Wednesday, October 15, 2008

Walimu Wetu Vipi Tena!!!!!

(pichani Mwalimu Mkoba akipigwa na Walimu wenzake! Picha kutoka Haki Ngowi Blog)

Hivi, hao walimu walishikwa na 'mob mentality' nini? Kwanza lazima nisema kuwa naogopa sana maana hao ndio wanaofundisha watoto wetu! Na kwa nini walitaka kumwua kiongozi wao? Waseme tu ni wavivu na wanatafuta kisingizio cha kutokwenda kazini!

Walivyofanya ni vibaya na washukuru kuwa si enzi za Mwalimu Nyerere. Wangesombwa wote hao na kupelekwa Gezaulole kulima kwa muda!

****************************************************************
Walimu wataka kumuua Rais wao

2008-10-15

Na Richard Makore

Rais wa Chama cha Walimu Nchini (CWT), Gratian Mkoba, jana alinusurika kuuawa na walimu wenzake baada ya kuwatangazia uamuzi wa kuahirisha mgomo wao uliopangwa kuanza leo, hali iliyowalazimu polisi kuingilia kati na kumtoa katika Ukumbi wa Diamond Jubilee kupitia mlango wa nyuma.

Kabla ya polisi kumuokoa, viongozi wenzake waliokuwa meza kuu, walimkinga dhidi ya silaha zilizokuwa zikirushwa, zikiwamo viti na chupa za maji.

Walimu hao wakiwa wanawaka hasira walivamia meza kuu na kuzonga huku wakimlaani kuwa amewasaliti kwa kukaa upande wa serikali, hivyo kupoteza heshima na imani aliyojijengea kwao.

Umati wa walimu kutoka manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam, walikutana katika ukumbi huo pamoja na mambo mengine ili kujua hatma ya mgomo huo na madai yao kwa serikali kama ulivyotangazwa na CWT kwa muda mrefu.

Baada ya Mkoba kutangaza kusitishwa mgomo huo, baadhi ya walimu, walianguka kwa mshtuko huku wengine wakiangua vilio, hali iliyosababisha ukumbi kugeuka eneo lililojaa huzuni kubwa na kutawaliwa na kelele za vilio.

Mkoba aliwaambia walimu hao kuwa, mgomo wao umefutwa kwa amri ya Mahakama na kuwataka leo wasigome kama walivyopanga kwa kuwa watakuwa wamekiuka amri hiyo halali.

Kabla ya kumalizia neno `` hakutakuwepo mgomo kesho``, ukumbi huo uligeuka kuwa kama uwanja wa vita kutokana na baadhi ya walimu kumrushia Rais huyo chupa za maji, viti, kuvunja meza kuu, alikokuwa amekaa hali iliyosababisha viongozi wote wa chama hicho waliokuwa wamekaa naye kukimbia.

Hata hivyo, jitihada za baadhi ya viongozi hao, waliojipanga kuwakabili walimu waliokuwa wameanzisha vurugu hizo kwa lengo la kumdhuru Rais huyo zilishindikana hadi walipofika askari wa Jeshi la Polisi kumuokoa kwa kumuondoa ukumbini hapo kwa kupitia mlango wa nyumba.

Wakati hayo yakijiri, walimu wasikika walikisema kuwa: `` Hatukutaki, umenunuliwa na serikali, acha gari letu na ngoja tukufundishe adabu kwani naona hutujui.``

Baada ya walimu kushtuka kwamba mlengwa wao ameondolewa ukumbini hapo kwa kupitishiwa nyuma, walitoka nje na kulizingira gari la polisi kwa lengo la kulizuia kuondoka na Rais huyo wakiwa wamebeba mawe.

Polisi walilazimika kufyatua risasi za moto hewani na kuwatanya walimu hao kisha kuondoa gari lao kwa mwendo wa kasi.

Kufuatia kiongozi huo wa CWT kuokolewa na polisi, baadhi ya walimu walirudi na kumalizia hasira zao kwa kutoa upepo kwenye magurudumu ya gari lake lililokuwa limesimama nje ya ukumbi huo na kutaka kulipasua vioo.

Dalili za kuzuka kwa vurungu hizo, zilianza kuonekana ukumbini hapo baada ya viongozi wa chini wa CWT kugusia habari za kusitishwa mgomo huo ambapo walimu walikuwa wakiguna kuashiria kutokuunga mkono uamuzi huo.

Kabla ya kutokea kwa vurugu hizo wakisubiri mkutano wao uanze, walimu hao waliimba nyimbo za kumsifia Mkoba wakati anaingia ukumbini na wakisema wana imani naye.

Baadhi ya nyimbo hizo ni ``tuna imani na Mkoba oyaa! oyaa!`` na nyingine nyingi, lakini hali ilivyogeuka walimuona kama mtu mbaya na mhalifu wa siku nyingi.

Wakizungumza na Nipashe ukumbini hapo, walimu hao walisisitiza kuwa mgomo wao uko pale pale na kwamba Mkoba hawezi kuwazuia kwani wao ndiyo watendaji.

Walidai mazingira yanaonyesha kwamba Rais wao amenunuliwa na serikali na hivyo amepoteza sifa za kushika wadhifa huo, hivyo ajiuzulu.

Wakati Mkoba akiwa amebana kwenye kona ya ukumbi huo huku akitetemeka, walimu walisikika wakimwambia kuwa kuanzia jana awaachie gari lao ambalo ni la CWT na atafute usafiri mwingine au aondoke kwa miguu.

Rehema Kimweri Mwalimu wa Shule ya msingi Mivinjeni wilayani Temeke alisema, ana miaka 25 kazini, lakini hajawahi kupewa fedha za likizo pamoja na kushindwa kumrekebishia mshahara.

Lyidia Mhina kutoka Shule ya Msingi Mtoni aliangua kilio na kushindwa kuzungumza zaidi ya kutamka jina lake na shule anayofundisha.

Atanas Mwinyi wa shule ya msingi Kimara B, alisema kuwa serikali na CWT ni kitu kimoja kwani anaamini kwamba Mkoba alikwenda ukumbini hapo kuwahadaa.

Alisema anaidai serikali zaidi ya Sh. 600,000, deni ambalo alidai amejibiwa hadi leo linafanyiwa uhakiki.

Rais huyo alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya vurugu zilizoibuka ukumbini hapo aligeuka bubu huku akiwaangalia waandishi wa habari.

Mahakama ya Kuu kitengo cha Kazi, juzi ilizuia kufanyika kwa mgomo huo, uamuzi ambao walimu hao wameupinga na kudai kuwa hawataingia madarasani, isipokuwa watakwenda kazini.

Walimu wameazimia kugoma kwa madai kuwa serikali imeshindwa kuwalipa madai yao licha ya kuipa siku 60 tangu Agosti mwaka huu.

Siku hizo zilimazika jana na leo ilikuwa ni siku iliyopangwa na walimu hao kugoma baada ya kupata baraka za CWT.

SOURCE: Nipashe

http://www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2008/10/15/124522.html

7 comments:

  1. chemi dada yangu usiharakishe kuhukumu (kuwa objective zaidi) what if there'z so much behind the issue that otherwise would make you change your opinion. najua sote tu very emotional bila kujijua .hata hao walimu pia they not exceptional
    mimi binafsi naunga mkono mgomo wa walimu na lolote watakalolifanya ali amradi no body gets killed or kuumizwa vibaya.Lakini suala la kuvunja sheria ninawaunga mkono let them do it.
    chemi umeshawahi kujiweka ktk position yao japo kwa fikira tuu?
    usisahau kwamba na wewe uliishi sana tanzania usiniambie kwamba umesahau tabu za walimu! chemi wewe hapo leo hii kama isingekuwa ni walimu wako wa vidudu na darasa la kwanza nk (yaani msingi)hii ukiachia jitihada za wazazi wako pia ,chemi usingekuwa hapo ulipo leo hii
    Hivi umeshawahi kusikia mbunge ameahirishiwa marupurupu na mshahra wake ?waziri na raisi na watu wengine wakubwa wa serikali ?
    Does it make sense kweli kwa mwalimu au daktari kuletewa mizengwe kwenye haki yake inayomwezesha kujisustain yeye na familia yake?
    jamani tuwaunge mkono walimu wetu masikini .na uamuzi wa kumpa kibano huyo mkoba ni sahihi in my opinion sababu watu wana uchungu na wamefika mahala maisha ya taabu ,dhihaka na umasikini wa kupindukia sasa basi .si kwa sababu eti wanataka kuwa matajiri jinsi nilivyoelewa ni kwamba wanadai haki zao ambazo ni sawia kwa kiwango cha huduma wanayoitoa , walimpa mkoba dhamana ya kuwakilisha msimamo wao na sio msimamo wa serikali na wala sio msimamo na mtazamo wake !
    Chemi umeshwahi kufikiri leo hii say wabunge waambiwe hakuna allowances ,a mean let alone their salaries ,kwa muda wa miezi miwili tuu au waziri aambiwe kwamba hakuna allowances kwa miezi miwili tuu na mishahara watacheleweshewa
    jaribu kufikiria hicho !
    Dada chemi mimi nimeona matatizo mengi ya jumuiya za kiafrika yanatokana na uongozi mbaya" ala Mkoba" na hiyo is so widely prevelent ktk nchi yetu ya tanzania viongozi wanatendency ya kufikiri kwamba wao ndio smart! na kwamba wanaoongozwa ni wajinga hivyo wanastahili kusaidiwa kufikiri na kufanyiwa maamuzi yanayowahusu.
    lakini ukweli ni kwamba kiongozi anachaguliwa kwa niaba ya wengi ili awakilishe matakwa na maoni ya wengi kwa faida ya wengi na siyo kuwakilisha maoni yake binafsi au kuchukua naoni ya mnyonga haki .kiongozi anahudumia waliomchagua na siyo vinginevyo.
    kwa maoni yangu mkoba amechemsha na kama ni kipigo ni sawa tuu kwa maoni yangu mimi ali mradi
    wasimwue!
    Raceznobar

    ReplyDelete
  2. Raceznobar,

    Asante sana kwa maoni, na kwa kweli umenifanya nifikirie hii suala zaidi.

    Ni kweli hao walimu hajatendewa haki. Lakini navyoona jinsi walivyoleta mzozo na kumpiga kiongozi wao umeleta picha mbaya sana.

    Ninambuka sana Mwalimu Hezekiel huko Zanaki Girls. Alitufundisha kuwa kupigana ni dalili ya ushamba, watu wenye akili wanakaa na kujadiliana matatizo yao. Ni kweli hao walimu wana matatizo na inaelekea huenda ni kweli huyo kiongozi kala pochi, lakini jamani si kuna sheria kwenye hicho chama. Si wangeleta, "Vote of No Confidence" halafu wamweke kiongozi mwingine? Kumpiga kwa kweli haifaii lakini pia ni dalali ya frustrations zao.

    Na ni muda mrefu walimu wetu Tanzania wameonewa. Nakumbuka nilipangiwa kwenda TTC lakini niliamua kuingia kwenye Uandishi wa Habari maana niliona jinsi walimu walivyodhauriliwa na mishahara yao ilivyokuwa midogo.

    Sijui sisi tuliyo nje ya Tanzania tunaweza kufanya nini kuwasaidia. Lakini ninaomba sana serikali iingilie mara moja na kutatua matatizo ya walimu hao ili watoto wetu waweze kuendelea na masomo yao bila bugudha.

    ReplyDelete
  3. Kuna siri kubwa iliyo nyuma ya huo mgomo wa walimu. Inasemekana kuwa mgomo huo mbali ya kuwa umewagawa walimu katika makundi ya wanachama wa Chadema wanaotaka mgomo ufanyike na wanachama waCCM wanaopinga mgomo una mkono wa watumishi wa serikali kama ilivyoripotiwa na gazeti la Raia Mwema la wiki iliyopita. Hao watumishi wa serikali wasio waaminifu wanawashawishi walimu wagome kwa kupitia baadhi ya viongozi wa walimu hao wanaoshirikiana katika suala zima la 'malipo hewa'. Imegundulika kuwa kuna walimu kibao ambao hawapo kabisa kazini, ama wamefariki au wameacha kazi ambao wanalipwa mishahara na wamo kwenye kundi la kudai malipo, malimbikizo na mengineyo. Vile vile kuna walimu ambao hawapo kabisa yaani majina hewa, nao wamo kwenye list. Hawa waalimu ni bora wakakubali tu huo uamuzi wa mahakama wanaweza kugoma na malipo ya mwanzo yakaenda kwa hao wafanyakazi hewa! Kwenye makaratasi itaonekana kundi kubwa la walimu walishalipwa kumbe ni hewa! Haya mambo pia yalitokea kwa waliokuwa wafanyakazi wa Jumuia ya Afrika Mashariki, watu walilipa watu hewa kwanza )pesa iliingia mifukoni mwao) ndio idadi ndogo ya wastaafu wakalipwa kuja kugundua pesa zishaliwa! Bongo hii jama walimu wadai madai yao taratibu kama serikali inasema unafanya uhakiki wa majina ili kugundua walimu hewa waache ifanye!

    ReplyDelete
  4. Chemi for the first time since I have known you, through this blog, you have gotten all this wrong. Kwa bahat mbaya pengine hukuwahi kuishi na walimu kama walimu. Pengine uliwahi kuishi na mwalimu ambaye ama mumewe ama mkewe si mwalimu na pengine anafanya kazi sehemu nyingine na hivyo kutojua machungu ya walimu katika nchi hii. Nasema pengine.

    Nakubaliana na wewe kuwa kugombana ni ushamba lakini inapofikia mtu baki anakushika anakushika pahala usipopenda kwa kurudiarudia pengine ugomvi unaweza usiwe ushamba tena. Nasema 'pengine' kwa sababu ninavyoona mimi sivyo pengine uonavyo ama aonavyo mwalimu.

    Huyo kiongozi ndiye aliyewaongoza kuandaa mgomo mpaka jana yake na alirudiarudia kupinga utararibu wa serikali wa 'kuwapoza' mpaka jana yake. narudia mpaka jana yake. Kwa kufupi mgomo mpaka uwe mgomo ni lazima tu usiwa halali. Narudia usiwe halali. Ukiwa halili si mgomo kwani hakutakuwa na kufeel pinch. You cant be a good commander if you join forces with the opponents at the elevent hour. Kiogozi wao kwanza kapingwa kidogo nathubutu kuandika kuwa ni kutokana na nidhamu ya ualimu tu. wangekuwa mainjinia(sorry engineers) pengine madhara yangekuwa makubw zaidi.

    Tukumbuke kuwa kada ya ualimu wamekuwa wakufundishwa kwa 'kulemazwa' kuwa watiifu. mpaka Wamefanya hivyo ujue uvumilivu wa kikazi na wa kibinaadamu tu ulishavuka viwango vya kimataifa na hata vya kimarekani vya uvumilivu. Kwa waalimu kufanya hivyo serikari inatakiwa ijiulize mara 800 as to what is in the cooking. Au mgomo mzuri, halali, mashuhuri ni wa wafanyakazi wa NMB na NBC. Wa walimu ni ushamba.

    Katika kundi la walimu kuna wasiopata promosheni toka 1981! narudia 1981.achilia mbali wa miaka 10, 9,7 na kadhalika. Wamo ambao hawajawahi kupandisha vyeo wala kwenda likizo toka waanze kazi miaka mingi haisemeki. Ukiuliza utajibiwa ngoja 'upembuzi yakinifu ufanyike. Years go by. Na wanadai jumla ya shilingi biloni 16 tu ambazo fisadi mmoja anaweza anayesemekaka kuficha mapesa uingereza anaweza kuwalipa na akabaki na chenji.

    I beg to difer.

    ReplyDelete
  5. Kam ulivyosema Dada chemi hawakutumia hekima kuchukua sheria mkononi ila ina kera sana ukifikiria wao pia wanamajukumu yao namahitaji ya kila siku kutokana na kipato chao wanachokitegemea kwa kufanyia kazi kwa nguvu zao halafu kinakuwa hakiwafikii walengwa

    ReplyDelete
  6. Bob alipoimba a hungry mob is an angry mob hakukosea. Nakubaliana na Da Chemi kuwa kuchukua sheria mikononi na kutwangana si hekima; hasa ukizingatia kuwa kwa kazi yao wamepewa dhamana ya kuwalea na kuwafundisha wadogo/watoto wetu. Ni ngumu (hasa kwa watoto wa msingi wasioweza kuelewa hali halisi ya maisha) kumuona mwalimu wako akitwangana ngumi, halafu kesho na keshokutwa aje kukupa adhabu wewe kwa kupigana na Joni.

    Ila saa nyingine bwana mtu unafikishwa mahala bwana unasema potelea pote. Sote tunajua walio katika system jinsi wanavyoweza kukufrustrate Bongo.

    1. Kama ushawahi kwend akuomba pasi ya kusaifiria (bila kumjua mtu au kutoa kitu kidogo) basi unaelewa nisemalo.

    2. Kama ulishadili na trafiki unaelewa nisemalo.

    3. Kama wewe au ndugu yako alishasafiri toka Kigoma kuja kudai mafao Dar kisha kuishia kuambiwa arudi wiki ijayo, ilihali hana mahali pa kukaa, fedha yote aliyokuja nayo imeisha, basi unaelewa nilisemalo.

    4. Kama unateka na shule, kisha kuteseka na kazi asubuhi mpaka jioni na kupata mshahara wa 150,000 (na hapo si mpaka uupate); wakati unaona wengine wanajichotea tu basi unaelewa nilisemalo.

    5. Kama ushapangishwa foleni masaa 6 NMB kudai chako na huku unakuwa treated kama unaomba msaada unajua nilisemalo.

    Saa nyignine inafikia wakati nidhamu ya namna hii inahitajika... tena wamemuonea Mkoba; wangeenda kuwachapa wafanyakazi wa halmashauri na wizara na hata wabunge. Fikiria mtu wanao wanalia njaa nyumbani, umekopa vigenge vyote vya jirani mpaka umemaliza; halafu watu wanakuletea utani na pesa yako. Haki elimu wakiweka matangazo, viongozi wanakasirika, ohh mbona mnaweka mabaya tu. Nchi yetu hatuthamini watoa huduma za jamii kama wauguzi, waalimu na waganga, wakati bila wao tusingekuwa hai pengine, na tusingesoma na kuwa wabunge, maCEO, n.k.

    ReplyDelete
  7. Kwa nyongeza tu. Juzi nimetazama TV mwenyekiti wao amewashukuru walimu kwa kumpiga kwa kuwa sasa uma wa watanzania umeelewa matatizo ya waalimu. Anadai wasingempiga hadithi ingekuwa ileile kuwa walimu wakorofi na ujumbe wao ungeendelea kupuuza. amesema kuwa mawe yale juzi yalikuwa kwake lakini serikali isishangae mawe yale yakamgeukia mtu mwingine (aliye juu) endapo madai yao yataendelea kupuuzwa.

    ReplyDelete