Marehemu Richard Masatu |
Wadau, mwezi uliopita nilisikia habari za kifo cha Mwandishi wa Habari huko Mwanza, Richard Masatu. Nilisikia kuwa huenda aliuawa ingawa watu wanadai alipata ajali ya gari. Kwa mwandishi wa habari ni jambo la kawaida kupokea vitisho dhidi ya maisha hasa ukiwa unafuatilia habari nyeti. Mimi mwenyewe nilionja vitisho nikiwa Daily News.
Someni habari ya Uchunguzi waliofanya gazeti la DIRA.
Mungu Ailaze Roho Yake Mahala Pema Mbinguni.
Mazishi ya Richard Masatu
**************************************************************************
Na Mwandishi Wetu.
Agosti 10, 2011, zilipatikana taarifa za kifo cha mwandishi wa habari Richard Masatu, kilichodaiwa kusababishwa na ajali ya gari. Hata hivyo uchunguzi wa daktari kuhusu kifo hicho ulibainisha kuwa Marehemu aliuawawa kinyama. Tangu kupatikana kwa taarifa hizo, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limekuwa likificha ukweli kuhusiana na kifo hicho. Kwa sababu ya umuhimu wa tukio hilo la kusikitisha, gazeti hili limeanza kufanya uchunguzi ha hii ni taarifa yake ndogo ya awali. Endelea.
SIKU chache baada ya jeshi la polisi mkioani Mwanza kushindwa kutoa taarifa za uchunguzi wa awali wa kifo cha mwandishi wa habari Richard Masatu (39) uchunguzi umebaini kuwa aliuawa kutokana na kufuatilia biashara ya madawa ya kulevya na sakata la noti bandia.
Jinsi alivyouawa:
Uchunguzi wa kina uliofanywa umebaini marehemu hakufa kwa ajali ya gari bali kwa kipigo ambapo inadhihirishwa na taarifa maalum ya uchunguzi wa Kitabibu iliyotolewa na daktari katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza, akitokea katika viwanjwa vya Nane nane Nyamhongolo akiwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Luninga cha Star TV (James George) alipitia katika Baa maarufu Igoma (Cross Park) na kukaa hapo kwa muda wa saba.
Katika baa hiyo, pamoja na mwandishi wa habari ambaye alikuwa ameambatana na marehemu, pia alikuwa akinywa na watu mbalimbali wakiwamo maofisa usalama wa Taifa wilaya ya Ilemela (DSO Mugoma), mkuu wa kituo cha polisi wilaya Ilemela (OCD Allan Bukwimba), mkuu wa kituo cha Mwatex (OCS Abubakar).
Imebainika kuwa Marehemu wakati akitoka katika baa hiyo majira ya saa 3: 35 alitekwa na wauaji hao kwa kuanza kushambuliwa na kitu kizito kichwani upande wa kulia ambapo kutokana na ulevi aliokuwa nao alishindwa kujimudu na hivyo kubebwa na wauaji hao ambapo walimkokoto hadi katika misitu ya Ndama kando kidogo ya barabara ya Mwanza Musoma na kuanza kushambuliwa na kudi la wauaji.
Vituko baada ya kufariki:
SIMU ya Mke wa Marehemu: Licha ya taarifa kusambaa kuwa marehemu alikuwa amepata ajali, wa kwanza kupingana na taarifa hizo alikuwa mwandishi wa Gazeti la Msanii na rafiki mkubwa wa Marehemu, George Nteminyanda ambaye baada ya kufika hospitalini na kumwangalia marehemu, alianza kumkagua kama anavyoeleza.
“Nilipata mashaka, kwani mwili wake ulivyokuwa ukionekana na jinsi taarifa zilivyo elezwa nilipata wasiwasi, niliamua kumkagua kuona anamajeraha ya aina gani, nilianza kumgeuza Kichwa, upande kuangalia kichwani, hapa ndipo nilistuka kwani kitendo hicho kilimfanya kutokwa damu iliyoganda mdomoni” alieleza.
Alisema baada ya kuona damu alilazimika kumfuata daktari wa wadi ambaye alimhoji ni kwanini marehemu hawakumrufaa kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi kutokana na hali aliyokuwa nayo, lakini alidai kujibiwa kuwa alikuwa akiendelea vyema.
“Niliambiwa na daktari kuwa hali yake ilikuwa inaendelea vyema na kwamba walikuwa wakingojea kuona hali yake inaimarika vipi baada ya dripi kumalizika. Basi sikuwa na la ziada lakini kwangu mimi ilinitia shaka sana,” alieleza.
KUPOTEA kwa PF-3: Kutokana na hali iliyoonekana kwa Marehemu na mashaka juu ya kifo chake, familia iliomba mwili wake kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kujua sababu ya kifo chake.
Kutokana na maelezo ya matabibu waliompokea Hospitalini usiku, maehemu alifikishwa hospitalini akiwa na fomu namba 3 ya Polisi (PF-3), ambapo ililazimu ichukuliwe na kupelekwa Polisi kwa ajili ya kuanza utaratibu wa kumfanyia uchunguzi (Postmortem), lakini fomu hiyo haikupatikana kama anavyoeleza Gelard Robert mwandishi wa habari aliyekuwepo katika ufuatiliaji wake hospitalini.
“Tuliomba ipatikane PF-3 lakini kila daktari na muunguzi aliyekuwa akiulizwa hakuna aliyejibu wala kutambua kuwa ilikuwa wapi, basi haikuweza kupatikana na ndipo ofisa mmoja wa polisi aliposhauri kuwa lifunguliwe jalada jipya la uchunguzi ili mwili huo ufanyiwe uchunguzi ambapo lilifunguliwa jalada jipya hivyo kufanyiwa uchunguzi huo.
Taarifa ya Uchunguzi wa Daktari:
Kwa mujibu wa Taarifa ya uchunguzi wa kifo cha Masatu uliofanywa na Daktari chini ya wanafamilia na jeshi la Polisi umebainisha kile ambacho kinadhihirisha kuwa Marehemu aliuawa.
Kwa mijibu wa msemaji wa Kampuni ya Sahara Media Group Ltd, Raphael Shilatu kwa aniaba ya familia ya marehemu, wakati akizungumza katika msiba mjini Mwanza na Musoma, alisema uchunguzi wa kitalaam umethibitisha kuwa mwili wake ulikuwa na majeraha ya kushambuliwa.
“Marehemu amefariki kutokana na kupigwa na kitu kizito kichwani ambacho kilisababisha kuvujia kwa damu ndani ya ubongo, ametobolewa jicho moja na kitu chenye ncha kali, alitobolewa chini ya kidevu, alivunjwa vunjwa kifua, mguu wa kushoto ikiwa ni pamoja na kupasuliwa bandama na pafu la kushoto” alieleza Shilatu.
Mbinu zilizotumika kumnasa:
Imebainika kuwa marehemu alikuwa akifuatiliwa na mwanamke aliyeandaliwa maalum na wauaji ambapo siku hiyo, walimtaka kukutana katika katika baa hiyo huku wakiwa wamejianda kwa ajili ya kumshambulia.
Akiwa katika eneo hilo, bila ya kujua kuwa alikuwa akifuatiliwa marehemu alikuwa na mawasiliano maalum na mmohja wa wanawake watatu (majina yao yanahifadhiwa kwa sasa) ambao mmoja alikuwa akieleza na bayana kuwa alikuwa na makubaliano naye ya kustarehe naye na ndiye inaeaminika kuwa baada ya kuondoka alimpigia simu na ndipo alipoondoka na kushambuliwa.
Uzushi wa ajali baada ya kushambuliwa:
Huku duru za uchunguzi zikieleza kuwa baada ya kutekwa huko na kushambuliwa katika Msitu wa Ndama, wauaji hao walimtoa katika eneo la shambulizi na kumpeleka hospitali ya Mkoa ya Mwanza Sekou Toure moja kwa moja.
Uchunguzi unabainisha kuwa wauaji hao walitaka kumtupa barabarani ili ibainike kuwa aliuawa kwa ajali, lakini kutokana na eneo hilo la Igoma kando ya Baa ya Ndama kuwa na watu wengi, walilazimika kumpeleka hadi katika hospitali hiyo ya mkoa huku wakijivika jina la wasamalia wema waliojidai kumuokota ‘baada ya ajali.’
Sababu za kumpeleka Sekou Toure:
Katika mpango wao kama nilivyoeleza awali, walipanga kumtupa barabarani, lakini baada ya kukwama waliamua kumpeleka huko, na sababu kubwa ikiwa ni kwamba katika hospitali hiyo hakuna utaratibu wa kundikisha majina, namba za magari ya wagonjwa wanaoingia kama ambavyo upo Bugando jambo ambalo lilisaidia wahusika kujificha.
Kutambulikwa kwa kushambuliwa Masatu:
Majira ya saa nne mkewe aliamua kumpigia simu mumuwe ili kujua angerudi saa ngapi nyumbani, lakini simu yake ilikatwa na baada ya muda aliapigiwa simu yake na watu ambao walijieleza kuwa wao ni wasamalia wema ambao walikuwa wamemuokota Marehemu katika maeneo ya Ndama akiwa amepata ajali ya gari.
“Walinieleza kuwa wanampeleka Hospitali ya mkoa, ambapo nilijiandaa name kufika baadaye huko, nilikuta marehemu akiwa amelazwa na kuwekewa drip, hakuwa anaonyesha kuibiwa, kwani alikuwa na kila kitu, simu yake na pochi yake ya mkononi,” alieleza mke wa Marehemu.
Duru za uchunguzi zinaeleza kuwa kutokana na marehemu kufuatilia biashara ya mihadarati, mkakati huo wa mauaji ulipangwa ukiwahusisha maofisa wa polisi, usalama wa Taifa na wanawake waliotumika kama chambo.
Simu ya Mke wa Marehemu yatoweka:
Siku moja baada ya marehemu kufariki, hali ilizidi kuwa tete huku tetesi zikizidi kuonyesha kuwa marehemu alikuwa ameuawa, kutokana na watu kuanza kufuatilia nyendo, mke wa marehemu Edda Ikologoti Masatu alieleza kuibwa simu yake ya mkononi ambayo waliombeba kama wasamalia wema waliitumia kumpigia kumfahamisha kuwa alikuwa apata ajali.
“Siku ya kushambuliwa mume wangu sikuwa najua lolote, niliamua kumpigia simu ilipofika majira ya saa 4:00 kujua kulikoni hajarudi nyumbani, simu yake ilipokelewa na watu ambao walinieleza wamemuokota maeneo ya Ndama akiwa kapata ajali na walikuwa wakimpeleka Hospitali.
Simu yangu ilikata, walinipigia kwa simu nyingine na kuniuliza niko wapi name niliwaeleza kuwa niko Nyakato Buzuruga, waliniomba nifike maeneo ya Stand ili wanipitie twende naye Hospitali, niliwaomba watangulie kwa vile kutoka kwangu hadi eneo ambalo walitaka nifike lilikuwa mbali na ulikuwa usiku,” elieleza.
Akifafanua zaidi alieleza kuwa simu hiyo iliibiwa wakati wakiwa nyumbani ambapo siku hiyo katika kumbukumbu zake, alidai kuwa alikuwa ameiweka katika pochi yake na mkoba huo kumkabidhi mdogo wake Elizabeth Ikologoti lakini alipotaka kuitumia simu hiyo haikuwepo.
“Imenipa hofu sana, japokuwa sijui kama imepotea tu kawaida au imepotea kutokana na njama za mauajia, sijui kwa kweli labda wanajua kuwa kwa vile walitumia simu hiyo kunipigia wakati wakinialifu kuwa wamemuokota ndiyo maana imepotea, yaani hata sielwe,” alieleza.
Ushahidi wa mazingira:
Kuna taarifa za ndani kutioka kwa watu waliokuwa na marehemu siku hiyo kiziwataja maofisa hao wa polisi na usalama wa Taifa kuwa walikuwa na wahusiano na wanawake watatu waliokuwa wameandaliwa kama chambo katika eneo hilo la baa.
Wakiwa hapo mmoja wa vijana ambaye alidaiwa kuwa ni mmoja wa wasaidizi wa karibu wa maofisa hao wa usalama, alifika na kueleza ametoka katika msitu wa Ndama kufuatilia mdeni wake jambo ambalo linaonyesha kuwa kauli hiyo ilikuwa ikimaanisha (Ishara) kuwa eneo la mauaji lilikuwa limeandaliwa na kuwa tayari kwa kazi ya uuaji.
Moja. Ukweli, eneo la Msitu wa Ndama ni pori ambalo mchana limekuwa likitumika kwa shughili za kulisha mifugo inayouzwa mnadani hivyo usiku lisingeweza kuwa na watu hivyo kutia shaka na madai ya kuwa ‘Mtu alikuwa ameenda kumfuatilia mdeni wake’.
Mbili. Mmoja wa watu waliokuwa hapo aliamuaga afisa usalama akitaka kutumia nafasi hiyo kumsindikiza marehemu kutokana na kuona amelewa alizuiliwa na afisa huyo kwa madai ya kuwa amwache kwa maana ya kwamba ‘Huyu atasafilishwa na serikali leo kwani yuko kazini’. Kutokana na hali hiyo inaonyesha wazi kuwa mpango wa mauaji ulikuwa ukitambulika.
Tatu: PF-3 iliyopotea ilifunguliwa katika kituo cha Polisi cha Mwatex na mkuu wake wa kituo ni mmoja wa maofisa usalama ambaye alikuwa akinywa pale baa na mwandishi huyo, hii inatia shaka mazingira haya.
Wauaji wakodiwa toka Bariadi:
Ingawa hakuna uthibitisho wa moja kwa moja lakini duru za uchunguzi zimebainisha kuwa wauaji hao ambao idadi yao inaaminika kuwa ni kundi la watu wasiopungua 6, inasemekana kuwa baada ya kukamilisha shambulio lao waliondoka wakiwa katika gari la polisi hali ambayo ilwafanya kupita kwa urahisi bila ya kujulikana.
Uchunguzi huru:
Kulingana na mambo haya jeshi la polisi halitoweza kufanikiwa katika uchunguzi huu kutokana na bnaadhi ya maofisa wake kuonekana kujihusisha na mauaji hayo.
Kukwama kwa uchunguzi wa jeshi la polisi mkoani Mwanza kunadhirishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Liberatus Baro kutoa taarifa kuwa jeshi lake bado halijafanikiwa kunasa wahusika wa mkasa huo hatua ambayo inakwenda sambamba na kuachiwa kwa baadhi ya watu wawili ambao walishikiliwa siku moja baada ya mauaji hayo pia kuachiwa huru.
Kutokana na polisi kutuhumiwa na kuhusika njia pekee ya kufanikisha uchunguzi huo ni kuwa na timu huru ya uchunguzi ambayo inaweza kusaidia kufichua mauaji hayo ya mwandishi wa habari.
Source: Dira ya Mtanzania (Jumatatu Septemba 5-7, 2011)
Hii nikipata nafasi, nitajiiba niisome vyema. Tupo pamoja
ReplyDelete