Edward Lowassa, Anguko la Upinzani
Nchini Na Hadithi ya Bora Shetani Nimjuaye Kuliko Malaika Nisiyemjua!
Na Dkt. Hamisi Kigwangalla
Raia Mwema. Agosti 26, 2015.
Nimekuwa na siku nyingi kidogo sijaandika. Leo nikiwa Arusha
nikitokea msibani Usangi kumzika Mzee wetu na muasisi wa TANU na CCM, Mzee
Peter Kisumo, nilikutana na marafiki zangu wa UKAWA na tukataniana kidogo; na
hapo nikasikia matumaini waliyokuwa nayo, si ya kushinda uchaguzi bali ya
kukidhoofisha chama changu, Chama Cha Mapinduzi, mmojawapo alisema: ‘baada ya
Oktoba CCM na uwanja wa siasa hautabaki sawa na leo…CCM haitokuwa imara na
salama tena.’
Mazungumzo yale yalinifikirisha. Nikafanya tafakuri
tunduizi. Nikaamua kuweka mawazo yangu kwenye rekodi.
Kwa hakika ushindi kwa CCM mwaka 2015 kwenye uchaguzi mkuu
kwa nafasi za Urais, wabunge na madiwani uko wazi kabisa. CCM itapata ushindi
wa kishindo. Kwa nini? Nitafafanua kwa ufupi tu hapa.
Sababu kubwa za kwa nini CCM itashinda mwaka huu ni
zifuatazo; kwanza, CCM ni chama ambacho kimejengwa kwenye misingi na itikadi,
na kina wanachama wengi zaidi wanaoamini kwenye itikadi na misingi hiyo kuliko
wale wachache wanaokiuka, mfano mzuri ni wale wanaofanana na Ndg. Edward
Lowassa ambaye aliondolewa kwenye kinyang’anyiro cha Urais bila maelezo ya
kina, japokuwa wengi wa wachambuzi wa mambo ya kisiasa walibaki wakisema kwa
kiasi kikubwa inawezekana ni historia yake ya kuhusika kwenye moja ya skendo
kubwa kabisa za ufisadi kuwahi kutokea nchini, maarufu kama ‘kashfa ya
Richmond’. Kashfa hii ilipelekea kujiuzulu kwake nafasi ya uongozi wa Waziri
Mkuu.
Pili, CCM ndicho chama pekee chenye muundo thabiti wa
kitaasisi – kutokea kwenye nyaraka mbalimbali zinazoeleweka, muundo wa
utumishi, watumishi na ofisi, muundo wa vikao na ratiba zake, sera, itikadi,
vifaa na majengo, na vitega uchumi vinavyoendeshwa kwa mfumo unaoeleweka,
ukilinganisha na vyama vya upinzani vinavyoendeshwa kwa matukio – ni tukio moja
baada ya jingine, hakuna mfumo wa muundo wa kitaasisi uliosimama na
unaoeleweka. Vyama vingi vya upinzani vinajaribu kuanza harakati za kuunda
mfumo na muundo wa kitaasisi lakini havijafika popote.
Tatu, CCM ni chama chenye wanachama wengi kuliko vyote; kwa
mtaji wa wanachama zaidi ya milioni saba, ukiongeza na wapenzi, washabiki na
watu wanaoamini tu kwenye uwepo wa dola imara inayotokana na CCM, kwa hakika
ushindi kwa CCM ni dhahiri. Namba zina sifa moja kubwa, kuwa huwa hazisemi
uongo.
Nne, CCM itashinda mwaka huu sababu imefanya kazi nyingi na
zinaonekana. Sintozitaja kwenye makala hii.
Tano, CCM inafanya mabadiliko ya uongozi, sera, mikakati
yake ya kuendesha shughuli zake na ina falsafa ya ‘kujikosoa na kukosoana’ na inakubali
kujirekebisha ama kurekebishwa. Tofauti na vyama vingi vya upinzani, ambavyo
toka vianzishwe, baadhi yavyo, mpaka leo hii havijawahi kufanya mabadiliko
kwenye sera, muundo na hata sura za viongozi wake, na badala yake vinaongozwa
na familia ama watu wa kanda ama kabila fulani. Ukitaka kubadilisha sura za
viongozi utakumbana na hasira za waasisi hao wenye vyama hivyo.
Sita, ngome za CCM hazijatikiswa hata kidogo na haziwezi
kuyumba ndani ya miezi hii miwili ya kampeni. Ushindi kwenye serikali za mitaa
wa takribani asilimia 80 ni kipimo tosha kuwa bado CCM ni chama kilichojikita
mpaka kwenye nyumba kumi za kila mtaa/kitongoji, na kwamba bado kinapendwa na
kuaminiwa na watanzania walio wengi.
Saba, kitendo cha UKAWA kuwa tayari kumpokea na kumteua Ndg.
Lowassa kuwa mgombea wao ni pigo kubwa kwao; kwanza ni kiongozi mbabe na
asiyeshaurika, hawezi kukubali kuendeshwa na taratibu za vyama hivyo –
anajiamini yeye ni ‘taasisi’, maarufu na ana timu ya kumfanyia kazi, tayari
tunavyoongea amekwisha wakatisha tamaa wenzake aliowakuta huko, baada ya
kuvijenga vyama vyao kwa jasho na damu kwa miaka zaidi ya 20, ameingia yeye tu
na kateuliwa kuwa mgombea wao, na tayari ameanza kuzitenga timu za kampeni
alizozikuta huko na mifumo ya uongozi aliyoikuta huko na kuanza kutumia makundi
yake ya Urais aliyotoka nayo anakokujua.
Nane, kuna hiki kitu wataalamu wa mambo ya siasa wanaita
‘incumbency advantage’, yaani ‘faida ya kuwepo madarakani’. Hii peke yake,
kisaikolojia, inaiweka CCM juu ya vyama vingine hata kabla hatujaanza kampeni.
Tisa, kwenda kwa Ndg. Lowassa na hatimaye kuteuliwa
kupeperusha bendera ya UKAWA kunafanya kambi ya upinzani, iliyoungana, kwa mara
ya kwanza kuwa kwenye upande wa kujitetea (defensive side) muda wote, nafasi
ambayo hawajazoea kucheza kwenye mechi hizi, badala ya ile ya kushambulia (offensive),
ambayo wameizoea. Pia kwenda kwake UKAWA na wao kumkubali kunajenga mazingira
ya kuwafanya wapinzani waonekane ni wenye tamaa ya kushika dola kwa nguvu zote
hata kama ni kwa kuchukua makapi; kwamba, wanataka kwenda kwenye pepo ya
mwenyezi Mungu hata kama ni kwa kupitia kwa shetani!
Maana kumchukua mtu kama Ndg. Edward Lowassa kuwa mgombea
wao, ambaye walitumia muda mwingi na nguvu zao zote kumchafua, na ambaye
wanapaswa wamshukuru kwa kuwapa umaarufu na heshima nchini – kipindi
wakimchafua, kunaondoa imani ya wananchi juu ya nguvu ya kimaadili (moral
authority) ya wao kukemea ufisadi, na kunazua maswali ya uhalali wao kisiasa
(political legitimacy) na maswali ya thamani yao kiitikadi na kimaadili
(ideological values and integrity): kwamba, kama wiki tatu zilizopita alipokuwa
akigombea kupitia CCM alikuwa shetani, na leo anagombea kupitia UKAWA amekuwa
malaika, kwamba alikuwa shetani kwa miaka 8, na leo amegeuka malaika kwa
kuingia UKAWA.
Kumi, Chama Cha Mapinduzi, kimeteua mgombea mzuri wa Urais.
Ndg. John Pombe Magufuli anamuacha mbali Ndg. Edward Lowassa kwa sifa za
kimaadili, mwonekano wa kiutendaji, imani ya wapiga kura kwenye uwezo wa
kutekeleza ahadi atakazotoa, uwezo wa kuhutubia, uwezo wa kiutendaji, na rekodi
ya mafanikio katika utendaji, uadilifu, elimu na hata uwezo wa kufanya kampeni
na kujieleza.
Kumi na Moja, kwenda kwa Ndg. Edward Lowassa UKAWA kumefanya
watu wanaoamini kwenye mabadiliko ya kweli kutokea nje waone kama wamesalitiwa
maana Ndg. Lowassa si mwanamabadiliko, ni mtu wa mfumo wa kizamani
(status-quo), lakini pia kumefanya wanasiasa walioupa upinzani nguvu na
umaarufu kidogo walionao leo, ni kama hawajui la kusema wala la kufanya.
Ndg. Wilibrod Slaa – hatujui kama amejiuzulu wadhifa wake wa
Katibu Mkuu wa CHADEMA na kama atarejea kwenye majukwaa kumsafisha Ndg. Lowassa
ama ameamua kukaa kimya kabisa – yote ni machungu kwake, amsafishe ili avunje
alichokijenga toka mwaka 2007 na astaafu kwa aibu? Na watanzania wamuone ni mtu
asiyeamini kwenye chochote kile, ama anyamaze kimya, athibitishe kuwa
aliyoyasema kwa kipindi chote hicho ni ya kweli, na kwamba wenzake ni walafi wa
madaraka tu.
Profesa Ibrahim Lipumba, aliyeamua kujiuzuru wadhifa wake wa
Mwenyekiti wa CUF kufuatia ujio wa Ndg. Lowassa amesema hakubaliani na uamuzi
huu wa UKAWA.
Kwa hakika kuna makundi makubwa yaliyodumu kwenye ufuasi wa
wanamageuzi hawa wakongwe kwa muda mrefu watakubaliana nao na hawatounga mkono
UKAWA.
Kumi na Mbili, watanzania watachagua CCM kwa sababu, kwa
wale wanamabadiliko walioamini kwenye mabadiliko kutokea nje ya mfumo hawatoona
jipya linalokuja na UKAWA, wataona hakuna tofauti kati ya CCM na UKAWA na
kwamba wataona bora hata ya CCM imekataa kwa vitendo, pamoja na vitisho vya ‘mafuriko
ya kuigiza ya Ndg. Lowassa’, kwa kumkata jina na hatimaye kumuondoa kwenye mbio
za Urais, kwa tuhuma za ufisadi uliokubuhu. CCM wamefanya hivyo bila kupepesa
macho. Wametoa uongozi kwa nchi, wameonesha kuwa kuna mambo wanayoamini na
wanayasimamia. Upinzani wamempokea na kumpa bendera yao apeperushe. Wapiga kura
wataona hawa wanasiasa wote ni mashetani tu (kama kipimo cha wanasiasa ni
ushetani), na watachagua bora shetani waliyemzoea kuliko malaika wasiyemjua na
ambaye ameanza safari kuelekea kwenye dola kwa kusajili shetani mkubwa kuliko
wote na kumwita ‘malaika’. UKAWA wamemomonyoka kimaadili (moral decay) zaidi ya
CCM kwa kumpa bendera yao Ndg. Lowassa.
Kumi na Tatu, lugha ya CCM kwenye kampeni itakuwa rahisi
sana kutokana na kuwa na mgombea wa upinzani wanayemjua vizuri, na lugha ya
kuwasambaratisha wasemaji wote wa UKAWA itakuwa rahisi sana, maana CCM itakuwa
na kauli zao wakimchafua Ndg. Lowassa alipokuwa CCM na watawakumbusha tu
wananchi.
Kumi na Nne, uwezo wa kifedha wa Ndg. Lowassa utaathirika
kwa sasa akiwa mgombea wa UKAWA kwa maana atahofia kutumia pesa zake nyingi
kwenye kutafuta Urais kupitia upinzani hali ya kuwa anajua hana nafasi ya
kushinda, pia marafiki zake waliokuwa wakimchangia kipindi akiwania Urais ndani
ya CCM wamebaki CCM ama wanahofia kutengwa na CCM mara atakaposhindwa na hawana
imani kuwa atashinda Urais kutokea nje ya CCM, na UKAWA hawana ruzuku ama
vitega uchumi vya kulingana ama kuishinda CCM, hivyo vifaa vya kampeni
(branding materials) ya CCM na uwezo wa kujitangaza utampoteza mgombea huyu
mtata wa UKAWA mara moja kampeni zitakapoanza.
Kumi na Tano, UKAWA hawana sera ambayo itamuunganisha
mgombea wao na kumuuza kwa wananchi sababu UKAWA siyo chama cha siasa, na hivyo
mbali na kumsafisha mgombea wao, hawatokuwa na jipya la kutoa kwa umma
ukilinganisha na CCM ambao watakuwa na ilani ya kueleweka na ambayo wataiuza
kwa wananchi bila shaka.
Je, wataweza kumsafisha Ndg. Lowassa ndani ya siku 64 za
kampeni na watanzania wakawaelewa? Ni maswali watakayopaswa kuyatafakari na
kuyajibu, pengine wakati wanayapatia majibu, muda wa kampeni utakuwa
umeishakwisha na watakuwa wameishashindwa uchaguzi.
Kwa vyovyote vile malengo ya Ndg. Lowassa, kudhoofisha CCM,
hayatotimia na huu utakuwa ni mwisho wake kisiasa, na hatoanguka peke yake,
ataanguka na vyama vyote vya upinzani vinavyounda UKAWA. Baada ya kushindwa
kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, siyo CCM itakayokuwa inarudi kwenye meza
kujipanga upya, bali ni vyama vitakavyosambaratika kutoka UKAWA vitakavyorudi
kujiuliza vilipoangukia na kuanza upya safari ya kujijenga, na hii ni kama hata
kutakuwa na mabaki ya vyama hivyo.
Mtu kama huyu ni kumpuuza... hakuna hata haja ya kumjibu!
ReplyDelete