Saturday, May 27, 2017
Mkutano Mkuu wa Vijana Kimataifa Kufanyika Arusha
Mkutano Mkuu wa Vijana Kimataifa Kufanyika Arusha kwa Siku 7
[caption id="attachment_79335" align="aligncenter" width="800"] Mratibu wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kwa Vijana Tanzania, Tajiel Urioh akizungumza na waandishi wa habari leo (hawapo pichani) kuzungumzia Mkutano Mkuu Kivuli wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa unaokutanisha vijana utakaofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 26 mwezi Mei, 2017 mjini Arusha katika Ukumbi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Arafat B. Lesheoe.[/caption]
AKIZUNGUMZA na waandishi wa habari Mratibu wa Mkutano Mkuu Kivuli wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa, Tajiel Urioh alisema mkutano huo ni maigizo ya vitendo ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa ambapo vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 30 kutoka sehemu mbalimbali wanapata fursa ya kujifunza Diplomasia, Uongozi na namna Umoja Wa Mataifa unavyofanya kazi.
Bw. Tajiel Urioh alisema kuwa, Mkutano huo unaojulikana kama kongamano kubwa kabisa la vijana nchini linalowaleta pamoja vijana wadogo kutoka nchi mbalimbali tangu mwaka 1997. Aidha aliongeza kuwa Mkutano huo Mkuu Kivuli wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa utafanyika mjini Arusha katika Ukumbi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kuanzia tarehe 22 hadi 26 mwezi wa Mei mwaka 2017, ambapo vijana takribani 200 kutoka katika nchi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria kujadili masuala yanayohusiana na Afya ya Uzazi na Uzazi wa Mpango, Demokrasia na Amani katika nchi zinazoendelea, Kuhama kuelekea kwenye Nishati safi na ya teknolojia mbadala na Elimu kwa Maendeleo Endelevu.
Aliongeza kuwa majadiliano ya mwaka huu yatajikita katika mada kuu: “Kuwawezesha Vijana katika Diplomasia na Uongozi”. Mada hii inalenga kuwezesha ushiriki wa vijana na kuwajengea uwezo kwenye masuala ya Diplomasia na Uongozi kwa kuwapa mafunzo ya vitendo katika mada ngumu ambazo zitawaongezea ujuzi wa majadiliano na kufikia muafaka wa masuala mtambuka yanayogusa maslahi ya mataifa.
"Tunaishi katika ulimwengu ambao diplomasia yenye ujasiri na uongozi vinahitajika sana hivyo basi kuwakuza vijana katika uwanja huu itachangia kukua kwa mataifa yenye watu wenye uwezo wa kuamua mambo yao. Katika mkutano wa mwaka huu wajumbe watakuja na maazimio mbalimbali ambayo kwa namna moja hama nyingine yatakuwa na manufaa katika maisha yao ya kila siku na watu wanaowazunguka katika jamii zao," alisema Bw. Urioh.
[caption id="attachment_79334" align="aligncenter" width="800"] Mratibu wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kwa Vijana Tanzania, Tajiel Urioh akizungumza na waandishi wa habari leo (hawapo pichani) kuzungumzia Mkutano Mkuu Kivuli wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa unaokutanisha vijana utakaofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 26 mwezi Mei, 2017 mjini Arusha katika Ukumbi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Kushoto ni Ofisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Bi. Stella Vuzo akiwa katika mkutano huo pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Arafat B. Lesheoe.[/caption]
“Ni matarajio yangu makubwa kwamba mtakuwa tayari kujifunza kuendana na mada kuu ya ‛ Kuwawezesha Vijana katika Diplomasia na Uongozi′ lakini pia kubadilishana mawazo na wajumbe wengine na kutengeneza mtandao wa vijana wenye fikra mnazoendana nazo,” aliongeza Tajiel Urioh, Mratibu wa Kitaifa wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2017.
Ofisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Bi. Stella Vuzo alisema kongamano kama hilo la vijana lina umuhimu mkubwa kwa vijana kwani huwajenga vijana kupitia Club za UN. Aliwataja miongoni mwa vijana ambao ni matunda ya Club za UN ni pamoja na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Antony Mavunde, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Benedict Kikove, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Salum Hapi, Mbunge wa Kibamba (Chadema), John John Mnyika na wengine wengi.
No comments:
Post a Comment