TAARIFA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DKT. ALI MOHAMED SHEIN,
KWA WAANDISHI WA HABARI, WAHARIRI NA WANANCHI KUHUSU HALI YA NCHI,
TAREHE 31 MEI, 2012
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Assalam Aleykum
Namshukuru Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote, kwa kutupa afya
njema tukaweza kuzungumzia mambo yenye mustakbal mwema wa hali ya nchi
yetu kwa jumla.
Napenda kutanguliza shukurani zangu kwa wananchi wa Zanzibar kwa
kuendeleza na kudumisha amani hasa tokea kupatikana kwa maridhiano ya
kisiasa baina ya vyama viwili vikuu vya siasa hapa Zanzibar, Chama cha
Mapinduzi na Chama cha CUF, yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa mnamo Novemba,
2010 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Maridhiano hayo yalidhihirisha silka, ustaarabu na utamaduni wa
Wazanzibari kuishi pamoja kwa kuheshimiana , kusikilizana na
kushirikiana katika mambo yao ya kiuchumi na ya kijamii na maendeleo
yetu.
Kama tunavyoelewa kwamba Zanzibar ina watu wa makabila na dini
tofauti. Wazee wetu wa asili walisema “Zanzibar ni njema atakaye na
aje”. Ustaarabu huu ulianza kutumika tangu ulipoanza kuingia Uislamu
na kuendelea hadi kufika wageni kutoka Uajemi (washirazi), Ureno na
Oman walioanzisha utawala wao katika karne mbali mbali hadi ya 18.
Uislamu uliingia Zanzibar mara tu baada ya kuwepo katika nchi ya Saudi
Arabia. Kadhalika, Ukristo uliingia Afrika Mashariki alipofika
Mvumbuzi wa Kireno, Vasco da Gama mwaka 1498 na hatimae kuja
Wamishionari wa kwanza wakiongozwa na Ludwig Krapf mwaka 1844. Mfalme
wa wakati huo wa Zanzibar aliwaruhusu kujenga Kanisa la Anglikana la
Church Missionary Society (CMS) liliopo Mkunazini. Krapf baadae
aliruhusiwa kujenga mishionary Mombasa. Madhehebu mengine ya kikristo
yaliingia Zanzibar katikati ya karne ya Kumi na Tisa na kuenea sehemu
za bara kutokea hapa Zanzibar, na kanisa la pili kubwa la Minara
Miwili lilijengwa katika eneo la Shangani Mjini Zanzibar.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Naelezea haya ili nikumbushe sifa ya Zanzibar kuwa ni pahala ambapo
watu wa dini mbali mbali walifika na kuweka makazi yao na kuendeleza
shughuli zao za maisha pamoja na kidini. Anayeijua Zanzibar vizuri
atakumbuka kwamba ilikuwa taabu kumtambua Muislam au Mkristo kwa
sababu wafuasi wengi wa dini hizo walikuwa na tamaduni za mavazi ya
aina moja, wakicheza na kusoma pamoja. Baadhi ya ndugu zetu hao leo
tunaishi nao pamoja.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Hii ndio hali ya dini ya Kiislamu na Ukristo hapa Zanzibar.
Kuvumiliana na kuelewana kulikuwa ni chachu ya amani kwa muda mrefu na
kulichangia kuondoa ubaguzi. Kwa mara nyingi sherehe zao zilikuwa
zinahudhuriwa na watu wa dini zote. Aidha, wafuasi wa dini hizo
walikuwa wakihudhuria shughuli za jamii kwa pamoja na kujadili mambo
ya maslahi ya nchi kwa pamoja. Katika Afrika Mashariki ukiongelea
uvumilivu wa kidini mfano mzuri ni wa hapa Zanzibar. Mnamo mwaka 1953
yalifanyika mashindano ya sanaa ya uchoraji katika eneo la Afrika
Mashariki ya kuonesha uvumilivu wa kidini. Mshindi wa mashindano haya
alitokea Zanzibar ambae mchoro wake ulionesha msikiti, kanisa na baina
yake palikuwa na temple. Mchoro huu uliashiria mfungamano wa kidini wa
watu wa Zanzibar tangu enzi .
Zaidi ya maelezo hayo ya kihistoria, Katiba ya Zanzibar ya 1984
kifungu cha 19(1) kimeelezea kuwa “kila mtu anastahili kuwa na uhuru
wa mawazo, wa imani na wa uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na
uhuru wa kubadilisha dini au imani yake”, ambapo pia, Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nayo inazungumzia hayo hayo. Aidha,
miongoni mwa masuala tunayokwenda nayo vizuri sisi viongozi ni hili
suala la kuheshimu imani za dini mbali mbali hapa Zanzibar.
Mfano ni tarehe 16 Septemba, 2011, mimi nikiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi nilikutana na viongozi wa dini mbali
mbali waliokuwa wakijihusisha na juhudi za kuendeleza amani nchini.
Pia, nilihudhuria kutawazwa kwa Askofu Michael Henry Hafidh wa kanisa
la Aglikana tarehe 15 Aprili mwaka huu na nilipewa fursa ya kuhutubia
wafuasi na kuwaelezea msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu
ya imani za watu na kutobagua dini.
Kadhalika, mimi na viongozi wenzangu tumekuwa tukikutana na
kujadiliana na viongozi kadhaa wa dini ya Kiislamu. Kwa mfano tarehe
25 Aprili, 2012 Kamati maalum ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ilikutana na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho, Maimamu na
Mashekhe kuzungumzia hali iliyotokea nchini katika kufanya mihadhara
ikiashiria kama kwamba kutatokea uvunjwaji wa amani tuliyonayo. Kamati
hiyo ilifanya kazi nzuri sana. Tutaendelea na utaratibu huu wa
kukutana na viongozi wa dini zote ili kujadiliana hali halisi katika
jamii. Hivi majuzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa
Emmanuel Nchimbi pamoja na IGP Said Mwema, wamefanya hivyo juzi na
mikutano kama hiyo itaendelea kufanywa kwa utaratibu wake.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Tunaelewa vyema kwamba mustakabali wa nchi yetu umo katika mjadala
mkubwa wa kisiasa. Msingi mkuu wa hayo ni mabadiliko ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa maridhiano ya viongozi wakuu wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania tulikubaliana kuwa na mchakato wa mabadiliko ya Katiba
yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika kikao cha pamoja na viongozi
wa dini zote Aprili 25, mwaka huu, iliwasihi sana viongozi hao watumie
busara na wafuate taratibu zilizowekwa kuhusu marekebisho ya katiba.
Walitakiwa kuwaomba wafuasi wao kuepuka matumizi ya lugha na vitendo
vinavyoashiria uvunjaji wa amani katika nchi yetu. Wote walitakiwa
kushiriki ipasavyo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba
utakapoanza.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Wakati huo huo, kabla ya kuanza mchakato wa mabadiliko ya katiba,
Serikali zetu mbili, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tangu mwaka 2006 tumekuwa
tukifanya mazungumzo ya pamoja kuhusu mambo ya Muungano kupitia Kamati
ya pamoja inayozungumzia mambo ya Muungano inayoongozwa na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuzungumzia kero za Muungano.
Mimi nilipata nafasi ya kuingonoza Kamati hii kuanzia mwaka 2008 hadi
2010. Hivi sasa Kamati hio inaongozwa na Mheshimiwa Dk. Mohammed
Gharib Bilal ili kujadili kero na mapungufu katika mambo mbali mbali
ya Muungano wetu.
Vikao mbali mbali vinaendelea kufanyika. Pande zote mbili zimekuwa
zikiwasilisha mambo ambayo yanajichomoza na yanayoendelea kuchomoza
kama kero kwa Sekretarieti ambayo ina wajumbe sita, watatu kutoka kila
upande wa Muungano.
Sekretarieti hii ina jukumu la kuandaa ajenda za mikutano ya ngazi za
Wataalamu, Makatibu Wakuu, Mawaziri na hatimae kikao cha juu kabisa
kinachowajumuisha Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar chini ya Uwenyekiti wa Mheshimiwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Miongoni mwa vikao vilivyofanyika ni:
1. Vikao 4 vya Sekretarieti vilivyofanyika kwa lengo ka kuratibu
utekelezaji wa yatokanayo katika kikao cha mambo ya Muungano.
2. Vikao 6 vya ngazi ya watendaji wa sekta mbali mbali husika kujadili
utekelezaji na taratibu za kisheria kwa mambo yote ambayo yameainishwa
katika kero za Muungano.
3. Vikao 4 vya ngazi ya Makatibu Wakuu kujadili maamuzi ya watendaji.
4. Vikao vitatu vya ngazi ya Mawaziri kwa ajili ya kuandaa mapendekezo
ya kikao cha juu cha mambo ya Muungano.
5. Kikao kimoja kati ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kilichoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kilichofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Januari mwaka huu.
Wana ratiba ya kuandaa kikao chengine hivi karibuni.
Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza hadi sasa na yaliyopata nafasi ya
kujadiliwa ni haya yafuatayo:
1. Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
2. Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
3. Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu.
4. Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za Nje.
5. Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
6. Uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa Ndani na Nje ya
Nchi.
7. Kodi ya Mapato.
8. Usajili wa vyombo vya moto.
9. Ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO.
10. Uharamia na utekaji nyara wa Meli.
11. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.
12. Taarifa ya utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Changamoto zipo na zitafanyiwa kazi.
Nimeona haya niyaseme ili wananchi waelewe mambo haya muhuimu
yanayofanywa na Serikali zote mbili juu ya suala hili.
Kutokana na jitihada hizi zinazochukuliwa na Serikali zote mbili,
pamoja na kuitumia vizuri fursa tuliyopewa ya kuweza kuwasilisha maoni
yetu katika marekebisho ya Katiba, matumaini yangu ni kuwa kwa pamoja
tutaweza kuondosha kero hizi na kuandaa Katiba mpya itakayotuletea
maendeleo makubwa nchi yetu. Haya ni masuala muhimu kwa ustawi wa nchi
yetu. Nawasihi wananchi wayakabili wakiwa na subira na busara ili
tuijengee mustakbali mzuri nchi yetu katika mambo 12 niliyoyaorodhesha
hapo juu mambo mengi tayari yamepatiwa ufumbuzi na yapo baadhi ambayo
yanafanyiwa kazi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kukubaliana
na Rais wa Zanzibar alitangaza majina ya Tume ya mabadiliko ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume hiyo inayoongozwa na
Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu
Mwenyekiti Mheshimiwa Jaji Agostino Ramadhani. Naelewa kuwa hadi sasa
sio wananchi wengi wanaoijuwa sheria hiyo. Tume inafanya utaratibu wa
kuwaelimisha wananchi juu ya sheria hii ili wapate kutoa maoni yao kwa
njia bora zaidi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yo yote ile, wako huru kutoa
maoni yao kwa njia ya amani na salama kwa Tume hiyo itakapokuja kuanza
kazi zake. Aidha, wananchi hawajawekewa vizuizi katika kutoa maoni
yao, ila tu ni kuzingatia sheria za nchi na taratibu zake. Tume nayo
imepewa uhuru wa kusikiliza maoni ya wananchi kwa kuzingatia sheria ya
Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 (Toleo la mwaka 2012).
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Ni jambo la kusikitisha sana na kutia majonzi kuwa katika siku chache
zilizopita kumezuka vitendo vya uvunjaji sheria. Tumeshuhudia
maandamano na mikutano yenye sura ya dini lakini yenye ujumbe wa
siasa, hasa kwa kuuzungumzia Muungano wetu. Vitendo hivyo vilikuwa
chachu ya machafuko yaliyojitokeza tarehe 26 Mei, 2012.
Viongozi na wafuasi wao wasiojali sheria, ustaarabu na utamaduni wa
kihistoria wa Kizanzibari walichoma moto majengo, mali za watu wasio
na hatia na makanisa, wamevunja maduka ya raia na kuiba mali zao na
wamekuwa wakitoa matamshi ya vitisho na ubaguzi ambavyo vimejenga
khofu kwa wananchi. Nimeshangaa sana uhusiano gani uliopo kati ya
kuzungumzia muungano na matukio hayo ambayo hatukuyatarajia kutokea.
Haya ni kinyumbe na Katiba na sheria zetu – lakini yametokea.
Mtakumbuka kwamba hivi karibuni, tarehe 21 Machi, 2012 nilikuwa na
ziara kwenye mikoa mitano ya Zanzibar. Katika mikutano yangu ya
majumuisho wakati wa ziara ya wilaya zetu zote za Unguja na Pemba,
nilikuwa nikitahadharisha sana na kueleza kwamba hatutovumilia kwa
hali yoyote uvunjaji wa sheria. Nilisema katika Mkutano wangu wa
mwisho wa majumuisho, tarehe 9 Mei, 2012 baada ya ziara ya Mkoa wa
Kusini Unguja, kwamba Serikali haitomuonea muhali mtu yeyote
atayethubutu kuharibu amani yetu. Hilo lilikuwa ni onyo kwa kila mmoja
wetu. Maana ishara tuliziona kupitia mihadhara yao na Serikali
ilichukua jitihada za kukabiliana nayo kwa kuzungumza nao.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Kutokana na matokeo hayo ya siku ya tarehe 26 Mei, 2012, Jeshi letu la
Polisi lilichukua hatua za haraka kuidhibiti hali iliyojitokeza, wengi
wenu mliiona hali ilivyokuwa. Kadhalika, Jeshi la Polisi walihakikisha
kwamba wale wote waliohusika na vitendo hivyo vya uharibifu na aibu
kwa nchi yetu na jamii ya Kizanzibari wanafikishwa kwenye vyombo vya
sheria kwa kuzingatia sheria za nchi ziliopo hapa Zanzibar. Hakuna
atakaeonewa wala kudhulumiwa na kila mmoja atahukumiwa kwa kesi
inayomuhusu na kwa mujibu wa sheria ziliopo.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Nachukua fursa hii kwanza kutoa pole kwa ndugu zetu waliotiwa hasara
ya mali zao. Pia, nawapa pole wananchi wote kwa usumbufu wote
uliojitokeza. Naelewa vyema kuwa wananchi wamepata hasara kubwa ya
kiuchumi kwa baadhi ya wananchi kuvunjiwa maduka yao, kuibiwa na pia
kukatizwa shughuli zao za kujitafutia riziki na maisha yao. Kwa bahati
mbaya, wako pia waliofikwa na matatizo ambayo hawakuyategemea wala
kuyazowea wakati polisi wakifanya kazi zao. Serikali inaendelea
kufanya tathmini ya hasara zilizotokea na pia inazingatia hatua za
kuchukua katika hasara hizo.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Baada ya hayo, napenda kuwaarifu wananchi wote kwamba hatua za
Serikali zetu mbili kuidhibiti hali ya usalama zitaendelea, ili amani
idumu na usalama wa wananchi, mali na maisha yao uwepo wakati wote.
Kwa wale wanao vunja sheria na viongozi wao tunawataka watambue kwamba
Serikali hatovumilia vitendo walivyovifanya. Hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya mtu ye yote atakayevunja sheria na yule mwenye
lengo la kuiharibu amani na utulivu wetu. Amani ambayo haikuja kwa
bahati tu, bali imehangaikiwa kwa muda mrefu, tutailinda hali hiyo kwa
nguvu zetu zote.
Kadhalika, nataka wananchi waelewe kwamba Serikali haitoingilia
shughuli za kweli za kidini au vitendo halali vya viongozi na wafuasi
wa dini yoyote. Kwa wale wenye maoni juu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, tungewasihi sana wasubiri utaratibu wa kutoa
maoni kama Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavyotangaza. Wafahamu fika
kwamba kwenda kinyume na sheria iliopo ni kosa la jinai, kwa sababu ni
sheria iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kama ilivyozoeleka, shughuli za ibada za pamoja zifanywe katika nyumba
za ibada na ikiwepo haja ya kufanya nje, iwe kwa kufuata taratibu
zilizowekwa nchini haya yanajulikana na lazima yazingatiwe. Kwa
kutunza amani na utulivu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari
imetangaza hatua kadhaa, miongoni mwa hatua hizo ni kupiga marufuku
mikusanyiko ya aina mbali mbali, maandamano na mihadhara ambayo
haijapata kibali cha Serikali hili ni lazima kila mmoja wetu
azingatie, huu sio wakati wa kubeza, na kila mtu azingatie sheria.
Mikutano ya halali ya kijamii haitaingiliwa hata siku moja na pale pa
kutaka ulinzi Jeshi la Polisi litafanya hivyo. Napenda kuwatoa hofu
waumini wa dini zote kwamba shughuli za ibada hazitoingiliwa na
waumini wa dini hizo wataendelea na ibada zao kama Katiba ya Zanzibar
ya 1984 na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Pamoja na kudhibiti amani na kuwahakikishia usalama wananchi, juhudi
za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea pia kudumisha sifa ya
kuendeleza amani ambayo kama itapungua seuze kuondoka kwake kutaathiri
utalii ambao ni tegemeo la uchumi wetu, ni jukumu letu kuendeleza
amani na ni jukumu letu kuwalinda wageni wetu wanaokuja kututembelea.
Kuathirika kwa utalii kutawaathiri wananchi ambao kwa kiasi ya
asilimia 60 za shughuli zao zinahusiana na sekta hiyo. Wananchi hawa
ni pamoja na wakulima, wavuvi na wafanyabiashara mbali mbali zikiwemo
zile biashara za usafiri, mikahawa na hoteli. Nimeshabainisha katika
mikutano mbali mbali kuwa sekta ya Utalii inachangia zaidi ya asilimia
80 ya fedha za kigeni tunazoingiza nchini. Tutambue kwamba hao
wanaofanya fujo ni waharibifu wa uchumi wetu na kamwe tusiwape nafasi
katika kutimiza malengo yao.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Natoa wito kwa wananchi wote wanaopenda amani washirikiane na Serikali
yao katika kudumisha amani hiyo. Wafuasi wa dini wazitumie nyumba za
ibada kwa kufanyia ibada na kutumia wakati wa ibada zao kuamrishana
mema na kukatazana mabaya. Wazazi wachunguze myenendo ya watoto wao na
wachukue dhamana yao ya kuwalea watoto hao katika maadili mema na kila
wakati wawatahadharishe juu ya kutokushiriki katika vitendo vya
uvunjaji wa sheria. Viongozi wa jamii nao wanajukumu la kuisaidia
jamii katika kufikia misingi ya kuwa raia wema na kutojiingiza kwenye
vitendo vya uvunjaji wa sheria. Ni jukumu letu sote kuilinda na
kuitekeleza misingi ya haki za binadamu na utawala bora, hili ni
jukumu la kila mmoja wetu si Serikali tu.
Ni jukumu letu sote tuidumishe misingi ya ustarabu na mila zetu, kwa
hakika si vizuri kutaka kuiga kila tuliloliona katika nchi za nje.
Lakini tuyaige yaliyo mazuri yenye kujenga uadilifu na utamaduni bora,
lakini katu mabaya tusiyaige hayana maana kwetu. Aidha, wakati
Serikali inaendelea kudhibiti usalama, nawataka viongozi hasa viongozi
wa jamii wawache kutoa lawama zisizokuwa na msingi katika hali hii.
Viongozi wa dini, siasa na jamii wawe waangalifu wa matamshi yao,
kwani Zanzibar na Tanzania ni yetu sote. Linapoharibika ni letu sote
na linapotengamaa ni letu sote.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wahariri na Wananchi,
Kwa kumalizia, natoa tena pole kwa wananchi wote wa Zanzibar na ndugu
zetu wa kikristo walioathirika na vitendo viovu vilivyotokea hivi
karibuni. Pia, nawapa pole wale wote walioathirika kwa njia mbali
mbali.
Nawasihi sana wananchi tuendelee kuvumiliana, tuheshimiane na
tushirikiane katika shughuli hasa zile za kuiletea maendeleo nchi yetu
na kila mmoja wetu kupata manufaa. Tuendele kupendana na tudumishe
umoja wetu kama ulivyo utamaduni na silka zetu. Jeshi letu la Polisi
litaendelea na kutimiza wajibu wao kwa faida yetu na amani ya nchi
yetu. Nataka niwahakikishie wananchi wote kwamba tutaendelea kuyalinda
Mapinduzi, tutayaendeleza kwa ajili ya maslahi ya kila mmoja wetu na
Wazanzibari wote. Nataka niwahakikishie wananchi wote kuwa Mapinduzi
yetu tutayalinda kwa maslahi ya wananchi wetu wote.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Umoja ni nguvu na utengano ni 'dhaifu sana'.
ReplyDeleteTujifunze kutoka kwa 'vidole'.