

Bila shaka wadau wengi mmesoma vitabu vya African Writers Series. Hivyo jina la Sembene Ousmane si ngeni kwenu. Alikuwa ni MSenegal. Alitunga vitabu vingi vikiwemo, God's Bits of Wood, na Xala.
Zaidi ya kuandika vitabu, marehemu Sembene alikuwa ni muongoza sinema maarufu barani Afrika. Alikuwa anaitwa, " The Father of African Cinema" yaani baba wa sinema Afrika. Hiyo ni kwa sababu alikuwa ni mwafrika wa kwanza kujulikana katika viwanjavya sinema vya kimataifa kama Hollywood. Huenda mmeona sinema zake za Xala, Faat Kine, Black Girl na Moolaade. Aliongoza kama sinema kumi na tano. Huko Afrika Magharibi hasa nchi zilizotawaliwa na Mfaransa (francophone) zimeendelea sana katika sinema kuliko nchi zilizotawaliwa na Mwingereza. Sinema zao huwa zina ubora zaidi kuliko za Anglophone.
Kwa kweli sijui kama alifariki mpaka jana nilipokuwa naangalia sherehe za Academy Awards (Oscars). Katika kumbukumbu ya waliofariki mwaka uliyopita alikuwemo. Mbona nilishutuka.
Sembene Ousamane alifariki nyumbani kwake Dakar, Senegal, mwezi Juni mwaka jana. Alikuwa na miaka 84.
REPOSE EN PAIX - REST IN PEACE


