Wednesday, March 12, 2008

Tuzo za vinara wa Filamu Tanzania 2008


FOMU ZA KUSHIRIKI TUZO ZA VINARA WA FILAMU TANZANIA KUTOLEWA WIKI HII

Baada ya kufana kwa uzinduzi wa Tuzo za Vinara wa filamu Tanzania,watayarishaji wanaalikwa kujaza fomu za ushiriki ili kuweza kuwasilisha kazi zao katika Tuzo za 2008. Fomu hizi zitapatikana katika ofisi za BASATA (Muulizie Omar Mayanga), Wananchi Wote, Kapico, GMC na Game First Quality.

Baada ya kujaza fomu, watengezaji wa filamu wanatakiwa kurudisha fomu na nakala ya kazi kwenye ofisi za BASATA kwa Omar Mayanga.Utoaji tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania, unalenga katika kuifanya sanaa ya Tanzania kupata nguvu mpya na kuwafanya watengenezaji na wadau sanaa kufanya bidii katika ushindani wa soko la sanaa na hivyo kutengeneza kazi zilizo bora zaidi zinazoweza kuuzika kimataifa ili kuiweka nchi yetu kwenye ramani ya dunia.

Tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania pia zinalenga kuwafanya wananchi kuendelea kuwa na mwamko wa kupenda kazi zinazotengenezwa na Watanzania wenzao ili kupata mafunzo mbalimbali yatokanayo na kazi za wasanii na pia kukuza soko kwa faida ya pande zote mbili.

Katika fomu hizo, kutaainishwa mambo muhimu ambayo mtengenezaji wa filamu atapaswa kujaza. Kama vile; Jina kamili la kampuni iliyotengeneza filamu au video na anwani kamili, Jina la Mtayarishaji Mkuu wa filamu (Executive Producer), Jina la Mtayarishaji wa filamu. (Producer), Jina la Mtunzi wa hadithi (Story Writer), Jina la Mwandishi wa skripti (Scriptwriter), Jina la Muongozaji (Director), Jina la Mhariri (Editor), Majina kamili ya wasanii wote waliyoigizia katika filamu husika (Characters), Jina la Muongozaji wa Taa (Lightsman), Jina la Mrekebishaji Sauti (Soundman), Jina la Mpiga Picha (Cameraman), Jina la Meneja wa Mandhari (Location Manager), Jina la Mpangiliaji wa Picha (Cinematographer), Jina la Mtunzi wa Muziki (Music Composer), Jina la Studio iliyofanya/zilizofanya kazi kwa filamu husika.

Fomu itakuwa na maswali mengine kama vile; filamu imetengenezwa lini, mahali ilikotengenezwa, maudhui ya filamu na lugha iliyotumika. Baada ya fomu hizo kujazwa kwa usahihi, zitatumwa kwenye ofisi za waandaji, kwa mkono au njia ya posta kwa anuani kamili ya waandaji. Watengenezaji wa filamu husika watapaswa kuambatanisha na mkanda wa filamu (VHS/DVD/VCD).

Kutakuwa na jopo la majaji wanane (8) watakaochaguliwa na waandaji kwa kushirikiana na Baraza la sanaa la Taifa nchini watakaokuwa na jukumu la kupitia filamu zote na kuzitolea uamuzi. Majina na wasifu za majaji zitawekwa bayana hivi karibuni. Pia vigezo zitakazotumika zitawekwa wazi.
Filamu zitakazoingizwa kuwania tuzo ni zile zilizotengenezwa na Watanzania kuanzia Januari 2007 hadi mwisho wa siku ya kualikwa watengenezaji kuingiza filamu zao ambayo itakuwa 31 Machi 2008.
Kushiriki kwa watengezaji wa filamu itasaidia kupata Filamu Bora ya Mwaka, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kike, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kike, Mwongozaji Sinema Bora wa Mwaka, Mchekeshaji Bora wa Mwaka, Mwandishi Bora wa Filamu, Mtunzi Bora wa Filamu, Filamu Bora ya kutisha, Muigizaji Mwandamizii Bora wa kike (supporting actor), Muigizaji Bora Mwandamizi wa Kike; Adui Bora kwenye Filamu,Mhariri Bora wa Filamu na mapambo na maleba ya mwaka.Pia itatolewa tuzo ya heshima kwa wale waliotoa machango wao kukuza sanaa nchini.

Tukio la utoaji wa tuzo hizi limepangwa kufanyika mwezi Mei 2008 na litafanyika kila mwaka.

Msemaji Khadija Khalili-Mratibu

No comments:

Post a Comment