Showing posts with label Mh. Shy-Rose Bhanji. Show all posts
Showing posts with label Mh. Shy-Rose Bhanji. Show all posts

Saturday, October 25, 2014

Mh. Shy-Rose Bhanji Ajibu Shutuma Dhidi Yake

Mh. Shy-Rose Bhanji
Mimi Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Afrika Mashariki-Tanzania, ninapinga vikali na kwa nguvu zote shutuma zilizotolewa dhidi yangu kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.
Shutuma hizi hazina ukweli wowote na zinalenga, si kuniharibia, bali kuchafua sifa yangu na utendaji kazi wangu katika Bunge la Afrika Mashariki.
Lengo kuu la shutuma hizo ni kunivunja nguvu na ari ya kutetea maslahi ya nchi yangu na Watanzania wenzangu kwani daima nimekuwa kikwazo na mwiba kwenye ajenda zinazokiuka maslahi ya Tanzania.
Kwa mfano ardhi ya Tanzania kugawiwa kwa wana Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kinyume na Sera ya Tanzania. Nimekuwa miongoni mwa wabunge wa Tanzania tulio mbele katika kulipinga suala hilo. Sishangai likinijengea uadui.
Isitoshe, kwenye ajenda ya kumuondoa madarakani Spika wa EALA, Dk. Margaret Zziwa, nilisimama kidete kwa kutounga mkono kwa sababu halikuwa na maslahi ya Tanzania na yalikuwa kinyume na malengo ya ushirikiano wa Jumuiya nzima.
Hoja ya kumuondoa Spika ilikuwa ni sehemu ya ‘mchezo mchafu’ ya ajenda ya siri ya kumweka kwenye nafasi hiyo mjumbe mwingine kwa maslahi ya wachache.
Jaribio hili la kumuondoka Spika lilifanywa na kushindikana mara tatu baada ya kukosa sahihi za kutosha kutoka Tanzania, ikiwamo ya kwangu.
Baada ya kampeni ya kumwondoa Spika kushindwa, wabunge kadhaa walikuwa wanasusia vikao vya Bunge wakati wameshachukua posho za vikao. Kwa mfano kikao kilichofanyika hivi karibuni hapa Dar es Salaam.
Malumbano ndio yamekuwa yakitawala na kuinyima Bunge akidi ya kuendelea na ajenda za mtangamano. Huu ni usaliti wa wazi kwa nchi zilizowachagua na kuwatuma katika Bunge la EALA.
Ukijaribu kuwaasa kwamba mwenendo huo si sahihi, unageuka kuwa adui.
Na sasa wameamua kunitukana na kuzusha tuhuma kadhaa kupitia mitandao ya kijamii ambako yote ni utunzi wa kisanii usiokuwa na chembe ya ukweli, uhalali wala ushahidi.
Wahenga walisema ‘akutukanaye hakuchagulii tusi’. Walete ushahidi wa tuhuma zote dhidi yangu.
Kwa mfano, shutuma kwamba nililewa pombe ndani ya ndege, kuvunja chupa, kufanya fujo na kufungwa pingu wakati wa safari ya Ubelgiji si kweli hata kidogo.
Kama hizi tuhuma ni za kweli, kwanini hazikupelekwa polisi, serikalini au vyombo vingine vya sheria baada tu ya tukio?
Ijewe wamesubiri wiki mbili baada ya madai hayo ya tukio la kutunga ndipo wajitokeze wakati wa kikao kinachoendelea mjini Kigali, Rwanda? Kwanini wasubiri kikao cha Kigali ndipo uzushi huu utolewe?
Tuhuma kwamba nimewatukana marais wa nchi tatu hazina mashiko isipokuwa kuhalalisha kampeni ya wale wanaonichafua na kuibua chuki kwa maraisi na raia katika nchi za Kenya, Rwanda na Burundi.
Ninayo heshima kubwa sana kwa marais wa nchi zote tano na raia wa nchi wanachama ambako mara zote nimepokewa na kuishi kwa amani na upendo katika nchi hizo. Naahidi kuedeleza heshima hii.
Hainiingii kichwani ni wapi nilipoteza heshima hii isipokuwa kwa wale wasionitakia mema ambao wamekusudia kufanikisha ajenda zao.
Shutuma zote dhidi yangu zimetengenezwa na watu ambao hatushabihiani katika hoja zetu na sishangai kwa hilo.
Mimi ni Mtanzania na ni Mbunge wa Tanzania. Hivyo nina wajibu wa kulinda na kutetea maslahi ya Watanzania ili kuleta mtangamano wenye uwiano sawa kwa nchi zote wanachama.
Ninaahidi nitaendelea kuwatumikia Watanzania kwa nguvu zangu zote na kutoa ushirikiano kwa wabunge wengine wa EALA kwa manufaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nimeyasema haya nikiamini kuwa: “Uongo ukiachwa usemwe mara nyingi unaweza kuaminiwa kuwa ni ukweli.”
Umoja Wetu Ni Nguzo Yetu
Mungu ibariki Afrika Mashariki
Asanteni,
Shy-Rose Bhanji
Mbunge EALA

Saturday, March 01, 2014

Mh. Shy-Rose Bhanji Aiomba Serikali ya Tanzania Kuwezesha WaTanzania Waifahamu EAC na Faida Zake

1069410_488216681262565_60269170_n

Katibu wa Wabunge wa Tanzania Katika Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Shy-Rose Bhanji (pichani) amerejea nchini baada ya ziara ya siku 10 ya Wabunge wa EALA nchini Kenya na hicho ndicho alichokisema kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nimerejea nchini baada ya ziara ya siku 10 nchini Kenya. Ziara hii ya wabunge wa EALA ilikuwa kwa mwaliko wa Serikali ya Kenya lengo likiwa kuhamasisha wananchi wa Kenya kupata ufahamu mkubwa juu ya Mtangamano wa Jumuiya na faida zake. Tulipata nafasi ya kuonana na wananchi, wafanyabiashara, wabunge, maseneta, magavana, asasi za kiraia na makundi mengine.

Ziara hii imenifungua macho zaidi kwamba bado tuna kazi kubwa mbele yetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa ni ya Wananchi (people Centred Integration).

Kama nilivojionea mwenyewe kwa upande wa maeneo mbalimbali tuliyoyafikia bado mwamko wa ufahamu wa masuala ya EAC mdogo sana na kiu wa kuifahamu ni kubwa.

Hata hivyo Serikali ya Kenya kwa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki kikamilifu juu ya masuala ya Jumuiya imefufua mpango huu wa wabunge wa EALA kufika Kenya kuendelea na zoezi la uhamasishaji.

Ni imani yangu kwamba na Serikali ya Tanzania itaiga mfano huu mzuri wa kuwaalika wabunge wa EALA kufika nchini ili kuwafikia makundi mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuhamasisha. Hata kwa upande wa Tz bado ufahamu wa wananchi wengi zaidi juu ya masuala ya Integration ni changamoto kubwa.

Lengo kuu la uanzishwaji wa EAC ni kuinua hali ya kiuchumi kwa wananchi wa EA ambao sasa ni takriban millioni 140. Na iwapo mwamko wa wananchi ni mdogo basi lengo hili litachukua muda mrefu sana kufikiwa au kutokufikiwa kabisa.

Monday, December 03, 2012

Mh. Shy-Rose Bhanji Akutana na Aga Khan



Kiongozi Mtukufu Aga Khan ambaye ndiye Mwenyekiti wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) na Kiongozi wa Waislamu wa Ismailia akizungumza mawili matatu ya kimaendeleo na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania Mh. Shy-Rose Bhanji wakati wa ufunguzi wa Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mkoni Arusha. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Kidiplomasia ya AKDN Dkt. Shafik Sachedina. ( Picha kwa Hisani ya Ikulu)

Tuesday, September 18, 2012

Mh. Shy-Rose Bhanji Atoa Shs. 2 Milioni Kwa TAMWA


Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ndugu Ananilea Nky, akikmkaribisha Mbunge wa Afrika Mashariki, Mh. Shy-Rose Bhanji kwenye ofisi za TAMWA, Sinza

Mbunge wa Afrika Mashariki, Mh. Shy-Rose Bhanji akikabidhi shs. milioni mbili (2,000,000/-)  kwa TAMWA ikiwa ni mchango wake kwa TAMWA kuendeleza harakati zake nchini.