Thursday, March 07, 2013

Mhariri Absalom Kibanda Ajeruhiwa Vibaya

Nimepokea kwa E-mail:

Mhariri Absalom Kibanda
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Atekwa na Kujeruhiwa


Kwa ufupi

“Nilifika nyumbani kwangu kama saa sita usiku nikitokea kazini na nilipofika kwenye lango la kuingia ndani nilipiga honi ili mlinzi anifungulie. Lakini ghafla nilivamiwa na kundi la watu

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda ametekwa na watu wasiofahamika na kisha kumjeruhi vibaya kwa nondo, mapanga na kisha kumng’oa meno, kucha na kumharibu jicho la kushoto.

Tukio hilo la kinyama linafanana kwa kiasi fulani na lile la alilofanyiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania, Stephen Ulimboka.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi usiku wakati Kibanda akirejea nyumbani kwake Goba Punguni, Kata ya Mbezi Juu, kutoka kazini.

Tayari mwandishi huyo mkongwe wa habari, amesafirishwa jana kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Aliondoka jana akisindikizwa na daktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimu (Moi).

Mkasa Wenyewe

Akizungumza kwa tabu alipokuwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), hospitalini Moi, Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006), alisema:

“Nilifika nyumbani kwangu kama saa sita usiku nikitokea kazini na nilipofika kwenye lango la kuingia ndani nilipiga honi ili mlinzi anifungulie. Lakini ghafla nilivamiwa na kundi la watu ambao walivunja kioo cha gari langu upande niliokuwa nimekaa. Nilitokea kupitia mlango wa abiria lakini sikuweza kuwakimbia watu wale kwani walinikamata na kuanza kunishambulia kwa vitu vizito.”

“Baada ya kutoka kwenye gari, nahisi nilikanyaga sehemu mbaya, nikateleza na kuanguka wakanifuata...niliona kama watu watatu hivi wakaanza kunishambulia. Sikuwa nafahamu kilichojiri, lakini nilisikia mwingine akimwambia mwenzake afande ‘mshuti... mshuti’ huyo alipoelekeza mtutu na kujaribu ‘kushuti’ (kupiga risasi) ilikuwa kama vile imegoma.

“Nikiwa bado niko chini, wakanipiga kwa kitu cha ncha kali kwenye jicho la kushoto, wakaning’oa meno na kucha katika vidole vya mkono wa kulia, walinipiga sana na nilipata maumivu makali. Baada ya kunipiga na kunijeruhi waliniburuza hadi bembeni ya nyumba yangu na kunitupa na wakaondoka, baadaye majirani na wasamaria wema walikuja kuniokoa.

Mashuhuda Baada ya Tukio

Akizungumza jana, mzazi mwenzake, Angella Semaya alisema wakati Kibanda alipovamiwa hakusikia lolote: “Niliamshwa na kelele za majirani ndipo nami nikaenda eneo la tukio. Sikuamini kama alikuwa Kibanda kwani alikuwa ametapakaa damu huku akigugumia maumivu makali... kwanza sikumjua kama ni yeye kwa jinsi alivyokuwa.”

“Nina wasiwasi na hawa watu kuwa wametumwa kwa kuwa hawakuchukua chochote zaidi ya kumdhuru mwili,” alisema. Angella aliondoka jana na Kibanda pamoja na Mwandishi wa Habari, Eric Kabendera ili kumsindikiza Afrika Kusini atakapokuwa anapata matibabu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006), Hussein Bashe alisema: “Tulikuwa na Kibanda hadi usiku kama 5:30 hivi, tukifuatilia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya na tulipoona hakuna kinachoendelea zaidi, tukaagana kurudi makwetu.”

“Kwa kweli taarifa za kuvamiwa na kushambuliwa kwake zimetushtua, kwani ameumizwa sana hasa jicho. Daktari alishauri jicho liondolewe lakini nilikataa, jopo la madaktari bingwa wa macho wamemtazama na kuthibitisha kweli limeumia sana, tumewasiliana na mwajiri wetu ameamua kumpeleka Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

“Nawashukuru madaktari kwa jinsi walivyompokea na kumshughulikia katika kiwango kinachotia moyo. Pia waandishi kwa umoja waliouonyesha kwa kujitokeza haraka na kumjulia hali.”

Tasnia ya Habari

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeelezea kushtushwa na tukio la kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa mwenyekiti wake.

Taarifa ya TEF iliyotolewa jana na Katibu wake, Neville Meena, imesema shambulio hilo ni uthibitisho kwamba mazingira ya kikazi ya waandishi wa habari Tanzania siyo salama tena... “Tunapaswa kuchukua hatua za kutathmini upya mazingira ya kazi zetu, ili kuhakikisha kwamba walau tunakuwa salama.”

Alisema mwendelezo wa vitendo vya kuwashambulia waandishi wa habari ambavyo katika siku za karibuni vimeibuka, vinalifanya jukwaa liamini kwamba wanahabari sasa wanatishwa ili wasiweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Utesaji huu aliofanyiwa Kibanda unafanana na ule aliofanyiwa Dk Ulimboka. (Rejea vitendo vya kupigwa kichwani, kung’olewa kucha na meno).

Aidha, Meena alisema: “Tunaamini kwamba yaliyomkuta Kibanda hayawezi kutenganishwa na msimamo wake kikazi au kama mtu binafsi. Tunasema hivyo tukizingatia kwamba wahusika hawakuchukua chochote liwe, gari au vitu vilivyokuwamo ndani ya gari hilo vikiwamo laptop, ipad, simu za mkononi na vinginevyo.”

"Tunaamini vyombo vya dola, vitachunguza na kuwatia mbaroni kisha kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa tukio hili na mengine kadhaa ambayo sasa yamegeuka kuwa sehemu ya utamaduni katika nchi yetu.”

Awali, Mjumbe wa Bodi ya TEF, Theophil Makunga alisema wakati huu wanahabari na wanafamilia wakisubiri uchunguzi juu ya tukio hilo, kitendo hicho hakina budi kulaaniwa.

“Hatuwezi kusema nini chanzo cha tukio hilo kwa sasa, lakini tunaamini limetokana na kazi yake. Tunalaani vikali kwani tunaweza kusema kazi yetu sasa si salama tena,” alisema Makunga.

Mhariri Mtendaji wa Nipashe, Jesse Kwayu alisema tukio hilo halina uhusiano na ujambazi kutokana na mazingira ya jinsi lilivyotokea na kutaka hatua za haraka za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Mhariri wa Habari wa Tanzania Daima, Edson Kamukara alisema: “Matukio ya kutekwa na kushambuliwa kwa waandishi wa habari yamekuwa yakishika kasi... ni jambo la kusikitisha na hatuwezi kukaa kimya kwa hili.”

Baada ya Tukio

Katika taarifa yake jana, Dk Nchimbi alisema Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema ameteua timu ya maofisa wa polisi wanne kutoka Makao Makuu ya Upelelezi kuungana na wapelelezi kutoka Kanda Maalumu ya Polisi Mkoa wa Kinondoni ili kuhakikisha waliohusika wanakamatwa.

Baadaye jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema ofisi yake imeunda jopo la maofisa wa polisi tisa ambao wameshaanza kazi ya upelelezi wa tukio hilo.

Kova alisema kitendo alichofanyiwa Kibanda si cha kihalifu, bali kukomoana na visasi kwa kuwa upelelezi wa awali umeonyesha kuwa waliomvamia hawakuchukua chochote.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene alisema Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia idara yake imepokea kwa mshtuko tukio la kupigwa na kutendewa ukatili.

Alisema kitendo kilichofanywa kwa mhariri huyo ni ukatili uliopitiliza na kwamba wanaliachia Jeshi la Polisi lifanye kazi yake.

Wamjulia Hali

Kabla ya Kibanda kupelekwa Afrika Kusini, viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal walifika kumjulia hali. Wengine ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene na Yussuf Omar Chunda na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk Reginald Mengi.

Mengi na Mbowe
Akizungumza tukio hilo, Dk Mengi mbali ya kulaani, aliwataka waandishi wa habari kuandika ukweli na kuhakikisha haki inapatikana kwa kuwa jambo hilo ni zito.

Alisema kuna haja ya polisi kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli halisi upatikane na wahusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.

Mbowe alisema: “Tuungane katika kutetea uhuru wa vyombo vya habari. Uvamizi wa Kibanda ni doa kubwa katika tasnia ya habari bila kujali yuko chombo gani na yeye ndiye mkuu wa Jukwaa la Wahariri, ni wazi atakuwa amezungukwa na maadui wengi.”

Imeandikwa na Joyce Mmasi, Aidan Mhando, Bakari Kiango, Salhim Shao, Beatrice Moses na Aziza .

No comments:

Post a Comment