Kutoka Hapa Kwetu Blog
Kuhusu Kunyanyaswa kwa Jaji Warioba
Kati ya mambo
yaliyonishtua sana mwaka huu ni kunyanyaswa kwa Jaji Warioba. Kadhia hii
imetokana na kazi murua aliyofanya Jaji Warioba na tume yake ya
kukusanya mawazo ya wananchi kuhusu Katiba Mpya.
Kumekuwa na mlolongo wa matukio kadhaa ya unyanyasaji huo, ambao, kwa
kadiri ninavyofahamu, mwanzilishi wake ni Ikulu. Tukio la kupigwa Jaji
Warioba mkutanoni, ambalo limeripotiwa sana, ni kilele cha utovu huu.
Wengi tunaamini kuwa Jaji Warioba ananyanyaswa kwa sababu ya uwazi na
uwakilishi wa mawazo ya wananchi, jambo ambalo ni mwiba kwa mafisadi.
Nimeshtushwa vile vile na kauli ya Rais Kikwete kuhusu tukio hili la
vurugu na kupigwa Jaji Warioba. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya
habari, Rais Kikwete aliishia tu kusema kuwa anaomba yasimkute
yaliyomkuta Jaji Warioba. Sikuona popote kama aliongelea suala hili kwa
undani na mapana kama linavyostahili.
Yeye kama Rais, nilitegemea kwanza atambue kuwa vurugu zile ni aibu kwa
nchi anayoiongoza. Nilitegemea awakemee walioleta vurugu zile
zilizohusisha pia kunyanyaswa kwa Jaji Warioba.
Nilitegemea Rais Kikwete atumie fursa ile kuwakumbusha wa-Tanzania,
wajibu wao wa kuheshimiana na kulumbana kwa hoja, sio kwa mabavu.
Angefanya hivyo, nigesema Rais ameonyesha busara za kiuongozi.
Nilitegemea angekemea utovu wa ustaarabu uliojitokeza. Angewakumbusha
wa-Tanzania njia ya usataarabu. badala ya yeye kujiwazia yeye binafsi,
kwamba anaomba yasimpate. Je, kauli yake hii si sawa na kumezea uovu?
Kauli yake haikuonyesha busara za kiuongozi.
Halafu, kuna pia kauli ya Samuel Sitta, ambayo nayo imenikera. Sitta
aliripotiwa akisema kuwa Jaji Warioba alijitakia yaliyomkuta. Niliposoma
taarifa hii, sikuamini kama mzee Sitta, anayetegemewa ana busara,
angeweza kuwa na msimamo kama huo.
Nasikia Sitta ni msomi. Nami najiuliza: ni msomi gani ambaye hatambui
wala kutetea mijadala au malumbano ya hoja. Kusema kuwa Jaji Warioba
alijitakia yaliyompata ni sawa na kumezea suala la mjadala kuingiliwa na
vurugu ambazo hazikubaliki katika mijadala. Kauli ya Sitta ni kama
inahalalisha ukosefu wa ustaarabu unaotegemewa hasa kwa wasomi.
Sijui Sitta alikulia wapi na katika maadili gani. Sisi wengine
tulilelewa katika maadili ya kuwaheshimu wazee. Kitendo cha kumpiga
mzee, kwa mujibu wa maadili yale, ni mwiko kabisa. Kama hukubaliani na
mzee, unapaswa kutafuta namna ya kujieleza, ambayo ni ya heshima kabisa.
Nilitegemea Sitta atambue na kuzingatia hilo. Atoe mfano kwa watoto na
vijana.
Tena na tena, katika jamii yetu, tumezoea kukemea tabia tunazoziiita
haziendani na maadili au utamaduni wetu. Nimeshangaa kuona kuwa Sitta,
ambaye ni mzee, anayetegemewa kuwa mlinzi na mtetezi wa maadili bora,
haonekani kutambua kuwa Jaji Warioba kama mzee, hawezi kuletewa vurugu
kama alizoletewa. Nimekerwa kabisa na kauli ya Sitta na kauli ya Rais..
No comments:
Post a Comment