Wednesday, January 21, 2009

Ajali ya Lifti Dar

Wadau, hivi lifti zinakaguliwa kweli Bongo?

********************************************************************
Kutoka Gazeti la Majira:

Ofisa CHADEMA Aporomoka na Lifti Ghorofani

*Ni kutoka ghorofa ya kumi, ashtuka ubongo

Na Joyce Magoti

OFISA Habari na Uenezi wa CHADEMA, Bw. Devid Kafulila, amenusurika kifo baada ya kuporomoka akiwa ndani ya lifti iliyokuwa mbovu kutoka ghorofa ya kumi hadi ya pili, katika Hotel ya Concord iliyopo mtaa wa Agrey, Dar es Salaam.

Mkurugrenzi wa vijana wa chama hicho, Bw. John Mnyika, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa moja usiku wakati Bw. Kafulila alipokuwa akitoka katika semina iliyokuwa ikifanyika hotelini hapo na kwamba amelazwa katika Tasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

"Bw. Kafulila alikuwa mtoa mada katika semina iliyokuwa ikifanyika katika hoteli hiyo iliyohusisha vijana na wanawake ambapo aliwahi kuondoka. Wakati akitoka, aliingia katika chumba cha lifti ambacho mlango wake ulikuwa wazi.

"Baada ya kuingia lifti hiyo, alimshusha hadi ghorofa ya pili wakati yeye akitokea gholofa ya kumi, tulimkuta ghorofa ya pili akiwa amepoteza fahamu tukamwahisha hospitalini kwa ajili ya matibabu," alisema Bw. Mnyika.

Alisema kabla ya tukio hilo, uongozi wa hoteli hiyo ulipewa taarifa za ubovu wa lifti hiyo na baadhi ya washiriki waliokuwa katika semina hiyo lakini kutokana na kutojali hawakuchukua tahadhari yoyote.

"Baada ya kutokea ajali hiyo tuliangalia eneo la tukio ambalo halikuwa na maandishi yoyote wala kitu chochote kilichoashiria kuwa lifti hiyo ni mbovu, tunaomba uchunguzi ufanyike, inaonesha lifti hiyo ni mbovu kwa muda mrefu lakini hakuna tahadhari yoyote iliyochukuliwa na uongozi wa hoteli hiyo," alisema.

Afisa muuguzi wa MOI, Bi. Mercy Temu, alisema vipimo vya X-Ray alivyofanyiwa ngonjwa huyo vinaonesha kuwa ameumia sehemu ya nyonga katika mguu wa kushoto ambapo amewekewa jiwe lenye uzito wa kilo nne kwa ajili ya kumpunguzia maumivu na kurudisha nyonga hiyo katika sehemu yake.

"Mbali na kuumia sehemu hiyo pia ubongo wake ulishtuka hali aliyosababisha kupoteza fahamu lakini hali hiyo itatulia na anaweza kurudia katika hali yake ya kawaida baadaye.

"Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu mgongo wake haujaumia anaweza hata kuinua miguu yake na kugeuka peke yake," alisema Bi. Temu.

Waandishi wa habari walifika katika hoteli hiyo kwa lengo la kupata ufafanuzi kuhusiana na tukio hilo ambapo msichana mmoja aliyekuwa mapokezi alimwita Meneja wa hoteli hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

"Mnataka niwasaidie nini, mimi sina shida na waandishi wa habari wala sitaki kuzungumza chochote na nyie, mnaweza kwenda sina habari ya kuwapa," alisema Meneja huyo.

1 comment:

  1. Hivi serikali iko wapi, maisha ya watu yapo hatarini, inabidi occupation certificate iwe revoked na hoteli ifungwe indefinetely ndipo watu wa mahoteli watakuwa serious na maintenance, basi kwa kuwa

    ReplyDelete