Saturday, December 17, 2016
Namna na Kuepuka Matumizi Makubwa ya Fedha Kiindi cha Sikukuu
Na Jumia Travel Tanzania
Kwa kawaida kipindi cha sikukuu ni wakati ambao watu wengi huwa na matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kusherehekea pamoja na wapendwa wao, famila, jamaa na marafiki.
Jumia Travel (www.travel.jumia.com) ingependa kukushauri kwamba ni vema ukawa na mpango madhubuti unaoeleweka wa namna gani pesa yako itakavyotumika ili pindi mwaka mpya utakapoingia uwe mwenye furaha na sio huzuni.
Tenga Bajeti Mapema
Kuna namna nyingi za kutenga bajeti kwa ajili ya matumizi yako kama vile manunuzi ya zawadi kwa watoto, wazazi, kutoa msaada pengine na mengineyo ndani ya nyumba. Endapo utapanga mapema itakusaidia sana kujua utahitajika kutumia kiasi gani kipindi hiki badala ya kukurupuka sikukuu zinapowadia.
Fuatilia Mwenendo wa Matumizi Yako
Kutenga bajeti pekee tu haitoshi bila ya kuwa na mbinu sahihi ya kufuatilia mwenendo mzima wa jinsi pesa inavyotumika. Tenga pembeni bajeti ya sikukuu kwa kufungua akaunti ya benki ili isiingiliane na ya matumizi ya kawaida. Unaweza kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha unafanikiwa katika hili, kwa mfano kuwa na programu ya simu, ambayo utakuwa unaweza kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa matumizi na kiasi cha pesa kilichobaki popote na muda wowote ulipo.
Punguza Matumizi Yasiyokuwa na Tija
Unaweza kuepuka au kupunguza matumizi ambayo si ya lazima ndani ya kipindi hiki ili kufidia gharama kwenye vitu vingine. Kwa mfano, kama ulikuwa na mazoea ya kwenda na familia yako kwenye hoteli ya kifahari kwa ajili ya mapumziko kila wikendi pengine gharama yake ni TSHS 100,000/- kwa wiki ambayo ni sawa na TSHS 400,000/- kwa mwezi, unaweza kuacha kwa mwezi huu ili kuitumia kwa mambo mengine.
Pendekeza Utaratibu wa Kununuliana Zawadi kwa Siri
Kwa bahati mbaya familia nyingi za kiafrika sio wenyeji wa utamaduni huu wa kununuliana zawadi kwa siri au ‘Secret Santa’ kama inavyojulikana kwa lugha ya Kiingereza. Mbinu hii ina manufaa makubwa sana kama utataka kuepuka gharama kubwa za kumnunulia zawadi kila mwanafamilia, kwa mfano, pengine una baba, mama, kaka, dada, binamu, wajomba na mashangazi unaweza ukautambulisha utaratibu wa kila mtu kumnunulia zawadi mwenzio kwa siri na kumkabidhi siku ya sikukuu. Nadhani inaweza kuleta msisimko zaidi na kila mtu akafurahia.
Epuka Mila Zitakazo Kugharimu
Kuna baadhi ya makabila bado yana taratibu ambao huwalazimu wanakoo kukutana kwa pamoja ifikapo kila mwisho wa mwaka. Watu hulazimika kusafiri na kutumia gharama kubwa kwa karamu ambazo huandaliwa na kujikuta mwaka unaanza wakiwa hawana fedha za kutosha. Unaweza kuepuka hayo yote kwa kufanya vitu vya kawaida ambavyo familia yako itavifurahia na kuvipenda.
Kuwa Mwangalifu na Ofa za Mauzo
Inabidi kuwa makini sana na ofa zinazotolewa na wauzaji wa bidhaa mbalimbali ndani ya kipindi hiki cha sikukuu. Wafanyabiashara ni werevu sana kwani hutumia mbinu mbalimbali za kuuza bidhaa zao kwa kuweka mabango makubwa ya ‘Ofa Ofa!’ huku bei ikiwa ni ileile sawa na siku za kawaida. Kuepuka hili unapaswa kufanya tafiti mapema kwa kutembelea maduka au mitandao ili kujua kama ni kweli kuna unafuu kwenye hizo bei zinazotangazwa.
Jitahidi Kutokuzidisha Manunuzi Yako
Kutokana na ofa kemkem ndani ya kipindi hiki cha sikukuu wateja wengi hujikuta njia panda kwa kushindwa kujizuia kuzidisha manunuzi wanayoyafanya. Inashauriwa kuwa na orodha pamoja na bajeti ya vitu unavyotaka kwenda kuvinunua ili pindi umalizapo usizidishe kwa kutamani vingine. Kama ikiwezakana fanya manunuzi mapema kabla ya sikukuu yenyewe ambapo kutokana na punguzo kubwa la bei ukajikuta unataka kununua kila bidhaa.
Mwisho kabisa Jumia Travel (www.travel.jumia.com)
inakukumbusha kufanya tathmini ya pesa na matumizi uliyoyafanya ili kujua kama ulikuwa ndani ya bajeti kama ulivyojipangia au la. Kwa kufanya hivyo, utakuwa na mkakati mzuri wa kuanza mwaka mpya bila ya msongo wa mawazo.
No comments:
Post a Comment