Na Swahilivilla blog. Washington D.C
Jana ililkuwa ni "Siku ya Maruhani" nchini Marekani. Siku hii ijulikanayo kama "Halloween" husherehekewa kila tarehe 31 Oktoba, na ina historia ndefu.
Siku ya Maruhani ilianzia huko barani Ulaya kiasi miaka 2,000 iliyopita ikifungamana na imani za kishirikina. Wazung walipoyavamia mabara ya Amerika walihamia pia na utamaduni mila, desturi, dini, na silka zao - na sema upendavyo. Miongoni mwa hayo ilikuwa ndiyo hii siku ya Maruhani ambayo jina lake la asili ni "Samhein".
Sherehe za Maruhani Photograph by treasuredragon/iStock.
Tuyaachie ya historia kwa wanahistoria, lakini kwa ufupi hii iliaminika kuwa ni siku ambayo pepo, majini, maruhani, mazimwi na mizimu au mizuka ya watu waliokufa hurejea hapa duniani katika maeneo yao ya asili na kujichanganya na watu waliohai.
Maudhui kuu ya siku hii ni kutisha, kuadhibu na mauti, ingawaje katika enzi zetu za leo imekuwa ni siku kuu ya watoto zaidi kuliko watu wazima. Sherehe zake hufanyika kuanzia familia, mitaa, makazini na hadi kufikia Ikulu yenyewe. Rejea kwenye toleo la jana la Swahilivilla uone Ikulu ya Marekani ilivyoadhimisha siku hii akiwepo rais Obama na familia yake.

Wana maruhani wakiwa katika kwaride. (Photo Jefferson Siegel/New York daily news)
Kama ambavyo kila siku kuu au sherehe huwa zinaaambatana na ada maalum ambazo zikikosekana basi siku hiyo huwa kana kwamba haijatimia, Siku ya Maruhani nayo pia ina ada na desturi zake. Na kama zilivyo sherehe nyingi hapa Marekani siku hii pia nayo imekuwa fursa ya wafanyabiashara kujipatia rizki zao.
Mapambo: Shamra shamra za Siku ya Maruhani huanza mapema, pengine tangu mwezi wa Septemba kwa kuweka mapambo kwenye majumba, mabarabara na hata sehemu za kazi na biashara.
Na kama tulivyotangulia kusema, mapambo yote huwa yanalenga kwenye hali ya kutisha, kuadhibu na mauti. Miongoni mwa mapambo hayo ni buibui na nyumba zao, popo wakining'inia, mifupa na mabufuru ya vichwa vikiashiria watu waliokufa, panga, paka weusi, masanamu ya mizuka au mazombi na vimbwanga vyengine. Almradi kuonesha kuwa nyumba zimesibiwa na maruhani (haunted house). Si hasha ukapita vichochoroni ukakutana na kitu ukashtuka. Kwa ufupi ni kama vile tunavyoona kwenye picha za kutisha (scary movies).





