Saturday, December 13, 2014

Internet Inapatika Bure Sasa Sinza!

MANISPAA YA KINONDONI YAZINDUA HUDUMA YA BURE YA INTERNETI KWA WiFi KWENYE KITUO KIPYA CHA DALADALA CHA SINZA

Dec 13, 2014
theNkoromo Blog, Kinondoni
Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, imedhihirisha jitihada zake za kwenda na wakati katika huduma zake, baada ya kuamua kutoa huduma ya bure ya mtandao wa intrenet wa WiFi kwenye Kituo kipya cha Mabasi cha Sinza, jijini Dar es Salaam.

Akizindua huduma hiyo, jana, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yussuf Mwenda alisema, mtandao wa WiFi umeunganishwa kwenye kituo hicho kupitia mkongo wa mawasiliano kupitia Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Mwenda alisema, mtandao huo utakuwepo usiku na mchana na kila mwenye kompyuta au simu zenye uwezo wa kunasa Wi-Fi ataona katika simu au kompyuta yake akitaarifiwa kuwepo mtandao wa bure wa KMC_FREE WiFi.

Alisema, mdau atakachofanya ni kujinga bure na kuendelea kupata taarifa mbalimbali zikiwemo za tovuti ya serikali na ya Manispaa hiyo ya Kinondoni na nyingine zote atakazotaka.

Mwenda alisema, baada ya kuweka mtandao kwenye Kituo hicho, mwakani Manispaa hiyo itaweka mtandao huo wa WiFi kwenye Kata zote 34 za Manispaa hiyo.

Alisema, mradi huo wa WiFi umegharimu sh. milioni 21, na Manispaa hiyo itakuwa ikiendelea kulipia huduma hiyo sh. milioni 2 kila mwezi ambazo itakuwa inalipa kwa mkupuo kwa mwaka.


Kuzinduliwa kwa huduma hiyo, kumeifanya Manispaa ya Kinondoni kuwa ya kwanza nchini kote, na pengine hata Afrika Mashiriki, kutoa huduma hiyo bure tena bila kutumia namba ya siri.

Mwandishi wa habari hii alishuhudia huduma ya aina hii kwa mara ya kwanza alipotembelea nchini China, ambapo WiFi inapatikana bure kwenye simu hata ukiwa barabarani.

No comments:

Post a Comment