Baada ya kulihutubia na kulizindua bunge la 11 la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt
JOHN POMBE MAGUFULI amehudhuria hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya
wabunge katika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma na kuagiza fedha
zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla hiyo zipelekwe Katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda vya
wagonjwa.
Mheshimiwa Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa
wadau mbalimbali wamechanga kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya
kugharamia hafla ya wabunge katika siku ya uzinduzi wa Bunge.
Dkt Magufuli amesema alipata taarifa za kuwepo kwa michango hiyo ya
fedha na kutoa maelekezo kuwa zitumike kwa kiasi kidogo kwa ajili ya
hafla hiyo na sehemu kubwa zipelekwe katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili ili zikatumike kununulia vitanda na hivyo kupunguza tatizo la
wagongwa wanaolala chini kutokana na uhaba wa vitanda unaikabili
hospitali hiyo.
“Nilipoambiwa kwamba zimechangwa shilingi milioni 225 zimekusanywa kwa
ajili ya sherehe, nikasema fedha hizo zipelekwe katika hospitali ya
Taifa Muhimbili zikasaidie kununua vitanda” alisema Dkt Magufuli na
kusisitiza kuwa “kwa kufanya hivyo tutakua tumejinyima sisi wenyewe
lakini tutakua tumewanufaisha wenzetu ambao wanamatatizo makubwa
yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo”.
Awali akitoa taarifa ya michango hiyo Ofisa wa Spika wa Bunge Bwana SAID
YAKUBU amesema jumla michango iliyopatikana na shilingi milioni 225 na
kwamba fedha zilizotumika katika hafla hiyo ni shilingi milioni 24 tu
baada ya kuzingatia maagiza ya Rais Magufuli.
Katika Hafla hiyo Rais Magufuli amekabidhi vyeti vya kutambua mchango wa
wadau waliochangia fedha wakiwemo Benki za NMB, CRDB na Benki ya Afrika
pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF na PPF.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano IKULU
November 20, 2015
No comments:
Post a Comment