi la Zanzibar (Petroleum Corporation
of Zanzibar – PetroZan) ili liweze kushiriki katika utafutaji na
uchimbaji wa Mafuta Zanzibar. Lakini Pia PetroZan ilinde maslahi ya
Zanzibar katika tasnia hii kwa kujijengea uwezo wa kusimamia ugawaji
bora wa Mapato kutoka katika Mafuta na Gesi Asilia.
Kama
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inachelea kuanzishwa kwa Shirika hili,
Wawakilishi wa pande zote (CCM na CUF) wapeleke muswada binafsi kuunda
Shirika la Mafuta la Wazanzibari. Hawatakuwa wamevunja Katiba ya
Muungano kwani hivi sasa hakuna Taasisi yenye mamlaka ya kusimamia
Tasnia hii kwa Upande wa Zanzibar.
Wakati
haya yote yanafanyika, shughuli za utafutaji Mafuta na Gesi katika
vitalu vilivyopo katika eneo la Zanzibar na hasa vitalu namba 9,10,11 na
12 na katika kitalu cha kati ya Pemba na Tanga ziendelee kufuatia
marekebisho ya Mkataba wa Utafutaji. Utafutaji wa Mafuta una faida zaidi
kwa Nchi hizi mbili kuliko kwa Kampuni za Mafuta kwani uwekezaji wa
Kampuni pekee na nchi zitapata taarifa za kijiolojia zitakazosaidia
mikataba ya baadaye kuwa bora zaidi.
Wakati
nasisitiza kwamba tuendelee na utafutaji katika vitalu tajwa, katika
Katiba mpya, utafutaji wa mafuta usimamiwe na Taasisi ya Muungano.
Uchimbaji na biashara ya Mafuta ufanywe na kila Serikali ya kila upande
wa Muungano. Mafuta kuwa jambo la Muungano halafu kusimamiwa na Shirika
la Tanganyika na Wizara ya Upande mmoja ya Muungano ndio chanzo cha
mgogoro. Suluhisho sio kuifanya TPDC kuwa Shirika la Muungano, bali kila
upande upewe uhuru wa kusimamia uchimbaji, Biashara na mlolongo mzima
wa tasnia ya Mafuta (value chain from midstream to downstream) isipokuwa
utafutaji (upstream). Hili ndio suluhisho la kudumu ninaloona linafaa.
Uwazi (declaration):
Zitto
Kabwe ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na mfuatiliaji wa karibu wa Tasnia
ya Mafuta na Gesi Asilia akiwa amesomea mfumo wa uchumi wa katika tasnia
ya madini na mafuta (fiscal regime in Mineral and Petroleum sector).
Zitto pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya
Umma ambayo inasimamia mahesabu na utendaji wa Shirika la TPDC. Makala
hii imeandikwa baada ya ziara ya Mafunzo ya Wabunge kutembelea nchi ya
Uholanzi kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo. Katika
ziara hiyo Wabunge hao walikutana na Wakuu wa Shirika la Mafuta la Shell
ambapo walizungumzia pia suala la vitalu namba 9, 10, 11 na 12.
Kwanza Zitto tatueni tatizo la MADINI Geita nk ambako BARRICKS wanavuna MADINI kama yao na WANANCHI hawajafaidika lolote na pia WANAKUFA kama KUKU kutokana na MAJI YAO kuwa na KEMIKALI,pia wanyama na mazao yanakufa.Kisha tuangalie hiyo LAANA ya MAFUTA kwa maana hayajapatikana watu wameshaanza kupigana je yakipatikana sijui itakuwaje.Kwa AFRICA NISHATI ni LAANA na SIO NEEMA mfano halisi ANGOLA,LIBYA na NIGERIA.
ReplyDelete