SEMA DA FLORA WINGIA! SEMA!!!!!
************************************
Na Flora Wingia
Heri ya Mwaka Mpya 2010 mpenzi msomaji wangu. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kutuvusha mwaka huu. Naamini sote tumejipanga vema katika kufanikisha malengo mapya kwa mwaka mpya.
Wakati wengine wamepania kuboresha maisha ya familia zao, wengine wameamua kumeguka na kuanza maisha mapya kwingineko. Je, unajua ni kwanini? Hebu sikia kituko hiki cha kufunga mwaka 2009.
Ukiona mwanaume anaukimbia mji wake na kwenda kutafuta maskani mapya, ujue maji yamemfika shingoni. Katika hali ya kawaida ya maisha, mwanaume ndiye anayemkaribisha mwanamke nyumbani kwake na wakati mwingine huishia kumuoa.
Ukiona mwanamke anayemtunza mwanaume nyumbani kwake, huwa inaelezwa kuwa ‘mwanaume huyo kaolewa’. Lakini si unajua tena kupenda wakati mwingine mtu huwa zuzu au wengine huita zezeta. Hata akikemewa na wenzake yeye hujifanya hamnazo na kujikausha kwani anajua nini anachofaidi pale.
Pengine yeye ni kula kulala. Kila kitu anagharimia mke kuanzia chakula, mavazi na kadhalika. Mwanaume anayempata mwanamke wa aina hiyo, kwanini ajivunge?
Tukiachana na hayo, yupo mwanaume anayeoa mwanamke iwe ni kwa gharama kubwa au za kawaida, lakini baadaye mke huyo anamnyanyasa kiasi cha kumfanya auhame mji huo na kutamani mji mwingine. Hebu sikia kituko hiki cha funga mwaka.
Yuko baba mmoja nilikutanishwa naye hivi majuzi ambaye amelikimbia jiji la Dar es Salaam na kuhamia kijijini mkoa wa Pwani kutokana na manyanyaso anayopata toka kwa mkewe.
Baba huyu mwenye watoto wawili na mwanamama huyo, ameapa kumwachia mkewe kila kitu hapa jijini, na kisha yeye kuhamia kijijini kuanza maisha mapya mwaka huu mpya.
Baba huyu amenifurahisha sana. Wenzake wanahama vijijini kuja mijini lakini yeye anaamua kurejea maisha ya kijijini kutokana na suluba toka kwa mkewe.
Baba huyu anasema; “Heri kuishi peke yangu eneo la kijijini kuliko kuishi na mwanamke mwenye kero kama mke wangu. Nilimpenda mwenyewe, lakini sikujua kama angenifanyia yale niliyobainisha kwake.
“Mwanamke hataki kufanya kazi yoyote, yeye ni kwenda saluni, kukaa na kujipodoa tu. Nina mifugo, ng’ombe wawili wa maziwa, nguruwe na kuku wa kienyeji. Kutokana na mama huyo kutoonyesha nia ya kujishughulisha, nimeweka wafanyakazi wa kuhudumia mifugo hiyo.
“Akiamua hutoa nguruwe na kuuza na ninapomuuliza anakuja juu na kudai eti ni kwa matumizi ya nyumbani. Hata hivyo, kila siku lazima niache hela ya chakula mezani. Nikirudi nyumbani lazima aninuse eti kama nanukia marashi ya wanawake.
Wakati mwingine tunapopumzika hataki nimguse…hugeukia ukutani. Vituko hivi na vingine vinaninyima raha vibaya sana. Hadi najiuliza ni mwanamke gani huyu?Au anaye mwingine ampendaye?
“Nilimchangua mwenyewe, nikamuoa mwenyewe, lakini sasa nimefikia mwisho sina budi kumtosa. Sitamfukuza, lakini nitamwachia kila kitu, nyumba, mifugo na vitu vyote vilivyo mzunguka. Watoto nitapeleka shule za bweni. Ila mimi nakwenda kuanza maisha mapya”, anasema baba huyu.
Nilipomuuliza kama uamuzi huo amewajulisha wazee alisema; “Nilishaitisha kikao cha pande zote mbili kulalamika vituko vya mke huyu. Napo nilieleza msimamo wangu wa kutengana naye na kumwachia kila kitu. Ingawa hakukubaliana na hilo lakini niliungwa mkono na wajumbe wengi kwamba kwa kuwa hataki kujirekebisha, hakuna jinsi.
Mpenzi msomaji, kwa maelezo ya baba huyu, tayari ameshapata eneo katika kijiji kimoja mkoani Pwani ambako atajenga makao yake mapya na atajikita kwenye Kilimo Kwanza kwani anazo ekari 15 za ardhi. Hataki wala mwanamke wake huyu ajue huko kujiepusha na bughudha zake.
Ama kweli ‘mwenye bahati habahatishi. Mwanamke anapata mume mchakarikaji, lakini yeye anabweteka. Wapo wanaotafuta bahati ya aina hiyo bila mafanikio.
Nijuavyo mimi, mwanaume ni nguzo ya nyumba. Anapoondoka iwe ni kwa mfarakano au kwa kifo, hakika maisha katika nyumba husika huyumba na wakati mwingine hubomoka kabisa.
Mama yule anaonyesha jeuri ile kwa kuwa anamuona mumewe karibu, lakini atakapotokomea kijijini alikopania, mwanamama yule ambaye amekuwa mbwete, hataki kujishughulisha na miradi ya pale nyumbani, atajikuta naye pia akihangaika kama hayawani.
Ninachokiona kwa mwanamke huyu ni majuto mjukuu. Anachoshindwa kufahamu ni kwamba mwanaume wake huyo aliyepania kumponyoka ni hazina kwa maisha yake. Ni vema ajitambue kwamba pamoja na uvivu wake lakini bwana yule alimvumilia. Maandiko ya dini yameweka bayana kwamba ‘mwanamke mvivu na asile’.
Inapofikia hatua hata ile haki yake ya msingi ya ndoa anaikosa, je, baba huyu afanyeje? Ni mfanyabiashara anayekimbizana na kazi zake huku na huko ili aweze kutunza familia yake na pia kusomesha watoto, lakini mkewe hatambui hilo, anamchunguza chunguza eti leo ananukia marashi ya kike au kwanini umechelewa au kwanini umelala nje na kadhalika.
Ebo! Kama unamwekea vigingi kwanini asitafute starehe mahali pengine? Mambo mengine baadhi ya wanawake wanachangia. Mwanaume ni mvumilivu sana hasa inapohusu mambo ya familia yake.
Lakini ukiona mwanaume anasema ‘inatosha’ ujue amefikiria mbali. Amevuta pumzi hadi za mwisho. Kwa maoni yangu kuhusiana na mwanamama huyo ni kwamba kama kweli mumewe amepania kumwachia mji, na hakuwa makini, mali zote zinazomzunguka zitatoweka kama umande.
Inavyoonekana mume huyo amepania kutengana na mwanamama huyu kwa sababu hizo nilizotaja hapo juu huku akionyesha kuwa zipo sababu nyingine zilizojificha ambazo hakutaka kuzitaja hadharani. Ama kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.
Mpenzi msomaji wangu, hayo ndiyo yaliyojiri mwishoni mwa mwaka jana, baba huyu aliyepania kumkimbia mkewe na kuhamia kijijini kisa eti anamnyanyasa ikiwa ni pamoja na kumnyima haki yake ya unyumba.
Kama hayo ni kweli, basi mwanamama huyo amemkosea sana mumewe na anapaswa kujilaumu kwa uamuzi wowote atakaochukua. Kila mtu anapenda kuishi kwa raha bila bughudha. Maisha yenyewe ni mafupi sana hivyo hayahitaji masharti ya kisanii. Jipe raha na mpe pia raha mwenzako. Maisha Ndivyo Yalivyo.
fwingia@yahoo.com
No comments:
Post a Comment