Saturday, July 12, 2014

Kuna nini Mbeya? Watu 135 Wameuawa!

Kamanda wa Polisi Mbeya Ahmed Msangi
KWA HISANI YA LUKWANGULE BLOG:

WATU 135 wameuawa katika matukio tofauti yaliyotokea mkoani Mbeya katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu.
 
Kiasi hicho cha matukio ya mauaji ni sawa na pungufu ya matukio 21 sawa na asilimia 14 ikilinganisha na yale 156 yaliyotokea katika kipindi kama hicho mwaka jana.
 
Akitoa taarifa ya utendaji wa jeshi la polisi mkoani Mbeya, Kamanda wa polisi mkoani hapa Ahmed Msangi alisema katika takwimu hizo mauaji yaliyotokana na wananchi kujichukulia sheria mikononi yalikuwa 33.
 
Alisema mauaji yaliyosababishwa na imani za kishirikina yalikuwa 23 sawa na matukio ya mauaji yaliyotokana na sababu nyingine huku matukio ya mauaji yaliyosababishwa na wivu au ugoni yalikuwa 20.
 
Matukio ya mauaji yaliyotokana na ugomvi wa majumbani yalikuwa 16, matukio ya ugomvi vilabuni 11 na matukio ya kulipiza kisasi yalikuwa tisa.
Alisema katika kipindi hicho wahamiaji haramu 159 walikamatwa kati yao 152 walikuwa raia wa Ethiopia, 23 raia wa Burundi,10 Wasomali, saba Wapakistani, wawili kutoka Malawi na mmoja akiwa ni raia wa Msumbiji.
 
“Katika kipindi hicho tumeweza kukamata bunduki 19 ambapo gobori zilikuwa 15, bastola mbili zilizotengenezwa kienyeji, Riffle moja na SMG moja. Pia zilikamatwa silaha mbili baada ya majambazi kuuawa katika jaribio la kufanya unyang’anyi. Silaha hizo ni SMG yenye namba 3514 na AK-47 namba 592058 na risasi 25 kwenye magazini,” alisema Kamanda Msangi.
 
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho kiasi cha lita 479 za gongo pamoja na mitambo 16 ya kutengenezea pombe hiyo vilikamatwa.
 
Kilo 296 na gramu 678 na miche 314 ya bangi zilikamatwa sambamba na mashamba matatu ya bangi yenye ukubwa wa jumla ya ekari moja na robo.

No comments:

Post a Comment