Showing posts with label Natural Gas. Show all posts
Showing posts with label Natural Gas. Show all posts
Saturday, October 26, 2013
Thursday, September 12, 2013
Reginald Mengi Ajibu Suala la Gesi
Kutoka Ipp Ltd.
Septemba 7, 2013 nilipokea barua pepe (email) yenye kichwa cha habari kisemacho “ubinafsi/ufisadi wa MENGI na Chuki/Fitina kwenye Maendeleo”.
Aliyetuma email hiyo alijitambulisha kama “CCM TANZANIA” na email ilisambazwa kwa vyombo vya habari, waandishi na watu wengine wengi wakiwamo wanasiasa. Kabla ya hapo nilifowadiwa nakala ya ujumbe (SMS) na watu ambao walitumiwa na Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge inayosema;
“Ambieni Watanzania: Kampuni za Mengi zimeshikilia vitalu 59 vya madini vyenye ukubwa wa mita za mraba 3,752.37 (sq km) Amevishikilia, ameshindwa kuviendeleza. Watanzania wanakosa mapato na ajira! Sasa anataka vitalu vya gesi na mafuta. Je huu ndio uzawa?
Na
“Mengi hana uzawa bali ubinafsi. Anataka kufanya udalali wa vitalu vya raslimali zetu. Waelezeni Watanzania ukweli huu.”
Vile vile Septemba 5, 2013 Profesa Muhongo akijibu swali la Mwandishi wa habari lililouliza;
“Mhe. Waziri tunataka ufafanuzi kuhusu kauli yako ya hivi karibuni kwamba waTanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika uwekezaji wa gesi asilia. Kwanza kauli hii ni kweli? Pili kauli kwamba Watanzania wanaweza kuwekeza kwenye sekta ya machungwa tu huoni kwamba si kwamba unawavunja moyo bali unadhalilisha wewekezaji wazalendo?”
Na Profesa Muhongo akajibu:
“Kila mtu alitoa mawazo ya sera ya gesi wakiwemo TPSF. Mengi na wenzake wanataka vitalu wafanye ulanguzi wa gesi na mafuta yetu. Tutatoa orodha ya vitalu vya madini vilivyoko mikononi wa Mengi ambavyo anafanya ulanguzi. Ukweli utaonyesha ubabaishaji na ulanguzi wa Mengi wa genge lake.”
Nimeona ni vyema nitumie haki yangu ya kujibu (right of reply), lakini kwa wale wanaohusika kusambaza taarifa hizo kuchafua jina langu wajue kwamba kujibu kwangu hakuondoi haki yangu ya kuchukua hatua za kisheria.
Kuingizwa kwa vitalu vya madini katika hoja ya gesi
Huo ni upotoshwaji wenye lengo la kututoa kwenye hoja ya msingi ya rasilimali yetu ya gesi. Sijawahi kufanya udalali kwenye vitalu vya madini. Huu ni uongo wa hali ya juu.
Tamko la TPSF na majibu ya Profesa Muhongo
Siku ya Agosti 28, 2013 Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) ilifanya kikao chake cha Bodi na baadaye kufanya mkutano na waandishi wa habari. Mambo mengi yalizungumzwa katika kikao hicho ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa Watanzania (Economic Empowerment).
Kuhusu uwezeshaji Watanzania, mambo muhimu matatu yalijadiliwa na kutolewa mapendekezo. Mambo hayo ni 1) Manunuzi ya Umma (Public Procurement); 2) Ardhi na uvuvi; na 3) suala la gesi asilia.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari, mimi nikiwa Mwenyekiti wa TPSF, niliwasilisha maoni ya TPSF kuhusiana na Manunuzi ya Umma, wakati Makamu Mwenyekiti wangu, Salum Shamte, aliwasilisha maoni yetu kuhusiana na sekta ya ardhi na uvuvi na mwishoni Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, aliwasilisha maoni TPSF kuhusiana na gesi asilia.
Katika maoni yake TPSF ilisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi wa gesi na kushauri kusitishwa ugawaji wa vitalu vya gesi hadi hapo sera ya gesi itakapokua tayari. Mwisho Bwana Simbeye alisema kwamba TPSF itaomba kukutana na Profesa Muhongo kuwasilisha mawazo na mapendekezo ya taasisi hiyo.
Siku chache baada ya TPSF kutoa maoni yake mambo mawili yalitokea. Kwanza Profesa Muhongo alijibu kupitia vyombo vya habari kwamba mpango wa kugawa vitalu vya gesi na kuingia mikataba utaendelea.
Profesa Muhongo pia alisema wazi kwamba hana mpango wa kukutana TPSF, kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda.
Matokeo yake Profesa Muhongo hajajibu hoja kuhusiana na barua aliyoandikiwa na TPSF. Binafsi nilishitushwa na msimamo wa Profesa Muhongo kwani Serikali ya awamu ya nne imepiga hatua kubwa katika kudhihirisha kuwa ni “serikali sikivu”. Ingemgharimu nini Profesa Muhongo kukaa na kutusikiliza? Hakuna ambacho angepoteza zaidi ya dakika chache za muda wake.
Jambo la pili ambalo lilitokea ni mimi binafsi kushambuliwa kana kwamba maoni yaliyotolewa kuhusiana na gesi ni maoni yangu binafsi na si ya TPSF.
Mifano ya mashambulizi dhidi yangu ni kama nilivyoonyesha hapo juu katika email na ujumbe mfupi wa simu (SMS).
Msimamo wa Profesa Muhongo katika gesi ni upi?
Msimamo wa Profesa Muhongo mara baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ulikuwa ni kutaka kupitishwa kwanza kwa sera ya gesi asilia kabla ya kuendelea na ugawaji wa vitalu vya gesi.
Septemba 2012, Profesa Muhongo alisema;
“Some of the agreements are really shoddy and they need to be revoked” and “I can’t tolerate agreements which are not in the country’s interests but they benefit a few individuals”.
Tafsiri yake ni:
“Baadhi ya mikataba ni ya ovyo, na inahitaji kuvunjwa” na “Sitovumilia mikataba ambayo haina maslahi kwa nchi na inawanufaisha wachache”.
http://www.energy-pedia.com/news/tanzania/new-151679
Baada ya hapo, Profesa Muhongo aliamrisha Bodi mpya ya TPDC kusitisha ugawaji wa vitalu vya gesi ambao ulipangwa kufanyika mwezi Septemba 2012 na kupitia upya mikataba yote. Profesa Muhongo alinukuliwa akisema:
‘Earlier this month, the state-run Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) delayed a licensing round for nine deep-sea oil and gas blocks previously set for this month until a parliamentary vote on a new gas policy in October. "Right now as a country, we are in the gas boom and we don't have gas policy in place.”
[…]
Recent gas strikes off east Africa's seaboard have led to predictions the region could become the third largest exporter of natural gas on the planet.
"Our country is reviewing its policy. Is that something new?" he said. "We want both the companies that are investing in the country and Tanzanians to benefit from the oil and gas projects."
[…]
"This is completely new business to us. We are learning," Muhongo said.’
Tafsiri yake ni:
‘Mwanzoni wa mwezi huu TPDC ilihairisha mchakato wa ugawaji wa vitalu tisa vya gesi asilia vilivyoko baharini hadi hapo Bunge litakapopitisha sera mpya ya gesi iliyowasilishwa bungeni mwezi Oktoba;
"Kwa sasa kama Taifa, tuko katika mazonge ya gesi na hatuna sera ya gesi.
"Nchi yetu inaandaa sera (ya gesi). Hicho ni kitu kipya?..."
"Tunataka kampuni zote, kampuni zinazowekeza nchini mwetu na Watanzania tunufaike na miradi ya gesi na mafuta."
"Hii ni biashara mpya kabisa kwetu. Tunajifunza."
http://www.reuters.com/article/2012/09/18/tanzania-exploration-idUSL5E8KIPEJ20120918
Zoezi wa la kugawa vitalu vya gesi asilia lilisitishwa lakini hadi sasa matokeo ya kupitia upya mikataba hayajatolewa hadharani.
Miezi michache baadaye, Februari 26, 2013, Profesa Muhongo alisisitiza msimamo wake wa kutaka Tanzania kuwa na sera ya gesi kabla ya kugawa vitalu zaidi. Aliyasema hayo alipokua akihutubia mkutano uliofanyika Chatham House, mjini London. Mkutano huo uliopewa jina “Tanzania: An Emerging Energy Producer”. Ulikuwa na madhumuni ya:
“Tanzania is drawing growing attention as a pivotal country in East Africa for oil and natural gas exploration, having led the region in terms of new discoveries of natural gas in 2012. With known gas reserves of approximately 7.5 billion cubic feet, the potential to transform Tanzania's international standing and domestic electricity production is considerable. However, recent protests against the construction of a pipeline to Dar es Salaam highlight the challenges that Tanzania faces in ensuring that the benefits of its natural resources are widely felt.
Tafsiri yake ni:
“Tanzania inaonyesha kuja juu katika Afrika Mashariki kwa uvumbuzi wa mafuta na gesi asilia baada ya kuongoza kwa uvumbuzi wa gesi asilia mwaka 2012. Ikiwa na wastani wa futi za ujazo bilioni 7.5, ni dhahiri itasaidia Tanzania kupaa katika anga za Kimataifa na kusaidia uzalishaji wa umeme kwa matumizi ya ndani. Hata hivyo, vurugu za hivi karibuni kupinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam inaashiria changamoto mpya ambazo Tanzania sasa inakabiliana nazo kuhakikisha kwamba manufaa ya gesi asilia yanawafikia watu wengi zaidi wa chini.”
Alichowasilisha Profesa Muhongo katika mkutano huo kwa ufupi kinapatikana katika tovuti hii;
http://www.chathamhouse.org/events/view/189235
Kama inavyonekana kwenye kiambatanisho, moja ya nyaraka aliyowasilisha Profesa Muhongo inaonyesha kwamba mchakato wa kuanza ugawaji wa vitalu ungeanza baada ya kupitishwa kwa sera ya gesi.
Hadi sasa hatuna sera ya gesi asilia.
Lakini jambo la kushangaza, Profesa Muhongo amebadilika na anataka vitalu vigawiwe kabla ya kuwapo kwa sera gesi.
Sababu za kubadilika kwa Profesa Muhongo hazina mashiko
Profesa Muhongo amenukuliwa na gazeti la Daily News la Agosti 31, 2013 akieleza sababu zake za kutaka vitalu vigawanywe kabla ya kupitishwa kwa sera ya gesi. Sababu kuu alizozisema ni tatu; (1) Ushindani wa soko na majirani zetu akitolea mfano wa Msumbiji (2) Sheria ya mwaka 1960 iliyoanzisha TPDC na Sheria ya Petroli ya mwaka 1980 kwamba zinatosha kusimamia ugawaji wa vitalu akimaanisha sera na sheria mpya zitafuata baada ya ugawaji wa vitalu; na (3) Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika sekta hii akimaanisha waachiwe wageni peke yao.
Maelezo kwamba tunashindana na Msumbiji haya halalishi ugawaji vitalu kabla ya sera. Utafiti wa gesi asilia ni jambo linachokua muda mrefu, ndio maana TPDC wanaingia kwenye mikataba ya muda mrefu (isiyozidi miaka 11 kwenye utafiti na miaka 25 kwenye uchimbaji). Kwa hiyo kusubiri miezi michache ili Bunge letu liidhinishe sera, haiwezi kuathiri ushindani wa kibiashara. Hata nchi Msumbiji anayoizungumzia hivi sasa inapitia upya mpango wake wa uwekezaji katika gesi asilia na kuingiza sera na sheria mpya zitakazo simamia rasilimali hiyo. Katika mahojiano yaliofanyika na jarida la Africa Report mwezi Julai mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati wa Msumbiji, Mh. Abdul Razak Noormahomed, alisema madhumuni ya mabadiliko hayo ni kuwapa kipaumbele wananchi wa Msumbiji.
Mohojiano haya yanapatikana katika anuani ifuatayo:
http://www.theafricareport.com/Interview/extractive-industry-the-goal-is-to-give-an-edge-to-mozambicans-noormahomed.html).
Kama nilivyoeleza hapo juu, mara baada ya Profesa Muhongo kuingia wizarani alisema kinaga ubaga kwamba sheria iliyopo haikidhi mahitaji ya sekta ya gesi asilia ndiyo maana akasimamisha ugawaji wa vitalu vya gesi na kuamrisha mikataba ipitiwe upya na sera ipatikane. Leo tunashuhudia Profesa Muhongo akila matapishi yake na kusema kwamba sheria zile zile alizoziponda sasa zinafaa.
Kauli ya Profesa Muhongo kwamba wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza tu kushiriki biashara ya juisi na soda na hawana uwezo wa kushiriki katika biashara ya gesi yao ni dharau.
Kigezo gani Profesa Muhongo anatumia kutoa kauli ya jumla yenye kutawaliwa na hisia? Amefanya utafiti gani kupima uwezo wa kifedha wa wafanyabiashara wa kitanzania? Kwa taarifa yake, wapo wafanyabiashara wengi ambao wanaweza kupata fedha kwa ajili ya kuchimba visima vya gesi.
Ni dhahiri kwamba Profesa Muhongo anathamini tu kampuni za kigeni, anasahau kwamba kuna mifano ya kuwapo kampuni za kigeni ambazo zimekua zikifanya udalali hapa nchini kwa miaka mingi kwenye rasilimali za nchi yetu ikiwa ni pamoja na madini na gesi.
Uzalendo wangu:
Ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi si mzalendo Wantanzania wanafahamu ukweli. Vile vile ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi ni mbinafsi na sipendi maendeleo ya Watanzania wenzangu kwa hili pia Watanzania wanafahamu ukweli
Kuhusu Kilimanjaro Hoteli na mgogoro na Yussuf Manji n.k, mtizamo wako unategemea wewe upo katika kundi lipi kati ya kundi safi la waadilifu au kundi chafu la wala rushwa. Watanzania wanafahamu msimamo wangu kwenye hili.
Mimi sipingi kuwepo kwa wawekezaje wageni katika sekta ya gesi lakini kuna mambo mawili napigania. Kwanza Watanzania wanufaike na rasilimali yao ya gesi na pili iwepo sera ya gesi inayotoa kipaumbele kwa Watanzania
Mimi napenda maendeleo ya nchi yangu; kwa hiyo hata siku moja siwezi kupinga uwekezaji ama ubia na wawekezaji. Ninachosimamia ni manufaa kwa nchi yangu.
Tuhuma kwamba nafanya kampeni dhidi ya wizara
Tuhuma kwamba nimeandaa kongamano kwa ajili ya vijana wa Chadema si za kweli. Huu ni uzushi usio na kichwa wala miguu. Vile vile madai kwamba naitumia vibaya vyombo vya habari vya IPP Media si ya kweli hata kidogo ikizingatiwa kwamba hata mahojiano ya Profesa Muhongo kwa simu akiwa Austria, yalirushwa na kituo cha redio cha Radio Stereo kinachomilikiwa na kampuni yangu ya ITV-Independent Television Limited.
Hitimisho
Julai mwaka huu, Rais wa Marekani Barack Obama, alihitimisha ziara yake ya Kiserikali nchini Tanzania, kwa kusema;
“Ultimately the goal here is for Africa to build Africa for Africans.”
Akimaanisha kwamba, Hatimaye Lengo ni Africa kujenga Africa kwaajili ya Waafrica
Profesa Muhongo asipingane na ushauri huu mzuri.
Nimalizie kwa kuwahakikishia Watanzania kwamba mashambulizi binafsi dhidi yangu yenye nia mbaya ya kunishushia heshima hayatakaa yafanikiwe.
Wenu,
Dk. Reginald A. Mengi
![]() |
| Dk. Reginald Mengi |
Labels:
\,
Gesi,
Mining,
Natural Gas,
Natural Resources,
Reginald Mengi
Thursday, January 03, 2013
Maandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji
![]() |
| Maandamano dhidi ya Bomba la Gesi
Picha Hisani ya: Mtwara Kumekucha Blog by Baraka Mfunguo |
Na Mh. Zitto Kabwe
Malumbano kati ya wananchi wa Mtwara na Serikali kuhusu matumizi bora ya utajiri wa nchi yameendelea kwa takribani wiki moja sasa. Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Waziri wa Nishati na Madini kuwaita Watanzania wa Mtwara Wahaini, wapuuzi na watu hatari, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye aliingia kwenye mjadala huo kwa kuonya watu wanaowaunga mkono watu wa Mtwara na kuwaita watu wanaotafuta umaarufu wa kisiasa na wanaotaka kugawa nchi. Siku moja baada ya hotuba ya Rais, Waziri wa Nishati na Madini alifanya mkutano na waandishi wa habari kueleza suala lile lile ambalo bosi wake alilielezea usiku wa kuamkia mwaka mpya 2013. Hii ni dalili ya Serikali kuweweseka.
Katika kauli ya Serikali, ambayo haikuwa na jipya zaidi ya wimbo ule ule wa ‘kugawa nchi’ ‘umaarufu wa kisiasa’ nk, Serikali ilitaka kuonyesha umma kuwa watu wa Mtwara hawana shukurani. Kwamba miaka yote toka Uhuru watu wa Mtwara wamekuwa wakilishwa na Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Sukari, Kidatu nk. Kwamba watu wa Mtwara na Lindi hawakuchangia hata kidogo kwenye hazina ya Taifa. Hivyo wao kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na roho mbaya na kukosa shukurani. Kauli ya Serikali ni kauli ya chombo kinachoendelea kukosa ‘legitimacy’ ya kuongoza taifa. Ni kauli ya kukata tamaa. Ni kauli hatari sana dhidi ya Watanzania waliojitolea damu kulinda uhuru wa nchi yetu.
Moja, Serikali katika kauli yake haitaji kabisa kwamba toka Uhuru watu wa Mtwara na Lindi wamekuwa wachangiaji wakubwa sana katika uchumi wa Taifa kupitia zao la Korosho. Takwimu za Uzalishaji wa Korosho zinaonyesha kwamba kuanzia mwaka 1965 mpaka 2011 Korosho imeliingizia Taifa fedha kigeni jumla ya dola za Kimarekani 4.58 bilioni ( Cashewnuts Sub-sector study 2003, Hali ya Uchumi 2012, Cashewnuts Tanzania Report 2010). Katika Mwaka wa Uchumi unaoishia Novemba 2012, Korosho imeliingizia Taifa jumla ya dola za Kimarekani 151 milioni. Katika mwaka 2011 zao hili liliingiza dola 130 milioni wakati Pamba iliingiza dola 53 milioni tu. Licha ya Zao la Korosho kuingiza fedha hizi za kigeni (sawa ni shilingi trilioni 7.2) kwa nchi mikoa ya Lindi na Mtwara ipo miaka 50 nyuma kimaendeleo kulinganisha na mikoa mingine ya Tanzania. Serikali inataka kufuta historia ya mchango wa zao la Korosho kwenye uchumi wa nchi yetu kwa sababu ya uroho wa gesi asilia. Kwa nini kauli rasmi ya Serikali haijataja Korosho kabisa? Kauli hii ilipitishwa na ngazi zote za Serikali? Mawaziri wa Serikali wanaotoka mikoa ya Lindi na Mtwara walikubali kauli kama hii itoke dhidi ya wananchi wao wanaoteseka na zao la Korosho miaka nenda miaka rudi?
Pili, Serikali imesahau kabisa mchango wa watu wa Lindi na Mtwara katika ulinzi wa Taifa letu. Moja ya sababu ya mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa nyuma kimaendeleo ni juhudi za ukombozi wa kusini mwa Afrika. Kambi ya wapigania uhuru wa Msumbiji ilikuwa Nachingwea. Kambi ya Frelimo iliwekwa kwenye Shamba la Mkonge kilometa 17 tu kutoka mjini Nachingwea ambapo ilikuwa makao makuu ya ukombozi wa Msumbiji. Rais Samora Machel, Rais Joaqim Chissano na Rais Guebuza waliendesha mapambano kutoka kusini mwa Tanzania. Makaburu wa Afrika Kusini na Wareno walikuwa wanashambulia nchi yetu na mikoa hii miwili ya Lindi na Mtwara ikawa ‘buffer zone’. Wakati Dar es Salaam inaendelea kwa kila aina ya maendeleo, mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa inalinda ili wanaoishi Dar es Salaam na mikoa mingine waishi wa amani na starehe. Serikali inapimaje mchango huu wa mikoa hii? Tunaipima kwa fedha? Uroho wa gesi asilia kuzalisha umeme wa kufurahisha walalaheri asilimia 14 nchini ndio inaifanya Serikali kusahau kabisa ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara katika kulinda uhuru wa Taifa letu?
Tatu, Serikali inasema lazima bomba lije Dar es Salaam kwa sababu Dar ndio inazalisha asilimia 80 ya Mapato ya Serikali. Kwanza huu ni uwongo. Ni aibu Serikali kujitetea kwa uwongo. Dar es Salaam ni kituo tu cha kukusanyia mapato ya Serikali. Uzalishaji mkubwa wa nchi yetu wenye kuzalisha kodi unafanyika nje ya Dar es Salaam. Walipa kodi wakubwa wengi Ofisi zao Kuu zipo Dar es Salaam lakini uzalishaji wao unafanyika nje ya Dar es Salaam. Serikali itoe orodha ya walipa kodi wakubwa 100 tuone uzalishaji halisi wa mapato hayo unafanyika wapi. Hata hivyo inawezekana kuwa ikawa kweli Dar es Salaam inakusanya asilimia 80 ya mapato ya nchi. Basi na tuseme Dar es Salaam inachangia asilimia 90 ya ufisadi wote nchini. Kashfa zote kubwa za Ufisadi zinafanyika Dar es Salaam na fedha nyingi za ufisadi zinatumika Dar es Salaam.
Mwisho, maandamano ya watu wa Mtwara ni kielelezo tosha kwamba watu wa mikoa ya Lindi na Mtwara wamechoshwa na longolongo za Serikali. Wananchi wa Mtwara na Lindi wanataka Uwajibikaji wa Serikali kuhusu utajiri wa nchi. Mtanzania yeyote mwenye tahadhari ya nchi yetu kutokuwa na laana ya rasilimali ataungana mkono na watu wa Lindi na Mtwara kudai maendeleo. Nilitoa mfano wa Mgodi wa Golden Pride ambao umemaliza dhahabu yote tani 76 katika eneo la Lusu wilayani Nzega. Kampuni ya Resolute ya Australia iliwekeza dola 370 milioni kuanzia mwaka 1998 (mkataba wao ulisainiwa 25th June 1997). Katika kipindi cha uhai wa mgodi, miaka 14, Kampuni hii imeuza dhahabu ya thamani ya dola za kimarekani 3.3 bilioni. Kabla Serikali haijawaita watu Mtwara wahaini, wapuuzi na watu hatari, iwaambie watu Watanzania kodi kiasi gani imekusanywa kutoka mgodi huu katika kipindi cha miaka 14. Mpaka mwaka 2008, kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Bomani, kampuni hii ilikuwa imelipa mrahaba wa dola 11 milioni na kodi nyingine dola 16 milioni. Serikali itwambie ilipofika Disemba 2012 kodi kiasi imekusanywa kutoka kampuni hii?
Pia watu wa Mtwara na Lindi wameona historia ya bomba la Songosongo. Hata kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (0.3%) ilikuwa inalipwa Halmashauri ya Manispaa Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Ilichukua juhudi za mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu kuingilia kati ndio kodi ikaanza kulipwa Kilwa ambapo uzalishaji unafanyika. Watu wa Mtwara ni werevu, wanajua wafanyalo. Wanataka utajiri wa nchi unufaishe nchi kwa kuanzia kule utajiri ulipo. Kuna dhambi gani?
Uwajibikaji katika uvunaji wa Rasilimali ya Gesi ndio chanzo cha maandamano ya watu wa Mtwara. Serikali isikimbilie kulaumu wanasiasa kwamba ndio wamechochea maandamano haya. Haya ni maandamno ya wananchi wakitaka Serikali yao iwajibike kwao. Serikali ithubutu kufanya ubabe wa kujenga bomba la gesi bila ridhaa ya Wananchi wa Lindi na Mtwara. Wananchi wanapohitaji uwajibikaji ni wajibu wa Serikali kuwajibika kwao ni sio kuwaita wahaini, wachochezi, watu hatari, wapuuzi. Watu wa Mtwara wamechangia maendeleo ya Taifa letu kwa jasho na damu. Serikali ina wajibu wa kuwasikiliza, kuwaelimisha na kupata mwafaka. Kauli ya Serikali imewatukana watu wa Mtwara na Lindi. Hawatakubali kudhalilishwa. Hawatakubali historia yao kufutwa. Hawatakubali waendelee kubaki nyuma kimaendeleo. Serikali ifikirie tena.
Labels:
Demonstration,
Gas,
Maandamano,
Natural Gas,
Protests,
Ufisadi,
Zitto Kabwe
Subscribe to:
Comments (Atom)




