Tuesday, April 18, 2017

Kuwanasa Wauji wa Albino, Mbinu za Kivita Zinatumika!


Mwandishi wa makala haya na mmiliki wa blogu ya MaendeleoVijijini, Bw. Daniel Mbega (mwenye jezi nyekundu) akiwa sambamba na wanausalama katika tukio la kukatwa kiganja mtoto Baraka Cosmas Songoloka. Hapa ni kwenye tukio katika Kitongoji cha Kaoze, Kilyamatundu wilayani Sumbawanga.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
Tabora: KWA wakazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora, takriban kilometa 90 kutoka Nzega mjini, saa 3:00 ni usiku mkubwa na wengi wamelala baada ya shughuli za ujenzi wa taifa.

Majira kama hayo, usiku wa Jumatatu, Juni 15, 2015 haukuwa na tofauti kubwa, isipokuwa giza lililotanda kutokana na mbalamwezi kuwa gizani.
Kama ilivyo kwa maeneo mengi ya vijijini ambako watu hulala mapema, sauti pekee zinazosikika majira hayo ni ng’ombe wakilia na mahali pengine mlevi mmoja akiimba nyimbo katika lugha ya Kinyamwezi ambazo hazina mpangilio maalum wakati akirejea kutoka kilabuni.
  Mwandishi wa makala haya na mmiliki wa blogu ya MaendeleoVijijini, Bw. Daniel Mbega akiwa na Margreth (kushoto) na kaka yake, Tano baada ya wanausalama kufanikiwa kumnusuru binti huyo aliyetekwa na mjomba wake asiweze kwenda kuuzwa katika Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Mwakashanhala wilayani Nzega.

Mwandishi wa makala haya, akiwa katika harakati za kufanya uchunguzi kuhusu mauaji ya albino, alijikaza kisabuni huku akiugulia maumivu ya mbigili zilizomchoma magotini wakati akiwa amejificha kwenye kichaka pamoja na askari wawili wenye bunduki.
Mmoja wa askari hao alikuwa na bunduki aina ya Sub-Machine Gun (SMG) ambayo alizibana magazine mbili kwa pamoja, na mwingine akiwa na bunduki ya mabomu ya machozi (Anti-Riot Gun) huku akiwa ameyapachika mabomu ya kutosha kiunoni mwake, ikiwa ni tahadhari endapo fujo zingetokea.
Silaha pekee ya mwandishi ilikuwa kalamu na daftari dogo la kuandika kumbukumbu pamoja na simu kubwa ambayo aliitumia kama kamera tu kwa sababu sehemu hiyo mtandao haupatikani.
Zoezi hili la kivita lilikuwa na lengo moja tu la kumnasa mtu aliyedaiwa kutaka kumteka nyara mtu mwenye albinism na kwenda kumuuza ili apate utajiri.
Mwandishi, ambaye alikwishazunguka kwa karibu miezi sita wakati huo kuchunguza mauaji ya albino akiongozana na vikosi vya usalama, alikuwa anataka kushuhudia kwa macho yake ili kukamilisha uchunguzi huo na kuandika ukweli wa matukio ya mauaji ya albino ambayo yameshamiri nchini Tanzania na Afrika Mashariki na Kati tangu yalipoibuka kwa kasi mwaka 2006.
Nyumba pekee ya jirani ilikuwa umbali wa takriban meta 120 kutoka mahali walikojificha, ambayo ndiyo nyumba ya tukio.
Lakini umbali wa meta 10 kutoka walikojificha kulikuwa na njiapanda ambako liliegeshwa gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado Hard Top jeusi ambalo pia lilikuwa na askari kanzu wanne wenye silaha, mmojawao akiwa mwanamke.
“Tulia wewe, ninyi si mmezowea kuripoti habari juu juu na kuona matukio mengine kama ya kutungwa? Mnatulaumu polisi hatufanyi kazi,” mmoja wa askari hao akamwambia mwandishi kwa sauti kali ya kunong’ona baada ya kuona anahangaika kutafuta sehemu salama isiyo na mbigili ambazo ni nyingi katika eneo hili.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa mwandishi huyu kufanya kazi katika mazingira hatarishi katika uchunguzi wa mauaji ya albino, kwani kwa kipindi cha miezi mitano nyuma alikuwa amepenya na kushuhudia operesheni hizo za kipolisi kuwasaka watuhumiwa usiku na mchana na kunusurika hatari mbalimbali.
Mwandishi wa makala haya na mmiliki wa blogu ya MaendeleoVijijini, Bw. Daniel Mbega akiangalia mfupa unaodhaniwa kuwa wa binadamu katika Kijiji cha Bulumbela wilayani Igunga.

Wakati fulani, akiwa na polisi wa kike mkoani Simiyu, waliwahi kuzingirwa usiku kwenye baa na wananchi wenye mapanga baada ya askari waliyeongozana naye kumkamata, bila kuwataarifu, mtu aliyehusishwa na utekaji nyara wa mtoto Pendo Emmanuel Nundi wa Kijiji cha Ndamhi wilayani Kwimba katika Mkoa wa Mwanza. Jinsi walivyonusurika, ni habari nyingine ambayo haina nafasi hapa.
Kusafiri usiku na mchana kwa siku tano mfululizo bila kupumzika lilikuwa jambo la kawaida, na mara kadhaa walinusurika ajali kutokana na uchovu na usingizi.
Pamoja na ujasiri aliokuwa nao, lakini kwa mazingira aliyokuwepo usiku huo, alishikwa na hofu kwa sababu hakukuwepo na mtandao wowote wa simu na barabara pekee kutoka hapo hadi barabara kuu ya Nzega-Tabora, umbali wa kilometa 35, ikiwa ni njia ya ng’ombe.
Kwamba hata kama polisi walikuwa na silaha, lakini kama ingetokea mwano (yowe) ukapigwa na wakazi hao wa jamii ya Wasukuma na Wanyamwezi, hata silaha zenyewe zingeweza kuwa hatarini kwa sababu kusingekuwa na uwezekano wa kupambana na kundi la watu ambao wanaweza kuwadhania wao ni majambazi.
Tukio la kuuawa kwa watafiti watano mkoani Dodoma mwaka 2016 walipopigiwa yowe na wananchi wakidaiwa ni ‘wanyonya damu’, ni mfano mzuri kwamba lolote linaweza kutokea unapokuwa kwenye operesheni za aina hiyo.
Ghafla akatokea mtu mmoja akikimbia kuelekea lilikoegeshwa gari huku akiwa amembeba mtu begani kwake, ambapo mwandishi akainuka kijeshi baada ya kuona askari wale wameinuka na kwenda haraka, lakini kwa tahadhari, liliko gari.
“Upo chini ya ulinzi!” Sauti kali kutoka kwa mmoja wa askari waliokuwa kwenye gari ilisema, huku akiwa nyuma ya mtuhumiwa ambaye tayari alikuwa amemkabidhi mtoto mwenye albinism kwa askari kanzu wa kike aliyekuwa ndani ya gari na mtuhumiwa akavishwa pingu.
Ni wakati huo ambapo mtoto huyo, Margreth Hamisi (6) alizinduka kutoka usingizini kwani mtuhumiwa alikuwa ameingia ndani na kumkwapua na kukimbia naye wakati mama wa binti huyo, ambaye naye ni albino, alikuwa anaota moto nje kwenye kikome.
Mshangao ulimpata mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa ameaminishwa na mtu aliyejiita ‘mganga’ kuwa baada ya kuoga dawa aina ya giti (neno la Kisukuma likimaanisha ‘giza’) basi ‘angepotea’ mara atakapomfikisha mtoto huyo kwenye gari na kupewa mamilioni ya fedha kutoka kwa ‘tajiri’ ili akaishi jijini Mwanza.
Naam. Hivi ndivyo mwandishi alivyoshuhudia kwa macho yake namna maofisa usalama walivyofanikiwa kuweka mtego na kumnasa mtuhumiwa Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, ambaye alitaka kumuuza hai binti wa dada yake kwa mamilioni ya fedha.
“Matukio mengi ya kuuawa au kujeruhiwa kwa watu wenye albinism yanapangwa na kufanikishwa na wanandugu wenyewe kwa sababu ya mawazo potofu ya kutafuta utajiri kwa njia za mkato,” kachero mmoja mwenye cheo cha Sajini Meja (D/SSGT), Mkwabi alimweleza mwandishi wa makala haya.
“Nina uzoefu wa kutosha, miaka 35 ninafanya upelelezi na tangu mauaji ya albino yalipoibuka, kila tukio lazima tu utakuta ndugu anahusika,” akaongeza askari huo akizungumzia uzoefu wake.
Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa wanausalama hao kwenda kijijini kwa nia ya kumkamata mtuhumiwa, lakini mara mbili ilishindikana kutokana na sababu mbalimbali za kiusalama.
Tukio hilo lilitokea takriban wiki tatu baada ya wanausalama kuwakamata watuhumiwa sita Mei 21, 2015 huko Kahama wakiwa katika harakati za kuuza mifupa inayodhaniwa kuwa ni ya watu wenye albinism kwa mamilioni ya fedha.
“Nadhani umeshuhudia, haikuwa kazi rahisi kumwokoa binti huyu akiwa hai na kumtia mbaroni mtuhumiwa, tulilazimika kujifanya ‘wanunuzi’ na ‘waganga’ ili kuweka mtego wa kumkamata na kumwokoa mateka,” akadokeza kachero D/SGT Kato, mmoja wa maofisa ambaye alikuwa kwenye operesheni hiyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora wa wakati huo, ACP. Juma Bwire, akitoa ripoti ya tukio hilo, alisema mtuhumiwa Masanja Mwinamila alithubutu kumnyakua mtoto Margret (6) majira ya saa 3 usiku na kukimbia naye gizani akiwa na lengo la kumuuza ajipatie utajiri.
Vyanzo vya habari vilieleza kwamba, mtuhumiwa huyo alianza mchakato wa kutafuta ‘soko’ la kumuuza binti huyo mapema mwezi Juni 2015, lakini wasamaria wema wakawaarifu wanausalama kuhusu kilichotaka kutokea katika eneo hilo.
“Alisema kuna dada yake mwenye albinism ambaye ana watoto wawili – wa kiume na wa kike – ambao nao wana albinism, huyo dada ni mtoto wa baba yake mdogo ambaye alifariki mwaka 2014, hivyo nyumbani hakuna mtu wa kiume wa kuleta upinzani.
“Akasema biashara hiyo ingefanyika sana, kwani alipanga kuanza kumuuza mtoto wa kike, halafu angemuuza yule wa kiume na hatimaye kummalizia dada yake!” kilisema chanzo cha ndani kutoka eneo la tukio.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kwamba, asilimia kubwa ya wakazi wa Kanda ya Ziwa ni wapagani na wanawaamini waganga wa jadi kuliko mtu yeyote, hivyo Masanja aliamini kila alichoambiwa na ‘mganga’ feki.
Mganga huyo feki, mbali ya kumpigia ramli na kumwogesha dawa kwenye njiapanda mchana wa jua kali, alimtaka mtuhumiwa kumleta mtoto huyo akiwa hai kwa maelezo kwamba inabidi ‘afanye tambiko ili dawa zifanye kazi’, lakini lengo likiwa kumzuia asimdhuru mateka na hivyo kupata nafasi ya kumwokoa.
Akiwa na shauku ya kupata utajiri na kuachana na umaskini, baada ya kukubali masharti ya mganga, Masanja alimuomba ‘tajiri’ atafute bunduki ili wakati yeye atakapomnyakua mtoto, wafyatue risasi hewani kuwatisha watu watakaokimbilia eneo la tukio ikiwa yowe litakapigwa.
“Kauli hii iliwatisha wanausalama na wakahisi mtuhumiwa angeweza kwenda kuwadhuru watu wengine hata kwa panga ili amchukue mtoto, hivyo mganga akatoa masharti kuwa hata kama bunduki itapatikana, lakini asingependa kuona damu inamwagika kwa yeyote, na akamhakikishia kuwa dawa atakazoogeshwa zitamfanya awe ‘kiza’ asionekane na mtu yeyote,” alifafanua mmoja wa maofisa wa polisi ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa vile siyo msemaji wa Jeshi la Polisi.
Inaelezwa kwamba, mtuhumiwa huyo alipewa masharti mtoto huyo afikishwe kwa mganga akiwa hai bila kujeruhiwa, familia itakayovamiwa pia isimwage damu, fedha za manunuzi kabla ya kukabidhiwa mlengwa lazima zifanyiwe tambiko na masharti ya matumizi, na hakutakiwa kufanya ngono siku nne kabla ya tukio.
Bi. Joyce Mwandu Nkimbui (33), ambaye ni mama wa Margret, alisema siku tatu mfululizo kabla ya tukio, kaka yake huyo anayeishi jirani na hapo alikuwa akija asubuhi na jioni akijifanya kusalimia na wakati mwingine hata kupikiwa chakula.
Hata hivyo, alishangaa kumuona ndiye aliyevamia nyumbani kwao usiku huo na kumwamuru asikimbie kabla ya kuingia ndani na kumkwapua mtoto.
“Walikuja usiku, sijui walikuwa wangapi, lakini wakanilazimisha ‘wewe mama tulia’, nikaogopa na kukimbilia kwenye majani, nikaanguka kwa sababu sioni vizuri usiku, nikakutana na mwenyekiti wa kitongoji, ambaye tulikwenda naye nyumbani na kukuta tayari mtoto hayupo,” Joyce alisema kwa masikitiko.
Wakati tukio hilo linatokea, tayari watu sita walikuwa wamefikishwa mahakamani Juni 3, 2015 na wengine watatu wakisubiri kuunganishwa katika kesi mbili za kujaribu kuua kwa kumkata mkono Bi. Mungu Masaga Gedi, mkazi wa Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji cha Buhekela, Kata ya Igoweko wilayani Igunga, na lingine la kumkata mkono mtoto Nkamba Ezekiel kwenye Kijiji cha Mwisole, Kata ya Lutende, wilayani Uyui.
Katika mahojiano na polisi, watu hao walikiri kuhusika na mauaji ya Mapambo Mashili katika Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji cha Buhekela wilayani Igunga yaliyotokea Agosti 16, 2014, ingawa kesi hiyo ya mauaji bado inaendelea kupelelezwa.
Taarifa za kipolisi zinasema, watu hao walimshambulia kwa mapanga Mapambo Mashili na kumuua wakati akipambana kuzuia mkewe, Mungu Gedi ambaye ana albinism asikatwe mkono.
Hata hivyo, taarifa za kipolisi zinasema, baada ya kumuua Mapambo, watu hao walimkata mkono wa kulia mama huyo na kutoweka nao.
Watu watano kati yao walikamatwa mjini Kahama Mei 22, 2015 wakiwa katika harakati za kuuza mifupa hiyo kwa mamilioni ya fedha.
Waliokamatwa wakati huo ni Bahati Kirungu Maziku (57), ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Mbutu wilayani Kahama, Elizabeth Makandi Sweya Masanja (43) mkazi wa Bungwa wilayani Nzega, Bilia Masanja (39), mkazi wa Bukene wilayani Nzega, Muhoja John maarufu kama Juma (29), mkazi wa Nyasa na Regina Kashinje (41), mkazi wa Isagenhe.
Mei 23, 2015 Polisi walifanikiwa kumkamata Mussa Njile Masanilo (31), mkazi wa Mmale, wilayani Uyui ambaye baada ya mahojiano alikiri kuhusika na matukio hayo na kuwataja washirika wengine ambao bado wanaendelea kusakwa polisi.
Katika mwendelezo wa upelelezi wa tukio hilo, polisi walifanikiwa pia kuwakamata watuhumiwa wengine watatu ambao ni Athumani Masoud Mohammed (56), diwani mstaafu na mkazi wa Kijiji cha Mbutu wilayani Igunga, Bi. Misuka Giti Malisha (51) mganga wa jadi ambaye ni maarufu kama Mwanagiti, mkazi wa Kitongoji cha Mwaningho, Kijiji cha Bulumbela, Kata ya Ziba wilayani Igunga pamoja na Omary Hussein Mkoma (28), mkazi wa Kijiji cha Buhekela wilayani Igunga.
Watuhumiwa hao walihusishwa na washirika wengine sita katika shauri hilo, na inaelezwa kwamba walikiri kushirikiana nao katika biashara mbalimbali ingawa walikana kuhusika na tukio la kukatwa mkono kwa Mungu Gedi na mauaji ya mumewe ingawa walikuwepo kijijini wakati matukio hayo yanatokea.
Kukamatwa kwa Masanja Juni 15, 2015 akitaka kumuuza hai binti wa dada yake kwa mamilioni ya fedha kumedhihirisha kwamba matukio mengi ya kuuawa au kujeruhiwa kwa watu wenye albinism yanapangwa na kufanikishwa na wanandugu wenyewe kwa sababu ya mawazo potofu ya kutafuta utajiri kwa njia za mkato.
Mwaka 2009, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliangua kilio bungeni kuonyesha uchungu alionao dhidi ya vitendo vya mauaji ya kikatili ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), na machozi yake yakayeyusha hoja ya wabunge wa upinzani waliokuwa wamepania kumbana, ili ajiuzulu kwa madai kwamba, alitoa amri ya kuua wauaji ambayo ni kinyume na Katiba ya nchi.

Kanda ya Ziwa balaa
Taarifa za kichunguzi zinaonyesha kwamba, mikoa ya Mwanza na Kagera ndiyo vinara wa matukio ya mauaji na kushambuliwa kwa albino nchini tangu kuripotiwa kwa tukio la kwanza dhidi ya walemavu hao lililohusisha mauaji ya Arip Amon, mkazi wa Kijiji cha Nyehunge wilayani Sengerema katika Mkoa wa Mwanza.
Tukio hilo, ambalo mpaka sasa hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa, lilitokea Jumatatu, Aprili 17, 2006 majira ya saa sita usiku katika Kijiji cha Nyehunge na lilipewa jalada lenye kumbukumbu namba KAH/IR/92/206.
 Takwimu za kipolisi zinaonyesha kwamba, Mkoa wa Mwanza ndio unaoongoza kwa matukio 12 ukifuatiwa na Kagera wenye matukio tisa (9).
Kwa mujibu wa takwimu hizo, mkoa unaofuatia kwa idadi ya matukio ni Geita ambao mpaka sasa jumla ya matukio sita yametokea wakati Tabora una matukio matano, Kigoma matukio manne, Mara, Rukwa, Shinyanga na Simiyu matukio matatu kila mmoja na tukio moja moja limetokea katika mikoa ya Mbeya, Katavi, Pwani na Tanga.
Inaelezwa kwamba, tangu mwaka 2006 serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kupambana na matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa watu wenye albinism nchini.
Jumla ya matukio 53 yametokea na idadi kama hiyo ya kesi zimefikishwa mahakamani tangu mwaka 2006 hadi 2015 ambayo yamehusisha mauaji, kujeruhi na kuteka nyara na katika kipindi hicho walemavu wa ngozi (albino) 39 waliuawa, 12 walijeruhiwa na wawili walitekwa nyara.
Kati ya waliotekwa nyara, mmoja aliokolewa na Jeshi la Polisi na mtuhumiwa aliyehusika na utekaji huo alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela, tukio ambalo lilitokea wilayani Nzega Juni 15, 2015.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, kesi 22 kati ya 53 zimeondolewa mahakamani na watuhumiwa 73 waliachiliwa huru na mahakama na vyombo vingine vya sheria baada ya kuonekana hawana mashtaka ya kujibu.
Aidha, washtakiwa 24 wamehukumiwa kunyongwa mpaka kufa katika mahakama mbalimbali nchini, wakati wawili walihukumiwa vifungo tofauti jela.
Katika Shauri la kujaribu kumuua Emmanuel Festo Rutema (14) wa Isebya – Kagoma wilayani Biharamulo lililotokea Novemba 12, 2007 ambalo lilikuwa na majalada yenye kumbukumbu namba BI/IR/1262/2007 na PI 68/2007 mshtakiwa Zacharia Petro alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Ijumaa Juni 19, 2015 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega, Saraphine Nsasa, alimhukumu kifungo cha miaka 10 jela mshtakiwa Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala, Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora baada ya kukiri kumteka nyara mtoto wa dada yake, Margret Hamisi (6) kwa lengo la kwenda kumuuza mzima mzima.
Katika kesi hiyo NZ/IR/807/2015 yenye kumbukumbu CC. NO. 116/2015, Masanja baada ya kusomewa mashtaka hakuisumbua mahakama pale alipokiri kutenda kosa hilo hasa kwa kuzingatia kwamba ushahidi ulikuwa umekamilika.
Fuatilia mfululizo wa ripoti hii maalum: ‘Unaweza kufukua kaburi la Nyerere?’.

+255 656 331974

No comments:

Post a Comment