Showing posts with label Waziri Mkuu. Show all posts
Showing posts with label Waziri Mkuu. Show all posts

Friday, November 27, 2015

Waziri Mkuu Majaliwa Aamuru Maafisa Kadhaa wa TRA Kukamatwa

Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa leo ameamuru kukamatwa kwa maafisa kadhaa  wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na wengine kufukuzwa kazi  baada ya kufanya ziara ya kushtukiza Bandarini na kukuta madudu ambayo hakuyafurahia.
Maafisa hao, ambao kwa sasa tunahifadhi majina ili Jeshi la Polisi liweze kuwashughulikia, wametakiwa pia kusalimisha hati zao za usafiri.
Hii imekuja baada ya kugundulika kwamba kuna makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 80 ambayo data za Mamlaka ya Bandari inazo lakini katika mtandao wa TRA hayaonekani.
Habari kamili inaandaliwa. Fanya subira....
Kwa sasa anza na picha....


Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na uongozi wa TRA na TPA alipofanya ziara ya kustukiza Bandarini leo asubuhi.
 Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa akiongea na viongozi wa TRA na TPA
Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa akikabidhi orodha ya makontena yaliyopotea na ambayo TRA haina taarifa nazo
Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa 
akiagana na viongozi wa TRA na TPA.


Tuesday, October 16, 2012

Waziri Mkuu Pinda Kuunguruma London!


Waziri Mkuu, Mh. Peter Mizengo Pinda

WAZIRI MKUU PINDA KUUNGURUMA LONDON.


*Ni siku chache baada ya uadilifu wake kumuokoa kupigiwa kura ya Imani Bungeni.

*Kuainisha mafanikio ya serikali kuhusu Uraia Pacha na Ardhi kwa wanadiaspora.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Peter Kayanda Mizengo Pinda (Mtoto wa Mkulima) leo Alasiri ya Jumanne tarehe 16 Oktoba, 2012 anatarajiwa kuunguruma Jijini London katika mkutano wake na Watanzania waishio hapa Uingereza.

Mheshimiwa Pinda ambaye yuko katika ziara fupi ya kibinafsi hapa London amerudia utaratibu wa kupenda kusemezana na Watanzania hata anapokuwa kwenye itifaki ya ziara fupi na ya binafsi, tabia ambayo imekuwa ikisifiwa na watanzania waishio nje ya nchi.

Aidha mkutano huu ni wa kwanza kwa Mheshimiwa Pinda hapa London tangu jaribio liloongozwa na wabunge wa Upinzani na wachache wa CCM kutaka kumng’oa madarakani liliposhindwa vibaya kwa kupata saini 70 tu kati ya 357 kupinga Ufisadi uliokithiri miongoni mwa watumishi vigogo ndani ya Serikali. Mkutano huu wa Waziri Mkuu unakuja katika kipindi ambacho Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania (CHADEMA) kimebadili ghafla mtazamo wake kwa watanzania nje ya nchi na kuanza kufungua utitiri wa matawi, kumwaga Ruzuku na kufanya ziara ya mara kwa mara kwenye matawi yao ili kuwapika makada wake kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Waziri kivuli wa Mambo ya Nje (CDM) Mhe. Dibogo Wenje ndiyo kwanza amemaliza ziara yake hapa London akiwa ameacha ahadi lukuki kwa wafuasi wao akiwataka wajiandae kushika majimbo ya Ubunge na nyadhifa mbalimbali serikalini kunako baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Awali, tofauti na CCM, CHADEMA walipinga sana uhusishwaji wa watanzania nje ya nchi katika miradi ya kisiasa na maendeleo ya kitaifa.

Katika hoja za msingi, Waziri Mkuu Pinda anategemewa kuainisha bayana msimamo wa serikali na hatua madhubuti ambazo imezichukua kutafsiri kwa vitendo Sera na Ahadi ya Chama cha Mapinduzi ya kujumuisha suala la Uraia Pacha katika marekebisho mapya ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa uwakilishi wake wa awali ulipokelewa kwa hofu miongoni mwa wabunge, baadhi ya wananchi, wanahabari na wafinyanzi wa Sera katika chelezo mbalimbali za kijamii.

Mashauri mengine yanayotarajiwa katika mkutano huu ni pamoja na maombi ya awali ya CCM UK ya kutaka Serikali iandae utaratibu maalum wa kuwasaidia watanzania waishiao nje ya nchi kupata na kuwekeza katika hazina ya ardhi nchini Tanzania kuliko ugumu uliopo sasa hivi. Aidha Serikali kuhamasisha sekta binafsi za kifedha na mitaji ya jamii kuwafikia watanzania ughaibuni ili kuhamisha teknolojia, ubunifu na uwezo wa kuwekeza katika maeneo kama Kilimo Kwanza na Ujasiria mali wa mizania ya kati.

Pamoja na mahudhurio kutarajiwa kuwa makubwa lakini watanzania wengi wanasemezana kuwa na imani na CCM lakini wanahisi Serikali na mamlaka zake bado hazija chukua hatua madhubuti kupunguza ufisadi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kitaifa.

Na Clement Mbawala

Tanzania Now: Freelance Observers Slough. St.Marys Road. SL3

Thursday, February 09, 2012

Maazimio ya Kikao Kati ya Waziri Mkuu na Madaktati Leo CPL

Asante Da Subi kwa Kuleta Taarifa Hii:


Tamko la Kamati: MAAZIMIO YA KIKAO CHA WAZIRI MKUU; MADAKTARI

09/02/20120 Comments Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoongoza mgomo wa Madaktari, Dkt. Stephen Ulimboka baada ya kuzungumza na madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es salaam, Februari 9, 2012. (Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu)
TAARIFA KWA UMMA NA MADAKTARI WOTE NCHINI JUU YA MAAMUZI YALIYOFIKIWA LEO FEBRUARY 9, 2012 KUFUATIA MKUTANO KATI YETU NA WAZIRI MKUU MHE. MIZENGO PINDA KATIKA UKUMBI WA CPL, HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

Kamati ya muda ya kushughulikia madai ya madaktari nchini inapenda kuwajulisha madaktari wote pamoja na kada nyingine zote za afya nchini juu ya kile ambacho kimejiri katika siku ya leo ya tarehe 09.02.2012 ikiwa ni matokeo ya kikao wanataaluma wa kada za afya na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda na baadaye kufuatiwa na kikao kati ya madaktari na kada nyingine za afya.

Ifahamike kuwa kama Kamati tulipata mwaliko wa kushiriki katika Mkutano huo ambapo ilitarajiwa kuwa Mhe, Waziri mkuu atafika kwa nia ya kutoa mrejesho wa madai ya madaktari yaliyowasilishwa mezani kwake mnamo tarehe 23.01.2012. Madai yetu yalikuwa manane na Mh Wazizri mkuu aliweza kutoa maelezo ya dai moja baada ya lingine.

Miongoni mwa madai ambayo mpaka sasa yamepatiwa majibu ya kuridhisha ni pamoja na;

Kuwawajibisha watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wakiwemo Katibu Mkuu Mama Blandina Nyoni , na Mganga Mkuu wa Serikali Dr. Deo Mtasiwa. Aidha Mh waziri mkuu alisema kuwa ameshalifikisha kwa Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania suala zima la kuwawajibisha watendaji wa wakuu wa kisiasa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao ni Waziri Mh Hadji Mponda na Naibu Waziri Mhe. Lucy Nkya.

Kama sehemu ya maridhiano, Mh Waziri Mkuu pia aliahidi mbele ya mkutano kuwa hakutawepo na unyanyasaji au vitisho vya aina yoyote ile kwa wale wote walioshiriki katika kushinikiza Serikali kutatua kero hizo. Aidha kama sehemu ya maridhiano, Mh waziri Mkuu pia alifuta zuio la madaktari kutokufanya mikutano. Lakini pia, Mh waziri Mkuu alisema kuwa Serikali haina kusudio la kumfukuza kazi mtumishi yeyote wa afya yule kazi aliyeshiriki katika mchakato huu wa kuishikiniza Serikali kutafuta ufumbuzi madai ya madaktari nchini.

Aidha, Mh waziri Mkuu amesema “Interns” wote waliokuwa wamehamishwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamesharudishwa bila masharti katika hospitali hiyo ili kuendelea na program kama kawaida. Hili pia linaambatana na kulipwa na kupewa stahiki zao zote.

Pia suala la madaktari na familia zao kuwa na Kadi ya Bima ya Afya ya kijani( Green Card) limekubaliwa na kwa sasa tusubiri utekelezaji.

Pia ilikubaliwa kuwa madaktari watapata fursa ya kukopeshwa magari kama watumishi wengine wa umma.

Mbali na madai hayo, pia Mh. Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya madai yanayuhusu maslahi ya watumishi wa afya ikiwa ni pamoja na Mishahara na Posho na stahiki mbalimbali. Lakini hata, Mh waziri Mkuu hakutoa majibu ya moja kwa moja ya kiwango gani kitakachoweza kulipwa na Serikali kama mishahara, posho na stahiki mbalimbali kwa minajili kwamba bado zinafanyiwa kazi na kamati ya wataalamu aliyoiunda ili waweze kumshauri. Aidha, Mh waziri Mkuu alisema kuwa kwa wakati huu inaweza kupandisha “on call allowances” za kada mbalimbali za afya kutoka shilingi 3,000 – 10,000/= na kufikia kati ya shilingi 5,000 hadi 25,000. Madaktari bado wanaona ongezeko hili halilingani na ukubwa wa kazi ifanywayo pindi mtumishi wa afya anapokuwa “on call” na hivyo basi kuendelea kupendekeza kuwa “on call” allowance iwe ni 10% ya mshahara wa mtumishi husika.

Pia Mhe, Waziri Mkuu hakuweza kueleza kinagaubaga mkakati kazi wa uboreshaji wa huduma za afya wapatayo wananchi wa Tanzania.

Baada ya tamko hilo la Serikali kumalizika, Mh Waziri Mkuu na ujumbe wake waliondoka, na Mkutano huo ukaendelea kwa Kamati kufanya Mkutano na madaktari wote, lengo ikiwa kujadili tamko hilo na kutoa maazimio.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, madaktari walikubaliana kwamba; kwa kuwa Serikali imeanza kuonyesha nia ya kutatua tatizo hili kwa kutekeleza baadhi ya maazimio yetu, wajumbe kwa niaba ya madaktari wote nchi nzima tulikubaliana na kuazimia yafuatayo;

Kurudi kazini mara moja kuanzia kesho tarehe 10.02.2012 bila masharti yeyote.

Kamati ya jumuiya ya madaktari kama sehemu ya MAT kuendelea kukaa mezani ya majadiliano na Serikali ili kuanza kupitia madai hasa yale yanayohusu maslahi.

Kukutana tena tarehe 03.03.2012 ili kupata mrejesho wa kiwango cha utekelezaji wa madai hayo kwa mujibu wa vikao vya majadiliano na makubaliano na hatimae kuchukua hatua zaidi.

Kujadili utekelezaji juu ya Kuwawajibisha Waziri na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi na Jamii.

Mwisho kabisa Madaktari wote kwa ujumla wake walilaani na kukemea kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji wanaharakati wa haki za kibinaadamu na mashirika ya kijamii wakiwemo Dr. Hellen Kijo-Bisimba na Mama Ananilea Nkya na wanaharakati wengine wote waliokumbwa na kamata kamata hiyo na hivyo basi tunalitaka jeshi hilo kuwaachilia huru mara moja bila masharti yeyoye.

Pamoja Tunaweza

Imetolewa na Kamati ya muda ya kushughulikia madai ya madaktari Tanzania

Dr, Ulimboka Stephen
Mwenyekiti.

Friday, November 21, 2008

Waziri Mkuu Pinda

Waziri Mizengo Pinda akiwa ndani ya vazi la jadi huku akishika silaha za jadi katika ziara yake ya "kuhimiza maendeleo" mkoani Dodoma hivi karibuni (Picha: Prime Minister's Office).

Asante Faustine's Baraza Blog: