Thursday, January 03, 2008

Hali inazidi kuwa mbaya Kenya!

Maiti za watoto waliouliwa. Picha imepigwa leo kwenye mortuari ya mjini Nairobi, rais Mwai Kibaki alivyoitembelea leo.

Miguu za maiti kwenye mortuari huko Nairobi leo. Mortuari haina nafasi ya kuweka waliouliwa sasa.


Jamani, wakimbizi kutoka Kenya wanajaa Tanzania, Uganda na Sudan! Kama hujui Kikalenjin unauliwa! Eti unaulizwa swali kwa lugha hiyo na kama huwezi kujibu kwa kiKalenjin ndo mwisho wako! Na sasa madai kuwa uchaguzi uliopita ulikuwa si wa haki yanazidi. Ni balaa gani inaotokea Kenya? Uchumi wa Kenya umeathirika pia! Wazungu na wageni wengine wanaikimbia!

Habari zinasema kuwa sasa watu zaidiya 600 wamekufa tangu ghasia zianze.

Nadhani sisi waTanzania ni mfano wa kuigwa na 'UNDUGU' yetu. Hatuna ujinga wa mambo ya ukabila kiasi hicho. Asante Mwalimu Nyerere!

Pia nimepata habari kuwa Uganda umeathirika kutokana na ghasia za Kenya. Mafuta yanasafirishwa kwenda Uganda kupitia Kenya. Sasa wamesimamisha usafirishaji. Lita moja ya petroli iliyokuwa 2,500/- za Uganda kabla ya ghasia leo ni Ug. 10,000/- lita! Nauli iliyokuwa U.10,000/- sasa ni 60,000/-!

Mungu Ibariki Kenya na Afrika Mashariki!

******************************************************************************

From ippmedia.com

Kenya haijatulia

2008-01-03

NAIROBI, Kenya

Hali bado ni ya kutatanisha nchini Kenya huku idadi ya watu waliokufa kufuatia machafuko yaliyozuka tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu kufikia zaidi ya watu 300 hadi jana, limeripoti Shirika la Habari la Uingereza, Reuters.

Huku hayo yakiendelea kutokea, Rais Mwai Kibaki jana amejitokeza na kuwashutumu wafuasi wa aliyekuwa mgombea urais kupitia Orange Democratic Movement (ODM), Bw. Raila Odinga kuhusika na ghasia za kikabila nchini humo. ``Wafuasi wa Raila Odinga wanahusika na mapigano haya ya kikabila,`` msemaji wa Ikulu nchini Kenya, Alfred Mutua alisema jana. Wafuasi wa Odinga ambao wengi wao ni wa kabila lake la Luo nao wamekaririwa wakitoa shutuma kama hizo kwa Wakikuyu ambao wanadaiwa kumuunga mkono Rais Kibaki.

Nchi kadhaa za magharibi pamoja na Uingereza zimetoa wito kutaka Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Madola kuwapatanisha Kibaki na Odinga ili kuweza kurejesha hali ya utulivu nchini humo. Katika taarifa ambayo waliitoa kwa pamoja jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Miliband na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice, walitoa wito wakitaka uhasama huo umalizwe.

Wakati katika baadhi ya maeneo ya vijijini kuna taarifa za kuwekwa kwa vizuizi barabarani huku wananchi wakiwa na mapanga, mjini Nairobi baadhi ya ofisi zilianza kufunguliwa jana na polisi kuendelea kuweka doria nzito. ``Hii ndiyo demokrasia gani?`` Alihoji mtumishi mmoja wa Benki Kuu mjini Nairobi ambaye alisimamishwa na polisi wa doria jana alipokuwa njiani kuelekea kazini. Juzi watu 30 wanaoaminika kuwa Wakikuyu waliuawa baada ya kanisa walimokuwemo wamekimbilia kujihifadhi dhidi ya machafuko kuchomwa moto mjini Eldoret.

Alipoulizwa kama ni kweli Kibaki alishinda uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK), Samuel Kivuitu alikaririwa na Reuters akisema: ``mimi sijui lolote,`` jambo ambalo limeendelea kuzusha utata wa ushindi huo. Nchi nyingi za magharibi tayari zimeshatoa tahadhari kwa raia wake kuacha kutembelea Kenya katika kipindi hiki cha ghasia zinazoendelea.
Mwenyekiti wa AU, John Kufuor alikuwa akitarajiwa kuwasili nchini Kenya jana kwa ajili ya kufanya upatanishi, huku Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown akiwasiliana na pande husika kwa njia ya simu. ``Suala la Kenya lina umuhimu mkubwa kwa namna demokrasia inavyotekelezwa tukizingatia kwamba kuna chaguzi nyingine miezi 18 ijayo katika nchi za Agola, Ghana na Malawi,`` alisema Miliband.

Mwandishi wa habari wa Reuters ambaye alikuwa kwenye ndege angani aliweza kushuhudia moshi mzito wa nyumba zinazoungua huko Eldoret jana huku baadhi ya vijana wakiranda mitaani na mawe, mapanga, mishale, pinde na mikuki kwenye vizuia vya barabara. Hali katika vitongoji vilivyopo nje ya mji wa Nairobi mapema jana ilikuwa shwari japo baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walisema kwamba watu wanaosadikiwa kuwa Mungiki walitawanya vipeperushi vilivyodai kwamba mapambano yataendelea dhidi ya Waluo.

Habari kutoka mji wa Naivasha uliopo kwenye Bonde la Ufa zimesema kwamba takribani wakazi 300 waliokuwa wamejawa na hofu kufuatia mauaji ya Eldoret walilazimika kulala kituo cha polisi. ``Tulilazimika kukimbilia kwenye sehemu ambayo tumeamini ni salama,`` alisema Agnes Alouch akiwa kwenye bwalo la wafungwa.

Alipohojiwa kupitia kituo kimoja cha televisheni nchini humo, Kivuitu alikaririwa akisema kwamba alilazimika kutangaza matokeo haraka kutokana na shinikizo alilolipata kutoka vyama vya PNU na ODM. ``Wendawazimu huu hauwezi kuruhusiwa uendelee,`` lilisema gazeti la Daily Nation. Wakati huohuo, maelfu ya wananchi wa kabila la Kikuyu analotoka Rais Kibaki wameripotiwa kuyakimbia makazi yao katika eneo la Bonde la Ufa wakihofia ghasia hizo.

Imeelezwa kwamba maelfu wa Wakikuyu wamelazimika kuomba hifadhi katika makanisa na vituo vya polisi wakihofu kuuawa kama ilivyotokea kanisani mjini Eldoret, umbali wa kilomita 300 kaskazini mwa Nairobi. ``Tumekuwa tukilala nje kidogo ya Uwanja wa Ndege ambako kuna baridi kali,`` alisema Patrick Karikuki (23) jana. ``Sikujua kama Kenya inaweza kugeuka na kuwa namna hii ambapo tunauawa kwa sababu tumempigia kura Kibaki.

Hata kama kura ziliibwa, kwa nini wasiende mahakamani?`` Aliuliza kijana huyo. Baadhi ya abiria waliweza kuonekana katika Uwanja wa Ndege wa Eldoret jana wakisubiri kupanda ndege kwenda mjini Nairobi baada ya vijana kuzuia barabara kuu iendayo Nairobi kwa magogo ya miti. Hadi jana mchana, polisi nchini Kenya wamekadiria kwamba watu wasiopungua 75,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Mjini Eldoret, Mwandishi wa Habari wa Reuters alielezwa kwamba watu walikuwa wakiulizwa maswali katika lugha ya Kalenjin kupata utambulisho, na wale walioonekana kuwa wageni kutokana na kushindwa kujibu waliuawa kwa mapanga. ``Wanakuuliza wewe nani katika lugha ya Kalenjin. Wanapobaini kuwa huijui unauawa kwa kukatwa na panga,`` alielezwa mwandishi huyo. Shirika la Haki za Binadamu Kenya (KHRC) na Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu (FIDH) yamesema kwamba watu waliouawa tangu Desemba 27 mwaka jana ni zaidi ya 300.

Wakati huohuo, Japan jana imeungana na nchi nyingine za Ulaya kuzitaka pande zinatofautiana nchini Kenya kushirikiana kumaliza ghasia za kikabila zinazoendelea kuleta maafa. Waziri wa Mambo wa Nje wa Uingereza, Gordon Brown amesema jana kwamba tayari amewasiliana na Rais Kibaki na Odinga kuwataka washirikiane kumaliza machafuko hayo. ``Nimewasihi wote Kibaki na Odinga kuwajibika ipasavyo katika nyadhifa zao ili kuyamaliza mapigano hayo,`` alisema Brown.

Wakati huohuo, Rais Kibaki jana aliwaalika Ikulu Wabunge wote wapya waliochaguliwa katika uchaguzi uliopita, hatua ambayo wachunguzi wanaona ni ya kuwapoza. Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni haikufahamika kama wabunge wote waliitikia wito huo na kambi ya upinzani ilikuwa haijatoa tamko. Katika uchaguzi uliopita, mawaziri 20 waliogombea Ubunge kupitia chama kipya cha Party for National Unity (PNU) kinachoongozwa na Kibaki waliangushwa huku chama cha ODM alichogombea Odinga kikipata takribani viti 100 bungeni.

Wakati huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki-Moon, amevitaka vyama vya siasa na viongozi wao nchini Kenya kumaliza tofauti zao kwa kufanya majadiliano ya amani kwa pamoja kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Katika taarifa yake aliyoitoa jana kuzungumzia vurugu zinazotokea nchini humo, Bw. Moon, alisema amekuwa akifuatilia kwa makini matokeo ya uchaguzi huo na vurugu zilizojitokeza ambazo zimesababisha maisha ya watu wengi kupotea.

Alivitaka vyombo vya usalama kufanya kazi yao na kuwaomba wananchi wa Kenya kuwa watulivu, mavumilivu na kuheshimu sheria za nchi. Naye Novatus Makunga wa PST anaripoti kutoka Arusha kwamba waangalizi wa Jumuiya ya Afrika waliokuwa wanafuatillia Uchaguzi Mkuu wa Kenya wanakamilisha taarifa ya tathimini nzima ya uchaguzi huo uliotawaliwa na machafuko na inatarajiwa kutolewa hivi karibuni.

Akiongea kwa njia ya simu na Shirika la habari la PST, kutoka Nairobi, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Bw. Abdulrahim Haithar, alisema kuwa Jumuiya hiyo ilikuwa na waangalizi wapatao 14. ``Tulikuwa na waangalizi kumi na wanne wakiongozwa na mheshimiwa Michael Sebalu kutoka Uganda na kwamba sasa wanafuatilia ripoti ya matokeo ya uchaguzi pamoja na yale yaliyojitokeza baada ya matokeo kutangazwa,`` alisema.

Alisema kuwa sekretarieti ya Jumuia ya Afrika ya Mashariki yenye makao yake makuu mjini hapa ndiyo itakayotoa taarifa kamili baada ya kukabidhiwa taarifa hiyo na waangalizi hao. Bw. Haithar alisema kuwa waangalizi hao walikwenda nchini Kenya kusimamia uchaguzi huo wiki moja kabla ya uchaguzi huo kufanyika.

Wakati huo huo, Idara ya Uhamiaji mkoani hapa katika hatua ya kudhibiti wahamiaji wanaotumia njia za panya kuingia nchini, imeimarishwa ulinzi katika maeneo yote yanayozunguka mpaka wa Namanga na wananchi wameelimishwa dhidi ya wahamiaji haramu. Hata hivyo, Ofisa Uhamiaji wa mkoa wa Arusha, Bw.Justin Kabigumira, alisema kuwa kwa sasa mabasi yanayosafirisha abiria kwenda Mwanza na Uganda ambayo yalikuwa yakipitia Kenya yameendelea kusimamishwa mpaka hali itakapokuwa shwari. A

lisema kuwa hatua hiyo inatokana na Uganda na Kenya kufunga mipaka yake kwa kuhofia machafuko zaidi.

SOURCE: Nipashe

Kwa habari zaidi soma;

http://africa.reuters.com/wire/news/usnL03651413.html

http://allafrica.com/stories/200801030536.html

http://www.cnn.com/2008/WORLD/africa/01/03/kenya.economy/index.html

6 comments:

  1. Chemi usikaribishe mjadala unaohusu uchaguzi wa Kenya kwenye blogu yako, watakushughulikia sasa hii. JamboForums walikuwa mstari wa mbele kujadili wameshamalizwa tayari!

    ReplyDelete
  2. Angalia watakushughulikia kama walivoifanzia JamboForums

    ReplyDelete
  3. Dada Chemi, sema usiogope sema!

    Hujasema kitu ambacho haijaripotiwa kwenye taarifa za habari.

    ReplyDelete
  4. Ngalamba amenena! Tafadhali usilete mjadala unaohusu uchaguzi wa Kenya.

    ReplyDelete
  5. NGALAMBA ACHA MKWARA JAMBOFORUMS WAMESHUGHULIKIWA VIPI?

    ReplyDelete
  6. Habari za Kenya ni za kusikitisha. Sijui mambo yataisha lini. Watoto. Wazee. Wenye ulemavu. Wanafunzi. Wanawake. Vijana wenye ndoto za maisha mazuri. Maendeleo. Ustawi wa Jamii. Vyote viko hatarini hivi sasa. Kibaki. Odinga. Tulizeni watu wenu. Fanyeni yale yatakayowasadia Wakenya, jirani zetu warejee kwenye amani waliyoizoea. Tafadhali.

    ReplyDelete