TAARIFA YA JUMUIYA YA MAIMAMU ZANZIBAR (JUMAZA) TAREHE 18/2/2013 KWA
VYOMBO VYA HABARI KUHUSIANA NA TUKIO LA KUUWAWA KWA KUPIGWA RISASI
PADRI EVARIST MUSHI WA PAROKIA YA KANISA KATOLIKI MJINI UNGUJA
Shukurani njema zote anastahiki
Allah Ambaye ametuwezesha kuwa hai tukiwa na afya njema. Tunamuomba
Allah atuwafikishe kufanya mema na aujaalie uhai wetu wote uwe kwa ajili
ya kumtumikia Yeye katika Dini hii ya Kiislamu. Rehema na amani ya
Allah zimwendee kipenzi chetu, mtukufu wa viumbe Mtume Muhammad
(Sallallaahu ‘alayhi wasallam), masahaba zake, jamaa zake na wale wote
waliomfuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.
Ama
baada ya hayo,Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) inachukua fursa hii
kutoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kufuatia tukio la kupigwa
risasi na kuuwawa kwa Padri Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mjini
jana tarehe 17/2/2012 Beit – El – Ras.
JUMAZA
kwa mshtuko mkubwa imepokea kwa masikitiko taarifa ya kuuwawa kwa Padre
Mushin na inalaani kwa nguvu zote kitendo hicho cha kiharamia ambacho
kinaashiria kuitia doa Zanzibar kisiwa cha amani na ukarimu tokea enzi
na enzi. Kufuatia kadhia hii JUMAZA inawataka Wanzanzibari wote wa dini
na madhehebu zote kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu na kuendelea
kutunza amani na mshikamano tulionao chini ya Serikali ya Umoja wa
Kitaifa na kutotoa mwanya kwa watu au vikundi ambavyo vina nia mbaya ya
kutaka kuleta kutokuelewana kwa wananchi kwa malengo yao binafsi.
Aidha
JUMAZA inaungana na kauli iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuliagiza Jeshi la Polisi
nchini kufanya uchunguzi wa kina na waharaka ili kubaini nani
waliohusika na tukio hili na hatimaye sheria ichukue mkondo wake.
Aidha
JUMAZA inaliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kiuadilifu na
usioambatana na shindikizo la mtu au kikundi chochote ili hatimae ukweli
halisi ujulikane na bila ya kuwadhuru wasiohusika.
JUMAZA
inakemea vikali kauli za baadhi ya vyombo vya habari vinavyonasibisha
waislamu na tukio hili na kuvitahadharisha vyombo vya habari ikwemo
magazeti na redio hizo kutoanza kutoa taarifa ambazo kwa makusudi
zinaweza kupandikiza chuki na uhasama katika jamii na hatimae kuotesha
mizizi ya fitna na kupelekea Taifa kuingia kwenye machafuko bali
viachiwe vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi wake na kutoa taarifa
sahihi. Aidha JUMAZA inaziomba Serikali zote mbili kuwa waamgalifu sana
katika kipindi hiki kwa kujizuia kutoa maneno yanayoashiria kuhusisha
tukio hili na upande fulani wakati bado uchunguzi unaendelea.
Imesaniwa na:
KATIBU WA JUMAZA
MUHIDDIN ZUBEIR MUHIDDIN.
No comments:
Post a Comment