Showing posts with label Prof. Mwesiga Baregu. Show all posts
Showing posts with label Prof. Mwesiga Baregu. Show all posts

Wednesday, May 28, 2008

Mkapa Hajajibu Hoja - Prof. Baregu

Prof. Baregu hachoki! Mwaka jana aliuliza maswali kadhaa kuhusu enzi za Mh. Mkapa. Hakupata majibu. Na jana kaongea tena!

*************************************************************

Kutoka ippmedia.com

Mkapa hujajibu hoja - Baregu

2008-05-28

Na Lucy Lyatuu

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, amemshangaa rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa kutoa majibu ya jumla dhidi ya tuhuma nzito zinazomkabili. Alikuwa anazungumza na Nipashe kwa njia ya simu kuhusu utetezi alioutoa Bw. Mkapa huko Masasi mkoani Mtwara kuwa wanaodai kuwa ni `fisadi` wana chuki binafsi kwa vile aliwanyima madaraka akiwa Ikulu.

Profesa Baregu ambaye ni mtaalamu wa sayansi za siasa alisema tuhuma dhidi ya Rais mstaafu zinajulikana na zinaeleweka, hivyo hakutakiwa kutoa majibu ya jumla na ya juu juu. Alimtaka kiongozi huyo kuweka wazi idadi ya watu aliowanyima vyeo au madaraka wakati akiwa madarakani ili kuipa nguvu hoja yake.

``Kwa mfano mimi sijawahi kutafuta kazi kwake sasa atatoaje majibu ya jumla kuwa wanaotoa madai hayo wana chuki binafsi wakati masuala ya Benki M na mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira unafahamika?`` alihoji Profesa Baregu.

Aliongeza kuwa kama Bw. Mkapa anataka kujibu tuhuma dhidi yake azungumze kwani mambo mengi yameandikwa kwenye vyombo vya habari. Alimtaka asiandame watu kwa ujumbe mbaya na kumkumbusha kuwa ni vyema akafahamu kuwa majibu ya jumla hayamsaidii.
" Asitake kumuua tarishi kwa kuleta ujumbe mbaya,`` alisema Profesa Baregu.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa awamu wa pili, Jaji Joseph Warioba alipohojiwa hakuwa tayari kutoa maoni na kuongeza kuwa yaliyosemwa dhidi ya kiongozi huyo yanatosha. Rais Mkapa alipochukua madaraka mwishoni mwa 1995 alianza kazi kwa kuunda Tume ya Kuchunguza Kero za Rushwa iliyoongozwa na Jaji Warioba.

Mkapa aliyeingia madarakani kwa jina la aliyetakata (Mr Clean) aliahidi kutumia ripoti ya Jaji Warioba kupambana na rushwa na kuondoa ufisadi serikalini, kitu ambacho hakikuwahi kuonekana waziwazi.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, akizungumzia utetezi huo alisema , Bw. Mkapa hajajibu hoja badala yake ameleta propaganda na poroja za kisiasa. Akitoa maoni yake kwa njia ya simu kufuatia majibu ya Rais mstaafu, alisema Bw. Mkapa alitakiwa kujibu taarifa zilizopo kuwa amesajili makampuni wakati akiwa Ikulu na sio kuleta hoja za kwamba kuna waliokuwa wakitaka madaraka.

``Kama itakumbukwa, mwaka jana Septemba 27. mimi na Bw. Tundu Lissu, tulikuwa watu wa kwanza kutaja orodha ya mafisadi 11 akiwemo Bw. Mkapa,`` alisema. Alisema binafsi hajawahi kupiga magoti akimuomba Bw. Mkapa ampe cheo au madaraka na alichonacho ni uchungu na rasilimali za Watanzania.

Alisema Bw. Mkapa akiwa madarakani alisajili makampuni ya ANBEN na Tanpower Resources Ltd ambayo rais huyo mstaafu na Waziri wa zamani wa Madini na Nishati, Bw. Daniel Yona walitajwa kuwa na hisa ndani ya Tanpower Resources.

Aliongeza kuwa hajawahi kufanya kazi serikalini na hategemei kuwepo na pia hana chuki ya kutokuwa na madaraka kama anavyodai Bw. Mkapa, kwa misingi hiyo anadhani kauli aliyoitoa haina ukweli.

Alisema anachotakiwa kufanya mtuhumiwa huyo ni kujibu hoja ya kwamba ni kweli alisajili kampuni hizo kwa anuani ya biashara ya Luthuli Street namba 15 ambayo ni ya Ikulu.

``Tunataka tu kujua alilipa kiasi gani kama gharama ya pango la kutumia Ikulu?`` alihoji. Dk. Slaa aliongeza kuwa jambo lingine ambalo alitakiwa kujibu ni umiliki wa ANBEN, kampuni iliyokopa Sh. milioni 500 NBC na kushinikiza benki hiyo ibinafsishwe.

Aidha alisema jambo lingine ambalo anatakiwa kujitokeza na kulijibu ni nyaraka zilizoko kwa Wakala wa Kusajili na Kutoa Leseni kwa Kampuni (BRELLA) kwamba anamiliki makampuni hayo akiwa kama mjasiriamali.

Alimtaka kujitokeza hadharani na kujibu hoja hizo ili zionyeshe wazi ukweli wa kauli alizozitoa. Jitihada za kuwapata kwa simu Mwenyekiti wa CHADEMA Bw. Freeman Mbowe na Katibu Mwenezi wa CCM Bw. John Chiligati hazikufanikiwa.

SOURCE: Nipashe